Sehemu ya Ghala la kuhifadhi vitunguu Saumu liliojengwa na MIVARF, lipo Mkoani Manyara Wilayani Mbulu, kijijini Bashay. Ghala hilo lina uwezo wa kuhifadhi tani 50 za vitunguu Saumu.
Na. Ibrahim Hamidu
Programu ya Miundo Mbinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF) imeboresha Soko la Vitunguu Saumu kwa kujenga ghala la kuhifadhi vitunguu mkoani Manyara, wilayani Mbulu katika kijiji cha Bashay.
Ghala hilo lenye uwezo wa kuhifadhi tani 50 za vitunguu, limegharimu Jumla ya shilingi milioni 88 ikiwa MIVARF imechangia asilimia 95 ya fedha hizo na Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu imechangia asilimia 5 ya fedha hizo.
Akiongea na timu ya wataalam kutoka MIVARF ofisini kwake hivi karibuni wakati timu hiyo ilipokuwa ikikagua utekelezaji wa shughuli za Mradi huo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Bw. Nicholaus Haraba, alifafanua kuwa ujenzi wa ghala hilo umeongeza mnyororo wa thamani wa zao la vitunguu Wilayani Mbulu.
“Tunaushukuru Mradi wa MIVRAF kwa ujenzi wa ghala hili la kuhifadhi vitunguu ambalo ni ghala pekee kwa hapa nchini lenye viwango sitahiki na uwezo wa kuhifadhi tani nyingi za vitunguu. Kwa mantiki hiyo ghala hili limewawezesha wakulima wa zao hilo kuongeza thamani ya mazao yao ambayo awali yalikuwa yanapotelea shambani kwa kukosa eneo la kuyahifadhi ” alisema Haraba.
Haraba alieleza kuwa, kupitia MIVRAF wananchi wa Mbulu wamepata mafunzo ya jinsi ya kufungasha mazao yao pamoja na kuwezeshwa vifungashio vya vitunguu hali ambayo imelijengea ubora zao hilo katika soko.
“Wananchi awali walikuwa wanauza mazao yao huko mashambani, katika mabeseni na lumbesa lakini baada ya mafunzo ya MIVARF ya jinsi ya uhifadhi wa mazao yao hivi sasa wananchi wanauza vitunguu kwa vipimo kwa kutumia vifungashio maalum hii inamfanya mkulima kunufaika na mauzo hayo” alisisitiza Haraba.
Aliongeza kuwa, katika kuhakikisha Soko la Vitunguu linakuwa imara Wilayani Mbulu, MIVARF imejenga barabara kwa kiwango cha Changarawe kutoka Bashay, Diyomat, Dirima hadi Muslur yenye Urefu wa km 25 kwa gharama ya shilingi milioni 789 ikiwa asilimia 95 ya fedha zilizotolewa na MIVRAF na asilimia 5 zimetoka katika Halmashauri ya Mbulu.
“Ujenzi wa barabara hii pia utasaidia kwa wafanyabiashara kusafirisha kwa usalama mazao hayo baada ya kuyanunua kutoka Mbulu” alisisitiza Haraba Katika kuunga juhudi za MIVARF za kuboresha Soko la Vitunguu tayari Halmashauri ya Wilayani Mbulu katika bajeti yake ya mwaka 2015/2016 imetenga kiasi cha shilingi milioni 18 kwa ajili ya ununuzi wa mashine ya kusindika vitunguu ili wafanyabiashara wanunue vitunguu ambavyo tayari vimesindikwa na tayari kumuuzia mtumiaji wa mazao hayo.
“Tunategemea MIVARF iendelee kuliboresha soko hili la vitunguu na jukumu letu nikuchangia kwa kile tunachowezeshwa na MIVARF hivyo tumeamua kutenga fedha katika bajeti ya mwaka ujao ili tutakapowezeshwa kununua mashine ya kusindika vitunguu tuwe tayari kwa ajili ya ununuzi wa mashine yetu” alisema Haraba.
Akiongea na Wataalamu wa MIVRAF katika ghala la kuhifadhi Vitunguu la Bashay Wilayani Mbulu, Mkulima wa zao hilo, Bi. Wema Edward alibainisha kuwa Mradi wa MIVRAF umeliboresha soko la vitunguu wilayani humo kwa kuongeza mnyororo wa thamani wa zao hilo.
“Kutokana na uhifadhi bora wa vitunguu na vifungashio bora hivi sasa tunauza kilo ya vitunguu kati ya shilingi elfu 3,000/= hadi elfu 4, 000/= , wakati awali tulipokuwa tunatumia mabeseni kuhifadhi mazao yetu tulikuwa tunauza kilo kwa shilingi elfu 1,500/=. ” alisema Wema. Mradi wa MIVRAF ambao unahudumia wananchi 4,800 wilayani Mbulu ulianza kutekelezwa katika wilaya hiyo kuanzia mwaka 2013, katika kata tatu za Wilaya hiyo, kwa kuongeza thamani mazao na ujenzi wa miundo mbinu ya masoko.
Programu ya Miundo Mbinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF) ni Programu iliyobuniwa na Serikali Tanzania ikishirikana na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) na Taasisi ya Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRA). Programu hii ni ya miaka saba inayotekelezwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar. Utekelezaji wake ulianza rasmi mwezi Julai 2011.
No comments:
Post a Comment