Tuesday, February 10, 2015

Uongozi makini wa shule chini ya BRN ni nguzo ya Elimu Bora

Mwalimu Kassim Musa- Biolojia Na Kemia (kushoto) na mwalimu Erasto Daniel Fizikia na Hisabati (Kulia) wa shule ya sekondari Ntyuka iliyoko Dodoma wakijiandaa kuingia maabara na wanafunzi wao.

Annastazia Rugaba – BRN

“Sasa ninaifurahia kazi yangu. Ninajisikia vizuri kuwa mwalimu. Natamani BRN ingeanza toka kitambo. Hata hivyo naona mabadiliko makubwa yanakuja tukiendelea na kasi hii…” hayo yalisemwa na mwalimu Geza Musfapha Juma ambaye ni Mkuu wa shule ya sekondari Ntyuka iliyoko Dodoma, azungumza na watendaji wa BRN waliotembelea shule yake mwishoni mwa mwezi wa kwanza Mwaka huu. 

Mwalimu Juma alikikiri kuwa tangu kuanzishwa kwa BRN, shule yake imeanza kufanya vizuri. Mwaka 2013 matokeo ya kidato cha nne yalikuwa mabaya sana kwani wanafunzi walikuwa watoro. Kati ya wanafunzi 68 wa kidato cha nne wa mwaka 2013, ni wanafunzi watano tu ndio waliokuwa na bidii yakuja shuleni.

Baada ya kupata mafunzo ya uongozi yaliyoandaliwa chini ya BRN katika chuo cha uongozi wa elimu Bagamoyo Mwalimu Juma alipanga mkakati pamoja na bodi ya shule kuhakikisha wanatokomeza utoro shuleni.

Pia aliwahamasisha walimu kufundisha kwa bidii na amehakikisha walimu wanapatiwa motisha kwa ajili ya kufundisha kwa ziada watoto wenye shida ya kuelewa haraka darasani.  Shule ya Ntyuka sasa imeanza kupata mafanikio. Mwaka 2013 matokeo ya mtihani wa Manispaa, shule ilishika nafasi ya 45 kati ya shule 49.  Mwaka 2014 shule ilishika nafasi ya 94 kati ya shule 194 za mkoa. ‘Haya ni mafanikio makubwa sana kulinganisha na tulikotoka’ alisema Mkuu wa Shule bwana Juma.

Mwalimu Erasto Daniel na Mwalimu Kassim Musa ni walimu wa sayansi katika shule ya sekondari Ntyuka.  Walimu hawa wamehudhuria mafunzo ya BRN yanayolenga kuinua kiwango cha ufundishaji kwa walimu hasa wa masomo ya sayansi. Tangu wamepata mafunzo hayo wameongeza ari yao ya kuwasaidia watoto katika jamii yao kufikia ndoto zao za kuwa wanasayansi.

Walimu hawa wanaipenda kazi yao sasa kuliko zamani, “ilikuwa inavunja moyo sana kuingia darasani kuwafundisha watoto somo la Kemia, fizikia na Biolojia nadharia na vitendo bila vifaa. Hata watoto walitamani sana wajifunze kwa vitendo masomo ya maabara. Haikuwa rahisi kwetu na kwa wanafunzi kila ilipofika mtihani wa taifa.’ Alisema mwalimu Daniel

“Leo hii tunajisikia fahari kuwa walimu wa sayansi, tunaweza kuwasaidia wanafunzi wafanye vitendo, na hii itawasaidia kuelewa na kufanya vizuri katika mitihani yao” alisema Mwalimu Kassim.

Hawa ni miongoni tu mwa walimu 1,325 nchini, ambao wamepata mafunzo ya masomo ya sayansi katika Mwaka 2013.

Big Results Now - BRN ni mfumo wa kusimamia, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa mipango ya kipaumbele ya maendeleo ya Taifa. Mfumo huu wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) unalenga kuharakisha kufikiwa kwa malengo yaliyoainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa kufikia mwaka 2025 (Tanzania Development Vision 2015). BRN inasisitiza kuweka vipaumbele, kuwa na adabu katika utendaji na kufuatilia kwa kina na kwa tija utendaji na utekelezaji wa miradi mbali mbali ya serikari.

Sekta ya Elimu pia iko ndani ya BRN; na hadi sasa sekta imefanya kazi kubwa katika maeneo ya upangaji wa matokeo na shule, utoaji motisha kwa shule, walimu na wanafunzi waliofanya vizuri, ujenzi wa miundombinu ya shule, kulipa madeni ya walimu, kutoa miongozo ya uendeshaji wa shule kwa shule zote nchini, utoaji wa mafunzo kwa walimu na msaada kwa wanafunzi wenye uelewa mdogo.

Nia ya BRN ni kuwaona walimu na wanafunzi pamoja na wanajamii kwa ujumla ikiwemo wanaharakati wa masuala ya Elimu wakiunga mkono juhudi hizi ili kwa pamoja tuifikie dira ya maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025. Elimu Bora inawezekana Timiza wajibu wako

No comments: