Thursday, February 19, 2015

HAKUNA WASICHOWEZA NI MRADI UNAOLETA MATUMAINI MAPYA KWA WATOTO WA KIKE-MASHULENI

Wanafunzi wa shule ya msingi ya Mwenge iliyopo mkoani Lindi wakimsikiliza kwa makini mwalimu wa masuala ya Afya na Uzazi wa Mpango Monica Mfaume, wakati wa kuwagawia wasichana pedi na kuwapatia elimu ya Afya na uzazi, mpango huu uko chini ya mradi wa Hakuna Wasichoweza unaoendeshwa na taasisi ya T-Marc na kudhaminiwa na USAID na Vodacom Foundation na unawalenga wanafunzi waliopo mashuleni na wasio mashuleni zoezi hili limeanza kufanyika katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi ya Mwenge iliyopo mkoani Lindi wakifurahia baada ya kugawia pedi za kujikinga wanapokuwa kwenye hedhi .Mpango kwa kuwagawia wasichana pedi na kuwapatia elimu ya Afya na uzazi uko chini ya mradi wa Hakuna Wasichoweza unaoendeshwa na taasisi ya T-Marc na kudhaminiwa na USAID na Vodacom Foundation na unawalenga wanafunzi waliopo mashuleni na wasio mashuleni zoezi hili limeanza kufanyanyika katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

“Sasa nafurahia masomo yangu ikiwemo maendeleo yangu darasani kuwa mazuri darasani.Najisikia vizuri kuwa mwanafunzi.Natamani mradi wa Hakuna Wasichoweza ungeanza kitambo.Hata hivyo naona mabadiliko makubwa ya kumuwezesha mtoto wa kike na kumjengea uwezo wa kujiamini yanakuja tukiendelea na kasi hii…”Haya yalisemwa na Sharifa Hamis, mmoja wa wanafunzi wa sekondari mkoani ya msingi ya Mwenge iliyopo mkoani Mtwara wakati akitoa ushuhuda kwa niaba ya wenzake ni kwa jinsi gani wasichana wenzake zaidi ya 5,000 wamenufaika na mradi alipohojiwa hivi karibuni.

Mwanafunzi Sharifa alikiri kuwa tangu kuanzishwa kwa mradi wa Hakuna Wasichoweza maarufu kama Girl Power mahudhurio ya wasichana shuleni kipindi chote cha masomo yameongezeka pia ufanisi wao katika masomo umeongezeka kwa kiasi kikubwa tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Ushuhuda huo uliungwa mkono na mwalimu Masoud Issa anayefundisha katika shule hiyo. Baada ya kupatiwa mafunzo ya Afya na mafunzo kuhusiana na mabadiliko ya miili yao ikiwemo kuwapatia pedi wasichana wanaotoka katika familia maskini kwa ajili ya kujihifadhi wanapokuwa kwenye vipindi vya hedhi wasichana wengi wameanza kujiamini na kupunguza utoro wa kuja shuleni uliosababishwa na hali hiyo kutokana na shule wanazosoma kutokuwa na mazingira rafiki ya kujihifadhi katika kipindi hicho.

Mafunzo kwa wasichana na namna na kujihifadhi wakati wakiwa hedhi pamoja na afya ya uzazi yanafanyika chini ya uwezeshaji wa walimu na wauguzi waliopewa mafunzo hayo. Kitini cha kufundishia juu ya masuala haya kimeweza kuandaliwa na taasisi ya T-MARC kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania kupitia mradi huu wa ‘Hakuna Wasichoweza’ na kina maelezo ya kina juu ya umuhimu wa afya,elimu ya uzazi na matumizi ya Pedi.

Mmoja wa walimu wanaotoa mafunzo kwa wasichana Monica Mfaume,anasema kuwa mradi huu umeleta mabadiliko makubwa katika kipindi cha muda mfupi tangu uanze na aliwapongeza waliounzisha na kuwaomba waufanye kuwa endelevu na usambae nchi nzima na kuwafikia wasichana wengi zaidi. “Tatizo la mahudhurio hafifu ya wasichana na kufanya vibaya katika masomo ikiwemo kupata mimba katika umri mdogo kutokana na kutojua mabadiliko katika makuzi yao lilikuwa linatuvunja moyo lakini angalau hivi sasa linapungua kwa kasi eneo hili la mradi ”.Alisema

Meneja Uhusiano wa taasisi ya T-MARC inayotekeleza mradi chini ya ufadhili wa USAID na Vodacom Foundation,Maurice Chirimi, anasema kuwa mradi umeonyesha kuwa na mafanikio kwa muda mfupi wa miaka 2 ya awamu ya kwanza kwa mafunzo pamoja na pedi za bure kuwafikia wasichana zaidi ya 5,232 waliopo katika shule 24 za msingi na wengine 552 wasiokuwepo mashuleni katika kata 17 mkoani Mtwara.

Lengo la Mradi wa Hakuna Wasichoweza ni kuwapatia elimu ya uzazi,afya,kuwajengea uwezo wa kujiamini na kuwapatia Pedi watoto wa kike zaidi ya wasichana 10,000 waliopo katika umri wa kuvunja ungo katika mikoa ya Mtwara na Lindi.Mradi unatekeleza mpango wa taifa kwa vitendo wa kuhakikisha watoto wa kike hawabaki nyuma bali wanapata fursa sawa na wenzao wa kiume.

Nia ya Hakuna Wasichoweza ni kuwaona walimu ,watoto wa kike na wanajamii kwa ujumla ikiwemo wanaharakati wa masuala ya elimu wakiunga mkono juhudi hizi ili kwa pamoja tuifikie dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2015.Elimu Bora bila ubaguzi inawezekana,Timiza wajibu wako.

No comments: