Monday, January 19, 2015

TEKNOLOJIA YA KUTUMIA MAGOGO IMEPITWA NA WAKATI - BINILITH

Na Rashda Swedi- OMR

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira Mhe. Dkt. Injinia Binilith Mahenge amepiga marufuku matumizi ya magogo kama nishati ya kuzalisha bidhaa katika viwanda.

"Matumizi ya Magogo viwandani kama nishati ya uzalishaji ni uharibifu mkubwa wa Mazingira na ni adui wa maendeleo katika Taifa letu, pia ni teknolojia iliyopitwa na wakati".

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira Mhe. Dkt. Injinia Binilith Mahenge alipotembelea kiwanda cha kutengeneza Nguo cha Afirtex kilichopo Jijini Tanga. Alisema hayo baada ya kukuta kiwanda hicho kinatumia magogo kama nishati ya uzalishaji. 

Hata hivyo ameutaka uongozi wa kiwanda hicho kuhakikisha hatatumia tena magogo na badala yake watumie nishati mbadala kwa mfano makaa ya Mawe ili kuweza kulinda Mazingira.

Alisisitiza kwa kusema kuwa Matumizi ya Magogo katika uzalishaji ni Teknolojia ya zamani hivyo tunatakiwa tubadilike ili kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi ambayo kwa sasa ni pigo kubwa kwa Taifa letu kutokana na ukataji miti hovyo.

Aidha, amewapa miezi mitatu kuwacha kabisa kutumia magogo katika uzalishaji na endapo wakibainika wanaendelea kutumia magogo hatua za kisheria zitachukuliwa.

Hata hivyo, Mhe. Mahenge aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kuchimba bwawa litakalotumika kwa ajili ya kuondoa sumu zilizokuwa kwenye maji yanayotoka kiwandani kabla ya kutiririsha katika mfereji mkuu wa maji na kuathiri wananchi.

Wakati huo huo Mhe. Mahenge alitembelea kiwanda cha chokaa cha Neelkanth pamoja na kiwanda cha vipodozi LPPT kukagua hali ya Mazingira katika viwanda hivyo. 

Mhe.Mahenge amekipongeza kiwanda cha kutengeneza vipodozi (LPPT) kwa kushiriki usafi kila jumamosi ya mwanzo wa Mwezi ikiwa ni moja ya agizo lililotolewa na Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Mohammed Gharib Bilal.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira Mhe. Dkt. Injinia Binilith Mahenge, akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Tanga pamoja na Wadau wa Mazingira na Waandishi wa Habari kuhusu umuhimu wa kutunza Mazingira na athari mbalimbali zitokanazo na uharibifu wa Mazingira, alipowasili Jijini Tanga kabla ya kuanza ziara yake.
Sehemu ya wadau mbalimbali wa Mazingira wakisikiliza kwa makini Hotuba ya Mhe. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira Dkt. Injinia Binilith Mahenge (hayupo pichani).
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira Mhe. Dkt. Injinia Binilith Mahenge (aliyenyanyua mkono,) akitoa maelekezo kwa injinia wa kiwanda cha Afritex Bw. Joseph Mhando (wa tatu kushoto) ,kuhusu kutotumia magogo kama nishati ya uzarishaji, alipotembelea kiwanda hicho Jijini Tanga.
Injinia wa kiwanda cha Afritex Bw. Joseph Mhando (wa kwanza kulia), akitoa maelezo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira Mhe. Dkt. Injinia Binilith Mahenge (wa pili kulia), jinsi wanavyoyatibu majitaka yanayotoka kiwandani hapo kabla ya kutiririsha kwenye mfereji mkuu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira Mhe. Dkt. Injinia Binilith Mahenge (kulia),akikagua Mazingira ya kiwanda cha chokaa (Neelkanth Lime) kilichopo Jijini Tanga. pembeni yake ni Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Bw. Rashid A. Mahmoud.
Mwenyekiti wa kiwanda cha kutengeneza Vipodozi Bw. Mohammed Raza Hassanali (wa tatu kulia) akitoa maelezo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira Mhe. Dkt. Injinia Binilith Mahenge (wa pili kushoto), jinsi wanavyoyasafisha maji taka kabla ya kutiririsha kwenye mfereji mkubwa.

No comments: