Sunday, May 24, 2015

TANZANIA KATIKA UMOJA WA MATAIFA WIKI HII

Na  Mwandishi Maalum, New York
Umoja wa Mataifa wiki hii, umekamilisha mikutano  muhimu miwili kati ya mingi, ambapo  ujumbe wa Jamhuri ya  Muungano  wa Tanzania ulioshiriki majadiliano  ya mikutano hiyo waliiwakilisha vema nchi yao.
Moja ya mikutano hiyo  ni ule   wa  marejeo  ya Mkataba wa kuzuia usambaaji na uzalishaji   wa silaha za nyukilia, matumizi yake, ikiwa ni pamoja na silaha nyingine za maangamizi ( NPT),   Mkutano huu ambao umefanyika kwa mwezi  mzima,  ukitawaliwa na majadiliano   makali  juu ya  mada mbalimbali muhimu zinazohusiana na  marejeo  ya mkataba huo. Bado hadi siku ya mwisho  ya mkutano ( Ijumaa) wajumbe wamemaliza mkutano pasi kufikia makubaliano ya  pamoja ya vipengele kadhaa vya tamko la mwisho la mkutano.
Katika kile kilichooneka wazi  kwamba wajumbe wamekubali kuto kukubaliana,  ni kwa  baadhi ya  mataifa  hasa yale ya magharibi na yenye silaha za nyukilia kutoonyesha utayari na utashi wa kisiasa wa  kuungano  mkono  baadhi ya  mambo kadhaa  likiwamo  la  kufanyika kwa mkutano   wa Ukanda Huru  usio na  silaha za Nyukilia katika Eneo la Mashariki ya  Kati .
Mataifa kama vile Marekani,  Uingereza na Canada yalisimamia kidete misimamo yao ya kupinga kuingizwa katika   tamko  la mwisho la mkutano wa NPT sehemu inayopendekezwa kufanyika kwa mkutano huo huko  Mashariki ya Kati, kwa kile walichodai kwamba baadhi ya  mataifa yamelipenyeza suala hilo  bila ya   ushirikishwaji wa nchi  nyingine ikiwa Israel jambo ambalo wamesema hawakubaliani  nalo.
 Mkutano  kuhusu ukanda huru usio wa silaha za nyukilia katika  eneo la Mashariki ya Kati,  umeshindikana kufanyia kwa muda mrefu sasa licha  ya maazimio mbalimbali yanatoaka  ufanyika.
Kushindwa kwa mkutano huo ambao unaelekezwa kama muhimu kwa mustakabali wa hali ya  amani na usalama  katika eneohilo,  unatokana kwa kiasi kikubwa kukosekana kwa uungwaji mmono  usio na shaka kutoka kwa wadau mbalimbali ikiwamo Israeli ambayo imekuwa ikilalamikwa na baadhi ya mataifa ya Kiaarabu.
Israel si mwanchama wa NPT. lakini pia inasadikiwa   inamiliki silaha za nyukilia  ingawa  haijatamka hadharani.  Mataifa mengi yakiwamo yakiiarabu yamekuwa yakilitaka  taifa hilo kutamka mbele ya   Jumuiya ya Kimataifa kwamba inamiliki  silaha hizo lakini imekuwa ikikingiwa kifua na baadhi ya  mataifa makubwa.
Eneo jingine ambalo  wajumbe wameshindwa kukubaliana kwa kauli moja ni pendekezo   la kuingizia kwenye mkataba huo    sehemu itakayozungumzia  madhara ya kibinadamu yatakayo na  matumizi ya silaha za nyukilia.  Eneo hili nalo  limezua mjadala mzito kiasi kwamba licha ya  umuhimu  wake kwa uhai wa mwanadamua na viumbe hai likashindwa pia kufikia  makubaliano  ya pamoja.
 Rasmu ya tamko  la mwisho la mkutano  huo  limepitishwa kwa  vifungu kutokana na kile ambacho wajumbe wamesema ni kutoridhishwa kwa maudhui mazima ya  tamko hilo huku wengine wakieleza kwamba, baadhi ya vifungu ambayo vilipitishwa kwa  makubaliano wakati wa majadiliano ya wiki nne  havikuingizwa katika  tamko hilo

Wazungumzaji wengi  katika siku ya mwisho ya mkutano huu ambao ulikwenda hadi saa tatu  usiku, siku ya  ijumaa, wameelezea masikitiko yao  ya kukosekana kwa fursa ya  kusukuma mbele utekelezaji wa  NPT kwa sababu tu ya baadhi ya nchi kusimamia maslahi binafsi badala ya maslahi ya jumla.
Mkutano wa pili  ambao nao ulikuwa na mvutano wa aina yake  ni ule uliokuwa ukijadili  maandalizi ya  ajenda na malengo mapya ya maendeleo endelevu baada ya 2015 ( SDGs). Mkutano huu wa wiki moja na ambao  pia ulimalizika  siku ya ijumaa, wajumbe licha ya kukubaliana na  maudhui mazima ya  haja na umuhimu wa  kufanyika kwa tathmini na ufuatiliaji wa utekelezaji wa  SDGs,  wajumbe walishindwa kukubaliana kwa kauli moja mada au ajenda  zitakazo jadiliwa wakati wa mkutano wa  Kisiasa wa Ngazi ya Juu wa  viongozi  Wakuu wa Nchi na Serikali utakaofanyika  mwezi Septemba  2015
Mkutano huo wa Kilele wa Kisiasa wa viongozi  unatarajiwa  kupokea na kupitisha ajenda na malengo ya  maendeleo endelevu baada ya 2015,   mkutano ambao pia utakuwa na  miduara ya  majadiliano   ya maada mbalimbali.
 Katika  maandalizi ya   mkutano huo, Rais wa Baraza  Kuu la Umoja wa Mataifa aliziomba nchi wanachama  kuunda  mada zikazojadiliwa katika mkutano huo, maanda mabazo kimaudhui zinatakiwa kwenda na  SDGs.
Kwa wiki kadhaa  nchi wanachama   kupitia makundi yao ya kikanda  walikuwa na kazi kubwa ya kubuni mada hizo,  kuzijadilia na kisha kukubaliana zile ambazo wanaamini  ndizo muhimu.
Mada ambazo zimependekezwa  ni  pamoja na mada itakayojadili   kumaliza umaskini na tatizo la njaa, kukabiliana na ukosefu wa  usawa,  uwezeshwaji wa wanawake na wasichana bila kuacha mtu nyuma, kukuza  uchumi endelevu na  kuleta mabadiliko katika   uzalishaji na kiwango cha matumizi  na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi  ili kuilinda dunia.
Mada nyingine zinazopendekezwa ni  kujenga ufanisi, uwajibikaji ili kufikia maendeleo endelevu, kukuza ushirikiano wa kimataifa, kujenga misingi imara ya uwajibikaji na taasisi jumuishi ili kufikia maendeleo endelevu na  kukuza ushirikiano wa kimataifa.
Pamoja na kukuballiana juu ya mada hizo,  washiriki wa mkutano  huu walishindwa kukubaliana juu ya maudhui pana   iliyoainisha kila  mada. Kutokana nakwamba  kila nchi au kundi wakilishi lilikuwa na  tafsiri tofauti ya maelezo ya  ziada ya  mada hizo.
 Matokeo ya  kushindwa kukubaliana   kuhusu maudhui pana au maelezo yakina ya baadhi  mada na baada ya majadiliano ya kujaribu kupata muafaka kati ya pande zinazopinga kushindwa kuafikiana,   Wenyeviti- wenza wa majadiliano hayo  walieleza kwamba kutokana na wajumbe  kutokubaliana basi mada hizo zitapelekwa  kwa Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa maamuzi.
Ilikubaliwa katika mkutano huo kwamba  mada hizo ziwasiliwe kwa Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, bila  ya maelezo ya ziada kuhusiana na  mada zenyewe kwa vile nchi wanachama zilishindwa kukubaliana.

No comments: