Monday, January 26, 2015

MAKALA YA SHERIA: JE UMEFUNGUA/UNATAKA KUFUNGUA KAMPUNI, JIFUNZE KAMPUNI YAKO INAVYOTAKIWA KULIPA KODI KISHERIA

Na   Bashir   Yakub

Vijana wengi  wajasiriamali wadogo wamefungua makampuni. Hakika wote waliofanya  hivi  wamefanya  jambo jema  linaloendana  na  wakati. Niliwahi kuandika wakati  nikielekeza namna nyepesi  kabisa  ya  kufungua kampuni kuwa,  ni  vigumu kwa leo kufanya biashara  na  ukawa  na  mafanikio nje ya  kampuni. Nikasema hata kama unauza maziwa, mama ntilie, unauza mayai, kibanda cha huduma ya fedha kupitia simu,unauza mihogo, haizuiwi kufungua kampuni. 

Kuna kampuni   hata  za mtaji wa milioni moja  na  pesa hiyo si lazima uwe nayo mkononi  ila  ni  katika maandishi   tu. Nikasema anayetaka mafanikio  kwa sasa ahakikishe hiyo biashara yake ndogo kabisa anaifungulia kampuni. 

Kwakuwa wapo wengi ambao tayari  wamefungua  makampuni  basi zipo  changamoto nyingi wanazokumbana  nazo  na kubwa zaidi ni  taarifa au ujuzi wa mambo mbalimbali  ya  namna  ya kuendesha kampuni  ili kampuni  iwe kampuni  kweli. 

Moja ya eneo lenye shida au ambalo  wajasiriamali  wadogo hawana taarifa  nzuri  kuhusu ni taarifa za kodi  zinavyolipwa  na kampuni kisheria. Hawajui  ni kiasi gani, kwa muda gani  na  vipi. Leo hapa nitaeleza kwa  uchache  kuhusu  kodi  za kampuni. Kampuni hulipa  kodi ya mapato,  swali ni  kodi  ya  mapato nini.

1. KAMPUNI  HULIPA  KODI  YA  MAPATO, JE  KODI  YA  MAPATO  NINI ?

Kodi ya mapato Tanzania ni tozo kwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  inayotokana na vyanzo vitatu ambavyo ni ajira, biashara pamoja na uwekezaji. Aina hii ya kodi inatozwa kwa mamlaka ya Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004, kama ilivyorekebishwa.Kwa upande wetu wa kampuni  kodi inayolipwa kwa tafsiri hiyo hapo juu ni kwakuwa kampuni ni biashara na pia ni kwakuwa ndani kampuni waweza kuwamo uwekezaji.Hii ndio sababu kampuni hulipa kodi ya mapato.

2. JE  WAJUA  KUWA   SI  KILA  KAMPUNI   HUTAKIWA  KULIPA  YA  MAPATO.

Mjasiriamali  anatakiwa  kujua kuwa si kampuni zote hutakiwa kulipa kodi ya mapato. Kampuni zinazotakiwa kulipa kodi ya mapato ni kampuni zenye  Dhima ya  ukomo. Kampuni zenye dhima ya ukomo ni zile zote ambazo  ni Limited. Kama kampuni yako ni Limited (LTD) basi inatakiwa kulipa kodi ya mapato. Nyingine zinazotakiwa kulipa kodi ni kampuni za kudumu za ndani  na matawi  ya  Kampuni za wageni/wasio wakazi. Hizi hazihusiki na wajasiriamali sitazifafanua  zaidi.

Aidha,kama kampuni umeiunda na umeingia ubia  na kampuni  nyingine basi hutakiwi kulipa kodi ya mapato.

3. USIOGOPE KODI  HUTOZWA  KATIKA  FAIDA TU NA SI KUTOKA  KILA FEDHA    UNAYOINGIZA.

Kodi  ya mapato ya kampuni hutozwa kwenye faida tu iliyotokana na shughuli za biashara  za kampuni  au faida uliyoipata kutokana  na uwekezaji. Umeunda kampuni umempata mtu ana mtaji akawekeza mtaji, faida inayopatikana hapo ndiyo faida  kutoka  katika  uwekezaji. Ifahamike kuwa si kweli kuwa kila unachoingiza lazima kilipe kodi. 
4. JE  MAMLAKA  YA  MAPATO WANAJUAJE  FAIDA  ULIYOPATA  ILI  WAKUTOZE KODI  SAHIHI.

Hapo juu tumeona kuwa faida tu ndio hutozwa kodi ya mapato lakini tujiulize swali, biashara unafanya wewe ,akaunti za kampuni unazo wewe, kila kitu kuhusu kampuni yako ni wewe, je hawa watu wa mapato wanajuaje  faida unayopata ili wakutoze kodi sahihi .Kuna yafuatayo ;

( a )  Kuna kitu kinaitwa utangazaji wa Mapato na Kodi ambacho ni tamko linalowasilishwa TRA kuonesha mapato na kodi inayopaswa kulipwa kwa kila mwaka wa mapato. Kwa mujibu wa sheria ya kodi, kampuni inalazimika kuwasilisha makisio hayo hata kama haina  faida. Wewe mwenyewe unajitathmini umepata nini na unatakiwa kulipa nini na unapeleka mwenyewe makadirio hayo. Kinyume chake ni kosa na asiyefanya  hivyo  adhabu  inamsubiri.

( b ) Hesabu za makadirio hayo  unayopeleka TRA lazima ziwe zimefanywa na mhasibu ambaye anatambuliwa na bodi ya uhasibu Tanzania na kukaguliwa na mkaguzi wa hesabu anayetambulika pia. Hawa ndio wanaotegemewa na TRA kupeleka ukweli wa umepata faida kiasi gani na unatakiwa ulipe kiasi gani. Ndio maana wanaitwa wahasibu wanaotambulika.

5. KODI  YA KAMPUNI  NI  30%  TU  YA  FAIDA.

Kiwango kinachotumika cha kodi ya mapato ya kampuni ni kukatwa asilimia 30 ya faida, na kwa kawaida hulipwa katika hatua mbili. Kodi ya kwanza hulipwa kulingana na makadirio ya mlipa kodi mwenyewe mwanzo wa mwaka wa biashara kama nilivyoonesha hapo juu, na kodi ya mwisho hulipwa baada ya utathmini rasmi wa mapato kamili mwisho wa mwaka wa mapato. 

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.    0784482959,         0714047241                bashiryakub@ymail.com

2 comments:

Unknown said...

UBARIKIWE SANA MTUMISHI WA BWANA KWA ELIMU NZURI KAMA HII.
MUNGU AKUONGEZEE HEKIMA NA MAARIFA.
AKUJAALIE AFYA NJEMA DAIMA!

Unknown said...

Je ni aina hii tu ya kodi inayokipwa na makampuni? Na je kama kodi iliyolipwa kwenye mwanzo wa mwaka sijafanikiwa kufikisha yale mauzo kadalio mwisho wa mwaka, je vipi pesa hiyo niliyolipa infanywaje?