Saturday, January 31, 2015

Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela washauriwa kutumia ujuzi kujiajiri

 Mwezeshaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi Ester Riwa wa pili kulia akizungumza na Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Kyela Dr. Festo Dugange jana wakati wa ziara ya kuhamasisha vijana wa Kyela. Wa kwanza kulia ni Afisa Maendeleo ya Vijana Bi. Amina Sanga, wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Kituo cha Vijana Sasanda Mbeya Bw. Laurean Masele na wa pili kushoto ni Afisa Vijana Mkoa wa Mbeya Bw. George Mbijima.
 Afisa Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Amina Sanga akiwaelimisha vijana wa Wilaya ya Kyela kuhusu mwongozo unaosimamia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana wakati wa semina ya Ujasiriamali, Stadi za Maisha, Ujuzi na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana iliyofanyika jana katika Wilaya ya Kyela Mkoa wa Mbeya.
 Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela Mkoa wa Mbeya walioudhuria semina ya Ujasiriamali, Stadi za Maisha, Ujuzi na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana wakifuatilia mambo mbalimbali yaliyokua yakiendelea wakati wa semina hiyo.
 Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela wakiwa katika kikundi kujadiliana namna ya kuandika andiko la mradi baada ya kupata mafunzo ya jinsi ya kuandika andiko la mradi wakati wa semina ya Ujasiriamali, Stadi za Maisha, Ujuzi na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana iliyofanyika jana katika Wilaya ya Kyela Mkoa wa Mbeya.
Mwenyekiti wa Wadau Self Supporting Group Bw. Godbless Konga wanne kulia akizungumza na maafisa kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo walipotembelea kikundi hicho kuangalia mradi unaoendeshwa na vijana wa kikundi hicho jana wakati wa ziara ya kukagua miradi ya vijana wa Wilaya ya Kyela Mkoa wa Mbeya.



Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela washauriwa kutumia ujuzi kujiajiri.


Na: Genofeva Matemu



Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela wameshauriwa kuachana na fikra potofu za kusubiria kuajiriwa na serikali mara tu wanapomaliza elimu ya chuo kikuu bali kutumia ujuzi walioupata kujiajiri wenyewe na kutoa fursa kwa vijana wengine ambao hawakupata fursa ya kujiendeleza.


Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kyela Bibi Magreth E. Malenga alipokua akizungumza na wadau wa vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo walipofika ofisini kwake kabla ya kukutana na Vijana wa Wilaya hiyo kwa ajili ya kutoa elimu ya Ujasiriamali, Stadi za Maisha, Ujuzi, na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana jana katika Wilaya ya Kyela Mkoa wa Mbeya.


Akizungumza na wadau hao Bibi Malenga amesema kuwa amefurahishwa na ujio wa wadau kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwani anaamini kuwa ujio huo utawasaidia vijana wa Kyela kujitambua na kupata mbinu mbalimbali za kiujasiriamali ili waweze kujitegemea.“Vijana wa sasa hawapendi kujiajiri wanapomaliza elimu ya chuo kikuu wanabaki mitahani wakiilalamikia serikali haitaki kuwaajiri, naamini kwa semina hii vijana wa Kyela watajitambua na kutumia elimu waliyoipata kuibua miradi mbalimbali itakayowaingizia kipato” alisema Bibi Malenga.


Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Vijana Bi. Amina Sanga amewataka vijana wa Kyela kutumia fursa mbalimbali zilizopo katika Wilaya hiyo kwani kwa kufanya hivyo watakua wameweza kujiendeleza na kujitegemea hivyo kuondokana na dhana ya kuwa tegemezi katika jamii.


Naye mwenyekiti wa kikundi cha vijana kijulikanacho kwa jina la Wadau Self Supporting Group Bw. Godbless Konga amesema kuwa vijana wa Kyela walikua na ufikiri mdogo katika masuala ya aunzishaji na usimamiaji wa shughuli ndogondogo kutokana na kutokuwa na mbinu za kibiashara lakini kutokana na eimu waliyoipata  anaamini kuwa vijana watawekeza na kuachana na dhana ya kuwa tegemezi katika jamii. 


Bw. Konga amewataka vijana wote nchini kuwa wabunifu na kujaribu kuanzisha miradi mbalimbali kwa kutumia mbinu za kibiashara zitakazowakwamua kimaisha ili kuachana na tabia ya kuitegemea serikali kwa kila jambo.

No comments: