Monday, January 5, 2015

UNATAKA NYUMBA/KIWANJA, HAKIKISHA HAYA KISHERIA USITAPELIWE

Na  Bashir   Yakub

Kwa muda mrefu sasa kumekuwepo na migogoro ya mashamba, viwanja na nyumba  hasa maeneo ya mijini.  Kwa utafiti wa kawaida utagundua kwa haraka baadhi ya sababu ambazo husababisha hali hii.Uaminifu, tamaa, kutelekeza maeneo kwa muda mrefu, utendaji mbovu wa  baadhi ya watumishi katika mamlaka za ardhi, uzembe na kutojali ni baadhi ya sababu  ambazo huchangia kuwapo  na kukua kwa tatizo hili. 

Baada ya kuwapo  tatizo hili wajibu mkubwa umebaki kwa watu wenyewe kuwa makini na waangalifu  katika mununuzi ya ardhi. Ni uangalifu na umakini pekee ambao waweza kumsaidia mtu kuepukana na  migogoro hii.  Katika kuwa mwangalifu yapo mambo ambayo mtu anaweza kuyafanya . Moja ya mambo hayo ni kuwa makini  kwa kuhakikisha unafuata taratibu zote unapokuwa unafanya mkataba wa manunuzi. 

Mkataba wa  manunuzi ya  kiwanja, nyumba si jambo jepesi kama wengi wanavyolifikiria. Ni jambo nyeti  hasa ikizingatiwa kuwa  ardhi ni mali ya kudumu . Hii maana yake ni kuwa umri wote wa kiwanja au nyumba yako  itakaoishi iwe miaka mia au mia mbili itakuwa inalindwa na mkataba huohuo. 

Hakika si jambo  jepesi. Nataka nieleze kuwa watu wengi wanafanya  mikataba ya manunuzi ya viwanja nyumba kienyeji na kiholela. Wanafananisha mikataba hii na mikataba ya ununuzi wa vitu ambavyo haviishi hata miaka kumi kama magari. 

Ni hatari sana na wengi wamepoteza nyumba  na viwanja kimchezomchezo. Ubaya zaidi ni kuwa unapokuwa na mkataba wa  kiwanja au nyumba ambao haukidhi viwango vya kisheria  na bahati mbaya ukatokea mgogoro ni rahisi sana kupoteza  eneo lako bila kujali ni kiasi gani  umewekeza katika kulimiliki.

 Niseme tu kuwa kila mkataba si mkataba mikataba mingine ni maandishi  tu na wala haikidhi viwango vya kuitwa mikataba. Mikataba ya aina hii ni mikataba ambayo haiwezi kumlinda wala kumtetea mnunuzi anapokuwa na mgogoro. Nazungumzia zaidi wanunuzi  kwakuwa  ndio waathirika wakubwa wa migogoro kwa kuwa upande wao ni wa kupoteza. 

Mkataba wa ununuzi wa kiwanja au nyumba unatakiwa kuwa na baadhi ya mambo ya msingi sana ambayo kwa fursa hii baadhi nitayaeleza ili wenye kufaidika na wafaidike. Nitaeleza kwa mtindo wa dondoo mambo ya msingi ambayo hutakiwa kuwa katika mkataba wa mauziano ya kiwanja au nyumba.

MKATABA WA  NYUMBA   LAZIMA  UWE  KATIKA  MAANDISHI.
Sura ya 345 Sheria ya mikataba ya 2002 huwa inatambua mikataba ya aina mbili yaani mikataba ya  maneno  na mikataba ya maandishi. Suala msingi huwa ni kuthibitisha ule mkataba wako wa maneno au maandishi kwa kuleta mashahidi au ushahidi.Hata hivyo hali ni tofauti katika upande wa ardhi kwa kuwa kifungu cha 34(1)(a) cha Sheria ya Ardhi kinasema kuwa mkataba wowote wa kuhamisha umiliki wa ardhi(kuuza,kununua) au kuweka rehani ardhi utalindwa na sheria iwapo utakuwa katika maandishi. Hii maana yake ni kuwa mtu ahakikishe kuwa anapouza au kununua ardhi ni muhimu mkataba ule ukawa katika maandishi .Watu wazingatie hapa kuwa iwe ardhi unainunua kwa mzazi wako  , ndugu yako au rafiki yako kipenzi ni lazima mkataba uwe katika maandishi . Bila hivyo athari zake ni kuwa  kiwanja au nyumba yako haina ulinzi wa sheria.
Yafuatayo ni muhimu kuonekana katika mkataba:                   

( a ) MAJINA  YA  WAHUSIKA  YAONEKANE  KWA  UREFU
Lazima kuwe na majina ya wahusika ambayo yatakuwa yameandikwa kwa urefu  na kwa kueleweka.Mfano jina liwe Aloys Anold Ntagazwa . Epuka kuandika vifupi  mfano A.A. Ntagazwa. Jina linatakiwa liwe katika ukamilifu wake na hasa pawe na majina matatu kamili. Pia majina  ya pande zote mbili yaani muuzaji na mnunuzi yatokee hivyohiyvo  si tu majina ya upande mmoja. Yawezekana mkataba mwingine unahusisha watu wengi zaidi  pia ni muhimu  majina matatu ya kila mmoja yaonekane hata kama  wako ishirini.Umuhimu wake ni kuwa jina linapoonekana kwa ukamilifu wake inaepusha uwezekano wa mtu kukataa jina lake au  kumsingizia mwingine ambaye ana majina yanafanana. Wapo watu wanafanana majina mawili lakini hali hiyo si rahisi kwa majina matatu. Pia katika majina hayo hadhi ya kila mmoja iainishwe mbele ya jina lake. Mfano kama ni muuzaji  au mnunuzi mbele iandikwe kuwa huyu ni muuzaji na huyu ni mnunuzi. 

(  b ) ANUANI   KAMILI   YA MAKAZI  YA   MUUZAJI NI LAZIMA.
Anuani za muuzaji au mnunuzi  ziwepo ikiwa ni pamoja na namba ya simu. Anuani ya muuzaji ni lazima kuliko ya mnunuzi kutokana na nafasi yake. Anuani hapa sio tu  P.O BOX…. hapana  anuani ni kwa maana ya maelekezo kamili ya makazi ambapo akihitajika panapo mgogoro atapatikana. Pia kuna suala la namba ya simu  ni muhimu sana kwasasa kutokana na msaada mkubwa wa mawasiliano haya endapo mtu atahitajika. Anuani yaweza kuwa hivi Muuzaji ni Abdu Salum Galio wa Dar es salaam, Mwananyamala A, ccm Mwinjuma mtaa wa kisiwani nyumba no 123 ( 0784 788 987) .Hapa ni rahisi kumpata mtu hata likitokea la kutokea.

( c ) KUWEPO  NA  KIFUNGU KINACHOONESHA  NIA  NA UHALALI  WA  MMILIKI
Awali kabisa  wakati mkataba unapokuwa unaanza ni vema kikawapo kipengele kinachoonesha nia ya kuuza na nia ya kununua ikiwa ni pamoja na  uhalali wa muuzaji kumiliki eneo. Mfano Muuzaji ana nia ya kuuza kiwanja/nyumba na mnunuzi ana nia ya kunnuna kiwanja/nyumba tajwa na muuzaji  anathitibitisha kwa kusema kuwa yeye ni mmiliki halali wa kiwanja/nyumba husika. Muonekano uwe hivyo. Muuzaji anapothibitisha umiliki anakuwa amejifunga na ni vigumu kukana kuwa hamiliki chochote na hivyo hajawahi kuuza.

  (  d  ) BEI  YA  MAUZIANO  IANDIKWE   KWA  NAMBA  NA KWA  MANENO.                                                                                                                                                                                                                                                     
 Bei au gharama halisi ya mauziano ioneshwe. Iandikwe kwa tarakimu yaani namba mfano 1,000,000/= na kwa maneno katika mabano ( Milioni moja tu).Ni muhimu yote mawili yaonekane , hii huondoa utata.Tarehe ya mkataba ioneshwe sambamba  na maelezo kama fedha imelipwa yote au kiasi.Iwe hivi, Leo tarehe 12. 12  2014 mnunuzi  mtajwa hapo juu amekubali kununua kiwanja/nyumba tajwa kwa  kiasi cha Tshs 1,000,000/= ( Milioni moja tu). Hii inaondoa ile habari ya sikuelewa zile namba zilimaanisha nini au sikuelewa maneno yalimaanisha nini.

( e ) KAMA  PESA  IMELIPWA YOTE  AU  KIASI  KIPENGELE  KIONESHE.
Pia  lazima kuwepo na kipengele kinachoonesha kuwa pesa imelipwa yote au hapana mfano, pesa hiyo imelipwa yote na hivyo mnunuzi hadaiwi .
Kama kuna kiasi kilichobaki kianishwe kwa tarakimu na pia kwa maneno  kama nilivyoonesha hapo juu. Muda wa kulipa kilichobaki nao uainishwe ikiwa ni pamoja na hatua za kuchukua ikiwa muda uliowekwa utapita. Mkataba  lazima uoneshe muda ukipita  nini kifanyike mfano ikifika tarehe 7. 12. 2015 saa kumi jioni kiasi cha pesa iliyobaki hakijalipwa basi mali itamrudia mwenye nayo na mnunuzi hatakuwa na deni lolote dhidi ya muuzaji, au itahesabika kuwa mkataba umevunjika  na  mnunuzi atatakiwa kumlipa fidia ya kiasi fulani muuzaji kwa kuvunja mkataba. 

( f  )HADHI  YA  KIWANJA/NYUMBA  KUHUSU  KODI   IONESHWE
Mkataba wa  kiwanja au nyumba  uoneshe kama kimelipiwa kodi ya ardhi ( Land rent) na kama hakijalipiwa mkataba ueleze nani atalipa kodi hiyo kati ya anayenunua au anayeuza.Mfano Muuzaji anamhakikishia mnunuzi kuwa amelipa kodi ya ardhi( Land Rent) pamoja  na kodi ya jengo( Property Tax).

(  g ) MALI   ILIYOUZWA  ICHAMBULIWE   VYEMA
 Mali inayouzwa au iliyohusishwa kwenye mkataba ichambuliwe vyema. Kama ni kiwanja au nyumba ielezwe mtaa, kata, tarafa kitongoji,mkoa,plot namba kama ipo, urefu, upana, ikiwezekana  jirani wa kushoto na kulia.au magharibi, mashariki.Mfano nyumba hiyo ipo  Dar es salaam, Mwananyamala A . ccm Mwinjuma mtaa wa kisiwani  plot no 123. Hapa ni muhimu taarifa zote zilizo kwenye hati au leseni ya makazi kuingia katika mkataba .

 ( h ) KIPENGELE KINACHOMBANA  MUUZAJI KUTOA  USHIRIKIANO  UKITOKEA  MGOGORO
Ni muhimu sana  mkataba uweke wajibu  kwa muuzaji kuwa tayari kumpa ushirikiano   mnunuzi iwapo mali aliyomuuzia itaonekana kuwa na mgogoro mbeleni.Mfano muuzaji atampa ushirikiano mnunuzi endapo kutatokea mgogoro wowote kuhusiana na mauziano haya. Hii huwa inasaidia kumlazimisha muuzaji kuwa shahidi  kama litatokea tatizo mbeleni. Bila kipengele hiki muuzaji anaweza akakataa kukutolea ushahidi au akahitaji  malipo ili akutolee ushahidi wakati yeye  pengine ndo amekuuzia kiwanja chenye mgogoro. Anakuingiza katika matatizo halafu hataki kutokea. Kwa kipengele hiki kutokea  haitakuwa hiyari tena isipokuwa wajibu usio na mjadala kwakuwa  ni sehemu ya makubaliano.

( i ) IONESHWE   NANI  ATATATUA  MGOGORO  IWAPO UKITOKEA
Pia ni muhimu sana mkataba uoneshe iwapo mgogoro wowote utatokea kuhusiana na mkataba huo nini wahusika wafanye. Mfano endapo mgogoro utatokea kuhusiana na mkataba huu mahakama ya ardhi ya Tanzania  ndio itahusika na utatuzi wa mgogoro. 
Mara nyingi kipengele hiki huwa cha mwisho kabisa kabla ya sahihi za mashahidi na wahusika
( j ) MASHAHIDI  KUWEKA  MAJINA  NA SAHIHI
Kila upande hata ukiwa na shahidi mmoja wala si mbaya. Shahidi awe mtu wa kuaminika , mtu mzima na mwenye akili timamu. Wataandika majina yao matatu kwa urefu kama yalivyo  ya wahusika  na pia wataweka sahihi zao huku  ikioneshwa shahidi yupi wa upande upi na yupi wa upande upi. Wakili ni mtu muhimu sana kwa wakati huu kwani  wakili anaweza kuwa shahidi pekee bila kuwapo shahidi mwingine yeyote. Wakili  anakuwa shahidi wa  wote wawili na panakuwa hapahitajiki mwingine yeyote.Pia wakili ni shahidi wa kuaminika  zaidi na anaaminiwa na kila mamlaka ikiwemo mahakama na hivyo uwepo wake katika mkataba  ni ulinzi tosha kwa mkataba wako.Basi shahidi kama ni wakili au mwingine ataandika jina lake kwa urefu na kusaini mbele yake. Wakili ataweka na muhuli pia.

( k ) KUBANDIKA  PICHA  YA MUUZAJI  NA  MNUNUZI
 Picha  ndogo yenye kuonesha taswira ya mtu kwa ukamilifu (passport size) ni  muhimu sana na ibandikwe mbele ya jina la mtu. Si muhimu sana kwa mashahidi lakini  kwa wahusika wenyewe ni muhimu sana. 

( l ) KUWEKA  ALAMA  YA  DOLE GUMBA
Alama ya  dole gumba mbele ya jina nayo ni muhimu sana. Hii ni kutokama na alama hii kutoweza kwa namna yoyote kuingiliwa au kughushiwa.Tia dole kwenye kablasha ya muhuri na weka dole gumba mbele ya kila jina. Hii pia si lazima kwa mashahidi.

Kwa ufupi hayo ni baadhi  tu ya mambo ya msingi katika kukufanya kuwa salama na kiwanja/nyumba yako. Kutokufanya hivi kunakuweka katika hatari kubwa ya kupoteza. 

Mwandishi  wa   makala  haya  ni  Mwanasheria   na  Mshauri  wa sheria  kupitia  gazeti  la  serikali  Habari  Leo  kila  jumanne,   gazeti Jamhuri  kila  jumanne  na  Nipashe  jumatano.

0784482959
0714047241
bashiryakub@ymail.com

7 comments:

Anonymous said...

Asante sana ancle Michuzi kwa kutupa elimu ya bure ila kwa bahati mbaya kwa kuwa taifa lets lime jana mazumbukuku wengi hivyo usishangae kutoona comment kwenye habari nzuri kama hii ila ukiwaekea habari za Diamond na Wema Sepetu utapata comments zaidi ya 1000

halludbadiasdaawias said...

je kipengele na k na l vipo katika sheria na 345 kifungu chochote?

Anonymous said...

Mzee kama wewe una comments usilazimishe wengine pia kuweka zao. inawezekana watu wanauelewa tayari!
Pengine mjinga ni wewe peke yako !

Anonymous said...

binafsi nimeifurahia hii article kwa saana! nilikuwa najiandaa kununua kiwanja katika eneo ambalo halijapimwa, hii doc imenipa hint za kutosha katika kuandikishana mkataba na muuzaji. je viongozi serikali za mitaa kama wenyeviti kutaka walipwe fedha katika manunuzi na sawa? JE viongozi hawa wanaweza kuwa mashahidi katika mkataba wa manunuzi?

Unknown said...

Uchambuzi wa namna hii ndo unaotakiwa katika kutujenga ndani ya jamii walau unapunguza changamoto za migogoro hasa pale pande moja inapopoteza uaminifu.Kazi nzuri Michuzi na Bwana Bashir Yakoub

Anonymous said...

na kiwanja ambacho hakijapimwa tutakihakiki vp????

Anonymous said...

Dah hakika nimepata mwanga juu ya hii mikataba nashukuru sana kwakweli na hizi ndio taarifa za kupata na ndio njia sahihi za kupunguza migogoro na kama si kumaliza kabisa .