Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii kanda ya Kaskazini.
CHAMA Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa zao la Kahawa mkoani
Kilimanjaro KNCU (1984) Ltd kimetumia kiasi cha dola laki 9.48 kununua
mtambo wa kukobolea Kahawa kutoka kampuni ya Pinhalense ya Brazil.
Ununuzi wa Mtambo huo wa kisasa unafanyika ikiwa ni sehemu ya maazimio
ya mkutano mkuu wa KNCU uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana wajumbe
wakiazimia kufanyika juhudi za makusudi ili kukinusuru kiwanda hicho
ambacho kilielekea kufa.
Katika hali ya kukiokoa kiwanda hicho,bodi ya kampuni ya kukoboa
kahawa ya Tanganyika (TCCCo) ililazimika kuuza sehemu ya mali zake ili
kukinusuru na madeni yanayokikabili baada ya kupata hasara ya zaidi
ya shilingi bilioni 2 .
Tanzania Daima Jumatano ilifika katika kiwanda hicho juzi na
kushuhudia sehemu za mtambo huo unaotajwa kuwa wa kwanza katika ukanda
wa Afrika Mashariki na kati zikishushwa toka katika magari matano.
Meneja wa TCCCO, Endrew Kleruu, alisema ujio wa mitambo hiyo utasaidia
kupunguza upotefu wa Kahawa ,ikiwa ni pamoja na kuongeza ubora wa
uzalishaji unaoendana na viwango vya ubora katika
soko la Kimataifa.
Alisema mitambo hiyo yenye uwezo wa kuzalisha tani sita kwa saa moja
itasaidia kuwapunguzia wakulima wa zao hilo gharama za uzalishaji
kutokana na uwezo wake wa kutumia umeme mdogo wa Kilo Voti 30 hadi 35
tofauti na mtambo wa zamani ambao ulikuwa unazalisha tani nne tu kwa
saa huku ukitumia zaidi ya Kilo Voti 100 ya umeme.
Kleruu aliwataka wakulima wa zao la Kahawa kuongeza juhudi katika
kilimo cha zao hilo chenye tija ili kukidhi hitaji la Kahawa yenye
ubora wakati wa uendeshaji wa mtambo huo mpya .
Kwa upande wake meneja wa usambazaji vifaa wa kampuni ya Brazafric
Enterprizes Ltd, Salim Mghweno,alisema kuwa ufungaji wa mtambo huo
utatumia miezi miwili ambapo matarajio ni hadi kufikia msimu wa
uzalishaji wa Kahawa ufungaji wa mtambo huo utakuwa umekamilika.
Alisema kukamilika kwa ufungwaji wa mtambo huo kutasaidia ongezeko la
kiwango cha zao hilo ukilinganisha na mtambo wa zamani ambao Kahawa
iliyokobolewa ilipungua kiwango licha ya ukubwa wa mitambo ambayo pia
imeelezwa kuwa ni chakavu.
Mwisho.
Mtambo mpya wa kisasa wa kukobolea Kahawa ulionunuliwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa zao la Kahawa mkoani Kilimanjaro kwa gaharama za dola laki 9.48 ukishushwa katika kiwanda. |
Mota ya kuzungusha mashine wakati wa ukoboaji ikishushwa ikiwa ni sehemu ya mtambo mpya wa kukobolea Kahawa utakaofungwa katika kiwanda cha Cofee Curing. |
Sehemu ya vifaa kwa ajili ya mtambo mpya wa kisasa wa kukobolea Kahawa. |
No comments:
Post a Comment