Na Mwandishi Wetu
Rais Jakaya Kikwete amepokea kwa majonzi makubwa kufuatia kifo cha mmoja wa
watumishi wa miaka mingi wa Serikali, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania (TPDF), Chama cha TANU na Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Africa –
Liberation Committee of the African National Unity (OAU), Brigedia Jenerali Hashim
Mbita.
Rais Kikwete amemwelezea marehemu Mbita kama mmoja wa viongozi ambao
wameifanyia Tanzania mambo mengi na kwa
miaka mingi.
Kutokana na taarifa za msiba
huo, Rais Kikwete ameelekeza Serikali na Jeshi kushirikiana na familia kusimamia
msiba huo na kuandaa mazishi yake.
Rais Kikwete alipokea taarifa hiyo ya msiba alipoingia tu Uwanja wa
Uhuru, Dar es Salaam, kuongoza maelfu ya wananchi kuadhimisha miaka
51 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, aliuelezea msiba huo kama msiba wa
simanzi kubwa.
“Ni wachache katika nchi yetu wanaoweza kulinganishwa na Mzee Hashim
Mbita kwa kiwango cha utumishi uliotukuka, wa miaka mingi na usiokuwa na
kasoro. Katika utumishi wa Serikali alipata kuwa Mwandishi wa Habari Mkuu wa
Idara ya Habari na pia kuwa Mwandishi wa Habari wa Rais kabla na baadaye kuwa
Balozi wa Tanzania katika Zimbabwe. Kazi zote alizifanya kwa ufanisi mkubwa
sana,”alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Katika Chama cha TANU alikuwa Katibu Mtendaji wa Chama na katika
Jeshi letu makini, Mzee Mbita alipata na kufikia cheo cha Brigedia Jenerali,
yote mambo makubwa kweli kweli.
“Lakini ilikuwa katika nafasi ya Katibu Mtendaji wa Kamati ya
Ukombozi ya Umoja wa Afrika ambako Mzee Mbita alikamilisha utumishi wake kwa
kusimamia shughuli nzito ya kuwasaidia ndugu zetu Kusini mwa Afrika kwa miaka
20 mfululizo, miongo miwili, na kuweza kupata uhuru wao.
Hakuna mpigania uhuru katika Msumbiji, Zimbabwe, Namibia, Angola na hatimaye katika Afrika Kusini ukiondoa nchi nyingine kama Cape Verde, asiyejua mchango wa Mzee Mbita.
Hakuna mpigania uhuru katika Msumbiji, Zimbabwe, Namibia, Angola na hatimaye katika Afrika Kusini ukiondoa nchi nyingine kama Cape Verde, asiyejua mchango wa Mzee Mbita.
Wote hawa amewatumia vizuri, kwa ufanisi, kama mlezi, kama kiongozi,
kama kamanda hadi wakafanikisha kazi ya ukombozi. Huu ni mchango mkubwa kweli
kweli.
“Kitendo chake cha mwisho cha
utumishi, kilikuwa kuongoza shughuli za Mradi wa Hashim Mbita wa Kuweka
Kumbukumbu za Harakati za Ukombozi Kusini mwa Afrika na Kuenzi Viongozi Wakuu
(Hashim Mbita Project to Honour Outstanding Leaders), kazi ambayo nayo
aliifanya kwa uwezo na ufanisi mkubwa na ripoti yake tukaizindua mwaka jana
pale Victoria Falls, Zimbabwe wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Nchi Wanachama wa
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC),”alisema Rais Kikwete.
Alisema Zimbabwe ilitangaza kumpa Mzee Mbita Nishani ya The Royal
Order Munhumutapa yenye kutambua mchango wake katika harakati za ukombozi wa
Zimbabwe.
Mzee Mbita amekuwa raia wa sita wa kigeni, na wa kwanza asiyekuwa
rais, kupata heshima hiyo ya juu kabisa ambayo hutolewa na Taifa la Zimbabwe
kwa wageni ambao wamechangia Uhuru wa Zimbabwe.
Viongozi watano wa mwanzo kupata Nishani hiyo, mwaka 2005, walikuwa
ni Marais na Viongozi Waanzilishi wa Kundi la Nchi za Frontline States dhidi ya
Ukoloni na Ubaguzi wa Rangi, Marehemu Julius Kambarage Nyerere, Mzee Kenneth
David Kaunda wa Zambia, Marehemu Sir Seretse Khama wa Botswana, Marehemu Samora
Moises Machel wa Musumbiji na Marehemu Augustinho Neto wa Angola.
Brigedia Jenerali mstaafu, Hashim Mbita amefariki dunia katika
Hospitali ya Kuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Lugalo, Dare
es Salaam.
Mbita ambaye alikuwa Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi ya
uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), alifariki dunia leo majira ya saa 3 asubuhi.
Akizungumza nyumbani kwa marehemu Chang’ombe,
Temeke, mtoto wa marehemu, Iddi Mbita amesema baba yake alifariki kutoka na
kusumbuliwa na shinikizo la damu.
“Mzee alikuwa anasumbuliwa na shinikizo la damu na leo (jana) ameamka
salama, akanywa chai na dawa, kisha akaomba kupumzika. Baada ya muda mfupi akafariki
dunia asubuhi muda saa 3,” alisema Iddi.
Alisema marehemu Mbita alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la hilo tangu
Agosti mwaka jana, hivyo kulazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Alisema akiwa katika hospitali hiyo, aliwekwa chini ya Uangalizi Maalum
wa Daktari (ICU).
Alisema alikaa katika hospitali hiyo kwa zaidi ya mwezi mmoja na
nusu na ilipofika Oktoba mwaka jana alipelekwa nchini India kwa matibabu zaidi.
Iddi alisema alikaa nchini India kwa miezi miwili na Januari mwaka
huu alirudishwa nchini na kuendelea na matibabu nyumbani kwake Chang’ombe
jirani na Klabu ya TCC Chang’ombe.
Alisema kwamba Machi 23 mwaka huu Jeshi la Ulinzi la Wananchi
Tanzania JWTZ walimfuata na kumchukua kwa ajili ya kumpatia matibabu zaidi.
Alisema baada ya vipimo mdaktari katika Hospitali ya Lugalo walibaini
kuwa kuna matatizo mbalimbali yaliyokuwa yakimsibu hivyo aliendelea kupata
matibabu hadi alipoaga dunia.
“Unajua ugonjwa ulikuwa umemla sana hivyo kusababisha organ (mfumo
wa viungo vya mwili) mbalimbali kupata
hitilafu,” alisema Iddi.
Alisema marehemu ataswaliwa nyumbani kwake Chang’ombe na mwili
utapelekwa katika msikiti wa kwa Mtoro, Kariakoo na baadaye mazishi yatafanyika
siku ya Jumatano katika makaburi ya Kisutu saa 10 jioni.
Mjane
wa marehemu Brigedia Jenerali mstaafu
Hashim Mbita, Ngeme Mbita (katikati) akiwa na waombolezaji wengine
nyumbani kwa
marehemu, Chang’ombe jijini Dar es Salaam leo. Brigedia Mbita amefariki
leo katika Hospitali ya Lugalo. (Picha na Francis Dande)
Mjane wa marehemu Brigedia Jenerali mstaafu
Hashim Mbita, Ngeme Mbita (katikati) akiwa na waombolezaji wengine nyumbani kwa
marehemu, Chang’ombe jijini Dar es Salaam leo. Brigedia Mbita amefariki leo katika Hospitali ya Lugalo.
Waziri
Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba akiwa nyumbani kwa marehemu, Brigedia
Jenerali Hashim Mbita Chang'ombe jijini Dar es Salaam. Kushoto ni
Mjumbe wa Heshima wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), Said El Maamry na Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku.
Waombolezaji
Ndugu na jamaa wakiwa katika msiba wa Brigedia Hashim Mbita.
Waombolezaji wakiwa na huzuni nyumbani kwa marehemu.
Wanafamilia wakiwa katika hali ya huzuni leo.
Baadhi ya ndugu na jamaa wakiwa wamekusanyika nyumbani kwa marehemu.
Mtoto
wa marehemu, Idd Mbita akitoa taarifa za shughuli za mazishi ambapo
marehemu atazikwa katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam siku ya
Jumatano saa 10 jioni.
No comments:
Post a Comment