Friday, May 15, 2015

WAZIRI SIMBA AZINDUA KITINI CHA ELIMU YA MALEZI KWA FAMILIA TANZANIA

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Mhe. Sophia M. Simba (Mb.) akikata utepe kuzindua Kitini cha Zana za Mawasiliano kuhusu Elimu ya Malezi kwa Familia, kushoto kwake ni Mhe. Dk. Pindi H. Chana (Mb) Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, kulia kwake ni Georgina Mtenga kutoka UNICEF na Anna T. Maembe Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.
Na  Erasto T Ching’oro- Msemaji Wizara ya 
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto

Katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Familia inayoadhimishwa tarehe 25 Mei, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Mhe. Sophia M. Simba (Mb) amezindua Kitini cha Elimu ya Maelezi kwa Familia Kuzuia Ukatili dhidi ya Watoto katika familia na jamii kwa ujumla.
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia huadhimishwa kila mwaka tarehe 15 Mei kulingana na  Tamko la Baraza la Umoja wa Mataifa Na. 47/237 la mwaka 1993. Tamko hili linahimiza nchi wanachama wa Jumuiya ya Umoja wa Mataifa kuwa na siku maalum ya familia ili kutafakari masuala yanayoikabili familia na kuchukua hatua za kukabiliana na changamoto zilizopo.  
Waziri Simba ameeleza kuwa huu, Tanzania itaadhimisha siku hii katika mikoa na wilaya. Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia 2015 ni: “Usawa wa Kijinsia na Haki za Watoto katika Familia: Wanaume Wawajibike”. Kauli mbiu hii inawakumbusha wanaume kutambua wajibu wao katika kuhudumia familia na kuachana na aina zote za ubaguzi wa kijinsia na kuwapatia watoto haki zao za msingi.
Katika kuenzi siku hii, Wizara Simba amezindua Kitini cha Elimu ya Maelezi kwa Familia Kuzuia Ukatili dhidi ya Watoto katika familia, tukio ambalo ujumbe wake unaendana na kauli mbiu ya siku ya familia mwaka 2015. Kitini hiki kinatoa elimu ya malezi kwa wazazi na walezi kuzuia ukatili dhidi ya watoto. Uzinduzi wa Kitini hicho umefanyika mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na wawakilishi wa Baraza la Watoto wa mkoa wa Dodoma, Viongozi wa Serikali, viongozi wa asasi za kiraia, wazazi na walezi.
Waziri Simba alieleza masikitiko yake kuona kuwa kufikia karne hii bado ukatili dhidi ya wanawake, watoto na watu wenye ulemavu unaendelea kuripotiwa katika jamii yetu. Wanawake wanafanyiwa vitendo vya kikatili na wenzi na hata kuuwawa. Aidha, watoto nao wanafanyiwa  vitendo vya kikatili kama vile kubakwa, kunajisiwa, kupigwa, kuchomwa moto, kukeketwa na kuozeshwa katika umri mdogo. Na kibaya zaidi, wenzetu wenye ualibino wamekuwa wahanga wa kukatwa viungo na kuuwawa katika familia zetu. Katika hali kama hii lazima sisi sote kulaani na kukemea ukatili. 

Simba alibainisha kuwa, katika ripoti ya utafiti wa ukatili dhidi ya watoto uliofanywa hapa Tanzania  mwaka 2011 ilionesha kuwa ukatili dhidi ya watoto ni wa aina tatu, wa kingono, kimwili na kihisia. Ukatili huu umekuwa ukifanywa na watu walio karibu na watoto wakiwemo wazazi, walezi, ndugu wa karibu na walimu mashuleni. Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 60 ya wasichana na wavulana walifanyiwa ukatili na ndugu ambapo asilimia 80 ya wasichana na 65 ya wavulana walifanyiwa ukatili wa kihisia. 
Katika kukabiliana na changamoto hii Mpango kazi wa Kitaifa wa miaka 3 wa kuzuia na kukabiliana na ukatili dhidi ya watoto (2013-2016) uliandaliwa. Mpango huu umeainisha majukumu ya wadau mbalimbali ya kukabiliana na ukatili dhidi ya Watoto Tanzania. Kutoka na Mpango huu Wizara ya Maendeleo ya jamii, Jinsia na Watoto imeandaa Kitini cha Kitini cha Elimu ya Maelezi kwa Familia Kuzuia Ukatili dhidi ya Watoto katika familia.
Imeelezwa kuwa Kitini hiki ni Mwongozo wa Kitaifa kwa Wawezeshaji katika ngazi ya Jamii Kuzuia Ukatili na Unyanyasaji wa Watoto Tanzania. Kitini hiki kinaainisha mbinu za kuelimisha wazazi na walezi kuwa na uelewa na stadi za kuzuia ukatili dhidi ya watoto. Akitoa maoni yake kuhusu umuhimu wa kitini hicho, washiriki walieleza kuwa elimu itajenga uelewa kwa wazazi na walezi kuhusu kulea watoto katika njia sahihi. Vile vile walezi na wazazi watapata mbinu za jinsi ya kuwasiliana na watoto wao katika lugha nyepesi na pia kutumia mbinu za kumsikiliza mtoto kujikinga na ukatili na kueleza ukatili ulivyotokea na kuwalinda watoto. 
Wizara ina uhakika kuwa, kama wazazi na walezi watapata elimu stahiki ya malezi, tutapunguza matatizo mengi ya mmomonyoko wa maadili kwa watoto na vijana wetu. Hii itapunguza hata idadi ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani kwa sababu tatizo hili kwa kiasi kikubwa linachangiwa na ukatili dhidi ya watoto. 
Waziri alitoa rai, kwa wanafamilia kwamba watafasiri kwa vitendo elimu ya malezi watakayofundishwa na Maafisa Maendeleo ya Jamii na wawezeshaji wengine wa jamii ambao wameandaliwa kutoa mafunzo haya. Aidha, aliwasihi wazazi na walezi hasa wanaume kuwajibika kikamilifu kwa kushirikiana na akina mama katika malezi bora ya watoto wao. Wito huu umetolewa kwa kutambua kwamba wanaume wana nafasi kubwa katika kuleta mabadiliko ikiwa ni pamoja na kutokomeza ukatili wa kifamilia. 
Wizara inatoa wito kwa kila mwanafamilia kushiriki maadhimisho ya Siku hii muhimu kwa kufanya shughuli mbalimbli za kimaendeleo na kushiriki katika maadhimisho. Aidha, tunaomba vyombo vya habari kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa Maadhimisho haya ili kuzuia na kulaani ukatili wanaotendewa watoto wetu katika familia na jamii kwa ujumla.


No comments: