Tuesday, December 16, 2014

Kuondoka kwa Maximo, wachezaji Yanga wamwaga chozi!

KOCHA wa Yanga, Mbrazil Marcio Maximo amewaaga rasmi leo asubuhi wachezaji wa timu hiyo kwenye mazoezi uwanja wa Sekondari ya Loyola huku akitarajia kuvuna zaidi ya Milioni 20 ndani ya klabu hiyo ikiwa ni mshahara wake wa dola 1200 na yupo kwenye harakati za kudai fidia ya kuvunjiwa mkataba na kuletwa mrithi wake kabla uongozi wa klabu hiyo haujamaliza nae.

Hata hivyo, tayari Maximo ameaga wachezaji wake kwenye mazoezi ya asubuhi leo ambapo mazoezi hayo yaligeuka shubiri baada ya Maximo  kuwakusanya wachezaji wake na kuwambia kuwa kuanzia leo  sio kocha wa timu hiyo tena na kuwatakia maisha mema ndani ya klabu hiyo ya Jangwani.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wachezaji wa klabu hiyo ambao pia hawajaridhishwa na uamuzi wa uongozi wa klabu hiyo kumuacha mshambuliaji Hamis Kiiza na kumsajili Amis Tambwe.

Mmoja wa wachezaji hao alisema  "Ni kweli kocha ametuaga asubuhi daa! ndio hivyo tumesikitika lakini hatuna jinsi."

Naye mchezaji mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema "Inaumiza sana jana (juzi) tumefanya nae mazoezi vizuri kabisa tena amechangamka kama kawaida kumbe nyuma kuna mambo yanaendelea, leo asubuhi tumeenda mazoezi kama kawaida tukijua tunafanya mazoezi matokeo yake anasema acheni kila kitu kaeni hapo nataka kuzungumza na nyinyi.

"Uwezi kuamini kidogo machozi yanitoke pale aliposema kuanzia leo yeye sio kocha wetu tena, dah inaumiza sana, mtu ambaye mmemzoea mnafanya nae kazi kuondoka, ndo hivyo wakubwa wemeshaamua bwana wenye timu yao.

Wakati huyo akisema hayo, mchezaji nguli wa timu hiyo yeye alisema "Hakuna mchezaji kwa kweli aliyependezwa na kitendo cha uongozi, yani kwenye mazoezi asubuhi ilikuwa kama msiba, 'mood' ya kufanya mazoezi iilisha kabisa, yani hakuna aliyekuwa na hamu ya kuendelea na mazoezi.

"Tumefanya kidogo mazoezi tukaondoka, ukiangalia ni sawa tumefungwa cha muhimu ilikuwa ni kukaa chini na kuzungumza na kuangalia cha kufanya, kama kuna mapungufu basi yafanyiwe kazi, mimi sijaona haja ya kumfukuza kocha hasa kipindi kama hichi."

Meneja wa timu hiyo Hafidhi Saleh alikiri Maximo kuaga wachezaji kabla ya mazoezi ya timu hiyo kuanza akiwapa moyo wajitume kwa kuwa ni wachezaji wazuri na timu ni nzuri na kuwataka kuongeza bidii ili wafike mbali.

"Kwa kweli inasikitisha hakuna mchezaji wala mtu aliyefurahia, kama yupo labda kimoyomoyo ila dah imetuumiza, ni mazoea cha muhimu tugange yajayo hayo mengine tuwaachie viongozi."alisema Saleh

Saleh alisema kuwa tayari kocha Hans van Der Pluijm ambaye amefikia kwenye hoteli ya Tansoma jana alikuwa kwenye mazungumzo na uongozi wa klabu hiyo ili aichukue nafasi ya mbrazil Marcio Maximo ambaye amekumbwa na kipunga cha kutimuliwa baada ya kunyukwa mabao 2-0 katika mechi ya mtani Jembe, akiwa ni kocha wa pili kutimuliwa Yanga baada ya matokeo ya mtani jembe mwaka jana alitimuliwa Ernie Brandts baada ya kunyukwa mabao 3-1 na nafasi yake kuchukuliwa na Pluijim ambaye nae hakukaa sana akaikacha timu hiyo baada ya kupata kibara nchini Saudi Arabia.

Wakati huo huo, uongozi wa Yanga umegwaya mchezaji Andry Countinouh kuvunja mkataba wake baada ya kuwa wangelazimika kuvunja kibubu cha Sh185 milioni ili kumlipa fidia ya mshahara wake ambao ni dola 2800 kwa mwezi.

Katika hatua nyingine, pamoja na Yanga kumfungashia virago Emerson De Oliveira Neves Roque imemuombea kibali cha usajili wa kimataifa (ITC) kutoka Bonsucesso Brasil kwenda Yanga.

Mkurugenzi wa mashindano ya TFF, Boniface Wambura alisema kuwa TFF haina taarifa za Yanga kumuacha mbrazili huyo.

1 comment:

Anonymous said...

YANGA ACHENI HASIRA, TATIZO SIO KOCHA TATIZO NI WACHEZAJI KUWA NA HOFU WANAPOKWENDA KUCHEZA NA SIMBA, UKITANGULIZA HOFU LAZIMA UTAFELI MTIHANI, MAKOCHA WANAJITAHIDI. NI BORA MNGEFUKUZA WACHEZAJI WOTE, MKASAJILI WAPYA, KULIKO KUFUKUZA MAKOCHA KILA MNAPOFUNGWA, HAMUONI TIMU ZA ULAYA JAMANI, WANAFUNGWA LAKINI WANAANGALIA WAPI WAMEFANYA MAKOSA ILI WAREKEBISHE, NYIE MKIFUNGWA HATA NA MTIBWA, TAYARI KOCHA HANA KAZI, PIMENI KWANZA KABLA YA KUFUKUZA, SASA KINACHOFUATA NI KUWAKATISHA TAMAA WACHEZAJI WANAPOKUWA UWANJANI, MAANA WANAJUA NAO WAKIVURUGA TU WATATIMULIWA. WAJENGEENI UWEZO WACHEZAJI WAACHE KUIOGOPA SIMBA, SIMBA NI WALE WALE, SASA KAMA WANAIOGOPA SIMBA, NGOJA KIPINDI CHA PILI CHA LIGI KUU MUJE MUONE CHA MOTO. ONDOA HOFU, MIE NI SHABIKI MKUBWA WA YANGA, LAKINI MNACHOFANYA SIO FAIR. ONDOA HOFU, HALAFU ACHENI KUTENGENEZA SIFA SANA KWENYE VYOMBO VYA HABARI, JIFUNZENI KUNYAMAZA KIMYA WATU WASHUHUDIE UWANJANI.
SIO KUJIGAMBA HOOO TUTASHINDA, SIFA HUWA SIO NZURI, SIMBA WANAPOJIGAMBA NYIE NYAMAZENI MUOMBENI MUNGU AWASAIDIE, SIO TAMBO, TAMBO NYINGI NDIZO WANAZOZITUMIA WENZENU KUWAFUNGA. BADILIKENI UONGOZI WOTE. JENGA UWEZO KWA TIMU. TAMBO MUZIACHE. KIMYA KINA MSHINDO.