Thursday, May 21, 2015

HOTUBA YA MHE. DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA UFUNGUZI WA MKUTANO KUHUSU UENDESHAJI WA SHUGHULI ZA SERIKALI KWA UWAZI KWA KANDA YA AFRIKA ULIOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA MWALIMU JULIUS NYERERE, DAR ES SALAAM TAREHE 20, MEI 2015

Mhe. George Mkuchika (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu, Utawala Bora;
Waheshimwa Mawaziri,
Katibu Mkuu Kiongozi;
Makatibu Wakuu;
Wakuu wa Taasisi za Serikali;
Wakuu wa Taasisi Zisizo za Serikali;
Wawakilishi wa Wabia wa Maendeleo;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana.
Nakushukuru Mheshimiwa George Mkuchika, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Utawala Bora kwa kunialika na kunishirikisha katika ufunguzi wa  Mkutano wa Pili wa Kikanda wa  Washirika wa Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi (Open Government Partnership-OGP). Pia nawashukuru waandaaji wa Mkutano huu kwa kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa mwaka huu. Ni heshima kubwa kwetu na kielelezo cha imani ya washirika wenzetu wa Mpango huu kwa nchi yetu.
Kwa washiriki wote nasema karibuni mkutanoni na nawatakia Mkutano wenye mafanikio. Wanaotoka nje ya Tanzania nawaambia karibuni sana kwetu. Tumefurahi kuwa nanyi na bila ya shaka wenyeji wenu watafanya kila wawezalo ukaazi wenu uwe mzuri na ushiriki wenu uwe wa mafanikio. 
Nawaomba baada ya mkutano mtafute wasaa mkatembelee vivutio vya utalii ambavyo nchi yetu imejaaliwa navyo. Visiwa vya marashi ya karafuu yaani Zanzibar viko mwendo wa robo saa kwa ndege na dakika 50 kwa boti iendayo kasi. Mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama za Serengeti, Ngorongoro na Ziwa Manyara na Tarangire ziko saa moja kutoka hapa kwa ndege. Nendeni ili mrudi kwenu na kumbukumbu nzuri ya nchi yetu na kushawishika kuja tena kwa kipindi kirefu.
Kwa namna ya kipekee nawakaribisha wajumbe kutoka nchi za rafiki za Botswana, Nigeria, Zambia, Uganda, Zimbabwe na Ivory Coast. Nchi zao bado si wanachama wa Mpango huu, lakini ushiriki wao leo kama wasikilizaji ni sawa na ule msemo maarufu wa waswahili usemao “nyota njema huonekana asubuhi”. Bila ya shaka kuwepo kwao ni dalili njema ya uwezekano wa nchi hizi kujiunga na Mpango huu siku za karibuni. Tunawakaribisha kwa mikono miwili.
Nimefurahishwa sana na uamuzi wa kutumia lugha ya Kiswahili katika sherehe hizi za ufunguzi kwa lengo la kuwezesha umma wa Watanzania kushiriki na kufuatilia kwa urahisi kinachoendelea katika Mkutano huu.  Huu ni mfano mzuri wa kutekeleza kwa vitendo moja ya nguzo muhimu ya Mpango huu ambayo ni kushirikisha wananchi. Ni jambo muhimu kwamba wananchi hawapati vikwazo katika kushiriki na kufuatilia mambo yanayowahusu kwa kutumia lugha wanayoielewa. Ningefarijika sana kama mkutano wote ungeweza kutumia lugha ya kiswahili.
Kauli Mbiu
Ndugu Washiriki;
Mabibi na Mabwana,
Kauli mbiu ya Mkutano huu yaani “Kuimarisha Uwajibikaji Kupitia Uwazi katika Uendeshaji wa Shughuli za Serikali” (Enhancing Accountability Through Open Governance) ni maridhawa kabisa. Kuendeleza uwajibikaji Serikalini ndiyo shabaha kuu ya Mpango wa Uwazi katika Serikali. Serikali kuendesha shughuli zake kwa uwazi ni jambo la msingi katika uwajibikaji. Wananchi ambao ndio walengwa na ndiyo sababu ya kuwepo kwa Serikali watatambua kwa uhakika jinsi serikali yao inavyowahudumia kama kuna uwazi. Uwazi unawawezesha watu kudai haki zao au kuwakumbusha viongozi na watendaji Serikalini kutimiza wajibu wao kwa raia wanaotakiwa kuwahudumia.
Kwa maneno mengine ushiriki wa wananchi wenye tija na uwajibikaji mzuri wa Serikali ni matokeo ya upatikanaji wa taarifa kutoka Serikalini. Taarifa hizo lazima ziwe sahihi na zipatikane kwa urahisi na uhakika.  Ili iweze kuwa hivyo hapana budi kuwepo kwa uwazi. Taarifa huwaongezea wananchi uwezo wa kuhoji, kufuatilia, na kuwawajibisha viongozi wao pale wasipotimiza ipasavyo wajibu wao. Halikadhalika huwarahisishia katika mambo yanayowahusu kuchangia na kutimiza wajibu wao kama raia wa nchi yao.
Ili Serikali na jamii iweze kutekeleza ipasavyo dhana za uwajibikaji na uwazi italazimu kubadili utamaduni wetu wa uendeshaji wa mambo. Hususan, tuwe na mitazamo na fikra chanya na kuondokana na imani potofu zilizojengeka miongoni mwetu yaani Serikali, vyama vya siasa, wananchi na asasi za kiraia kuhusu uwazi na uwajibikaji. Hali kadhalika, inatupasa tuondokane na mitazamo kinzani baina yetu. Badala yake tunatazamiwa kujenga madaraja ya mawasiliano, maelewano na kuaminiana. Tunawajibika   kuwa watu wamoja na wenye dhamira moja ya kuijengea nchi yetu na kuwahudumia wananchi wake. Katu hatutakiwi kuwa mahasimu. Ikiwa hivyo tutakuwa tumekosea sana.  Tutakuwa tumewaangusha kupita kiasi.
Dhana ya uwazi na uwajibikaji inawahusu wadau wote yaani Serikali na asasi za kiraia ambao ndio wadau wakuu wa OGP. Tutakuwa tunakosea sana kama tutadhani kuwa dhana hizi mbili zinaihusu Serikali pekee. La hasha! Uwazi na uwajibikaji unazihusu pia asasi za kiraia. Lazima nao wawe wawazi kuhusu shughuli wazifanyazo ili jamii na watu wajue wanachokifanya kwa niaba yao, kwa ajili yao na jinsi wanavyowajibika kwao. Na kuhusu mapato na matumizi, lazima asasi za kiraia nazo ziwe wazi kuieleza jamii wamepata pesa kiasi gani, kutoka kwa nani, kwa ajili gani na jinsi walivyozitumia fedha hizo?  Jamii na wananchi ambao ndiyo walengwa wa shughuli za asasi hizo wanastahili kujua kwani fedha hizo zimetolewa kwa manufaa yao na siyo ya viongozi na watendaji wa asasi za kiraia. 
Tabia ya asasi za kiraia kukataa kuwa wa wazi na kuwa wakali wanapotakiwa kufanya hivyo siyo sahihi.  Pia ni kinyume na misingi ya Open Government Partnership. Kutokufanya hivyo ndiko kunakozua mashaka wakati mwingine hata mizozo. Asasi za kiraia nazo lazima ziwe wazi na zitoe taarifa za shughuli ili wananchi ambao ndiyo walengwa waweze kujua kama kweli wamenufaika. Ili, pia, wananchi waweze kuhoji, kudai haki na kuwataka wahusika kuwajibika. Ni vyema ikaeleweka siku hizi sehemu kubwa ya fedha za misaada ya maendeleo hupitia asasi za kiraia hivyo kunapokosekana uwazi kupitia utoaji wa taarifa zilizo sahihi kuna hatari ya pesa za maendeleo ya wananchi kutokuwawafikia walengwa na kunufaisha watu wachache. Hivyo basi, serikali inapowakumbusha kuwa wawazi na kutoa taarifa watuelewe hivyo. Kuishutumu kuwa siyo rafiki na kuingilia asasi za kiraia si madai sahihi. Kila anayeshiriki katika Mpango wa Open Government Partnership hana budi kutambua kuwa anatakiwa kuwa muwazi na mkweli.  Ndiyo itikadi na falsafa kuu.
Tanzania na OGP
Ndugu Washiriki;
Mabibi na Mabwana;
 Tanzania ni mshirika wa Mpango wa OGP na ni ya pili kujiunga kutoka Afrika mara tu baada ya Mpango huu kuanzishwa mwaka 2011. Aidha, ni miongoni mwa nchi nane za Afrika (Afrika Kusini, Ghana, Liberia, Malawi, Sierra Leone, Tunisia na Tanzania) kati ya nchi 65 duniani zilizojiunga na Mpango huu ambao ni wa hiyari. Niliamua, kwa hiari yangu, Tanzania ijiunge katika Mpango huu kwa kutambua manufaa na umuhimu wa kuwepo uwazi katika uendeshaji wa shughuli za Serikali.  Husaidia uwajibikaji wa Serikali. Kwa kweli, Serikali kuwajibika kwa wananchi ndiyo makusudio na uhalali wa kuwepo kwake. Uamuzi huo ni kielelezo tosha cha utayari wangu na wa Serikali ya Tanzania kuunga mkono kwetu dhana na falsafa ya uwazi na uwajibikaji katika kuendesha Serikali. Kusisitiza ukweli huo, Tanzania pia ni mwanachama wa Mpango wa Afrika wa Kujitathmini Wenyewe (APRM) na Mpango wa Uwazi katika Uvunaji wa Rasilimali (EITI).
Ndugu Washiriki;
Mimi na wenzangu katika Serikali tumefanya mengi kuhusu uwazi na uwajibikaji. Tumepanua na kuongeza mawanda ya uwazi katika shughuli za serikali, demokrasia, uhuru wa wananchi kutoa maoni yao, uhuru wa habari, haki ya kupata taarifa na ushiriki wa wananchi. Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza Afrika na hata pengine duniani kwa kuwa na vyombo vya habari vingi.  Hivi sasa kuna magazeti na majarida 825, vituo vya TV 28, radio 95 ikilinganishwa na magazeti mawili, TV moja na radio moja mwaka 1992.
Kati ya vyombo vyote hivyo Serikali ina magazeti mawili, TV moja na radio moja. Hakuna uhakiki wa habari hivyo vyombo viko huru ingawaje maadili ya uandishi husisitizwa na hakuna ajizi yanapokiukwa.
Tumeongeza pia, uwazi katika uendeshaji wa shughuli za serikali. Habari hutolewa katika tovuti za Wizara na Idara husika za Serikali kwa wote kuona. Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iko wazi. Mikutano ya Bunge huonyeshwa kwenye Televisheni na kwa mara ya kwanza wananchi wameshirikishwa moja kwa moja katika mchakato wa kuandika upya Katiba ya nchi yetu.
Katika kutekeleza Mpango Kazi wa OGP, kama ilivyoelezwa na Mheshimiwa Waziri wa Utawala Bora, tumekwisha tekeleza Mpango Kazi wa Kwanza (2012/2013) na sasa tunatekeleza Mpango Kazi wa Pili (2014-2016).  Mipango kazi yote miwili imetayarishwa kwa kushirikisha asasi za kiraia na wadau wengine. Mafanikio yaliyopatikana katika kutekeleza Awamu ya Kwanza ya Mpango Kazi wa OGP ni pamoja na kutoa kijarida cha Bajeti ya Serikali (Citizen’s Budget) kwa lugha nyepesi ya Kiswahili na Kiingereza kwa ajili ya kutumiwa na wananchi wa kawaida ili waelewe vipaumbele vya bajeti ya Serikali; kuanzishwa kwa tovuti Kuu ya Serikali inayotoa taarifa muhimu zinazoweza kumsaidia mwananchi kupata huduma kwa urahisi; kuanzishwa kwa Tovuti ya Takwimu Huria (Open Data), inayoainisha takwimu mbalimbali. Tovuti ya “Nifanyeje” inayoweka taarifa muhimu kuhusu namna ya kupata huduma mbalimbali za umma imeanzishwa.
Ndugu Washiriki;
Mabibi na Mabwana;
Utekelezaji wa Mpango Kazi wa OGP Awamu ya Pili (2014/15 - 2015/16) umejikita katika maeneo matano ambayo ni Utungwaji wa Sheria ya Haki ya Kupata wa Habari (Access to Information), Uwazi katika upatikanaji wa takwimu za kibajeti, (Open Budget), Uwazi wa matumizi ya ardhi (Land Transparency), Uwazi katika masuala ya utafutaji na uchimbaji wa gesi, mafuta na madini (Extractive Industry Transparency) na kuanzisha tovuti ya open data kwa kuweka taarifa kuhusu afya, elimu na maji.
          Tunaendelea na utekelezaji wa Mpango Kazi huu na tayari tumeshapiga hatua mbalimbali. Muswada wa Sheria wa Uhuru wa Kupata Habari tayari umeshawasilishwa Bungeni na kusomwa kwa mara ya kwanza. Ni matumaini yetu kuwa katika vikao vinavyoendelea kati ya sasa na Julai utakamilika. Vile vile, tunaendelea na utekelezaji wa mambo mengine tuliyoahidi kuyapa kipaumbele. Tunauona mkutano huu kama fursa muhimu sana ya kubadilishana uzoefu utakaotusaidia kufanya mambo yetu kwa ufanisi zaidi.  Kwa ujumla wetu tutazungumza kwa uwazi shughuli zetu pamoja na mafanikio tunayopata na changamoto tunazokumbana nazo katika utekelezaji wa malengo tuliyojiwekea. Aidha, tutashauriana na kubadilishana uzoefu kuhusu kuzipatia ufumbuzi.
Ni matumaini yangu kuwa katika Mkutano huu mtatoka na Azimio la Dar es Salaam litakalosisitiza Uwazi, Uwajibikaji na Ushirikishwaji wa wananchi katika nchi zetu na Bara zima la Afrika. Ni lazima tufikishe ujumbe duniani kote kuwa ni muhimu kwa Serikali zetu kuwashirikisha wananchi na kukuza Uwazi.
Ahadi ya Serikali
Ndugu Washiriki;
Mabibi na Mabwana;
 Napenda kuwahakikishia washiriki wote kuwa Tanzania itaendelea kuwa muumini wa dhati na mwanachama asiyeyumba katika Mpango huu wa OGP. Tutaendelea kushiriki kwa kuwa tunauona Mpango huu, na haswa dhana ya uwazi na uwajibikaji kuwa na manufaa makubwa kwa nchi yetu na watu wake. Hatuna sababu wala dhamira ya kurudi nyuma wala hatujutii uamuzi wetu wa kujiunga na Mpango huu, ambao kwa kweli tumejiunga kwa hiyari yetu wenyewe. Tuko imara na tayari kuendelea na safari hii kuelekea kwenye viwango vya juu vya uwazi na uwajibikaji. Tunafahamu safari hii itakuwa na changamoto zake, ndogo na kubwa kwa nyakati fulani fulani wakati wote, hata hivyo, hatutakata tama. Maadam tuna hakika na matunda mazuri huko mbele tuendako tutasonga mbele bila ya ajizi.
Ndugu Washiriki;
Tunapoangalia nyuma tulikotoka na hapa tulipo sasa tunayo kila sababu ya kujivunia hatua kubwa tuliyofikia katika kuwa na taasisi na mifumo mizuri ya kiutawala na uendeshaji zinazoakisi dhana ya uwazi na uwajibikaji. Sina budi kuwashukuru sana wadau wa ndani yaani idara na taasisi za Serikali, Bunge, vyama vya siasa, asasi za kiraia na vyombo vya habari kwa mchango wao mkubwa katika kujenga misingi na mifumo ya uwazi na uwajibikaji. Hata hivyo hatuna budi kutambua kuwa safari yetu bado ni ndefu. Hivyo hatuna budi kuongeza bidii maradufu ya sasa.
Wito wangu kwa wadau wote na washiriki wa Mpango huu, haswa taasisi za Serikali na washirika wenzetu wa asasi za kiraia ni kuwa tuendelee kushirikiana kwa karibu. Tufanye kila tuwezalo na kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina yetu. Tujenge tabia ya kukutana mara kwa mara kuzungumzia shughuli zetu na namna ya kushirikiana.  Tukifanya hivyo tutapunguza au hata kuepusha kabisa kutokuaminiana, mizozo, migongano isiyokuwa ya lazima.  Kitu kilicho muhimu kwetu ni kuwa na dhamira ya dhati ya kutaka pawepo na maelewano na mashirikiano baina yetu.  Kama hilo lipo mambo  yatakuwa mazuri. 
Nayasema haya kutokana na uzoefu tulioupata katika uhusiano wetu na asasi moja kubwa ya kiraia na kupata mafaniko makubwa.  Nayo si nyingine bali Shirikisho la Wafanyakazi ambapo mikutano yetu ya mara moja au mbili kwa mwaka imesaidia sana kupata ufumbuzi wa masuala mbalimbali ya wafanyakazi.  Imepunguza mizozo na misuguano, Naamini tukiwa na utaratibu kama huo na shirikisho la asasi za kiraia mambo yatakuwa mazuri.  
Hata haya ya sheria ya Mitandao na Takwimu tukikaa pamoja yataisha tu. Kusema sheria mbaya haisaidii, na wengine kutishia kufuta misaada haisaidii pia. Waziri mwenye dhamana ameshasema mwenye mawazo atoe, basi pelekeni maoni. Sisi Serikali ni wasikivu sana.  Tumeshafanya mabadiliko ya sheria nyingi tu. Ni vyema mtambue kuwa Serikali nayo inahitaji heshima yake.  Ukitaka kuonyesha ubabe nayo itaonyesha ubabe pia. Vitisho havijengi, lakini fursa ya kuzungumza inatoa majawabu.
 Nitaangalia uwezekano wa kukutana na asasi za kiraia kabla ya kumaliza kipindi changu cha uongozi ili tujenge utaratibu maalum wa mazungumzo baina ya Serikali na asasi za kiraia.


Hitimisho
Ndugu Washiriki;
Mabibi na Mabwana;
Napenda kumaliza kama nilivyoanza kwa kuwashukuru kwa uamuzi wenu wa kuchagua Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano huu muhimu. Mmetupa heshima kubwa ambayo daima tutaikumbuka na kuienzi. Naamini nazungumza kwa niaba ya viongozi wenzangu wote Afrika pia, kwamba tuna matumaini makubwa na Mkutano huu kwamba utazaa matunda mema yenye manufaa kwa bara la Afrika kwa ujumla. Sisi tuko tayari kutimiza wajibu wetu, na tunatarajia kila mdau atatimiza wajibu wake. Tukumbuke kuwa, Uwazi na Uwajibikaji ni utamaduni, pia ni kama msumeno, unakata pande zote. “Inawezekana, timiza wajibu wako”.
Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania

Ahsanteni Sana Kwa Kunisikiliza!

No comments: