Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia Madini, Charles
Kitwanga, akisisitiza jambo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kuimarisha
ushirikishwaji wa watanzania katika sekta ya madini unaofanyika jijini
Mwanza
Baadhi wa washiriki wa mkutano wa kuimarisha ushirikishwaji wa
watanzania katika sekta ya madini wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri wa
Nishati na Madini, Charles Kitwanga anayeshughulikia Nishati (hayupo
pichani).
Kamishna Msaidizi wa Madini anayeshughulikia Migodi Mhandisi
Ally Samaje akiwasilisha taarifa wakati wa mkutano wa kuimarisha
ushirikishwaji wa watanzania katika sekta ya madini unaofanyika jijini
Mwanza.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia Madini, Charles
Kitwanga (waliokaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki
wa mkutano wa kuimarisha ushirikishwaji wa watanzania katika sekta ya
madini.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia Madini Charles
Kitwanga amewataka watanzania kujifunza na kutafuta fursa zilizopo
katika sekta ya madini yakiwemo matumizi ya teknolojia ili kuweza kushiriki
kikamilifu katika sekta hiyo nchini.
Naibu Waziri Kitwanga ameyasema hayo wakati akifungua mkutano
wa kuimarisha ushirikishwaji wa watanzania katika sekta ya madini
unaofanyika jijini Mwanza na kuwataka wamiliki migodi kuwafundisha
watoa huduma katika sekta hiyo namna bora ya ushiriki wao na hivyo
kuchangia pato na ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
“Wamiliki wa migodi wanatakiwa si kutoa fedha tu bali pia kuwafundisha
watoa huduma katika migodi yao kuzitumia fursa zilizopo katika sekta hiyo,
jambo hili litawezesha ushiriki wa watazania, litadumisha amani na hivyo
lengo la serikali litafikiwa.
“ Hivi sasa sekta ya madini ndiyo inaongoza kwa kutoa fedha nyingi
za kigeni madini yanapouzwa, hivyo uwepo wa watoa huduma
wengi na wananunuzi watachangia zaidi kuimarisha uchumi kupitia
madini”amesisitiza Kitwanga.
Kitwanga ameongeza kuwa, Serikali inalenga kuhakikisha kwamba,
watanzania na serikali wanafaidika na shughuli za uchimbaji madini na
kuongeza kuwa, lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa, ifikapo mwaka 2025
sekta ya madini inachangia asilimia 10 ya pato la taifa kiuchumi.
Aidha, amewataka wamiliki wa migodi kuhakikisha wanatoa taarifa
kuhusu fursa zilizopo kwa watoa huduma kwa kuzingatia usawa
ili kuwawezesha watanzania kushiriki katika uchumi huo. “ Lazima
watanzania washirikishwe , lazima shughuli za madini ziongeze mzunguko
wa fedha na faida za uchumi huu tunataka zibaki ndani,” amesisitiza
Kitwanga.
Vilevile, Kitwanga amesisitiza suala la kutii na kufuata sheria, kanuni
na taratibu kwa wadau wote katika sekta hiyo wakiwemo wananchi na
wachimbaji ili kuepusha migorogoro.
Naye Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Paul Masanja amewaeleza
washiriki wa mkutano huo kwamba serikali inataka kuona faida za shughuli
za uchimbaji nchini zikiwanufaisha watanzania moja moja.
Washiriki wa Mkutano huo ni pamoja na Wataalamu kutoka Wizara ya
Nishati na Madini, Taasisi zinazoshughulika na Masuala ya Madini nchini
likiwemo Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Wakala wa Ukaguzi wa
Madini Tanzania (TMAA), Mkuu wa Mkoa wa Geita Fatma Mwasha Mkuu
wa Wilaya ya Geita Manzie Mangachie, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu
Wilson Nkhambaku na Wawakilishi wa Kampuni za Madini.
No comments:
Post a Comment