Naibu Waziri wa Nishati na Madini (Nishati), Charles Mwijage (Kulia)
akielekeza jambo kwa baadhi ya Viongozi wa Kampuni ya Mafuta ya
TIPPER alipotembelea Kampuni hiyo hivi karibuni wakati wa ziara yake
kwa Kampuni mbalimbali zinazojishughulisha na biashara ya mafuta nchini.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini (Nishati), Charles Mwijage (Wa pili
kutoka Kushoto) akifuatana na baadhi ya Viongozi wa Kampuni ya Mafuta
ya GAPCO kukagua miundombinu ya kuhifadhia mafuta iliyoko eneo la
Kampuni hiyo, Kurasini jijini Dar es Salaam. Naibu Waziri alitembelea
Kampuni mbalimbali zinazojishughulisha na biashara ya mafuta nchini
kufanya mazungumzo na kukagua miundombinu inayotumiwa na Kampuni
husika.
Meneja wa Kampuni ya Mafuta ya HASS nchini Tanzania, Ali Hassan
Ahmed (Kushoto), akisikiliza maelekezo kutoka kwa Naibu Waziri wa
Nishati na Madini (Nishati), Charles Mwijage (aliyeinua mkono) kuhusu
utekelezaji wa mambo mbalimbali unaotakiwa kufanywa na Kampuni hiyo,
hususan kujenga mahusiano mema na jamii. Wa kwanza Kulia ni Mbunge
wa Temeke (Viti Maalum – CCM), Mariam Kisaka.
Joshua Mtunda (mwenye Fulana ya Njano), akizungumza na Naibu Waziri
wa Nishati na Madini (Nishati), Charles Mwijage (wa Tatu kutoka Kushoto),
kwa niaba ya Vijana wenzake wanaofanya biashara ya kusafirisha abiria
kwa Pikipiki/Bodaboda kuhusu msaada wanaohitaji ili kuboresha biashara
yao. Vijana hao wanafanya biashara yao eneo la Kigamboni karibu na ilipo
Kampuni ya Mafuta ya HASS.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini (Nishati), Charles Mwijage (wa kwanza
– Kushoto), akikagua miundombinu ya kuhifadhia mafuta ya Kampuni
ya Mafuta ya PUMA katika eneo la Kampuni hiyo, Kurasini jijini Dar es
Salaam. Pamoja naye pichani ni baadhi ya Viongozi wa Kampuni hiyo na
Maafisa wa Serikali wanaoshughulikia Sekta ya Mafuta.
Na Veronica Simba
Naibu Waziri wa Nishati na Madini (Nishati), Charles Mwijage amezitaka
Kampuni zinazojishughulisha na biashara ya Mafuta nchini, kutumia mbinu
mbalimbali za kuboresha mahusiano mema na jamii zinazowazunguka ili
kujenga imani kwa wananchi na hivyo kupata ushirikiano katika masuala
mbalimbali ikiwa ni pamoja na ulinzi wa miundombinu husika.
Aliyasema hayo katika ziara yake hivi karibuni alipotembelea Kampuni
mbalimbali za Mafuta zilizoko jijini Dar es Salaam pamoja na kukagua
miundombinu yao.
Mwijage alisema, matatizo kama vile kuharibiwa kwa miundombinu ya
kuhifadhia na kusafirishia mafuta, pamoja na wizi wa mafuta unaofanywa
na baadhi ya wananchi unachangiwa na wananchi kutokuwa na imani na
wafanyabiashara hao kwa kuwa hawaoni manufaa ya moja kwa moja kwa
jamii kutoka Kampuni hizo.
“Ikiwa wananchi wataona manufaa ya uwepo wa Kampuni zenu katika
maeneo yao, nina uhakika watajenga imani kwenu na hawatakuwa tayari
kuona mnaharibikiwa kwa namna yoyote kwani wao pia watakuwa ni
sehemu yenu,” alisema Mwijage.
Akifafanua kuhusu namna nzuri ya kujenga mahusiano mema na jamii,
Mwijage alisema inafaa Kampuni hizo ziwasaidie wananchi kuinua vipato
vyao kwa kuwapatia mitaji ya fedha na vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya
biashara mbalimbali.
Naibu Waziri alitoa mfano wa biashara ndogondogo za kusafirisha abiria
kwa kutumia Pikipiki maarufu kama Bodaboda zinazofanywa na vijana,
pamoja na biashara ya kuuza chakula maarufu kama Mama Lishe kwa
akina mama na mabinti.
“Pamoja na mambo mengine makubwa mnayosaidia jamii kama vile
kuchangia elimu, nashauri pia muone namna ya kusaidia mambo madogo
madogo kama kuwanunulia bodaboda vijana pamoja na kuwapa mitaji
akina mama lishe,” alisisitiza Mwijage.
Aidha, Mwijage alisisitiza Kampuni hizo kuwashirikisha Viongozi mbalimbali
wa maeneo husika wakiwamo Wabunge, Madiwani, Viongozi wa Kata na
Mitaa husika katika zoezi la kuainisha watu wanaohitaji misaada husika ili
kuepuka utapeli kwa kuwapatia wasio na sifa zinazostahili kupata misaada
hiyo.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri aliagiza Barabara ya Mafuta iliyoko
eneo la Mivinjeni-Kurasini jijini Dar es Salaam ifunguliwe ili kupunguza
msongamano wa magari unaochangia magari makubwa yanayosafirisha
mafuta kwenda sehemu mbalimbali nchini na nje ya nchi kutokusafiri kwa
wakati hivyo kusababisha hasara kwa Kampuni husika.
“Ninaomba Halmashauri ya Manispaa ya Temeke iangalie uwezekano wa
kuifungua njia hii ambayo wameifunga, ili itumike kama ilivyokuwa ikitumika
awali; magari yaingie na kutoka kwa urahisi ili kuepusha msongamano
uliopo,” alisisitiza Mwijage.
Naibu Waziri alilazimika kutoa agizo hilo kufuatia hali ya msongamano
mkubwa wa magari aliojionea kwa baadhi ya Kampuni alizotembelea
ikiwemo Kampuni ya GAPCO iliyoko eneo la Kurasini.
Kwa upande wao, wawakilishi wa Kampuni zilizotembelewa na Naibu
Waziri, waliahidi kuzingatia ushauri uliotolewa katika kuboresha mahusiano
yao kwa jamii husika.
No comments:
Post a Comment