Na Mwandishi Wetu
Mbunge wa Bumbuli na
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Habari na Masoko ya Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) ambaye hivi karibuni pia ametangaza nia ya kugombea Urais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa January
Makamba(Pichani juu) hivi karibuni ameainisha adhma yake ya kuinua kiwango cha michezo
nchini.
Azma hizo zimo katika katika mazungumzo yake na Padre Privatus
Karugendo ambayo yamechapishwa katika kitabu ambacho gazeti hili imekipata nakala
yake ambapo ameainisha azma ya kujenga vitua vya michezo vya kanda vyenye hadhi
ya kiolimpiki.
Kwenye kitabu hicho,
Makamba amejibu swali kwamba kitu gani kifanyike ili Watanzania waweze
kujivunia wanamichezo wao. Makamba alisema, “Inafedhehesha sana kuona kwamba
asilimia 79 ya Watanzania walikuwa hawajazaliwa mara ya mwisho tumeshiriki
katika fainali za kombe la mataifa ya Afrika.
Mwaka huo huo wa 1980
ndio mara ya kwanza na ya mwisho tuliweza kushinda medali za Olimpiki. Rafiki
yangu Mzee Suleiman Nyambui na Mzee wetu Filbert Bayi ndio walitutoa kimasomaso
kipindi kile. Ni muhimu kurekebisha hili.”
Ni ukweli usiopingika
kwamba Tanzania imekuwa kama kichwa cha mwendawazimu katika medani ya kimataifa
huku tasnia ya michezo ikiendelea kugubikwa na migogoro isiyokwisha. Kutokana
na migogoro hii, Tanzania inaendelea kupoteza matumaini ya kung’aa katika
medani za kimataifa.
Katika mazungumzo hayo na
Padre Karugendo, Makamba alinukuliwa akisema,
“Lazima tutambue kwamba maendeleo ya michezo yanatokana na vitu muhimu vitatu.
Kwanza, ni lazima kuwepo na vipaji, bahati nzuri nchi yetu ina vipaji vya
kutosha katika aina zote za michezo. Pili, ni miundombinu na mfumo wa kubaini
na kuviendeleza vipaji hivyo, hii bado
ni changamoto . Tatu, ni utawala, uongozi, na uendeshaji wa tasnia ya michezo,
hii pia ni changamoto. Hivi vitu vitatu ni lazima viwepo ili tuweze kupata
mafanikio kwenye medani ya michezo.”
Kama mgombea wa kwanza
kutangaza nia yake ya kugombea nafasi ya Urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba
mwaka huu, Makamba anaungwa mkono na vijana wengi kutokana na kuendesha siasa
zake kisasa, kibunifu na kuepuka malumbano ya jukwaani.
Katika mazungumzo hayo Makamba
alielezea fikra zake alizonazo hasa hasa kwenye kuendeleza vipaji vya
Watanzania ambapo alisema, “Ni lazima tuanzishe vituo vikubwa vya michezo au ‘sports
academies’ kwenye kila kanda ya nchi yetu vyenye hadhi ya Kiolimpiki.”
Makamba aliongeza kwamba, “Kutakuwa na vituo sita vya aina hii katika
nchi yetu ambavyo vitazungukwa na shule za msingi na sekondari za ‘boarding’.
Vituo hivi vitakuwa na lengo la kukusanya wanafunzi wote kwenye kanda husika
ambao wameonekana kuonyesha vipaji ambavyo vinapaswa kuendelezwa. Ukweli ni
kwamba bila kuendeleza vipaji katika mazingira mazuri, basi tusahau kabisa
kufanya vizuri kwenye michezo. Hili linaweza kufanywa kwa ushirikiano wa
serikali na sekta binafsi”.
Mheshimiwa January
Makamba anakuwa mgombea wa kwanza wa Urais kuweka bayana mipango yake ya
Tanzania Mpya katika maandishi. Anaendelea kufunguka kwamba katika tasnia ya
michezo ni muhimu sana kuwekeza katika watoto. Zaidi ya hapo, kila timu ya ligi
kuu ni lazima iwe na akademi na TFF iendeshe ligi kuu ya timu za watoto.
“Tufikie wakati ambapo timu za taifa za miaka
10 ijayo ziwe zinaandaliwa kuanzia sasa, na serikali itenge bajeti kila mwaka
kwa timu hizo ili kuziwezesha kukaa
kambini, kufanya mechi za majaribio na kuziwezesha kushiriki kikamilifu katika
mashindano ya kimataifa. Mimi sio muumini wa hizi kamati za zimamoto kusaidia
timu ishinde ghafla ghafla wakati siku zote watu hawafanyi maandalizi ya muda
mrefu” alimalizia Makamba.
Makamba pia aligusia
kuhusu suala la ukata na ufinyu wa bajeti unaokabili tasnia za michezo. Siku
zote tunaona timu za taifa za olimpiki au jumuiya ya madola kukosa fedha za
kukaa kambini ambapo huchangia katika matokeo hafifu.
“Huko nyuma, taasisi na
mashirika ya umma yalikuwa na timu za michezo zilizokuwa zinafanya vizuri na
kutoa michango kwenye maendeleo ya michezo. Kwa mfano, Pamba ya Mwanza, Sigara,
Reli ya Morogoro, ushiriki huu ulichangamsha sana michezo na ni lazima
turudishe utamaduni huu,” alimalizia Makamba.
1 comment:
Give thankx mawazo c mabaya
Post a Comment