Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) Prof. Emanuel Mjema akizungumza wakati wa mkutano wa wadau na wataalam wa elimu kutoka Taasisi za Elimu, vyuo, walimu wa masomo ya Biashara wa shule za Sekondari waliokutana kupitia Mtaala wa kufundishia mafunzo ya taaluma ya Ualimu katika Biashara leo jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi wa Mafunzo ya awali wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Dkt. Esther Mbise akitoa ufafanuzi kwa wadau wa Elimu kuhusu uandaaji wa mtaala wa kufundishia walimu wa masomo ya Biashara leo jijini Dar es salaam.
Menejimenti na watendaji wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufunguliwa kwa mkutano wa wadau na wataalam wa elimu kutoka Taasisi za Elimu, vyuo, walimu wa masomo ya Biashara wa shule za Sekondari na vyuo na wadau mbalimbali wa Elimu leo jijini Dar es salaam.
Na. Aron Msigwa.
Chuo cha Elimu ya Biashara Kampasi ya Dar Es salaam (CBE) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu nchini kiko katika hatua za mwisho za kukamilisha Mtaala wa kufundishia Walimu wa masomo ya biashara kwa ngazi ya shahada utakaoanza kutumika katika mwaka masomo utakaoanzia mwezi Septemba 2015.
Akizungumza wakati wa mkutano wa wadau na wataalam wa elimu kutoka Taasisi za Elimu, vyuo, walimu wa masomo ya Biashara wa shule za Sekondari na vyuo na wadau mbalimbali wa Elimu leo jijini Dar es salaam, Mkuu wa chuo hicho Prof. Emanuel Mjema amesema chuo chake kimeamua kuanzisha programu hiyo ili kuziba pengo la uhaba wa walimu wa kufundisha masomo ya Biashara wenye taaluma ya ualimu.
Amesema chuo hicho kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kimefikia uamuzi huo kufuatia utafiti uliofanywa na jopo la wataalamu wa maandalizi ya Mtaala huo kuanzia mwaka 2012 uliobaini uwepo wa kiwango kikubwa cha uhitaji wa waataalam wa kufundisha masomo ya biashara wenye taaluma ya ualimu.
Prof. Mjema amesema katika utafiti huo ilibainika kuwa asilimia 27 ya walimu wanaofundisha masomo ya Biashara katika maeneo mbalimbali nchini wana taaluma ya ualimu huku asilimia 73 wanafundisha kwa kutumia uzoefu jambo linalochangia kupungua kwa ubora wa ufundishaji darasani.
“Sisi kama chuo cha Elimu ya Biashara tumeona uhitaji uliopo nchini wa kukosa wataalam wa kufundisha masomo ya Biashara wenye taaaluma ya ualimu ndio maana tumeamua kuanzisha mtaala huu wa kufundishia wanafunzi wa Shahada ya Elimu katika Biashara ili tupate wahitimu bora watakaofundisha wanafunzi wetu na kukidhi mahitaji ya soko” Amesisitiza.
Amesema mafunzo yatakayotolewa yatachukua muda wa miaka 3 na kubainisha kuwa katika mahafali ya kwanza ya shahada hiyo wanafunzi wapatao 300 wanatarajia kuhitimu mafunzo hayo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mafunzo ya awali wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Dkt. Esther Mbise akitoa ufafanuzi kuhusu uandaaji wa mtaala huo amesema timu ya wataalam wa maandalizi ya mtaala huo ilikutana na wadau mbalimbali kutoka Wizara ya Elimu,Taasisi za elimu, wanafunzi, wazazi na Taasisi za Mitaala ya Elimu ili kupata maoni yao na kupata maoni yaliyoanisha maeneo ya kufanyia marekebisho ili kuwa na mtaala bora wenye kukidhi mahitaji ya elimu ya biashara nchini.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya mtaala huo ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Masoko wa CBE akiwasilisha mtaala huo ili upitiwe na wadau wadau waliohudhuria mkutano huo amesema sababu za kuwepo kwa mabadiliko ya kuwepo kwa mtaala huo ni kuwepo kwa mahitaji ya wataalam wa kufundisha masomo ya Biashara wenye taaluma ya Ualimu.
Amesema mtaala huo utakaoanza kutumiwa mwezi Septemba, 2015 utatoa fursa ya wanafunzi wengi zaidi waliohitimu kidato cha sita na vyuo kujiunga katika masomo hayo ya miaka 3 ya Shahada ya Elimu katika biashara.
No comments:
Post a Comment