Friday, March 27, 2015

ASILIMIA 40 YA WANAWAKE Z’BAR WANAISHI MAISHA DUNI

DSC_0081
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi (aliyefunikwa mwamvuli) akiwasili kwenye sherehe ya siku ya wanawake duniani iliyoandaliwa na Zanzibalicious Women Group na kufanyika ndani ya ukumbi wa Salama, Bwawani Hotel mwishoni mwa wiki.

Na Mwandishi wetu, Zanzibar
UTAFITI uliofanywa na taasisi ya wanawake nchini Zanzibar ya Zanzibalicious Women umeonyesha kuwa asilimia 40 ya wanawake Zanzibar, wanaishi katika mazingira duni ya umasikini kwa kutojitambua na kukosa elimu ya uelewa jinsi ya kukabiliana na mazingira waliyomo.

Akisoma risala siku ya wanawake mbele ya mgeni rasmi mke wa rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi , Mama Mwanamwema Shein , katika siku ya wanawake hafla iliyofanyika hoteli ya Bwawani, Mweka hazina wa Zanzibalicious Women Group, Shekha Hilal alisema hali hiyo ni changamoto kubwa na sasa kunatafutwa namna ya kumfikia mwanamke huyu ambaye ameshagota katika jamii yetu.

“Mama Shein asilimia hii ni kubwa saana, na sisi kama wanawake ambao tayari tumejaaliwa elimu na tunajitambua, ikiwa ni pamoja na tayari tumepiga hatua kimaendeleo katika nyanja mbalimbali, tumeguswa sana sana na suala hili.” Alisema Shekha.

Zanzibalicious ni umoja wa wanawake wanaoishi Zanzibar,ulioanzishwa mwaka 2011,na kusajiliwa rasmi mwaka 2013, ikiambatana na uzinduzi uliofanyika tarehe 28 Machi 2014.
DSC_0227
Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Mwanamwema Shein akiwasili kwenye sherehe ya siku ya Wanawake duniani iliyoandaliwa na Zanzibalicous Women Group mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa Salama, Bwawani Hotel.

Mweka hazina huyo alisema kwamba wanajiuliza maswali mengi kama mwanamke huyo elimu ya kujikwamua imemfikia au kama kuna jitihada zozote za kumfikishia elimu hiyo.
“Je hili ni jukumu la serikali peke yake? Au sisi tunatakiwa tujumuike na serikali? mheshimiwa mgeni rasmi tumeona ya kwamba tuungane pamoja na serikali katika kutekeleza suala hili.” Alisema Shekha akielezea nia ya taasisi hiyo ya kuondoa umaskini miongoni mwa wanawake nchini Zanzibar.

Alisema taasisi yao inajipanga kutoa elimu za aina mbili ili awali kumuwezesha kujikimu kupitia ujasiriamali, kwa kumpatia elimu kwa vitendo,kwa mfano:-ushonaji,ufugaji na utengenezaji wa bidhaa mbali mbali na pili kumtoa katika hali ya upweke ili elimu atakayopata imfikishe kwenye mifuko mbali mbali pamoja na mfuko wa Rais Dk. Ali Mohammed Shein .
Alisema katika program hiyo wanatarajia baada ya miaka 2 wanawake 100 watakuwa wanajitegemea wenyewe na kuwa mabalozi katika kuelimisha wanawake wengine zaidi.
DSC_0471
Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Mwanamwema Shein akisoma hotuba wakati wa sherehe ya siku ya wanawake duniani iliyoandaliwa na Zanzibalicous Women Group na kufanyika ndani ukumbi wa Salama, Bwawani hoteli mwishoni mwa wiki. Kushoto ni Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akifuatiwa na Mwenyekiti mstaafu wa Zanzibalicious Women Group, Bi. Ummukulthum Ansel.

“Na kama kila mwanamke akiweza kuelimisha wanawake katika kaya yake ,baada ya miaka kadhaa, Zanzibar itakuwa na wanawake walioweza kujikomboa katika dimbwi hili la kuishi maisha duni.” Alisema.

Akizungumzia mafanikio ya asasi hiyo alisema kwamba imefanikiwa kutoa elimu na kuwawezesha kina mama kuunda vikundi vidogo vidogo vya maendeleo kwa kuanzisha miradi mbalimbali, kwa mfano kina mama wa Chaani na Matemwe.

Aidha imetoa misaada ya hali na mali kwa waathirika wa madawa ya kulevya ikiwa ni moja ya kumkwamua mwanamke na kutoa misaada mbali mbali kwa wanawake wasiojiweza ikiwemo hospital kuu ya Mnazi mmoja na kina mama wajane.

Alisema pamoja na mafanikio hayo bado wanawake wanakabiliwa na changamoto za ndoa za utotoni, uzazi salama, ukatili wa kijinsia,mfumo dume, ubaguzi na mimba za utotoni.
Mhe.Mgeni rasmi, Umoja huu umekuwa ukiendesha shughuli zote tokea mwaka 2011 kwa kutegemea michango yetu sisi binafsi.
DSC_0314
Baadhi ya wakinama waliohudhuria sherehe hiyo wakionekana kufurahishwa na hotuba ya Mke wa Rais wa Zanzibar (hayupo pichani).

Changamoto hii imesababisha kutokutimiza kwa malengo yetu kwa muda tulioupanga kutokana na kukosa fedha za kutosheleza utekelezaji wa malengo hayo.

Akijibu risala hiyo Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Mwanamwema Shein, ameikumbusha jamii kuunganisha nguvu zao kuwakomboa wanawake kujiendeleza kimaisha na kujiongezea kipato.

Alisema hatua hiyo itaongeza kasi ya kuimarisha ustawi wa familia na jamii hususan wanawake wanaoishi vijijini ambao wanakabiliwa na changamoto zaidi.

Alisema sherehe ya siku ya wanawake duniani inakuwa na maana zaidi kama juhudi zitafanyika kuangalia changamoto na kujipanga kuzifanyia kazi.

“Rai yangu ni kuwa tuwazingatie zaidi akina mama wanaoishi vijijini na wenye mahitaji maalum kutokana na kukosa fursa kama hizo za kuwaendeleza kimaisha”, alisisitiza.
DSC_0344
Mweka hazina wa Zanzibalicious Women Group, Bi. Shekha Hilal akisoma risala kwa mgeni rasmi Mke wa Rais wa Zanzibar (hayupo pichani) Kulia ni Mwenyekiti wa Zanzibalicous Women Group, Bi. Evelyne Wilson.

Aidha, aliongeza kuwa wanawake ni jeshi kubwa ambalo likiandaliwa vyema linaweza kushinda katika mapambano yanayokusudiwa huku akisisitza mshikamano ili kufikia malengo yanayowekwa.

Akizungumzia ujumbe wa sherehe hizo ambao ni kuhamasisha hatua mathubuti kumwendeleza na kumtambua mwanamke, alitoa rai kwa wanawake kushirikiana na serikali katika kampeni za kupambana na madhila wanayokabiliana nayo ikiwa ni pamoja na ukatili wa watoto na wanawake.

Kuhusu uzoefu wake katika maisha na malezi ya watoto, alisema amebahatika kupata watoto 11 ambao amewalea katika mazingira mbalimbali ikiwa ni kwenda na kurudi kazini na kuwa pekee huku mumewe akiwa safarini kikazi.

Aidha, aliwataka wanawake kuwa wastahamilivu katika malezi ya watoto hasa watoto Njiti ambao huzaliwa kabla ya kufikisha muda.
Hata hivyo aliwaonya wanawake wanaojali kujiremba na kuwa sahau watoto na kukumbusha kwa ‘watoto ni wageni’ kwamba wanahitaji matunzo na ukarimu mkubwa kutoka kwa wazazi wao.
IMG_6571
Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein, akizindua Mfuko wa Zanzibalicious Women Group kwa kuchangia shilingi milioni tano, wakati wa maadhimisho ya sherehe ya wanawake duniani visiwani Zanzibar yaliyoandaliwa na Zanzibalicious Women Group na kufanyika katika ukumbi wa Salama uliopo Bwawani Hotel Zanzibar. Kulia ni Mwenyekiti wa Zanzibalicious Women Group, Bi Evelyne Wilson Baruti.
DSC_0082
Mweka hazina wa Zanzibalicious Women Group, Shekha Hilal akinakili majina ya watu waliokuwa wakichangia kwenye harambe ya mfuko wa Zanzibalicous Women Group uliozinduliwa rasmi na Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein (hayupo pichani).
DSC_0074
Mbunifu nguli wa mavazi Mama wa mitindo, Asia Idarous akinadi moja ya nguo alizotengeneza kwa ajili ya kuchangia mfuko wa Zanzibalicious Women Group.
DSC_0075
Mke wa Naibu Waziri wa Afya serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bi. Zakhia Kombo akitangaza dau la kununua nguo hiyo iliyokuwa ikinadiwa kwenye harambe ya mfuko wa ZWG iliyozinduliwa na Mama Mwanamwema Shein.
DSC_0091
Meza kuu kwenye picha ya pamoja na Zanzibalicous Women Group.
Unaweza kutembelea mtandao wao na kuona shughuli mbalimbali walizozifanya hapa http://www.zanzibalicious.org/
DSC_0388
Mmoja wa wadhamini ZANLINK wanaotoa udhamini kwa Zanzibalicious Women Group wakisikiliza kwa makini yaliyokuwa yakijiri ukumbini hapo. Kwa picha zaidi bofya link hii

No comments: