Naibu Balozi wa Tanzania nchini Oman Juma Othaman (mwenye Kaunda suti) akipokea Tunzo ya ushiriki iliyotolewa na Mwakilishi kutoka Manispaa ya Mji wa Muscat ambao ni Waandaaji wa Maonesho ya Kimataifa ya Sanaa, Ubunifu na Utamaduni. Tanzania imepeleka zaidi ya Watu 40 kuonesha kazi wanazoifanya za sanaa ikiwemo,Uchongaji,uchoraji na ufumaji wa nguo. Kulia ni Kiongozi wa Msafara huo Khadija Battashy na kushoto ni Msaidizi kiongozi Masha Hussein. Picha na Faki Mjaka, Muscat Oman
Naibu Balozi wa Tanzania nchini Oman Juma Othman (katikati) akiwa kashika Tunzo ya ushiriki wa Maonesho ya Kimataifa ya Sanaa, Ubunifu na Utamaduni nchini Oman waliyopewa kutoka Manispaa ya Mji wa Muscat ambao ndio waandaaji wa Maonesho hayo. Kulia kwake ni Kiongozi wa Msafara wa Washiriki kutoka Tanzania Khadija Battashy na kushoto ni Msaidizi kiongozi Masha Hussein na Mkuu wa mambo ya kiufundi wa Msafara Moza Habib.
Na Faki Mjaka, Muscat Oman
Msemo wa Kiswahili usemao ‘aisifiaye Mvua huwa imemnyeshea’ unafanana kwa mbali na ule usemao ‘adhabu ya Kaburi aijuaye Maiti’. Misemo hii huonesha jinsi ambavyo muhusika kwenye tukio husika ndiye mwenye uelewa mpana zaidi wa kufahamu umuhimu au madhara ya jambo fulani.
Hata kunapotokea tatizo la kihalifu na kutakiwa ushahidi mara nyingi Polisi huanzia kuwakamata wale waliokuwa katika tukio hilo ili kusaidia kutoa ushahidi wa awali.
Mantiki ya utangulizo huo ni kusifia namna gani Ofisi ya Balozi wa Tanzania nchini Oman ilivyofanikisha Maonesho ya kimataifa ya Sanaa,Ubunifu na Utamaduni yanayofanyika nchini Omani na namna Maonesho hayo yanavyoweza kuisaidia Tanzania kupiga hatua mbele katika Sekta ya Kiutalii.
Sifa hizo za Ubalozi hazitakuwa lolote bila kuisifia Manispaa ya Muscat na Serikali ya Omani kwa ujumla kwa kuialika nchi ya Tanzania kushiriki katika Maonesho hayo yanayofanyika kwa muda wa mwezi mmoja. Ushiriki huo unaonesha namna gani Tanzania ilivyokuwa na mahusinao mema na nchi hiyo. Katika maonesho hayo ni nchi chache Rafiki wa Omani zilizoalikwa kuonesha bidhaa na vivutio vyake ikiwemo China, Ufaransa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, India, Thailand, Morocco, Uzbekistan, Misri na Tanzania.
Kwa hakika kuna faida nyingi zilizopatikana katika Maonesho hayo lakini kubwa kuliko ni namna ambavyo Tanzania ilivyotumia nafasi hiyo kikamilifu kujitangaza kwa Wanachi wa Omani na Wageni lukuki ambao walifanikiwa kufika katika Banda la Tanzania au kupata taarifa kupitia Vyombo vya habari vinavyoripoti Maonesho hayo.
Mkuu wa Utawala katika Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Oman Abdallah Kilima anasema walitakiwa kualika Wanasanaa na Wajasiriamali wa kitanzania watakaoonesha kazi zao wanazozitengeneza kwa mikono, hivyo likaja wazo la kutafuta Kampuni ya Utalii ambayo itakuja kutoa huduma ya kutangaza Vivutio vya Tanzania kwa vile uwepo wa bidhaa hizo huambatana na uwepo wa Wageni(Watalii).
“Kwanza Banda tuliliweka strategically, wenyeji wetu walitaka tuepeleke watu wa bidhaa za Mikono, moja kwa moja tukajua tu kuwa bidhaa hizi zinaambatana na ujio wa wageni wengi kwani ni kivutio cha Watalii hapo ndio ikawa bahati ya kuwaalika Pongo Safaris&Tours”Alisema Kilima.
Kweli banda liliwekwa Kimkakati maana Unapoingia katika Banda hilo la Tanzania unakutana na Bango kubwa lenye Mlima Kilimanjaro linalosomeka “Welcome Tanzania, The Land of Kilimanjaro, Zanzibar and The Serengeti” ambapo harufu ya viuongo kama vile Karafuu inahanikiza uzuri na upekee wa Banda hilo.
Screen kubwa inayoonesha vivutio mbalimbali kama vile Mbuga za Wanyama, Maziwa ,Fukwe nzuri za Zanzibar na Hoteli zake huku Mavazi ya kimasai na Vinyago katika Banda hilo vikiwa ni vivutio tosha kwa wageni kuingia.
Kwa vile Ubalozi ulidhamiria haukumuacha mkono Mwakilishi kutoka Kampuni ya Pongo Safaris&Tours na hivyo kumsaidia kwa kumkutanisha na Wadau wakubwa wa Kampuni za Omani zinazojishughulisha kusafirisha Watalii ili kubadilishana uzoefu na kupanga namna ya kufanya kazi kwa pamoja. Kampuni hizo nipamoja na Marmul Travels, Khimji Travel House na National Travel and Tourism (NIG).
Kilima anasema Ofisi zingine na Wadau wengine wa Utalii wafahamu kuwa Soko la Utalii ni kubwa nchini Oman na halijaharibiwa hivyo kuna haja Watu kuchangamkia fursa hiyo ili Watalii badala ya kwenda kutembea nchi za Mashariki ya Mbali na Magharibi waje nchini Tanzania.
Kwa hakika kama watahamasishwa vilivyo kuna uwezekano mkubwa wa kubadili mwelekeo na hilo linawezekana.
Katika kuonesha namna ambavyo Tanzania imejitangaza zaidi ya Makundi ya watu 150 wamejisajili kuja Tanzania kwa ajili ya kufanya shughuli ya Utalii kupitia Kampuni ya Kusafirisha Watalii maarufu kama Pongo Safaris&Tours.
Bi Annah Shangvi Mwakilishi kutoka Pongo Safari&Tours anasema katika Watu waliojisajili kuja Tanzania wapo pia Wanafunzi wa Vyuo Vikuu, Shule za kawaida na watu mbalimbali wenye hadhi tofauti baada ya kuvutiwa na Tanzania.
Anasema wapo pia Wenyeji wa Oman na wageni mbalimbali kutoka nchi za Asia kama Wahindi, Wairani, Wachina na Wazungu kutoka nchi mbalimbali ambao zaidi wamevutiwa na kupanda Mlima Kilimanjaro, Kuwinda na kutembelea Zanzibar.
Bi Anna Shangvi amedai kuwa katika kuchunguza kwake amebaini kuwa Makampuni kutoka Kenya yanayojishughulisha kusafirisha Watalii huwa wanaongopa kwa kusema kuwa Mbuga ya Masai Mara ndio Manyara na Mlima Kilimanjaro haupo Tanzania bali upo Kenya.
“Kwa kweli Maonesho haya yamesaidia sana kuweka ukweli hadharani, Wageni wanaokuja hapa Wanalazimika kuamini kuwa Kilimanjaro ipo Tanzania na Mbuga ya Manyara ni tofauti na Masai Mara..CD na Ramani zinasaidia sana tunapowaonesha kutufahamu kwa haraka” Bi Annah alisema.
Vipeperushi na Machapisho mbalimbali zaidi ya 1,000 kutoka Mamlaka ya Mbuga Taifa (TANAPA) na vile vilivyotoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar viligawiwa kwa Wageni mbalimbali waliokuwa na shauku ya kuijua Tanzania.
Ukweli nikwamba Wananchi wa Oman wanapenda kuzuru nchi mbalimbali duniani kiutalii mfano mdogo ni nchi ya Thailand ambapo kwa mujibu wa Gazeti la Oman ‘Times of Oman’ toleo la jana Februari 14, amekaririwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Utalii nchini Thailand Bw. Chalermsak Suranant akisema makadirio yao ni kupata Watalii 90,000 kwa mwaka 2015 kutoka nchi ya Oman.
Suranant anasema kupitia Kampeni mpya waliyoipa jina la “2015 Discover Thainess” wanatarajia hamasa itaongezeka zaidi kwa Wananchi wa Oman kwenda kutalii Thailand mwaka huu ambapo kwa mwaka jana Jumla ya Watalii 75,000 walitembelea nchi hiyo.
Katika hali ya kawaida mtu hawezi kwenda sehemu anayotarajia kwenda kupumzika au kustarehe huku akiwa na kasumba au upofu wa taarifa ya huko anakokwenda. Uwingi wa Watalii hao kutoka Oman bila shaka umechangiwa na Waoman wenyewe kuwa na Taarifa sahihi zinazoshawishi vivutio vya huko.
Maonesho haya kwa hakika imekuwa ni Mwanzo mzuri kwa Tanzania maana Vyombo vya habari vya Oman havikuwa na ubinafsi katika kuyatangaza maonesho hayo kupitia mtangazo ya moja kwa moja kwa moja au ya kurikodiwa.
Taarifa mbalimbali na Makala maalum za kuisifia Tanzania na Vivutio vyake katika Magazeti na Majarida yao yanayoandikwa kwa Kiarabu na yale yanayoandikwa kwa Lugha ya Kingereza zimehanikiza sifa ya Tanzania kuzidi kujulikana kwa Wenyeji na Wageni wa Oman.
Kwa vyovyote iwavyo ni wakati sasa wa kukaa Mkao wa kula na kuzidi kuandaa mazingira rafiki ya kupokea Watalii wapya kutoka nchi Tofauti ambao ni Matokeo ya Ushawishi unaotokana na nafasi waliyoipata Tanzania ya kushiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Sanaa, Ubunifu na Utamaduni nchini Oman.
Mkuu wa Msafara wa Watanzania hao Bi Khadija Battashy anasema imefika wakati wa kubadilika na kuepuka kutegemea soko la nchi za Ulaya na Marekani kwa ajili ya Utalii nchini Tanzania. Vivutio vingi na vyaupekee na hali ya Usalama iliyopo Zanzibar na Bara haiendani sawa na Idadi ndogo ya Watalii wanaukuja Tanzania.
Bado kuna kazi kubwa ya kufanya kuitangaza Tanzania na Vivutio vyake. Kazi iliyofanywa na Ofisi ya Balozi wa Tanzania Nchini Oman chini ya Bw. Ali Ahmed Saleh ya kufanikisha Ushiriki wa zaidi ya Watanzania 40 walioenda kuonesha vipaji vyao katika Maonesho hayo inafaa kuigwa na Ofisi zingine za Kibalozi pale fursa zinapotokea.
No comments:
Post a Comment