Thursday, February 12, 2015

NI SAFARI YA MIAKA 15 TAMASHA LA PASAKA

DSC_0333
 
“NILIAMUA kuanzisha Msama Promotions baada ya kuona muziki wa Injili umesahaulika na unashuka thamani yake.“Hivyo kwa kushirikiana na wenzangu nikaona ni busara kuuinua ili tuwe kama wenzetu Afrika Kusini ambao wana waimbaji wa nyimbo za Injili wanaotamba kama Rebecca Malope, Itani Madima, Steve Kekane, Vuyo Mokoena na wengine wengi,” hiyo ni kauli ya Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama.
 
Msama ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Pasaka, anasema alitaka watu wajue na kutambua kuwa muziki wa Injili unaweza kupigwa kama burudani katika kumbi mbalimbali za starehe na kuondoa dhana potofu kwamba muziki huo wa Injili haufai kupigwa katika kumbi hizo.
 
“Kupeleka muziki wa Injili kwenye kumbi ambazo hupigwa muziki wa miondoko mingine ya kidunia si dhambi kama baadhi ya watu wanavyofikiri,” anasema.Anasema ni zaidi ya miaka 15 tangu walipoanzisha Tamasha la Pasaka wakati wa sikukuu hiyo kila mwaka na sasa jamii imelikubali na limekuwa gumzo kubwa kwa jamii.
 
Anasema pia dhamira yao nyingine ya kuanzisha tamasha hilo ilikuwa kusaidia jamii kwa namna mbalimbali kutokana na fedha za viingilio, lakini pia kuwapa ajira vijana kutokana na tamasha hilo.“Ninachoweza kusema ni kwamba mwaka huu tumedhamiria kwa dhati kusaidia jamii kwa namna mbalimbali kutokana na fedha zitakazopatikana kwenye viingilio vya tamasha.
 
“Haitakuwa mara ya kwanza kwetu kusaidia, tumefanya hivyo miaka ya nyuma na tutaendelea na juhudi hizo kila tutakapopata nafasi ya kufanya hivyo, “ anasema.Anatolea mfano kuwa miaka ya nyuma wamesaidia watu mbalimbali ikiwemo  waathirika wa mabomu yaliyotokea kwenye kambi ya jeshi Gongo la Mboto, Dar es Salaam. Pia anasema wamepata kutoa fedha kwa ajili ya kuwasomesha watoto yatima na kuwasaidia mitaji ya biashara wanawake wajane.
Msama anabainisha kwamba kutokana na dhamira hiyo, ndiyo maana wamekuwa mstari wa mbele kuandaa matamasha ya muziki wa Injili, lengo likiwa ni kusaidia masuala mbalimbali.Anasema mwanzoni wakati wanaanza tamasha hilo mwaka 2000, wamewahi kuandaa matamasha kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee kwa ajili ya kuchangia watoto yatima wa mikoa ya Morogoro na Pwani, ambao wazazi wao walifariki kwa ugonjwa wa Ukimwi, ambapo yote waliyopanga yalifanikiwa.
 
Pia anasema fedha wanazopata wamekuwa wakitumia kusomesha yatima na kuwatafutia ajira mbalimbali wasiojiweza ikiwa ni pamoja na wengine kupata mafunzo ya kunadi vitu kupitia kampuni yake ya udalali ya Msama Auction Mart. Mkurugenzi huyo anasema mpaka sasa wanasomesha wanafunzi katika shule mbalimbali Dar es Salaam.
 
Pia anasema kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali wamekuwa wakitoa semina za kusaidia wajane, yatima na vijana wasio na ajira ikiwa ni pamoja na kuwapa mbinu za kufanya biashara na kuachana na dawa za kulevya.
Anasema wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha huduma wanazotoa zinawafikia walengwa.
 
“Mimi naamini mtoaji wa vyote ni Mwenyezi Mungu, hivyo ni busara upatapo kidogo ugawane na wasiojiweza ili kuongeza thawabu zako.
“Ndiyo maana tumekuwa tukijitolea kuwasaidia wasiojiweza ikiwa ni pamoja na  kuwasomesha yatima na wasiojiweza na tumekuwa mstari wa mbele kutoa ajira kwa  baadhi ya vijana wa Tanzania,” anasema.
 
Mkurugenzi huyo wa kampuni hiyo iliyo mstari wa mbele kuinua muziki wa Injili nchini, anawaasa vijana kuwa na moyo wa ujasiri na uvumilivu na wa kupenda kujituma kufanya kazi ili kufikia lengo la kupiga hatua kimaendeleo.Anasema vijana wengi wamekuwa wakipenda kukaa na kubweteka badala ya kufanya kazi na kuwa wabunifu.
“Binafsi sipendi maendeleo yangu peke yangu, bali napenda pia kuwa mstari wa mbele kushirikiana na wenzangu,” anasema.
 
Kuhusiana na tamasha lenyewe anatamba kuwa wamewaandalia mashabiki wa muziki wa Injili mambo mazuri yatakayowaburudisha na kuridhika.Anaeleza kuwa tamasha la mwaka huu 2015 ambalo lipo katika hatua za awali za maandalizi litafana kwa vile kutakuwa na waimbaji wengi wa muziki wa Injili watakaowapa mashabiki vionjo mbalimbali.
 
Anasema anatarajia tamasha hilo litahudhuriwa na maaskofu wa madhehebu mbalimbali aliosema wameanza kufanya mazungumzo na baadhi yao, ambao wapo katika kamati yake ya maandalizi.
Anajinasibu kuwa tamasha hilo litafana kwa vile kutakuwa na 
waimbaji wengi wa muziki wa Injili watakaowapa mashabiki vionjo mbalimbali. 
 
Kwa mujibu wa Msama, mpaka sasa wadau wa muziki wa Injili wa mikoa ya Mbeya, Mwanza, Arusha, Dodoma, Tanga, Dar es Salaam, Mtwara, Shinyanga na Zanzibar ndiyo ambao wameomba kufanyika tamasha hilo mikoani mwao.
 
“Tutaheshimu mno maoni ya wapenzi wa tamasha hili kutoka sehemu mbalimbali na kila watakalotushauri tutalifanyia kazi, lengo kubwa ni kiboresha tamasha letu,” anasema Msama.Pia Msama anasema, kampuni yake ipo katika mkakati wa kujenga kiwanda cha kisasa kwa ajili ya kuzalisha bidhaa zinazohusiana na kazi za wasanii.

No comments: