Thursday, January 1, 2015

TUWAKUMBUKE WAZEE WASIOJIWEZA -LULU MTEMVU

Mjumbe wa Baraza la Vijana (UVCCM) wilaya ya Morogoro vijijini, Lulu Mtemvu, katika picha ya pamoja , Desemba 31, 2014 na baadhi ya wazee wasiojiweza wa Kambi ya Funga Funga iliyopo Manispaa ya Morogoro.
Mjumbe wa Baraza la Vijana (UVCCM) wilaya ya Morogoro vijijini, Lulu Mtemvu, akimkabidhi zawadi ya vyakula na mbuzi kwa ajili ya sikukuu ya mwaka mpya 2015 kwa Wazee wasiojiweza wa Kambi ya Funga Funga iliyopo Manispaa ya Morogoro, mnamo Desemba 31, 2014, zawadi hiyo ilipokelewa na Mwenyekiti wao Joseph Kaniki. ( Picha na John Nditi).

Na John Nditi, Morogoro

VIJANA wa chama cha Mapinduzi UVCCM wameshauriwa kujenga tabia ya kusaidi wazee wasiojiweza, kwa kuwapatia misaada mbalimbali kwa lengo la kuwapa faraja badala ya kuachia jukumu hilo kwa serikali pekee kama  ilivyo sasa.

Kauli hiyo ilitolewa Desemba 31, 2014  na Mjumbe wa Baraza la Vijana (UVCCM) wilaya ya Morogoro vijijini, Lulu Mtemvu,wakati alipotembelea kituo cha kuwatunza wazee wasiojiweza cha Fungafunga cha Kichangani Manispaa ya Morogoro.

Lulu  ambaye pia ni mtoto wa mbunge wa jimbo la Temeke , Abbas Mtemvu, alisema ametoa msaada wa mchele, mbuzi,sukari na sabuni za kufuria kwa wazee hao zenye thamni ya sh  milioni moja.

‘’ Pamoja na kuwa mimi ni mwanafunzi  lakini nilijikusanya kwa muda mrefu ,kwaajili ya kutoa zawadi hii ya sikukuu kwa wazee hawa ili nao waweze kufurahia katika sikuu ya mwaka mpya’’ alisema.

Hivyo alitoa wito kwa vijana nchini kujenga tabia ya kusadia wazee, wajane na watoto yatima ili kuwawezesha kuishi kwa matumaini na faraja, na kuona jamii inawathamini.

‘’ Tukumbuke pia sisi ni wazee watarajiwa, hivyo tuone ni jukumu la jamii nzima hususani viojana kusadia makundi hayo maalumu ambayo kwa hakika yanahitaji msaada’’ alisema.

Kwa upande wao wazee hao wa Funga funga walisema wamepata faraja kuona vijana  kama hao wanaona umuhimu wa kuwasaidia ili nao waweze kupata chakula hasa katika sikukuu kama hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya wazee wa kituo hicho, Mwenyekiti wao ,Josefu Kaniki, alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kuwapatia zawadi ya mchele Kg 400, mafuta ya kura na mbuzi.

‘’ Tunapenda kutuma salamu zetu kwa  Rais wetu Kikwete kwa kutukumbuka sisi wazee, tunamhakikishia msaada umetufikia na tumefurahia  na tunamwombe dua ili aweze kutuongoza vema kwa hekima na busara katika kipindi chake hiki" alisema Mwenyekiti  wa wazee  kituo hicho.

Pamoja na kutoa shukrani hizo, aliiomba  Serikali kuangalia uwezekeano wa kuwalipia bili ya umeme, kwani kwa sasa wamekatiwa umeme kutokana na kituo hicho kudaiwa deni la sh milioni nne.

‘’ Kwa kweli tunakula tunashiba, lakini ikishafika jioni saa 12 , wazee wote tunakosa amani, hatuna muda tena hata wa kuzungumza kama ilivyokuwa zamani" alisema na kuongeza kuwa.

" ...Inatulazima kila mmoja awahi kitandani mwake kulala na hata kwenda chooni ni  shida hasa kwa wazee wasioweza kutembea’’ alibainisha.

Kituo hicho cha Fungafunga kilichopo katika eneo la Kata ya Kichangani, Manispaa ya Morogoro lina milikiwa na Idara ya Ustawi wa Jamii chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na kina jumla ya wakazi 50, wakiwemo wazee, wajane na watoto  wasiojiweza.

No comments: