Na Bashir Yakub
Makala zilizopita nilieleza mambo au taarifa muhimu zinazopaswa kuwa kwenye mkataba wako unapokuwa unanunua nyumba/kiwanja. Nikasema katika niliyosema kuwa mkataba lazima uoneshe ukitokea mgogoro utatatuliwa vipi, ueleze kuwa utapotokea mgogoro muuzaji lazima awajibike kuhakikisha anakupa ushirikiano mnunuzi ili kumaliza mgogoro huo na kuwa muuzaji kama ana mke basi mke wake ni lazima aandaiiwe nyaraka iitwayo ridhaa ya mwanandoa ambayo ni tofauti na mkataba na aisaini pamoja na kuweka picha yake. Nilieleza mengi lakini hayo ni baadhi tu.
Kwa wale ambao hawakubahatika kuyasoma hayo basi waandike neno MAKALA SHERIA kwenye google watapata makala hizo. Leo tena naeleza hatua muhimu sana au ya lazima na lazima haswaa kwa mnunuzi wa kiwanja/nyumba ambayo anatakiwa apitie kabla ya kufanya manunuzi.Hatua hii kwa jina la kitaalam huitwa OFFICIAL SEARCH kwa lugha rahisi tu waweza kuiita utafiti,upekuzi, upembuzi au upelelezi rasmi ambayo hufanywa na wanasheria. Mi napenda niite upelelezi.
( 1 ) AINA ZA VIWANJA/NYUMBA UNAPOTAKA KUFANYA UPELELEZI KUJUA KAMA KUNA MGOGORO.
Nyumba/viwanja tunavyouziana kila siku vimegawanyika katika hadhi mbalimbali. Kwanza kuna nyumba/viwanja vyenye hati, vyenye leseni za makazi, vyenye ofa na ambavyo havina hati, leseni ya makazi wala ofa.
Kutokana na makuzi ya miji yetu viwanja/nyumba zenye hati mara nyingi huwa ni chache sana.Zenye leseni za makazi ni nyingi kiasi na haya ni maeneo ambayo hasa hujulikana kama uswahilini. Zenye ofa huwa ni chache nazo kwakuwa ofa ni hatua anayopitia mtu anapoelekea kupata hati au leseni ya makazi.
Pia maeneo ambayo hayana hati wala leseni ya makazi wala ofa nayo ni mengi sana pia. Kwa Dar es salaam haya ni maeneo ya pembeni pembeni mwa mji Tegete,bunju, pugu, chanika, mbagala, baadhi ya maeneo ya kigamboni n.k. Hata hivyo eneo liwe na hati leseni ya makazi au hapana bado kisheria linatambulika .
( 2 ) NAMNA YA KUJUA KAMA NYUMBA/KIWANJA KINA MGOGORO
Kama kiwanja/nyumba ina hati kuna maombi rasmi ya kisheria ambayo huwa yanafanywa kwenda ardhi wizarani, wizara ya ardhi makao makuu kwa Dar es salaam na kwa mikoani maombi hayo mara nyingi huenda makao makuu ya mkoa ambapo katika maombi hayo mnunuzi anaiomba mamlaka ya ardhi imjulishe mambo yafuatayo;
( a ) KUJUA JINA LA MMILIKI HALALI WA NYUMBA/KIWANJA.
Kwanza kujua jina la mmiliki. Jina hili linatakiwa kufanana sawasawa bila tofauti yoyote na yule mtu anayetaka kukuuzia eneo. Hii husaidia kuthibitisha kuwa anayeuza ndiye kweli mmiliki wa eneo.Kama majina yatatofautiana basi haraka sana achana na hilo eneo ili kuepuka mgogoro.
( b ) KUJUA KAMA NYUMBA/KIWANJA UNACHONUNUA KIMEWEKWA KAMA DHAMANA YA MKOPO.
Kitu kingine unachouliza kwenye hayo maombi rasmi ni kama hiyo nyumba/kiwanja kimewekwa kama dhamana kwa ajili ya vitu kama mkopo . Wakati mwingine yawezekana mtu kukuuzia eneo ambalo limewekwa dhamana kwa mkopo wa hela nyingi tu. Na kisheria kama eneo limewekwa dhamana yule anayelimiliki kwa dhamana ndiye mwenye nalo kwa muda huo na wewe uliyenunua sheria iko wazi unakuwa umeliwa.
Ieleweke kuwa ni vigumu sana kujua kama eneo unalouziwa limewekwa dhamana au hapana ikiwa hukufanya upelelezi huu. Wakati mwingine mtu huweka dhamana eneo lake na kubaki na hati . Kwa hati ile wewe mnunuzi ni rahisi kuhadaika kuwa eneo ni lake lakini kumbe ni eneo lenye deni kubwa. Ukinunua eneo kama hilo utakuwa umenunua mgogoro mkubwa ambao wewe mnunuzi kushindwa na kunyanganywa ulichonunua ni lazima tu.
( c ) KUJUA KAMA KUNA MGOGORO WA KIFAMILIA.
Kitu kingine ambacho utaomba kujua katika yale maombi ni kama kuna mgogoro wowote wa kifamilia kama migogoro ya mirathi, migogoro ya kindoa ambapo mwanandoa mmoja anaweza kuwa ameweka zuio kuhusu uuzwaji wowote wa nyumba/kiwanja hicho. Usipofanya upelelezi huu utanunua halafu siku ya kubadilisha jina ndio siku utajua kuwa eneo lile lilikuwa haliruhusiwi kuuzwa.
Aidha ifahamike kuwa mamlaka za ardhi hupata taarifa hizi za viwanja vya watu kupitia utaratibu wa mazuio uitwao CAVEAT.
( 3 ) MNUNUZI WA ENEO LENYE LESENI YA MAKAZ I AKAFANYE UPELELEZI WAPI.
Maeneo yenye leseni za makazi maombi haya ya upelelezi wa kiwanja/nyumba yanapelekwa manispaa. Manispaa inayohusika ni ile ambayo lilipo eneo husika . Kwa mfano ukitaka kununua eneo kinondoni manispaa ya kinondoni ndiyo inayopelekewa maombi, kama eneo unalotaka kununua lipo temeke basi manispaa ya temeke ndio ipelekewe maombi. Aidha kuhusu mpangilio wa maombi na kile unachotaka kujua kuhusu eneo ni kama nilivyoeleza hapo juu kwenye hati .
( 4 ) MAENEO AMBAYO HAYANA HATI, LESENI ZA MAKAZI UPELELEZI HUFANYIKAJE.
Kwakuwa maeneo ya namna hii yanakuwa hayana nyaraka yoyote maalum katika mamlaka za serikali basi wakati mwngine huleta ugumu kidogo katika kujua ukweli ili kuepuka mgogoro. Lakini kitu ambacho huwa tunashauri katika maeneo ya hivi ni kuwa kwanza muuzaji akueleze eneo alilipataje. Kama alilinunua kwa mtu ni vema akaonesha ule mkataba alionunulia na kama mauzo yatafanyika basi ni lazima mnunuzi apate kopi ya ule mkataba.
Pili kama amelirithi ni lazima aoneshe fomu ya usimamizi wa mirathi ambayo ndiyo itakuwa inampa mamlaka ya kuuza. Na kama alipewa zawadi basi aonesha waraka wa zawadi ( deed of gift) ambao umesajiliwa.
Jingine la msingi sana katika maeneo yasiyo na hati wala leseni za makazi huwa ni kuuliza majirani.
Eneo unalonunua kama wapo majirani hebu waulize tu kwa nia njema na mara nyingi ukiwapata wawili watatu hivi ni rahisi kupata ukweli au kukuwezesha kujenga shaka. Na majirani usiwaulize kwa pamoja, mtafute mmoja mmoja kila mtu kwa muda wake ili kuepusha kuoneana haya katika kusema ukweli. Pia hakikisha wakati wa kuwahoji majirani muuzaji asiwepo, we tafuta tu muda wako nenda peke yako na pata taarifa. Uwepo wa muuzaji unaweza kuingilia( influence) ukweli. Usikurupuke utalia, ni hayo kwa leo.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241
bashiryakub@ymail.com
2 comments:
tunashukuru kwa nakala nzuri uliyo iandika lakini bado cjafahahu huo uchunguzi wa eneo ambalo limewekwa dhamana au mgogoro naanzia kuufanyia wap, nitanfulize shukurani zangu
tunashukuru kwa nakala nzuri uliyo iandika lakini bado cjafahahu huo uchunguzi wa eneo ambalo limewekwa dhamana au mgogoro naanzia kuufanyia wap, nitanfulize shukurani zangu
Post a Comment