Tuesday, December 23, 2014

Tuache kufanya kazi kwa mazoea - Kairuki

Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Fanuel Mbonde akijaribu baiskeli ya mazoezi aliyokabiodhiwa kama zawadi katika hafla ya kuwapongeza watumishi wa Wizara waliostaafu iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Angellah Kairuki na kulia ni Katibu Mkuu Bi. Maimuna Tarishi.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Angellah Kairuki (kushoto) akimkabidhi zawadi Mtunza Kumbukumbu Mstaafu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Clara Mlamlyingu katika hafla ya kuwapongeza watumishi wa Wizara waliostaafu iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. Kushoto kwa Bi. Mlamlyingu ni Katibu Mkuu Bi. Maimuna Tarishi na kulia ni Jaji Dkt. Gerrald Ndika, Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania.
Watumishi Wastaafu wa Wizara ya Katiba na Sheria wakiwa na vyeti vyao katika picha ya kumbukumbu na viongozi wa Wizara wakiongozwa na Naibu Waziri Mhe. Angellah Kairuki na Katibu Mkuu Bi. Maimuna Tarishi. Hafla ya kuwapongeza ilifanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Fanuel Mbonde akikabidhiwa cheti na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria katika hafla ya kuwapongeza watumishi waliostaafu iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. Kushoto kwa Katibu Mkuu Mstaafu ni Katibu Mkuu Bi. Maimuna Tarishi.
Baadhi ya watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria wakisakata rhumba katika hafla ya kuwapongeza Watumishi waliostaafu iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. (Picha: Wizara ya Katiba na Sheria).

Na Mwandishi Wetu

Watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria wakumbushwa kuwa chachu ya mabadiliko katika utumishi wa umma na kuondokana na utendaji kazi wa mazoea kwa kila mtumishi kufanya kazi kwa malengo yenye kutoa matokeo yanayopimika.

Akizungumza katika hafla ya kuwaaga watumishi waliostaafu katika Wizara hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Angellah Kairuki amesema utendaji kazi wenye kujali matokeo unawezekana na kuwataka watumishi wote kubadilika kimtazamo na kifikra ili kufikia lengo hilo.

Watumishi waliostaafu na kuagwa katika hafla hiyo ni Bw. Fanuel Mbonde aliyekuwa Katibu Mkuu. Bi. Christina Sonyi (Mkurugenzi wa Sera na Mipango), Bi. Anna Mayawalla (Mkurugenzi Msaidizi – Sera), Bi. Mariam Mwaisabila (Mtunza Kumbukumbu Mkuu Msaidizi), Bi. Giditha Peter (Mwendeshaji Mkuu wa Mifumo ya Kompyuta) na Bi. Clara Mlamyingu aliyekuwa Mtunza Kumbukumbu Mkuu Msaidizi.

Akifafanua, Naibu Waziri Kairuki amesema ni muhimu kwa watumishi wote kujenga uelewa wa pamoja wa majukumu ya Wizara ya kupanga mkakati wa kuyatekeleza kwa ushirikiano.

“Hatuna budi kujenga uelewa wa pamoja wa majukumu tuliyonayo katika Wizara yetu na kujenga ushirikiano wa hali ya juu. Tunapaswa kuondokana na utendaji kazi wa mazoea, lazima ukome sasa. Kila mmoja wetu kwa nafasi yake anapaswa kufanya kazi kwa malengo yenye kutoa matokeo,” amesema Kairuki katika hafla iliyohudhuriwa na Katibu Mkuu Bi. Maimuna Tarishi, wastaafu na watumishi wengine wa Wizara hiyo na wawakilishi wa taasisi zilizo chini ya Wizara.

Kuhusu watumishi waliostaafu, Naibu Waziri Kairuki amesema watumishi wote waliostaafu wanapaswa kupongezwa na kutimiza wajibu wao kwa uadilifu, umoja na ushirikiano hadi kufikia hatua ya kustaafu kwa mujibu wa sheria.

“Katibu Mkuu alitufanya sote kujisikia kama timu moja iliyolenga kutekeleza majukumu ya Wizara kwa ufanisi huku ikizingatia maslahi ya watumishi. Kipekee, ninamshukuru sana kwa uongozi wake katika Wizara hii ambao umeweka misingi ambayo sisi viongozi tuliopo tunaisimamia, tunaiendeleza na kuiboresha,” alisema Naibu Waziri Kairuki na kuongeza:

“Katibu Mkuu huwa hafanyi kazi peke yake. Ana Timu. Nyie wote kwa umoja wenu ndiyo timu yake. Na kama mnavyofahamu, mchezaji mmoja akiwa mzembe basi timu yote inaathirika. Kwa msingi huo, Ndugu Mbonde alikuwa na timu ambayo baadhi ya wachezaji wake ni wastaafu tunaowaaga leo na sisi tunaoendelea na utumishi,” aliongeza Mhe. Kairuki.

Aidha, Naibu Waziri Kairuki alitumia hafla hiyo kuwakumbusha watumishi kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa likiwemo la kushiriki katika Kura ya Maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa na mapambano dhidi ya UKIMWI.

“Sisi kama watumishi wa Wizara yenye dhamana ya mambo ya Katiba na Sheria, tunapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuisoma, kuielewa na hatimaye kushiriki katika kupigia Kura ya Maoni Katiba Inayopendekezwa ifikapo tarehe 30 Aprili mwakani (2015)” alisema na kuongeza watumishi wa Wizara wanapaswa kuwa waangalifu na kujikinga na maambuikizi ya virusi vya UKIMWI.

“Sote tunajua jinsi janga hili linavyoathiri nguvu-kazi ya taifa na hata familia zetu. Sidhani kama kuna mtu kati yetu ambaye hajaguswa na tatizo hili. Wito wangu ni kuwa waangalifu na kujikinga na maambukizi. Kwa wale wanaoishi na virusi, Serikali itaendelea kuwahudumia kwa mujibu wa miongozo iliyopo,” alifafanua.

Akizungumza kwa niaba ya Wastaafu, Katibu Mkuu Mstaafu Mbonde aliwashukuru watumishi wa Wizara kwa kutambua mchango wake na watumishi wastaafu wengine na kuahidi kutoa ushirikiano pale utakapohitajika.

“Sisi tupo na ujuzi wetu, wakati wowote mtakapoona mnatuhitaji tuwasiliane na tupo tayari kutoa mchango wetu ili kufanikisha majukumu ya Wizara,” alisema Bw. Mbonde.

Kuhusu maadili, Katibu Mkuu huyo Mstaafu aliwakumbusha watumishi kuzingatia maadili na kuepuka vitendo vya rushwa ili kulinda heshima ya Wizara na utumishi wa umma.

No comments: