Monday, May 18, 2015

TPDC YAANZA UTAFITI TANGA

Mkurungezi wa Utafiti Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania, Dkt. Emma Msaky, akizungumza na wataalam wanao endelea na uchimbaji wa visima vifupi katika Mradi Ujulikanao kama MP 10 GOMBERO DRILLING PROJECT kwa ajili wa utafiti wa mafuta na gesi kijiji cha Jihirini, wilayni Mkinga mkoani Tanga.
Mkurungezi wa Utafiti Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania, Dkt. Emma Msaky, akionyesha sampuli za utafiti mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) katika Mradi wa utafiti wa mafuta na gesi Ujulikanao kama MP 10 GOMBERO DRILLING PROJECT kijiji cha Jihirini, wilayni Mkinga mkoani Tanga.
Meneja wa Mradi wa MP 10 GOMBERO DRILLING PROJECT, Dkt. Amina Karega, akionyesha sampuli za utafiti mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) kijiji cha Jihirini, wilayni Mkinga mkoani Tanga.

Na. Augustino Kasale - Kitengo Cha Mawasiliano-TPDC

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania limeanza utafiti wa mafuta na gesi eneo la Gombero, Wilayani Mkinga, Mkoani Tanga.

Mkurugezi wa Utafiti kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania, Dkt. Emma Msaky, mwishoni mwa wiki alitembelea kujionea shughuli inayo fanya na Shirika hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari alioambatana naye Dkt. Msaky alisema kuwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), limeanza Mradi wa uchorongaji wa visima vifupi kumi (10) vya utafiti wa kijiolojia wa utafutaji mafuta na gesi katika vijiji mbalimbali mkoani Tanga ujulikanao kama MP 10 GOMBERO DRILLING PROJECT.  

“Mradi huu unafanywa na kumilikiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa asilimia mia moja (100%),” alisema Dkt. Msaki.

Alifafanua kuwa TPDC inatumia wataalam wake wataaluma mbalimbali waliobobea kwenye fani ya  utafutaji wa mafuta na gesi katika kufanikisha Mradi huu. Lengo likiwa kuwapa mafunzo (internal capacity builiding) wataalam vijana (young geoscientists) wa TPDC kwa kuwatumia wataalam wa ndani ya Shirika waliobobea.

“Kazi hii imepangwa kufanyika ndani ya siku arobaini (40), ikiwa ni wastani siku nne (4) kwa kila kisima kifupi, visima vyote vifupi kumi (10) vipo maeneo ya Gombero, Nairobi, Pangalawe na Kijiji cha Jirihini wilayani Mkinga, Mkoani Tanga,” alisisitiza Dkt. Msaky.

Dkt. Msaky aliongeza kuwa TPDC imeingia mkataba na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambao wanatumia mashine ya uchorongaji (drilling Rig) aina ya Long year 38 kwa ajili ya uchorongaji mashimo vifupi.

“STAMICO na TPDC, zote ni taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Madini hii inaonesha uzalendo wa hali ya juu wa kutumia kampuni ya ndani (ya kitanzania) na wataalam wa kitanzania katika kufanikisha mradi huu,” alisisitiza Dkt. Msaky

Alisema malengo makuu ya mradi huu (MP10 Gombero Drilling Project) ni kuzidi kuyaainisha maeneo ya utafutaji wa mafuta na Gesi ili kujua uwepo wa miamba ya uzalishaji wa gesi na mafuta  (source rocks), miamba ya kuhifadhia gesi/mafuta  (reservior rocks) na miamba ya kuzuia mafuta yasitoke (seals /caprocks).

“Pamoja na uwepo wa Mradi huu wa MP 10 GOMBERO DRILLING PROJECT, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa sasa linaendesha tafiti katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa na lengo la kuongeza thamani ya vitalu vya utafiti nchini,” alisema Dkt. Msaky.

Na kuogeza kuwa Shirika linayo imani kuwa upatikanaji wa taarifa mpya za kijiolojia kupitia tafiti hizi itafungua milango ya kuwavutia wawekezaji zaidi ili waweze kuyaendeleza maeneo hayo na kuleta tija kwa Shirika na Taifa zima.

Kwa upande wa Meneja wa Mradi huo Dkt. Amina Kalega kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania, alisema hadi hatua waliyo fikia Mradi unaendelea vizuri na hakuna changamoto kubwa waliyo kumbana nayo.

“Kwa kweli hadi kufikia hapa kisima kifupi cha kwanza kimeisha hatuja kumbana na changamoto sana na tunatumaini mradi utaisha vizuri kama tulivyo panga,” aliongeza Dkt Amina.

Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Jihirini Bw. Jumaa Kasidi Jumaa, ambapo kisima hicho kifupi cha kwanza kilipo alisema ushirikishwaji wa serikali ya kijiji umekuwa mzuri toka Mradi ulipo anza, 
“Huu mradi Wananchi aliukubali kwa furaha kubwa sana na walifurahi zaidi kuwa vijana wao kupata kazi katika mradi huu,” aliongeza Bw. Jumaa.

Mradi huu ilianza rasmi mwaka 2010 ukiwa na malengo ya kuwajengea uwezo wataalam wa sayansi ya utafutaji wa mafuta na gesi ambao hawakuwa na msingi wa taaluma ya kijiolojia (kama wale wa fani ya Jiolojia na Uhandisi) kwa kuwapatia mafunzo na elimu ya vitendo katika mabonde (sedimentary basins) ya Tanzania likiwemo eneo la Gombero (Bonde la Tanga).

Mradi huu unahusisha wataalam kukusanya sampuli za Jiolojia, Jiokemikia na kuchambua sampuli, kufanya tafiti mbalimbali kuhusisha sampuli hizo na utengenezaji wa ramani za kijilojia katika maeneo husika.

Mwaka 2012 hadi 2013 baada ya kazi za vitendo (Geological Field) katika maeneo ya Kakindu na Mto Kivundo karibu na bwawa la Nairobi, Gombero mkoani Tanga, wataalam waligundua uwepo mkubwa wa miamba tabaka aina ya Shale, Silt shale na makaa ya mawe.  Hapo ndipo wazo la kupanua mradi kuingia kwenye hatua ya uchorongaji wa visima vifupi lilianza.

Gharama za uchorongaji wa visima hivyo vifupi ni takribani Dola za Kimarekani laki moja na tisini na tano elfu (Us Dollars 195,000) sawa sawa na shilingi za Tanzania Tshs. 370,500,000. Fedha zote hizo zinalipwa na TPDC kutoka kwenye mfuko wake wa fedha za miradi ya maendeleo.

No comments: