TAASISI ya kifedha ya Bayport Financial Services inayojihusisha na mambo ya mikopo kwa watumishi wa wa umma na kampuni zilizoidhinishwa, mwishoni mwa wiki ilizindua tawi lake jipya la 80 wilayani Ileje, mkoani Mbeya, huku Mkuu wa wilaya hiyo, Rosemary Staki Senyamule, akiwataka wananchi wake kukopa kwa sababu maalum.
Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Mheshimiwa Rosemary Senyamule kulia, akionyeshwa nyaraka za ofisi ya Taasisi ya Kifedha ya Bayport Financial Services, inayojihusisha na mambo ya mikopo katika uzinduzi wa taasisi hiyo katika wilaya hiyo ya Ileje, mkoani Mbeya. Kushoto ni Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Alpha Akim. Uzinduzi huo ulifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita na kuhudhuriwa na watu mbalimbali wilayani humo.
Kufunguliwa kwa tawi hilo si kutainua uchumi wa wananchi wa Ileje watakaotumia fursa ya uwapo wa ofisi hiyo, bali pia kutarahisisha utoaji wa huduma wa taasisi hiyo ya Bayport nchini Tanzania.
Wageni mbalimbali wakiangalia shughuli za uzinduzi wa tawi jipya la taasisi ya kifedha ya Bayport Financial Services, wilayani Ileje, mkoani Mbeya, mwishoni mwa wiki iliyopita, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa wilaya hiyo, Rosemary Senyamule.
Akizungumza katika uzinduzi wa tawi hilo jipya, Mkuu huyo wa wilaya Ileje, Rosemary alisema kuwa wananchi wakiitumia fursa ya tawi hilo kutainua pia kiwango cha uchumi cha watu wake.
Baadhi ya wageni waalikwa wakisoma vipeperushi vya taasisi ya kifedha ya Bayport Financial Services, wilayani Ileje, mkoani Mbeya.
Alisema suala la mikopo ni jambo jema kutokana na uwezo mzuri unaoweza kuwaendeleza wananchi, wakiwamo watumishi wa umma na wafanyakazi wa kampuni zote zilizoidhinishwa, ambao kimsingi ni watu wanaotakiwa kuendelezwa kwa mambo mengi.
Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wa Bayport Financial Services, Alpha Akim, akizungumza jambo katika uzinduzi wa tawi lao la 80 wilayani Ileje, mkoani Mbeya, mwishoni mwa wiki iliyopita na kuhudhuriwa na watu mbalimbali.
“Kwanza nawapongeza mno wenzetu wa Bayport Financial Services kwa kuamua kuja kufungua tawi hapa katika wilaya yetu ya Ileje, ila ni muhimu wananchi kukopa kwa sababu maalum ili waweze kuendeleza maisha yao kwa kutumia vyema fursa za mikopo Tanzania.
“Tukifanya hivyo tunaweza kupata maisha bora kwa sababu tutajimudu kiuchumi, hivyo ni wakati wetu kufurahia kuanzishwa kwa huduma za taasisi hii hapa kwetu ileje, maana ndio kwanza wanafungua tawi lao hapa,” alisema.
Naye Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Alpha Akim, alisema kufungua kwa tawi hilo pia ni sehemu ya kutoa ajira kwa vijana sanjari na kuongeza kipato kwa watumishi wa umma na wafanyakazi wa kampuni zilizoidhinishwa kwa kupitia fursa nzuri ya mikopo.
“Watu mbalimbali watapata mwangaza mzuri wa kiuchumi wakiwamo wale watakaopata nafasi ya kufanya kazi nasi, hususan ile ya uwakala, bila kusahau wale watakaokopeshwa bila amana wala dhamana.
“Naomba wananchi na wakazi wa Ileje watumie vyema fursa ya uwapo wa taasisi hii wilayani kwao kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wote kwa pamoja tunafanikisha kwa vitendo ndoto ya kukuza uchumi wetu na wa Tanzania kwa ujumla,” alisema Akim, Meneja wa Nyanda za Juu Kusini wa Bayport.
Bayport Financial Services ni taasisi ya kifedha inayojihusisha na utoaji mikopo mbalimbali kama vile fedha taslimu, mikopo ya bidhaa, bima ya elimu kwa uwapendao, ambapo mikopo hiyo inaweza kutolewa ofisini au kwa njia rahisi ya mtandao wa www.kopabayport.co.tz.
No comments:
Post a Comment