Na Bashir Yakub
Katika adhma ya ya mwendelezo wa makala za namna ya kuendesha
kampuni leo tena tuangalie kuhusu hisa
na hasa namna ya kuhamisha hisa.
HISA
NININI.
Kwa maana ambayo inaweza kueleweka kwa
wepesi zaidi ni kusema kuwa hisa ni aina ya maslahi ya mtu ya katika kampuni.Natumia
neno aina kwakuwa maslahi katika kampuni ni mengi si hisa tu isipokuwa hisa ni
mojawapo ya maslahi. Hivyo kile ambacho mtu anamiliki katika kampuni ndio hisa zake. Hisa hutofautiana kutokana na
uwezo wa mtu kwa maana wapo wenye hisa ndogo wapo wenye kubwa na kati.
KUUZA NA
KUNUNUA HISA.
Hisa ni mali inayohamishika. Ni mali sawa na mali nyingine zozote zinazohamishika.
Kama ambavyo mali
nyingine zinaweza kununuliwa au kuuzwa, kutolewa zawadi na kurithiwa ndivyo pia
hata hisa zinavyoweza kuwa.Hii yote huitwa kuhama kwa hisa. Kuhama kwa hisa kwa
lugha ya kitaalam ambayo ndio hutumika
katika katiba za makampuni ni ( Transfer of shares). Mara nyingi suala la kuuziana hisa linawahusu wanahisa wenyewe na
hivyo wanahisa wanapokuwa wameuziana
hisa au wamepeana zawadi ni lazima
nyaraka inayoonesha muamala huo wa mauziano au zawadi ambayo ina muhuli wa
wakili iwasilishwe kwenye uongozi wa
kampuni kwa ajili ya kusajiliwa. Kama hakuna nyaraka yoyote iliyowasilishwa mbele ya
kampuni kuthibitisha uhamisho ni kosa kampuni kusajili uhamisho au mauziano
hayo.
KAMPUNI
KUKATAA MAUZIANO
Pamoja na hayo kampuni inao uwezo wa
kukataa mauziano ya hisa. Sababu zinazoweza kuifanya kampuni ikatae uhamisho ni
pamoja na iwapo taratibu za uhamisho
zimekiukwa kwa mfano nyaraka ya mauziano
haina muhuli wa wakili, pia kampuni yaweza isitambue uhamisho wa hisa iwapo mtu anayepewa hisa ambaye sasa ndo anaingia
katika kampuni wanahisa wengine hawamtaki
. Na hili zaidi linawezekana katika
makampuni binafsi ambako mtu hawezi kuwa
mmoja wa wanakampuni bila ridhaa ya
wenzake aliowakuta. Au kama ni suala la
kifo na hisa inabidi zihamishwe kwenda
kwa msimamizi wa mirathi pia wanahisa
wanaweza wakamkatalia.Haya yote ni mazingira ambamo uhamisho wa hisa unaweza
kukataliwa na kampuni. Wakati kampuni itapokataa uhamisho wa hisa itatakiwa
ndani ya siku sitini kutoa taarifa ya maandishi kwenda kwa mtu aliyekuwa amewasilisha nyaraka ya
kuuziwa,kuuza au kurithishwa kwenye kampuni.Taarifa ya maandishi
itamtaarifu kukataliwa kwake ikiwa ni pamoja
na sababu za kukataliwa huko. Kukataa kwa kampuni hapa inamaanisha kukataa kwa wakurugenzi.
Sheria imewapa wakurugenzi mamlaka ya kumkatalia yoyote na hata bila kutoa sababu za kukataa.
KAMPUNI KUKUBALI MAUZIANO.
Aidha kama
aliyepewa hisa atakuwa amekubaliwa basi moja kwa moja atapewa cheti cha
umiliki wa hisa(certificate of share) kikieleza kiasi cha hisa anazomiliki
ikiwa ni pamoja na tarehe ambayo ameanza umiliki. Aliyepewa hisa ataingizwa
katika kumbukumbu za kampuni na atawajibka kwa masharti yaleyale kama
aliyokuwa akiwajibikia yule aliyemuuzia,
aliyempa zawadi au aliyemrithisha. Pamoja na hayo ikiwa ni suala la
kuhamisha hisa kwa njia ya kutoka kwa marehemu kwenda kwa msimamizi wa mirathi basi ni
lazima kwa msimamizi wa mirathi kuleta hati ya usimamizi wa mirathi kutoka
mahakamani ili kuthibitisha uhalali wa kuhamishiwa hisa na iwapo atafanikiwa kufanya
hivyo na akakubaliwa na kampuni basi atakuwa na haki sawa na haki alizokuwa
nazo marehemu ikiwa ni pamoja na kuuza
ikiwa atataka kufanya hivyo.
KUGUSHI KATIKA
MAUZIANO
Lipo jambo jingine ambalo huwa linajitokeza
sana katika
kuuziana hisa ambalo ni kughushi. Mara nyingi muhuri sahihi au hata tarehe huwa
vinaghushiwa ili kutimiza malengo fulanifulani. Juzijuzi katika sakata la ya Escrow hili limejitokeza sana . Hata kipindi cha Richmond na EPA kughushi katika kuuziana hisa kulijitokeza.
Nje ya kuwa kosa la jinai katika Kanuni za Adhabu(Penal Code) katika masuala ya kampuni pia lina athari
zifuatazo ;Kwanza mauziano hayo yanakuwa haramu na aliyenunua hawezi kuhesabika
kama mwanahisa katika kampuni. Pili, kama kuna
uzembe kampuni ilifanya mpaka mtu
kuuziwa hisa ghushi kampuni itatakiwa kumlipa
mnunuzi fidia pamoja na gharama, na tatu
kama kampuni haikufanya uzembe isipokuwa ni mtumishi fulani au mwanahisa
basi huyohuyo atalazimika kurudisha hasara
za kampuni ilizopata katika kulipa fidia
kwa muathirika. Wiki ijayo tena katika mwendelezo wa namna ya kuendesha
kampuni.
MWANDISHI
WA MAKALA HAYA
NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA
MASUALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA
HABARI LEO KILA JUMANNE, GAZETI JAMHURI JUMANNE
NA NIPASHE JUMATANO.
0784482959
0714047241
bashiryakub@ymail.com
No comments:
Post a Comment