Wednesday, May 20, 2015

Balozi Seif Ali Idd akagua ujenzi wa Jengo jipya la Abiria wa usafiri wa Anga katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wa Tatu kutoka kushoto akikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Abiria { Terminal 11 } katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar wa Abeid Amani Karume akiwa pamoja na uongozi wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar. Kushoto ya Balozi Seif ni Katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Dr. Juma Malik Akio na Msimamizi wa ujenzi wa jengo la Abiria katika uwanja wa ndege wa Zanzibar upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Nd. Yassir De Costa.
Msimamizi wa ujenzi wa jengo la Abiria katika uwanja wa ndege wa Zanzibar upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Nd. Yassir De Costa akimpatiamaelezo Balozi Seif hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa mradi huo.
Mshauri wa mradi wa ujenzi wa jengo la abiria { Terminal 11 } kutoka Kampuni ya ADPI ya Nchini Ufaransa Mhandisi Guillaume Verna akifafanua hatua zilizochukuliwa katika utaalamu utaotumika katika ujenzi wa mikonga kwenye jengo hilo jipya la abiria.
Eneo litakalotumika kwa huduma mbali mbali ikiwemo maduka na katika jengo jipya la abiria linaloendelea kujengwa katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar.
Eneo la Nje ya jengo la Abiria litakalotumiwa na abiria wanaosafiri na kuingia Nchini kwa kutumia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume uliopo Kiembe Samaki Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar. Picha na – OMPR – ZNZ.

Harakati za ujenzi wa Jengo jipya la Abiria wa usafiri wa Anga katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa   Abeid Amani Karume  ulipo Kiembe Samaki Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar  zimekuwa zikiendelea kama kawaida kufuatia marekebisho ya ujenzi wa jengo hilo  utaozingatia kiwango cha Kimataifa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipata fursa ya kukagua harakati za ujenzi huo unaofanywa na wahandisi wa  Kampuni ya Kimataifa ya Beijing Construction Engineering  Group { GCEG } ya Nchini Jamuhuri ya Watu wa China Chini ya Usimamizi uelekezi wa Kampuni ya ADPI ya Nchini Ufaransa.

Msimamizi wa ujenzi wa Mradi huo kwa  upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Nd. Yassir De Costa alimueleza Balozi Seif kwamba ujenzi huo hivi sasa uko katika hatua za uwezekaji paa na baadaye kuwekwa vioo.

Nd. Costa alisema Jengo hilo kubwa litakuwa  na lango kuu kwa ajili ya abiria wote wa ndege za kimataifa na Kitaifa ambapo baadaye watajigawa kwa mujibu wa safari za abiria hao katika huduma za ndani.

Alieleza kwamba mizigo ya abiria itafanyiwa ukaguzi mbara mbili kabla ya kuingizwa ndani ya ndege utaratibu ambao utathibitisha usalama wa abiria, mizigo na eneo lote la uwanja wa ndege.

Msimamizi huyo wa mradi wa ujenzi wa Jengo la abiria wa Serikali alifahamisha kwamba abiria wapatao 500 watakuwa wakihudumiwa ndani ya saa moja katika eneo la jengo hilo la abiria.

Naye mshauri wa mradi wa ujenzi wa jengo la abiria { Terminal 11 } kutoka Kampuni ya ADPI ya Nchini Ufaransa  Mhandisi Guillaume Verna alisema kwamba ujenzi wa Mikonga itakayohudumia ndege kubwa katika jengo hilo imezingatiwa katika kiwango kikubwa.

Mhandisi Guillaume alisema utafiti wa kina umefanywa katika kuona mikonga itakayopjengwa haiathiri jengo hilo kwa mujibu wa vipimo vinavyokubalika Kimataifa.

Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Maiundombinu na Mawasiliano Zanzibar Dr. Juma Malik Akio alisema Serikali ya Jamuhuri ya China ambayo ndio mfadhili wa Ujenzi huo Kupitia Benki ya Exim imeridhia kuendelea kutekelezwa kwa mradi huo.

Dr. Malik alisema Wizara ya Miundombinu na Mawasliano kwa kushirikiana na wadau wa Mradi huo wanaandaa utaratibu wa kumaliza ujenzi huo kwa mujibu wa ushauri wa Kitaalamu.

Alisema  mategemeo ya mradi wa ujenzi huo yalipangwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu lakini kutokana na kusita kwa muda ujenzi huo unatazamiwa kukamilika si zaidi ya mwishoni mwa mwaka huu.

Alieleza kwamba  mategemeo ya mradi wa ujenzi wa jengo hilo yalipangwa kukamikia mwezi oktoba mwaka huu lakini kutokana na kusita kwa muda ujenzi huo unatazamiwa kukamilika si zaidi ya mwishoni mwa mwaka huu.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alielezea faraja yake kutokana na kuendelea kwa  ujenzi wa jengo hilo  ambao uko katika hatua inayoridhisha.

Balozi Seif aliwapongeza wahandisi wa ujenzi huo pamoja na usimamizi mahiri wa mshauri muelekezi wa mradi huo hatua ambayo kumalizika kwake kutatoa faraja kwa abiria wanaotumia uwanja wa ndege wa Zanzibar.
Balozi Seif alifahamisha kwamba matarajio ya abiria wanaotumia uwanja huo wataondokana na  usumbufu wa kushuka au kufuata ndege masafa marefu kwa miguu hasa wakati wa mvua.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
20/5/2015.

No comments: