Na Bashir Yakub.
Malalamiko ya raia dhidi ya jeshi la polisi hayataishi kama polisi wenyewe hawatajirekebisha. Na ieleweke kuwa si kweli kwamba wanaolalamika ni wajinga au hawana sababu za msingi. Mara zote ukiangalia malalamiko ya raia huwa ni ya msingi na mzizi wake ni mmoja tu. Ni utamaduni wa askari wetu kutopenda kutenda hatua kwa hatua kama sheria inavyoagiza. Sheria imetoa maelezo mazuri tu ya namna ya kuyaendea mambo. Tatizo watekelezaji ndio hakuna.
Sheria husema kingine na watekelezaji hufanya kingine. Namna hii huwezi kuepuka chuki na migongano kati ya hawa watekelezaji askari na raia. Na migongano na kutokuelewana kunapokuwa kukubwa na usalama nao unayumba kwakuwa ili askari afanye kazi ya usalama vizuri anategemea msaada wa raia karibia kwa asilimia zaidi ya 80. '
Na raia huyu hatatoa ushirikiano wakati jana umempiga bila sababu, umemtukana na kumtolea maneno ya kebehi. Makala iliyopita nilizumgumzia namna sheria inavyomruhusu raia kukataa kukamatwa na polisi iwapo polisi huyo atakiuka taratibu katika ukamataji. Leo nazungumzia namna sheria inavyokataza kumchukua mtu mwingine baada ya kumkosa mtuhumiwa halisi wa kosa. Tutaona hili likoje.
1.ASKARI KUONDOKA NA MTU MWINGINE BAADA YA KUMKOSA MTUHUMIWA HALISI.
Hii ni tabia ambayo imezoeleka sana na ipo kwa muda mrefu. Yumkini kuzoeleka kwake na kuwepo kwake kwa muda mrefu hakuifanyi hata kwa sekunde moja tabia hii kuwa halali kisheria. Mara nyingi wanaokutwa sana na tabia hii ni watu wa vijijini hasa wa hali ya chini. Lakini hata mijini pia ipo sana. Nazungumzia tabia ya kuondoka na mtu mwingine baada ya kumkosa mtuhumiwa halisi. Kwa mfano askari wamekuja nyumbani kumtafuta JOHN kwa kosa analotuhumiwa nalo. Bahati mbaya au nzuri JOHN hayupo nyumbani.
Kutokana na hilo askari wanaamua kuondoka na mke wa JOHN au mtoto wake ili kumfanya JOHN aweze kutokea. Hiki ndicho ninachozungumzia. Na wanaokuwa wakichukuliwa mara kwa mara ni mke wa mtuhumiwa , mtoto au ndugu. Lengo eti ni kumfanya mtuhumiwa halisi aweze kujisalimisha.
2. SHERIA INAKATAZA KABISA KUMCHUKUA MTU MWINGINE BADALA YA MTUHUMIWA HALISI.
Ni lazima ieleweke na askari wetu wafahamu kuwa sheria iko wazi kuwa aliyetenda kosa ndiye anayewajibika na kosa. Haiwi na haitokuwa kosa la fulani akaliwajibikia fulani. Askari wajue kuwa kamwe kisheria hakuna anayesimama kujibu kosa la mwingine . Ni kutokana na msimamo huu mahakama kuu katika kutafsiri sheria mbalimbali zinazokataza jambo hili ikasema katika kesi ya LULU TITU vs R ( 1968 ) HCD No. 330 kuwa ni kosa kubwa kwa askari kumkamata au kuondoka na na mtu mwingine baada ya kumkosa mtuhumiwa .
Katika kesi hiyo askari walikuwa wamemkamata na kumchukua mke wa mtuhumiwa baada ya kumkosa mme wake ambaye alikuwa anatuhumiwa. Mahakama ilikemea vikali jambo hilo na kutia msisistizo juu uharamu wake kisheria. Maamuzi ya mahakama ( mahakama kuu na ya rufaa) ni sheria na hivyo msimamo huo ni sheria.
3. NINI UFANYE HILO LIKIKUTOKEA AU KAMA LIMEKUTOKEA TAYARI.
Kwanza kesi hiyo niliyotaja hapo juu haikuishia kukemea jambo hilo bali ilienda mbele zaidi kwa kutoa mwongozo wa nini mtu afanye iwapo limemtokea hilo . Mahakama ilisema kuwa iwapo mtu amechukuliwa bila kuhusika basi anayo haki ya kufungua shauri la madai na kudai kulipwa fidia.
Katika shauri la madai la namna hii utamfungulia askari husika lakini pia utaliunganisha jeshi la polisi ambalo ni mwajiri wa askari huyo/hao. Lengo la kuliunganisha jeshi la polisi ni ili hukumu itakapotoka ya kulipwa fidia basi jeshi hilo ndilo lilipe fidia kwa niaba ya askari wake. Ndugu Mtanzania hakuna shaka fidia utalipwa tu kama hili limekutokea kweli.
Pili kitu kingine ambacho unaweza kufanya ni kugomea kukamatwa/kuchukuliwa. Katika kesi ya JUMA NZIGE vs R (1964) EA 107 mahakama ilitoa mwongozo kuwa raia ana haki ya kugomea ukamataji wowote ambao si halali. Kwa maana hii ikiwa we si mtuhumiwa basi unaweza kukataa kukamatwa na hakuna lolote litakutokea kwakuwa uko sahihi mbele ya macho ya sheria. KATAA UNYANYASAJI, CHUKUA HATUA.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com
KUSOMA ZAIDI LINKS goes to sheriayakub.blogspot.com
No comments:
Post a Comment