Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia (wa kwanza kushoto), pamoja na Konseli Mkuu wa Tanzania nchini Dubai Bw. Omar Mjenga wakifuatilia kwa makini mazungumzo kati ya Mh. Membe na Askofu Wilson (hawapo pichani)
Picha na Reginald Philip
=================================================
Waziri Membe atoa rai kwa madhehebu
kuwaombea viongozi kuwa waadilifu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Membe ametoa rai kwa waumini wa Kanisa la Waadiventista Wasabato nchini kushiriki kikamilifu katika kutengeneza viongozi bora wa Serikali wanaozingatia misingi ya uadilifu, upendo na unyenyekevu.
Waziri Membe ameyasema hayo wakati akitoa hotuba ya kufunga Kongamano la Kimataifa la Utume la Kanisa la Waadventista Wasabato lililofanyika katika Uwanja wa Taifa, Jijini Dar es Salaam tarehe 07 Februari, 2015.
Mhe. Membe alisema kuwa Dini na madhehebu yanayo nafasi kubwa katika kujenga jamii yenye maadili na hofu ya Mungu wakiwemo viongozi na hivyo kupelekea taifa kuwa na amani, upendo na mshikamano. Alieleza kuwa kama Waziri wa Mambo ya Nje, amejifunza kuwa diplomasia na hofu ya Mungu vikifanya kazi pamoja hakuna changamoto yoyote isiyoweza kukabiliwa.
“Dini na Diplomasia vina husiana pale masuala ya amani, ulinzi na usalama yanapoguswa. Hivyo nawaomba mshiriki katika kutengeneza viongozi bora katika jamii zetu kwa misingi ya uadilifu ambao watasimamia amani na kujiepusha na vitendo viovu ikiwemo rushwa,” alisema Mhe. Membe.
Aidha, alilipongeza Kanisa hilo kwa kuwa mfano mzuri wa ustahimilivu na uvumilivu wa kidini hapa nchini. Alieleza kwamba kamwe hajawahi kusikia Kanisa la Waadiventista Wasabato limeingia katika mgogoro na Serikali, dhehebu au dini nyingine na hilo ni funzo kubwa kwa Watanzania, kwamba kutofautiana kiitikadi, kidini, kikabila au rangi si sababu tosha ya kuwagombanisha na kuvuruga amani ya nchi.
“Nalipongeza Kanisa lenu kwa kuwa mfano mzuri wa uvumilivu wa kidini na imani, mnaendesha mambo yenu kwa uvumilivu mkubwa na kushirikiana na dini zote na hili linatufundisha kuwa kutofautiana kwetu sio sababu tosha ya kugombana” alisisitiza Membe.
Pia, Mhe. Membe alilihakikishia Kanisa hilo dhamira ya Serikali ya kuendelea kushirikiana nalo kwa ajili ya ustawi wa nchi na kufafanua kuwa Serikali itaendelea kulinda uhuru wa kuabudu kwa dini zote kama inavyoelezwa kwenye Katiba ya nchi. “Serikali inao wajibu wa kusaidia dini na madhehebu kufanyakazi kwa uhuru. Bahati nzuri Katiba inayopendekezwa imezingatia kulinda uhuru huo hivyo tuiunge mkono” alifafanua Waziri Membe.
Vilevile alilisifu Kanisa hilo kwa kuanzisha miradi ya huduma zikiwemo Shule15 za Sekondari na Msingi, Chuo Kikuu na Hospitali mbili ambavyo vinatoa mchango mkubwa kwa Serikali na Wananchi kwa ujumla.
Awali akimkaribisha Waziri Membe kufunga Kongamano hilo, Rais wa Baraza Kuu la Makanisa ya Sabato Duniani, Askofu Ted Wilson alisema kuwa anawaombea Viongozi wa Tanzania waendelee kuwa na maono kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na kwamba wakimtumaini Mungu atawawezesha kupata maono mapya kwa ajili ya kulitumikia Taifa hili.
Kwa upande wake, Mwenyeji wa Mkutano huo, Mchungaji Blasius Luguri aliipongeza Tanzania kwa kudumisha amani ambayo imepelekea Tanzania kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa Kongamano hilo ulioyashirikisha Mataifa zaidi ya 20. Aidha, alimwomba Mhe. Membe kufikisha ujumbe kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa wana imani na Tanzania kuwa ni nchi ya amani, usalama na utulivu.
Kanisa la Sabato ni Kanisa linalokua duniani likiwa na Waumini milioni 307 huku Waumini milioni 30 wakiwa Afrika na takriban milioni 5 wakiwa Tanzania.
-Mwisho-
|
1 comment:
Nimekukubali Michuzi kwa Utoaji Taarifa bila upendeleo. be blessed more.
Post a Comment