Monday, January 5, 2015

Ajali za barabarani zapungua nchini - Kamanda Mpinga

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Kamanda Mohammed Mpinga(kulia)akiongea na waandishi wa habari hivi karibuni kuhusiana na maswala ya usalama barabarani,anaeshuhudia kushoto Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Umma wa Vodacom Tanzania, Rosalynn Mworia.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Kamanda Mohammed Mpinga amesema katika mahojiano maalum kuwa madereva wameanza kuelewa kuwa tabia ya kuongea na simu au kutuma na kupokea ujumbe wa maneno (SMS) wanapokuwa wanaendesha vyombo vya moto ni uvunjaji wa sheria za barabarani.

Kampeni hii ya usalama barabarani ya kuwataka madereva nchini kuzingatia sheria za usalama barabarani ilizinduliwa hivi karibuni na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Mathias Chikawe hivi karibuni na sasa imeanza kuonyesha mafanikio.

“Tangu kuanza  kampeni hii ambayo tayari imefanyika katika mikoa mbalimbali ujumbe umeanza kuwafikia madereva kwa kuwa wanapokuwa wanatumia simu na kuwaona askari wa usalama barabarani wanashtuka na kuacha kuzitumia. Hii inadhihihirisha kuwa wameanza kuelewa kuwa ni kosa kufanya hivyo na tutazidi kuwapatia elimu na wanaovunja sheria kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria,” alisema Kamanda Mpinga.

Alisema madereva wakizingatia sheria za barabarani  kwa kiasi kikubwa ajali zinazoendelea kutokea kila siku zitapungua  na aliipongeza kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania kwa kuunga mkono jitihada za serikali katika kupambana na tatizo hili ambalo limekuwa sugu .

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Umma  wa Vodacom Tanzania, Rosalynn Mworia, alisema Vodacom itaendelea  kushirikiana na serikali kuunga mkono jitihada za kuondoa  matatizo kwenye jamii kama lilivyo tatizo hili la ajali ili kuhakikisha wananchi wanaishi maisha murua na marefu. “Tunatoa rai kwa madereva wote kuzingatia kauli mbinu ya Wiki ya Nenda Kwa Usalama barabarani mwaka huu isemayo ‘Maamuzi yako barabarani ni hatma yetu - Fikiri kwanza’.”

Aliongeza kuwa Vodacom itakuwa mstari wa mbele kuelimisha jamii athari za kuendesha gari wakati huo huo unatumia simu  ya mkononi  kupitia kampeni  ya "Wait to Send" pia itaendelea kuhamasisha madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Alisema kampeni hii itaendelea kufanyika katika mikoa mbalimbali nchini ili ujumbe uwafikie madereva wengi ambako hadi kufukia sasa imeshafanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Pwani, Morogoro, Dodoma,Singida na Shinyanga.

Katika kampeni hizi wafanyakazi wa Vodacom kwa kushirikiana na askari wa  usalama barabarani  na wajumbe wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani wamekuwa wakifanya uhamasishaji kwa madereva kuacha kuongea na simu wanapoendesha vyombo vya moto na kuwagawia madereva pete maalum za kuwatahadharisha kutotuma ujumbe wa simu za mkononi wanapokuwa wanaendesha vyombo vya moto pamoja na zoezi la kupima madereva kubaini kama wanatumia vilevi linafanyika ambapo wadereva wanaokutwa wanaendeshwa vyombo vya moto wanachukuliwa hatua kali za kisheria.

Baadhi ya madereva na abiria ambao wameshuhudia  kampeni hii ikifanyika  katika sehemu  mbalimbali wamesema ni ya muhimu na itasaidia kupunguza ajali nchini. “Hivi sasa ajali nyingi zinazotokea hapa nchini zinasababishwa na uzembe wa madereva,kampeni hizi zikiendelea zitapunguza ajali kwa kiasi kikubwa,” alisema Bi. Zainab Khalfan mkazi wa Singida.

Naye James Mshiu mkazi wa Dar es Salaam alilipongeza Jeshi la Polisi na wadau wa kampeni hii kuwa kwa kiasi kikubwa imepunguza matukio ya ajali katika msimu wa Krismas na mwaka mpya. “Katika miaka iliyopita kumekuwepo na matukio mengi ya ajali katika msimu wa sikukuu ya Krismas na Mwaka Mpya lakini mwaka huu uhamasishaji wa kuzingatia sheria  za barabarani uliofanyika katika kipindi hiki kwa kiasi kikubwa umepunguza matukio ya ajali za barabarani,” alisema.

No comments: