Naibu kamishna wa jeshi la polisi kikosi cha Usalama Barabarani SACP Johanes Kahatano(katikati) akiwafafanulia jambo Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Vodacom Tanzania, Rosalynn Mworia(kushoto) Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kamishna Msaidizi wa Polisi Mohamed Mpinga, Mkurugenzi wa Radio One Stereo, Deogratius Rweyunga kuhusiana na kampeni ya kuzuia ajali barabarani inayojulikana kama“Zuia Ajali Sasa,Toa Taarifa Mapema” kupitia namba 0800757575.Kampeni hiyo inaendeshwa na jeshi la polisi kikosi cha Usalama barabarani,Vodacom Tanzania na kwa vyombo vya habari vya kampuni ya IPP .
Mkuu wa jeshi la polisi kikosi cha Usalama Barabarani Kamanda Mohamed Mpinga (kulia) akipata maelezo kutoka kwa Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Vodacom Tanzania, Rosalynn Mworia (kushoto) kuhusiana na kampeni ya kuzuia ajali barabarani inayojulikana kama“Zuia Ajali Sasa,Toa Taarifa Mapema” kupitia namba 0800757575,Katikati ni Mkurugenzi wa Radio One Stereo, Deogratius Rweyunga.Kampeni hiyo inaendeshwa na jeshi la polisi kikosi cha Usalama barabarani,Vodacom Tanzania na Vyombo vya habari vinavyomilikiwa na kampuni ya IPP .
Mkurugenzi wa Radio One Stereo, Deogratius Rweyunga(katikati)akishuhudiwa na Mkuu wa jeshi la polisi kikosi cha Usalama Barabarani Kamanda Mohamed Mpinga(kushoto) Rosalynn Mworia Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Vodacom Tanzania akibandika stika yenye namba 0800757575 ambayo imetolewa mahususi kwa abiria wanaotumia vyombo vya moto kusafiria kutoa taarifa bure kupitia namba hizo wakati wa uzinduzi wa kampeni inayojulikana kama “Zuia Ajali Sasa,Toa Taarifa Mapema” Kampeni hiyo inaendeshwa kwa usirikiano baina ya Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama barabarani,Vodacom Tanzania na vyomo vya habari vinavyomilikwa na kampuni ya IPP
Wananchi watakiwa kutoa taarifa za ukiukaji wa kanuni na sheria za usalama barabarani
· Ni kupitia kampeni ya zuia ajali sasa,toa taarifa mapema
Dar es Salaam, Mei 27, 2015: Kufuatia wimbi la ajali lililosababisha vifo vya mamia ya watu na maelfu wengine kujeruhiwa,wananchi wametakiwa kuunga mkono jitihada za kupunguza ajali nchini kwa kutoa taarifa kwa vyombo ya usalama waonapo kanuni na sheria za barabarani zinakiukwa na madereva wazembe hasa wanapokuwa wanasafiri na magari yaendayo masafa marefu.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kamishna Msaidizi wa Polisi Mohamed Mpinga wakati wa uzinduzi wa kampeni mpya ya kuhamasisha usalama barabarani ijulikanayo kama “Zuia Ajali Sasa,Toa Taarifa Mapema” inayofanyika kwa ushirikiano wa serikali kupitia Jeshi la Polisi, kampuni ya mawasiliano ya Vodacom na kampuni ya vyombo vya habari vya IPP. Uzinduzi huo umeambatana na kuzinduliwa na namba maalumu ya kutoa taarifa za ukiukwaji wa kanuni na usalama barabarani ambayo ni: 0800757575.
“Matukio ya ajali hapa nchini yatapungua iwapo watumaji wa barabara hususan madereva watazingatia sheria na kanuni za usalama baabarani na ni jukumu letu sote kuvalia njuga tatizo hili na kutoa taarifa za madereva na watumiaji wa barabara wazembe kwa vyombo vinavyohusika ili wachukuliwe hatua za kisheria. Nayapongeza makampuni ya Vodacom na IPP Media kwa kuungana na Jeshi la Polisi katika kampeni hizi,” alisema Kamanda Mpinga.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo Mkuu wa Mawasiliano ya makampuni na Uhusiano wa Vodacom Rosalynn Mworia amesema “Tukiwa kampuni ya mawasiliano tutaendelea kuunga mkono jitihada za kupunguza ajali nchini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali walioko katika mapambano haya. Leo tumetoa namba ya simu ya kutoa taarifa za ukiukwaji wa sheria barabarani ambayo ni ya bure kwa wateja wa Vodacom.
Mteja atakayepiga kutoa taarifa kupitia namba hii hatatozwa gharama zozote bali tutazibeba ikiwa moja ya jitihada za kuunga mkono kampeni hizi. Nawakumbusha watumiaji wa barabara tuzingatie sheria na kanuni na tusisite kutoa taarifa kwa vyombo husika tunapoona vitendo vya kuhatarisha maisha kutoka kwa watumiaji wa barabara wazembe,” alisema.
Vodacom imekuwa mstari wa mbele katika kampeni za uhamasishaji usalama barabarani na mwaka jana ilizindua kampeni ya “Wait to Send” inayohamasisha madereva kutotumia simu za mkononi wanapokuwa wanaendesha vyombo vya moto na kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani.
Wakati wa uzinduzi wa kampeni hii uliofanyika katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo ambapo madereva waligawiwa pete maalumu za kuwakumbusha kuacha matumizi ya simu wanapokuwa wanaendesha vyombo vya moto, pia waligawiwa vipeperushi ya kuwakumbusha kanuni na sheria za usalama barabarani. Pia abiria walihimizwa kutoa taarifa za uzembe wa madereva wanapokuwa safarini kupita vibandiko vyenye ujumbe wa kampeni hii usemao “Zuia Ajali Sasa,Toa Taarifa Mapema” vyenye namba ya kutoa taarifa ya: 0800757575..
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Radio One Stereo, Deogratius Rweyunga alisema kuwa kampeni hii muhimu ina uwezo wa kupunguza kwa kiasi kikubwa nap engine kutokomeza kabisa kupitia teknolojia za mawasiliano.
“Kampeni tunayoizindua leo itahusisha kurushwa kwa taarifa na matukio ya ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani kupitia Radio One Stereo, ITV na Capital Radio. Kusudi kubwa la kufanya hivi ni kuendeleza ujumbe wa usalama barabarani ka upana zaidi na pia kuwaweka bayana wale wote wanaokiuka na kuvunja sheria za usalama barabarani kwa makusudi kabisa. Tutatumia pia uwepo wetu katika mtandao kupitia Twitter na Facebook katika kuhakikisha tunatumia kila nafasi kusambaza ujumbe huu muhimu,” alisema Rweyunga.
Aliongeza kuwa ushirikiano kati ya vyombo vyao vya habari na Vodacom Tanzania utafanikiwa na kuchangia kwa kiasi kikubwa kampeni hii ya uhamasishaji wa umma. Kujitolea kwa vyombo hivi vya habari kutaisaidia kampeni hii kufikia malengo yake yote, kubwa haswa likiwa kufanya barabara kuwa njia salama kuliko zote za usafiri.
No comments:
Post a Comment