Na Bashir Yakub
Katika adhima ya ya mwendelezo wa makala za namna ya kuendesha kampuni leo tena tuangalie kuhusu hisa na hasa namna ya kuhamisha hisa.
HISA NININI.
Kwa maana ambayo inaweza kueleweka kwa wepesi zaidi ni kusema kuwa hisa ni aina ya maslahi ya mtu ya katika kampuni.Natumia neno aina kwakuwa maslahi katika kampuni ni mengi si hisa tu isipokuwa hisa ni mojawapo ya maslahi. Hivyo kile ambacho mtu anamiliki katika kampuni ndio hisa zake. Hisa hutofautiana kutokana na uwezo wa mtu kwa maana wapo wenye hisa ndogo wapo wenye kubwa na kati.
KUUZA NA KUNUNUA HISA.
Hisa ni mali inayohamishika. Ni mali sawa na mali nyingine zozote zinazohamishika. Kama ambavyo mali nyingine zinaweza kununuliwa au kuuzwa, kutolewa zawadi na kurithiwa ndivyo pia hata hisa zinavyoweza kuwa.Hii yote huitwa kuhama kwa hisa. Kuhama kwa hisa kwa lugha ya kitaalam ambayo ndio hutumika katika katiba za makampuni ni ( Transfer of shares). Mara nyingi suala la kuuziana hisa linawahusu wanahisa wenyewe na hivyo wanahisa wanapokuwa wameuziana hisa au wamepeana zawadi ni lazima nyaraka inayoonesha muamala huo wa mauziano au zawadi ambayo ina muhuli wa wakili iwasilishwe kwenye uongozi wa kampuni kwa ajili ya kusajiliwa. Kama hakuna nyaraka yoyote iliyowasilishwa mbele ya kampuni kuthibitisha uhamisho ni kosa kampuni kusajili uhamisho au mauziano hayo.
KAMPUNI KUKATAA MAUZIANO
Pamoja na hayo kampuni inao uwezo wa kukataa mauziano ya hisa. Sababu zinazoweza kuifanya kampuni ikatae uhamisho ni pamoja na iwapo taratibu za uhamisho zimekiukwa kwa mfano nyaraka ya mauziano haina muhuli wa wakili, pia kampuni yaweza isitambue uhamisho wa hisa iwapo mtu anayepewa hisa ambaye sasa ndo anaingia katika kampuni wanahisa wengine hawamtaki . Na hili zaidi linawezekana katika makampuni binafsi ambako mtu hawezi kuwa mmoja wa wanakampuni bila ridhaa ya wenzake aliowakuta. Au kama ni suala la kifo na hisa inabidi zihamishwe kwenda kwa msimamizi wa mirathi pia wanahisa wanaweza wakamkatalia.Haya yote ni mazingira ambamo uhamisho wa hisa unaweza kukataliwa na kampuni. Wakati kampuni itapokataa uhamisho wa hisa itatakiwa ndani ya siku sitini kutoa taarifa ya maandishi kwenda kwa mtu aliyekuwa amewasilisha nyaraka ya kuuziwa,kuuza au kurithishwa kwenye kampuni.Taarifa ya maandishi itamtaarifu kukataliwa kwake ikiwa ni pamoja na sababu za kukataliwa huko. Kukataa kwa kampuni hapa inamaanisha kukataa kwa wakurugenzi. Sheria imewapa wakurugenzi mamlaka ya kumkatalia yoyote na hata bila kutoa sababu za kukataa.
KAMPUNI KUKUBALI MAUZIANO.
Aidha kama aliyepewa hisa atakuwa amekubaliwa basi moja kwa moja atapewa cheti cha umiliki wa hisa(certificate of share) kikieleza kiasi cha hisa anazomiliki ikiwa ni pamoja na tarehe ambayo ameanza umiliki. Aliyepewa hisa ataingizwa katika kumbukumbu za kampuni na atawajibka kwa masharti yaleyale kama aliyokuwa akiwajibikia yule aliyemuuzia, aliyempa zawadi au aliyemrithisha. Pamoja na hayo ikiwa ni suala la kuhamisha hisa kwa njia ya kutoka kwa marehemu kwenda kwa msimamizi wa mirathi basi ni lazima kwa msimamizi wa mirathi kuleta hati ya usimamizi wa mirathi kutoka mahakamani ili kuthibitisha uhalali wa kuhamishiwa hisa na iwapo atafanikiwa kufanya hivyo na akakubaliwa na kampuni basi atakuwa na haki sawa na haki alizokuwa nazo marehemu ikiwa ni pamoja na kuuza ikiwa atataka kufanya hivyo.
KUGUSHI KATIKA MAUZIANO
Lipo jambo jingine ambalo huwa linajitokeza sana katika kuuziana hisa ambalo ni kughushi. Mara nyingi muhuri sahihi au hata tarehe huwa vinaghushiwa ili kutimiza malengo fulanifulani. Juzijuzi katika sakata la ya Escrow hili limejitokeza sana. Hata kipindi cha Richmond na EPA kughushi katika kuuziana hisa kulijitokeza. Nje ya kuwa kosa la jinai katika Kanuni za Adhabu(Penal Code) katika masuala ya kampuni pia lina athari zifuatazo ;Kwanza mauziano hayo yanakuwa haramu na aliyenunua hawezi kuhesabika kama mwanahisa katika kampuni. Pili, kama kuna uzembe kampuni ilifanya mpaka mtu kuuziwa hisa ghushi kampuni itatakiwa kumlipa mnunuzi fidia pamoja na gharama, na tatu kama kampuni haikufanya uzembe isipokuwa ni mtumishi fulani au mwanahisa basi huyohuyo atalazimika kurudisha hasara za kampuni ilizopata katika kulipa fidia kwa muathirika. Wiki ijayo tena katika mwendelezo wa namna ya kuendesha kampuni.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA MASUALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE, GAZETI JAMHURI JUMANNE NA NIPASHE JUMATANO.
0784482959
0714047241
bashiryakub@ymail.com
No comments:
Post a Comment