Shukrani
Mheshimiwa Makamu wa Rais;
Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti wa CCM;
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Viongozi wa CCM Mkoa;
Viongozi Wenzangu;
Viongozi wa Dini;
Wazee Wangu;
Wananchi Wenzangu;
Nawashukuru sana wazee
wangu wa Dar es Salaam, kwa kukubali mwaliko wangu na kuja kuzungumza nami siku
ya leo. Natambua kuwa taarifa ilikuwa ya
muda mfupi lakini mmeweza kuja kwa wingi kiasi hiki. Naomba radhi kwamba ilikuwa tukutane Ijumaa
lakini kwa sababu zilizo nje ya uwezo wangu tukaahirisha mpaka leo. Asanteni
sana kwa uvumilivu wenu.
Kama mjuavyo, kila
ninapoomba kukutana nanyi ninalo jambo au mambo muhimu kitaifa ambayo napenda kuzungumza
nanyi, na, kwa kupitia kwenu taifa zima linapata habari. Leo nina mambo mawili.
Wazee Wangu;
Kwanza kabisa, nataka
kurudia kuwashukuru Watanzania wenzangu kwa moyo wenu wa upendo mliouonyesha
kwangu katika kipindi chote cha matibabu yangu nikiwa nje na hata baada ya
kurejea nchini. Kwa kweli nina deni kubwa kwenu. Lazima nikiri kuwa, salamu zenu na taarifa kwamba
watu wamekuwa wananiombea uponaji wa haraka na uzima zinanipa faraja kubwa na
kunitia moyo. Nadhani zimechangia sana
kuifanya afya yangu kuendelea kuimarika kila kukicha. Bado sijawa “fit” kabisa lakini naendelea vizuri. Hali yangu ilivyo sasa sivyo
ilivyokuwa wiki iliyopita au siku niliporejea nchini.
Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa
Ndugu
Wananchi;
Jambo la kwanza
ninalotaka kulizungumzia leo ni uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika
Jumapili iliyopita tarehe 14 Desemba, 2014 na jana tarehe 21 Desemba, 2014
katika maeneo ambayo uchaguzi huo uliahirishwa.
Bila ya shaka sote tumesikia taarifa ya awali ya zoezi la upigaji kura
iliyotolewa na Mheshimiwa Hawa Ghasia, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,
TAMISEMI tarehe 17 Desemba, 2014. Katika
taarifa yake hiyo, Mheshimiwa Waziri alieleza kwamba kwa jumla zoezi limeenda
vizuri kwenye maeneo mengi nchini.
Uchaguzi ulifanyika kwa ukamilifu katika Halmashauri 141 kati ya 162. Katika Halmashauri 21
uchaguzi wake uliahirishwa na umefanyika jana tarehe 21 Desemba, 2014.
Kwa jumla, katika maeneo
mengi uchaguzi ulifanyika kwa salama na amani na hivyo kuwapa wananchi fursa ya
kuchagua viongozi wanaowapenda kuongoza vijiji vyao, vitongoji vyao na mitaa
yao. Kufanyika kwa uchaguzi huu ni
uthibitisho mwingine wa kuendelea kukomaa kwa demokrasia nchini. Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi za
dhati kwa wale wote walioshiriki katika uchaguzi huu kwa maana ya vyama vya
siasa na wagombea. Natoa pongezi maalum
kwa walioshinda. Nawaomba sasa wakae
chini kutengeneza mikakati na mipango ya kuwaongoza wananchi wa maeneo yao
katika kupata ufumbuzi wa changamoto za maendeleo na za maisha, zinazowakabili.
Ndugu wananchi;
Katika taarifa yake hiyo
pia, Waziri Hawa Ghasia alielezea masikitiko yake kuhusu kasoro za uendeshaji
wa zoezi zilizojitokeza katika maeneo mbalimbali. Aidha, aliahidi kuchukua hatua stahiki za
kinidhamu dhidi ya watendaji na viongozi wa Serikali waliosababisha kasoro
hizo. Alifafanua kuwa miongoni mwa hatua
zinazoweza kuchukuliwa ni pamoja na kufukuzwa kazi, kusimamishwa kazi,
kushushwa cheo, kukatwa mshahara au kupewa onyo.
Napenda kuelezea
kufurahishwa kwangu na msimamo huo wa Waziri wa TAMISEMI na nampongeza kwa
hatua alizochukua. Namuunga mkono na
namtaka aendelee na msimamo huo katika kukabili vitendo vya utovu wa nidhamu wa
watumishi wa umma. Lazima kila mtumishi
wa umma ajue kuwa asipotimiza ipasavyo majukumu yake kuna adhabu inayolingana
na kosa alilofanya. Isitoshe, watu hao
ndio watakaoendesha na kusimamia Uchaguzi Mkuu wa mwakani wakiwa mawakala na
wasaidizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Hivyo
basi, kuwajibishwa wale waliozembea katika uchaguzi, itakuwa fundisho kwao na
kwa wengine katika uchaguzi wa mwaka 2015 na chaguzi nyingine zijazo.
Ndugu wananchi;
Kwa upande wa ghasia,
fujo na ugomvi uliotokea wakati wa zoezi la uchaguzi, nimezungumza na viongozi
wa juu wa Jeshi la Polisi na kuwataka kuhakikisha kuwa wale wote waliofanya vitendo
vya kuvunja sheria wanatiwa nguvuni na kufikishwa kwenye vyombo vya
sheria. Nimewataka wasifanye ajizi na
watu wa aina hiyo. Hawa ni watu hatari
ambao hawana budi kuchukuliwa hatua thabiti za kuwadhibiti na kuwaadabisha.
Tusipofanya hivyo tunawakatisha tamaa raia wema na watiifu wa sheria. Aidha, watu wakikamatwa na kuachiliwa muda
mfupi baadae, wakati mwingine hata bila dhamana ya namna yo yote inawachanganya
sana watu wema. Isitoshe tutakuwa
tunalea maradhi ya watu wabaya na kuwafanya waendelee kusumbua jamii. Nimewakumbusha kuwa wasipokuwa wakali sasa tunaweka mazingira ya hatari ya kuja kutokea
mambo mabaya zaidi mwaka ujao kwenye
uchaguzi mkuu.
Sakata
la Akaunti ya Tegeta ESCROW
Ndugu
Wananchi;
Jambo
la pili ninalotaka kulizungumzia si geni masikioni kwenu, nalo ni sakata la
Akaunti ya Escrow ya Tegeta. Bila ya shaka mtakumbuka kuwa wakati wa kikao cha
Bunge la Bajeti mwezi Juni, 2014, kulitolewa madai kuwa fedha zilizokuwemo katika
Akaunti ya Escrow ya Tegeta iliyoko Benki Kuu zimechotwa kinyemela na mmiliki
wa Kampuni ya Pan African Power Solution (PAP) akishirikiana na Maafisa wa
Serikali.
Serikali iliahidi kufanya mambo mawili. Kwanza, kumtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa Akaunti hiyo na kwamba taarifa yake itawasilishwa
Bungeni. Na, pili, kumuagiza Mkurugenzi
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi
wa mwenendo mzima wa miamala katika Akaunti hiyo na kama kuna uhalifu wo wote uliopo
kwenye mamlaka yake achukue hatua zipasazo kwa mujibu wa mamlaka na madaraka
aliyonayo.
Ndugu Wananchi;
Yote
mawili tuliyoahidi tumefanya. Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amefanya ukaguzi wa miamala katika
Akaunti ya Escrow ya Tegeta iliyoko Benki Kuu na taarifa yake ilishawasilishwa
Bungeni. Pia niliagiza taarifa hiyo
ichapishwe kwenye magazeti na tovuti ya Serikali ili watu waweze kuisoma. Agizo
hilo nalo limetekelezwa. TAKUKURU
wameendelea na uchunguzi wao na watakapomaliza na kuridhika kuhusu
makosa yaliyofanywa watawafikisha wahusika Mahakamani. Mkurugenzi Mkuu wa PCCB alifika kwenye Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali na kutoa baadhi ya mambo kuhusu suala
hili aliyoyaona ni muhimu Kamati iyajue.
Mambo
Manne Makuu
Ndugu
Wananchi;
Tarehe
8 Desemba, 2014 nilipoanza kazi baada ya mapumziko ya ugonjwa nilikabidhiwa
taarifa mbalimbali kuhusu sakata hili.
Tangu wakati huo nimekuwa nazisoma pamoja na kuzungumza na watu mbalimbali
na kuagiza nipatiwe ufafanuzi wa mambo mbalimbali kutoka kwa wahusika. Shabaha yangu ni kuyaelewa vizuri mambo hayo ili
niweze kufanya uamuzi ulio sahihi na wa uhakika. Nimebaini kuwa yapo mambo makuu manne:-
(a) Akaunti ya ESCROW
(b) Miliki
ya PAP kwa IPTL
(c) Kodi
za Serikali, na
(d)Tuhuma
za Rushwa
Akaunti
ya ESCROW
Ndugu
Wananchi;
Katika
Mikataba ya Kununua Umeme (Power Purchase
Agreements) ambayo TANESCO imetiliana sahihi na kampuni binafsi za
kuzalisha umeme za IPTL, SONGAS, SYMBION POWER na AGGRECO, kuna malipo ya namna
mbili yanayofanywa na TANESCO. Kwanza, hulipia
umeme ilionunua kutoka kwa kampuni hizo yaani tozo ya umeme (energy charges). Na, pili hulipia
gharama za uwekezaji uliofanywa na kampuni hizo, yaani tozo ya uwekezaji (capacity charges). Katika mikataba yote hiyo
imekubaliwa kuwa iwapo kutatokea kutofautiana, au mzozo unaohusu uwekezaji, upo
utaratibu wa usuluhishi. Utaratibu huo unataka kwanza kufanyike mazungumzo,
wakishindwa kuelewana watafute mtu wa kuwashauri na kuwasuluhisha; wakishindwa
kukubaliana wapeleke shauri lao kwenye Kituo (Mahakama) cha Kimataifa cha Usuluhisi
wa Migogoro ya Uwekezaji, (International Centre for Settlement of Investment
Disputes – ICSID) kilichopo London, Uingereza
Ndugu Wananchi;
Mwaka 1998 TANESCO
walifikisha kwenye Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji,
London, malalamiko kwamba gharama za uwekezaji za IPTL ni kubwa mno kuliko
kiasi halisi walichowekeza. Mwaka 2001
Kituo cha Usuluhisi kilifanya uamuzi wa shauri hilo. Madai ya TANESCO yalikubaliwa kuwa uwekezaji
halisi uliofanyika ni Dola za Marekani
127 na siyo Dola milioni 163.17 walizodai
IPTL. Kutokana na kupungua huko kwa
gharama za uwekezaji, tozo ya uwekezaji (capacity
charges) nayo ilipunguzwa kutoka Dola
za Marekani milioni 3.6 kwa mwezi mpaka Dola za Marekani milioni 2.6 kwa mwezi. Kituo pia, kilitoa mwongozo kuhusu ukokotoaji
wa tozo hiyo.
Ndugu Wananchi;
Miaka minne baadaye
TANESCO ilianza vuguvugu la kutaka kupata nafuu zaidi. Waliamua kugomea kulipa tozo ya uwekezaji kwa
mkokotoo wa mwaka 2001. Nimeambiwa kuwa wanasheria
wa TANESCO walishauri Shirika hilo lidai ukokotoaji kiwango cha tozo ya
uwekezaji wa IPTL ufanyike kwa kuzingatia thamani ya hisa walizolipia wawekezaji
ambayo ni shilingi 50,000 badala ya kutumia
msingi wa mtaji uliotokana na mkopo wa Dola
za Marekani milioni 38.16 wa wanahisa uliotumiwa na usuluhisho wa kwanza ICSID-1.
Wakati wakisubiri mchakato
wa usuluhishi wa mzozo huu mpya kuanza, pande zote mbili zilikubaliana
kuanzisha Akaunti ya Escrow ya Tegeta. Tarehe 5 Julai, 2006, akaunti hiyo
ikaanzishwa kwa mkataba uliyotiwa sahihi na IPTL upande mmoja na Wizara ya
Nishati na Madini kwa niaba ya TANESCO upande mwingine. Aidha, Benki Kuu iliteuliwa kuwa wakala wa
kutunza akaunti hiyo nayo ilitia sahihi.
Ndugu Wananchi;
Kwa mujibu wa mkataba
huo, Kampuni ya IPTL iliendelea kupeleka madai ya tozo ya uwekezaji kwa TANESCO
ambayo nayo iliwajibika kulipa madai hayo.
Malipo hayo yalitakiwa kupelekwa kwenye Akaunti ya Escrow ya Tegeta tofauti
na ilivyokuwa kabla ambapo yalipelekwa IPTL moja kwa moja. Utaratibu huu mpya ulikubaliwa kutumika hadi
pande mbili zitakapofikia mwafaka kuhusu kiwango cha ukokotoaji. Kwa upande wa malipo ya gharama ya umeme (energy charges) TANESCO imeendelea
kulipa moja kwa moja kwa IPTL bila kupitia Akaunti ya Tegeta ESCROW maana hizo
hazikuwa na mgogoro.
Ndugu Wananchi;
Kwa miaka saba tangu tarehe
5 Julai, 2006, akaunti hiyo ilipoanzishwa mpaka tarehe 5 Septemba, 2013, wakati
Mahakama Kuu ilipokabidhi shughuli zote za IPTL kwa PAP, hakuna hatua stahiki
zilizochukuliwa kutafuta ufumbuzi wa mzozo wa tozo ya uwekezaji baina ya ITPL
na TANESCO. Pande mbili husika
hazikuwahi kukaa kuzungumza na wala hakuna shauri lililofikishwa kwenye Kituo
cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Mogogoro ya Uwekezaji kama ilivyofanyika mwaka
1998.
Wakati
wote huo, TANESCO iliendelea kulipa madai ya tozo ya uwekezaji ya IPTL na kupeleka
malipo hayo kwenye Akaunti ya Escrow.
Ulipaji ulisimama katika kipindi kifupi wakati kampuni ya IPTL ilipowekwa
kwenye ufilisi. Kwa mujibu wa taarifa ya
CAG, wakati akaunti hiyo inafungwa tarehe 20 Novemba, 2013, kulikuwa na fedha
taslimu shilingi 8,020,522,330.37;
Hatifungani zenye thamani ya shilingi
159,231,370,000 na Dola za Marekani
22,198,544. Fedha zote hizo ni sawa na shilingi
bilioni 202.9.
Ndugu Wananchi;
Kwa mujibu wa taarifa
hiyo, kama TANESCO ingelipa tozo ya uwekezaji ipasavyo, wakati huo Akaunti hii
ingekuwa na shilingi bilioni 306.7. Kwa sababu ya kutolipa fedha zote ipasavyo, wakati
Akaunti inafungwa TANESCO walikuwa wanadaiwa na IPTL shilingi bilioni 103.8.
Kwa mujibu wa Mkataba wa Mauzo ya Umeme (PPA) malipo yaliyocheleweshwa, yanatozwa
riba ya asilimia mbili ya fedha zote
ambazo hazikulipwa kwa wakati. Hivyo
basi, riba iliyotokana na TANESCO kuchelewesha malipo ilikuwa Dola za Marekani milioni 33.6.
Ni matumaini yangu
kuwa ufafanuzi uliotolewa katika Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali unasaidia kuweka kumbukumbu sawa na sahihi kuhusu kiasi gani
kilichokuwepo kwenye Akaunti ya ESCROW siku uamuzi wa Mahakama ulipofanya akaunti
hiyo ifungwe. Kwa kifupi Taarifa ya Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaeleza kuwa Akaunti hiyo ilikuwa na shilingi bilioni 202.9 na siyo shilingi bilioni 306.7 kama inavyodaiwa
na baadhi ya watu.
Fedha
za Nani
Ndugu Wananchi;
Ni
matumaini yangu pia kwamba maelezo haya kwa kiasi fulani yamesaidia kutoa jibu
kwa swali maarufu la fedha za kwenye akaunti hii ni za nani? Je ni za umma au za IPTL? Pengine nianze kwa kuelezea Akaunti ya ESCROW
ni nini? Akaunti ya ESCROW ni tofauti na
akaunti nyingine tunazozijua katika Benki zetu ambazo mtu anaweka fedha
zake. Kama tujuavyo, katika Benki zipo
Akaunti za aina tatu ambazo wengi tunazifahamu na kuzitumia yaani Akaunti ya
Akiba (Savings Account), Akaunti ya Hundi (Current Account) na Akaunti ya Muda
Maalum (Fixed Deposit Account). Akaunti
ya Escrow ni akaunti maalum inayoanzishwa kwa ajili ya kufanya kazi maalum, kwa
masharti maalum na kazi hiyo ikiisha akaunti yenyewe hufungwa. Akaunti hiyo husimamiwa na wakala aliyeteuliwa
kwa makubaliano ya wale wanaofungua akaunti hiyo. Wakala ndiye mwenye jukumu la kusimamia
akaunti na kumlipa mwenye fedha wakati ukifika.
Kwa akaunti ya Escrow ya Tegeta pande mbili husika zilikubaliana kuwa
Benki Kuu ndiyo iwe Wakala. Ni muhimu
kujua kuwa akaunti hiyo ingeweza kufunguliwa kwenye Benki yoyote siyo lazima
BoT.
Akaunti ya Tegeta
ESCROW ilifunguliwa BoT mwaka 2006 kwa ajili ya kuhifadhi fedha za malipo ya
tozo ya uwekezaji (capacity charges)
zilizokuwa zinalipwa na TANESCO kabla hazijakabidhiwa kwa anayelipwa ambaye ni
IPTL. Kabla ya hapo TANESCO ilikuwa
inalipa moja kwa moja kwa IPTL. Kama nilivyokwishasema, awali ilifanyika hivyo ili
kutoa nafasi kwa pande hizo mbili husika kumaliza tofauti zao kuhusu kiwango
cha tozo ya uwekezaji ya IPTL.
Kimsingi basi, fedha
hizi ni za IPTL kwani ndiye mlipwaji na ni malipo yanatokana na madai ya IPTL
kwa TANESCO kuhusu tozo ya uwekezaji.
Hata hivyo, kwa mujibu wa CAG, inawezekana katika fedha hizo kuna fedha
za umma. Hi ni kwa namna mbili.
Kwanza,
kama mgogoro baina ya TANESCO na IPTL ungetatuliwa na kiwango cha tozo ya
uwekezaji kupungua kama ilivyofanyika mwaka 2001 katika ICSID-1 na kama pande
mbili husika zingekubaliana au kuagizwa kuwa punguzo hilo lianze kuhesabiwa tangu
tarehe ilipofunguliwa Akaunti hiyo (tarehe 5 Julai, 2006), basi kungekuwepo
pesa za kurejeshwa TANESCO. Maadamu hili halikufanyika mpaka Mahakama
ilipofanya uamuzi uliosababisha akaunti hiyo kufungwa. Katika mazingira hayo fedha zote zinakuwa ni za
IPTL maana hakuna madai ya TANESCO.
Ndugu Wananchi;
Namna ya pili ni ile ambapo
katika fedha hizi kunaweza kuwepo fedha za umma na iwapo kuna kodi za Serikali
ambazo hazijalipwa. Kwa mujibu wa
Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kuthibitishwa na
TRA ni kwamba kulikuwa na kodi ya VAT ambayo haikulipwa. Nimeambiwa kuwa TANESCO ndiyo ilikuwa na wajibu
wa kukata kodi hizo kabla ya kulipa madai ya IPTL lakini kwa baadhi ya malipo
haikufanyika hivyo. Hivi IPTL inastahili kudaiwa kodi ya Serikali? Kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa, kodi
inayotakiwa kulipwa na IPTL ni shilingi
bilioni 21.7. IPTL wameshapelekewa madai na TRA, na IPTL wamekubali kulipa.
Katika ukaguzi wa
Hesabu za TANESCO za mwaka 2012, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
aliwaelekeza TANESCO kuacha kuhesabu fedha zilizopo kwenye Akaunti ya ESCROW
kama ni fedha zao. CAG aliwaambia
TANESCO kwamba fedha hizo si zao.
Maagizo hayo ya CAG
yanasomeka kama ifuatavyo:
“As
a result, the deposit balance in Escrow account does not meet the definition of
an asset of the Company and therefore an adjustment has been made to
de-recognize the asset and related liability to the tune of the amounts
available in the Escrow account”
Kwa tafsiri yake ni
kuwa: “Hivyo basi, fedha zilizowekwa kwenye akaunti ya Escrow hazina sifa ya
kutafsiriwa kama ni mali ya kampuni (TANESCO) hivyo, marekebisho yamefanywa ili
kutotambua mali na madeni yanayohusu fedha hizo kwa kiasi cha fedha zilizopo
kwenye akaunti ya Escrow.”
Kutokana na maelezo
haya ni dhahiri kwamba, fedha zilizokuwa kwenye Escrow siyo za TANESCO na
hazikupaswa kuingizwa kwenye vitabu vya TANESCO kama mali yake.
Chimbuko
la Sakata
Wazee Wangu;
Chimbuko la kadhia
yote hii Bungeni na kwenye jamii ni uamuzi wa tarehe 5 Septemba, 2013, wa
Mahakama Kuu ya Tanzania wa kuitambua PAP kuwa mmiliki halali wa IPTL na kuagiza
Mfilisi akabidhi shughuli zote za IPTL kwa PAP.
Katika utekelezaji wa uamuzi huo wa Mahakama Kuu ukazuka mjadala mkali kuhusu fedha zilizomo kwenye
akaunti ya ESCROW kukabidhiwa kwa PAP.
Kwanza kabisa mjadala ulikuwa ndani ya Serikali miongoni mwa viongozi na
watendaji wa Wizara na Taasisi zinazohusika moja kwa moja na akaunti hiyo. Hizi ni Wizara ya Nishati na Madini, TANESCO
na Benki Kuu. Viongozi na Watendaji
husika walikuwa wanajiuliza na kuuliza kama walipe au wasilipe. Walipotaka ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali wakaelekezwa watekeleze uamuzi wa Mahakama Kuu. Alisema uko sawa na hauna matatizo. Halikadhalika, Benki Kuu walipoulizia kuhusu
kodi za Serikali, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alielekeza kuwa hakuna kodi ya
kulipwa.
Kwa kuzingatia
ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, malipo yakafanyika kwa IPTL tena bila
ya kodi kulipwa. Baada ya malipo
kufanywa ndipo mjadala huo ukahamia katika jamii na Bunge na kugeuka kuwa
kadhia kubwa iliyochukua sura ya kashfa yenye dalili za rushwa na wizi.
Uamuzi
Unaotiliwa Shaka
Wazee
Wangu na Ndugu Wananchi;
Kwa jumla uamuzi wa
Mahakama Kuu kuhusu akaunti ya Escrow, ushauri wa Mwanasheria Mkuu kwa Serikali
wa kuelekeza uamuzi huo utekelezwe na viongozi wa Serikali kutekeleza ushauri
huo vimetiliwa shaka. Umeonekana kuwa
haukuwa uamuzi sahihi na kwamba umeitia hasara nchi. Isitoshe uamuzi huo umeibua hisia za kuwepo harufu
na vitendo vya rushwa. Wapo waliosema si bure iko namna! Wapo waliotaja majina na watu wanaodai
wamepata mgao wa Escrow tena wengine wamechukua fedha kwa viroba, sandarusi na
rumbesa. Bahati mbaya sana katika
mjadala ilijengeka dhana isiyokuwa sahihi kwamba jambo hili lilianzishwa na Maafisa
hao wa Serikali kwa nia ya kujinufaisha wao binafsi. Ukweli ni kwamba uamuzi ulifanywa na Mahakama
Kuu na kwenye Serikali ilikuwa utekelezaji wa amri hiyo.
Wazee Wangu;
Nilipokutana na aliyekuwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupata maoni yake kuhusu kadhia hii ameendelea
kusema alichosema Bungeni kuwa hakukosea katika ushauri wake na wala Mahakama
haikufanya makosa. Hivyo basi, hakuona
sababu ya kwenda Mahakamani kuomba marekebisho ya uamuzi wa Mahakama kuhusu fedha
zilizokuwepo kwenye akaunti ya Escrow ya Tegeta kukabidhiwa kampuni ya PAP
mmiliki wa IPTL. Vilevile haoni kama
kuna hasara yo yote ambayo nchi imepata kwa sababu fedha zile ni za IPTL na
imelipwa IPTL.
Akifafanua, alisema
kuwa akaunti ya Escrow ilianzishwa kwa ajili ya kutunza fedha za malipo ya tozo
ya uwekezaji kwa IPTL yaliyokuwa yanafanywa na TANESCO. Kabla ya mzozo kuhusu ukokotoaji wa tozo hiyo
na kuanzishwa kwa akaunti ya Escrow ya Tegeta, TANESCO ilikuwa inalipa tozo ya
uwekezaji moja kwa moja kwa IPTL. Baada
ya kutokea mzozo na akaunti kuanzishwa mambo mawili hayakubadilika. Kwanza kwamba IPTL haikuacha kupeleka madai
ya tozo ya uwekezaji kwa TANESCO. Na,
pili, kwamba TANESCO haikuacha kulipa madai hayo. Mdai na mdaiwa hawakubadilika. Kuwepo kwa akaunti ya Escrow hakubadili
mwenye fedha zake. Akaunti hiyo iliundwa
kuhifadhi fedha za IPTL wakati suluhu inatafutwa kuhusu kiwango cha tozo. Matumaini ni kwamba kama kiwango kitapunguzwa,
TANESCO inaweza kupata nafuu ya malipo.
Kuhusu uamuzi wa
Mahakama Kuu kuruhusu IPTL ilipwe fedha za akaunti ya Escrow, Mwanasheria Mkuu
wa Serikali alisema ni uamuzi sahihi na wala taifa halikupata hasara kwa sababu
pesa zimelipwa IPTL na siyo mtu mwingine.
Isitoshe anaona uamuzi wa Mahakama umeisaidia TANESCO kutua mzigo mkubwa
iliyokuwa nao kwa miaka saba.
Kama
mjuavyo, akaunti ya Escrow ilianzishwa kuhifadhi pesa za malipo ya tozo ya
uwekezaji ya IPTL. Ilianzishwa kwa
matumaini kuwa TANESCO watapata nafuu ya tozo ya uwekezaji. Lakini, hapakuwahi kufanyika mazungumzo baina
ya TANESCO na IPTL kuhusu jambo hilo na wala suala hilo halijafikishwa
ICSID. Haikuweza kufanyika hivyo kwa
sababu washauri wa kisheria wa TANESCO hawajafanya hivyo. Wapo wanaodai kuwa hawafanyi hivyo kwa sababu
hakuna sababu mpya zinazoweza kupatikana kuifanya ICSID ibadili uamuzi wake wa
2001 kuhusu kiasi cha tozo na namna ya ukokotoaji wake.
Matokeo
yake ni TANESCO kuwa na akaunti ya Escrow ambayo mwisho wake haujulikani. TANESCO inaendelea kudaiwa na IPTL tozo ya
uwekezaji na kulazimika kulipa kwenye akaunti hiyo. Kwa masharti ya akaunti ya Escrow
wanaposhindwa kulipa wanatozwa riba. Kwa
mujibu wa taarifa ya CAG mpaka tarehe 20 Novemba, 2013, TANESCO ilikuwa
inadaiwa shilingi bilioni 103.8
ambazo hawajalipa kwenye akaunti ya Escrow na riba ya Dola za Marekani milioni 33. Kwa sababu hiyo basi uamuzi wa kufunga Akaunti
ya Tegeta Escrow unalipatia unafuu TANESCO dhidi ya kulimbikiza madeni na riba.
Kwa
upande wa kodi za Serikali ambazo hazikulipwa, Mheshimiwa Jaji Werema alisema
yeye alitoa ushauri tu. Hata hivyo, kama
mamlaka husika inaona zipo kodi zinazostahili kulipwa izidai. Hakuna kilichopotea kwa sababu anayedai,
yaani TRA yupo, na mdaiwa yupo, IPTL.
Uamuzi
wa ICSID II Kuhusu Tozo ya Uwekezaji
Wazee Wangu;
Yalitolewa mawazo
kuwa kama fedha za akaunti ya Tegeta Escrow zingelipwa baada ya uamuzi wa Mahakama
ya Kimataifa ya Kusuluhisha Migogoro ya Uwekezaji (ICSID II) kutoa uamuzi wake,
TANESCO ingepata nafuu ya kupungua kwa tozo ya uwekezaji. Kuhusu jambo hilo nimeambiwa kwamba kuna
mambo mawili ya msingi. Kwanza kwamba
Mahakama hiyo haikutoa viwango vipya vya tozo kama ilivyofanya mwaka 2001
kwenye ICSID–I. Haikubadili mwongozo wa
ukokotoaji wa tozo. Imesema madai
yanaweza kuzungumzwa na kusisitiza kuwa katika mazungumzo hayo TANESCO watambue
kwamba wanahisa waliwekeza mtaji wao binafsi wakati wa kununua mtambo na pia
walikopa madeni, na kwamba kiasi cha fedha walichowekeza kilitakiwa kiwe na
kiwango cha juu zaidi cha faida.
Jambo la pili ni
kwamba, shauri hili la pili la ICSIDI II halikuihusisha kampuni ya IPTL mwenye
Mkataba wa Kuuza Umeme na TANESCO na siyo Benki ya Standard Charterd. IPTL wameweka pingamizi la utekelezaji wa
uamuzi wa shauri hilo hapa nchini, hivyo inakuwa vigumu kwa TANESCO kufanya
mazungumzo kwa msingi wa shauri hilo.
Kinga
Dhidi ya Madai
Wakati wa kufunga
akaunti ya Escrow, upande wa Serikali ulielezea hofu yake ya uwezekano wa siku
za usoni mtu kudai tena kulipwa fedha hizi hizi ilizolipwa PAP. Nimeambiwa kuwa suala hilo haliwezi kutokea
kwani limetengenezewa wigo imara wa kimkataba kuzuia. PAP imetiliana sahihi na Serikali kwamba
iwapo kutatokea mdai yo yote PAP itawajibika kulipa.
Mashaka
ya Miliki ya PAP kwa IPTL
Ndugu
Wananchi;
Hofu
nyingine kuhusu uwezekano wa Serikali kupata hasara ni yale madai kuwa huenda
miliki ya PAP kwa asilimia 70 za hisa za IPTL zilizokuwa za kampuni ya Mechmar
Berhard ya Malaysia siyo halali. Pale
mwanzoni ilidaiwa kuwa kampuni ya Mechmar ilipouza hisa zake kwa kampuni ya
Piper Link ya British Virgin Islands ilikuwa chini ya mchakato wa ufilisi kule
Malaysia. Kama ingekuwa hivyo, kisheria
mtu hawezi kuuza hisa zake akiwa kwenye mazingira hayo. Katika uchunguzi wa CAG alieleza kuwa
amethibitisha kwamba madai hayo si kweli,
Mechmar walipouza hisa zao tarehe 9 Septemba, 2010 kampuni haikuwa kwenye
ufilisi. Iliingia kwenye mchakato wa
ufilisi mwaka 2012.
Lakini
kwa upande wa kampuni ya Piper Link ya Uingereza inasemekana iliuza hisa hizo
baada ya kuwa wamepokea amri ya Mahakama ya Malkia ya BVI kuizuia isiuze hisa
hizo. Je ni kweli? Imefanyika hivyo? Kama ni kweli je PAP waliponunua hisa hizo
walijua kama kuna zuio au hapana? Kama
walijua basi na wao ni sehemu ya njama za kufanya udanganyifu. Kama
hawakuwa wamejua basi wametapeliwa. Nimeagiza
uchunguzi wa kina ufanyike kupata ukweli.
Natambua hivi sasa Mahakamani zipo kesi zinazohoji uhalali wa PAP
kumiliki asilimia 70 za hisa za Mechmar Berhad.
Uchunguzi wetu hautaingilia mchakato huo lakini unaipa Serikali fursa
nzuri ya kuchukua hatua zipasazo kuhusu suala hili lenye mjadala mkubwa. Jambo
lingine muhimu ambalo limeleta matatizo kwa Mahakama zetu nchini na BRELA ni
uuzaji wa hisa za IPTL au kuwekwa rehani hisa hizo bila ya uamuzi huo
kusajiliwa BRELA na kwenye Mahakama zetu.
Sheria zetu ambazo ndizo za nchi
ya Jumuiya ya Madola kama ilivyo kwa Hong Kong, Malaysia, na BVI, inaitaka kampuni
ya Piper Link ya BVI iliponunua hisa za Mechmar katika IPTL kusajili BRELA
ununuzi huo. Hali kadhalika, inaitaka SCB
ya Hong Kong na kupata amri ya Mahakama kuzuia deni la Mechmar na kuwekwa
dhamana ya hisa za Mechmar katika IPTL.
Piper Link isiuze hisa 70 za Mechmar katika IPTL. Walitakiwa wasajili na BRELA na Mahakama
yetu. Kutokufanya hivyo ndiko kunazua
maneno mengi na mzozo kuhusu uuzaji wa hisa hizo kwa PAP. Kwa SCB wanapata usumbufu wa kudai madeni yao
IPTL kwa sababu hiyo hiyo. Uchunguzi
utakaofanyika utapata ukweli wa yote kwa uhakika.
Ndugu Wananchi;
Taarifa
niliyopewa wakati najiandaa kuzungumza nanyi ni kuwa katika Mahakama zetu nchini kuna mashauri yahusuyo
miliki ya PAP ya hisa 70 zilizokuwa za Mechmar katika IPTL na yapo mashauri
yahusuyo PAP kupewa fedha za akaunti ya Escrow.
Zipo pia nyingine za masuala mbalimbali yakiwemo mashauri
yaliyofunguliwa na PAP dhidi ya watu, na makampuni binafsi na vyombo vya
Serikali. Naamini uamuzi wa Mahakama
zetu utatoa majibu kwa masuala yote hayo.
Pamoja
na hayo yatakayokuwa yanaendelea Mahakamani, Serikali itaendelea kufanya
uchunguzi wake na kuamua namna ya kushughulikia taarifa zitakazopatikana ili
nayo iweze kwenda Mahakamani itakapolazimu kufanya hivyo.
Jambo
lingine muhimu nataka uchunguzi wa kina ufanyike ni kujua nani ni nani katika
uuzaji na ununuzi wa hisa za Mechmar.
Hususan nataka tujue kwa ukweli na uhakika hisa hizo zimeuzwa kwa bei
gani. Je, ni kweli gharama zinazosemwa ndizo zenyewe? Nataka kuthibitisha ukweli huo ili tujue kodi
yetu ya ongezeko la mtaji (Capital Gains
Tax) inayostahili kulipwa Tanzania ni kiasi gani? Je kiasi gani kimelipwa
na kipi hakijalipwa ili kidaiwe?
Tuhuma
za Kuwepo kwa Harufu ya Rushwa
Wazee
Wangu;
Kumekuwepo
na tuhuma za vitendo vya rushwa katika mchakato mzima wa kufunga akaunti ya
Escrow na kukabidhi fedha hizo kwa kampuni ya PAP. Halikadhalika, kumekuwepo na hisia hizo hizo
kwa upande wa jinsi kampuni ya VIP Engineering and Marketing ilivyotumia pesa
zake zilizoko kwenye Benki ya Mkombozi.
Yamesemwa mengi sana na mmeyasikia na kuyasoma.
Rushwa
ni kosa la kijinai ambalo kwa Serikali yetu ni kosa ambalo ni vigumu
kulivumilia wala kulifumbia macho. Mara baada ya kupata fununu za uwezekano wa
vitendo hivyo kufuatia taarifa ya awali ya CAG ya kwenda kukagua miamala, niliagiza
taarifa husika zifikishwe kwenye Taasisi ya Kupamba na Kuzuia Rushwa (PCCB) kwa
uchunguzi zaidi. Naambiwa taarifa hizo
zimefika na kazi ya uchunguzi inaendelea.
Tayari watu kadhaa wamehojiwa na wengine wanaendelea kuhojiwa. Wakati nawasihi wananchi kuvuta subira ili tuwape
nafasi PCCB wakamilishe kwa ufanisi wa hali ya juu kazi yao waliyokwishaianza,
nawaomba PCCB waongeze kasi ya uchunguzi.
Napenda kufafanua kwamba kwa upande wa miamala iliyotoka katika akaunti
ya kampuni ya VIP Engineering and Marketing ya Ndugu James Rugemalila, Serikali
inashughulika na watumishi wa umma kwa kuzingatia Sheria ya Maadili ya Utumishi
wa Umma, maana suala lao ni la kimaadili.
Hatuwahoji wasiokuwa watumishi wa umma.
Maazimio
ya Bunge
Ndugu
Viongozi;
Wazee
Wangu;
Ndugu
Wananchi;
Niliona
nianze kwa kutoa maelezo hayo ya utangulizi kabla ya kuyazungumzia maazimio ya
Bunge. Serikali imepokea maazimio hayo ya
Bunge na kuyafanyia kazi kwa ajili ya utekelezaji wake. Nawapongeza Wabunge wetu kwa moyo
waliouonesha wa kuchukia maovu na kutaka yashughulikiwe ipasavyo. Napenda kuwahakikishia kuwa niko pamoja
nao. Nampongeza Mheshimiwa Anna Makinda,
Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai, Naibu Spika na Mwenyekiti wa Bunge
Mheshimiwa Mussa Zungu kwa uongozi wao mahiri.
Hakika haikuwa kazi rahisi, lakini chini ya uongozi wao mambo yameisha
salama na tumepata maazimio nane yanayozungumzika
na kutekelezeka. Nawashukuru na
kuwapongeza sana Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC), chini ya uongozi wa Mheshimiwa Zitto Kabwe na Mheshimiwa Deo Filikunjombe na pia Wajumbe waliounda
Kamati ya Mapendekezo kwa kufikia mwafaka wa mapendekezo haya 8 ambayo
yaliazimiwa na Bunge.
Mwisho lakini si ya
mwisho kwa umuhimu, nawapongeza Wabunge wote kwa michango yao mizuri. Jambo lililonifurahisha sana ni ushirikiano
wa Wabunge wa kambi zote katika kutafuta ufumbuzi wa suala hili muhimu,. Hivi ndivyo inavyotakiwa Bunge liwe. Kwa kweli lazima nieleze mshangao wangu
niliposikia kambi ya upinzani ikijaribu kufanya maamuzi yale ni yao wao na
wenzao hawamo. Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Hesabu za Serikali ina Wajumbe 19
wa CCM na wa Upinzani 5. Bunge lina
Wabunge wa CCM asilimia 74 na wa
upinzani asilimia 26. Hivi kama ni
yao wao pekee na wa upande wa CCM wangepinga yangekuwa? Yasingefika po pote, yangefia kwenye
Kamati. Huku ni kutafuta umaarufu kwa
mgongo wa wengine. Na, Wabunge wengi wa
CCM na nyie semeni msikike kwa uamuzi mliyofanya wote.
Napenda kuwahakikishia kuwa mimi na wenzangu
Serikalini hatuna upungufu wa dhamira ya kutekeleza yale maazimio yanayoangukia
katika dhamana yetu. Napenda kuainisha
mtazamo na mwelekeo wa Serikali katika utekelezaji wa maazimio hayo manane kama ifuatavyo:-
Azimio
la kwanza: Serikali iangalie uwezekano wa kuchukua
mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa TANESCO kwa mujibu wa Sheria
za nchi.
Pendekezo
tumelipokea, ni jambo linalowezekana kufanya.
Hata hivyo, tunapopima ujumbe tunaoupeleka kwa jumuiya ya wawekezaji
tunachelea kuwa inaweza kuleta hofu na kuwatisha wawekezaji waliopo na wajao.
Nalisema hivyo kwa sababu sisi tuna historia ya kutaifisha mali za
kamapuni binafsi. Hofu hiyo bado
ipo. Tukichukua mitambo hii tunaweza
kurudisha hofu za kurudi tulikokuwa na kukimbiza mitaji tunayohitaji kwa uchumi
kukua na nchi kupata maendeleo. Nashauri
tuendelee kuyapatia ufumbuzi matatizo ya IPTL kila tunapoyabaini. Aidha,
Mahakama imetusaidia sana kwa kuamuru mitambo ya IPTL ibadilishwe ili itumie
gesi asilia na kutoza bei ya umeme isiyozidi senti nane za Marekani. Tuyafuatiliye haya kwanza.
Azimio
la Pili: Azimio hilo linazungumzia kuhusu uwazi wa
Mikataba linasomeka ifuatavyo: “Bunge
limeazimia kwamba Serikali itekeleze Azimio husika la Bunge mapema iwezekavyo
na kwa vyovyote vile kabla ya kumalizika kwa Bunge la Bajeti. Serikali iwasilishe taarifa ya utekelezaji wa
mapitio ya mikataba ya umeme”.
Azimio hili
tumelipokea na tunaangalia namna bora ya kulitekeleza ili kuweza kuua ndege
wawili kwa jiwe moja. Kwanza, kuitikia
kilio cha muda mrefu kuhusu uwazi katika mikataba ambayo Serikali inaingia na
wawekezaji; na pili kuhakikisha usiri wa mikataba hiyo ambayo ni haki ya
wawekezaji hao dhidi ya washindani wao inazingatiwa. Serikali na Bunge tutakaa chini hivi punde kutafuta
namna bora ya kisheria na tutafanya hivyo kwa kujifunza pia kutokana na uzoefu wa
nchi ambazo zina utaratibu wa aina hii.
Azimio
la Tatu: Linasomeka; “Bunge linaazimia kwamba
TAKUKURU, Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama
vichukue hatua stahili kwa mujibu wa sheria za nchi yetu dhidi ya watu
waliotajwa kwenye taarifa maalum ya Kamati husika na vitendo vyote vya kijinai
kuhusiana na miamala ya Akaunti ya ESCROW, na watu wengine watakaogundulika
kufuatia uchunguzi mbalimbali unaoendelea kuhusu kuhusika kwao katika vitendo
hivyo vya jinai”
Vyombo husika vimekwishaagizwa kufanya hivyo
na kazi imeanza na inaendelea. Ikiwa wapo
watu wenye makosa hatua zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria.
Azimio
la nne: Linasomeka, “Kamati za Bunge kuwavua nyadhifa
zao wenyeviti wa Kamati za Bunge waliotajwa kupewa fedha na kampuni ya VIP
Engineering kabla ya kikao kijacho cha Bunge”
Azimio
hilo liko chini ya mamlaka ya Bunge lenyewe.
Nawaachia wao waamue.
Azimio
la Tano: Linasomeka; “Bunge linaazimia kwamba Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aunde Tume ya Kijaji ya Uchunguzi kuchunguza
utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes
Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania”
Azimio
hili nimelipokea, tumelijadili hata hivyo, itabidi tufuate utaratibu wa
kikatiba na kisheria wa kushughulikia masuala ya namna hiyo. Inatakiwa suala kama hili lianzie kwenye Mhimili
wa Mahakama yenyewe na siyo kwa Rais au Bunge.
Tume ya Mahakama ndiyo yenye mamlaka ya kumtaka Rais aunde Tume ya
Kijaji ya kumchukulia hatua Jaji yeyote pale inaporidhika kuwa amepoteza sifa
za kuendelea kufanya kazi hiyo. Nashauri
suala hili tumuachie Jaji Mkuu wa Tanzania alishughulikie atakavyoona
inafaa.
Azimio
la Sita: “Bunge linaazimia kwamba mamlaka husika za
kifedha na za kiuchunguzi kuitaja Stanbic Bank Ltd. na benki yeyote
itakayogundulika kufuatia uchunguzi wa mamlaka ya uchunguzi, kujihusisha na
utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika akaunti ya ESCROW kuwa ni taasisi
zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu (Institutions of money laundering
concerns).
Pendekezo
la Bunge ni zuri kwamba mamlaka husika na udhibiti wa vitendo vya utakatishaji
fedha vifanye uchunguzi kwa mujibu wa Sheria.
Serikali imelipokea na mamlaka husika yaani Financial Intelligence Units
kulishughulikia. Naamini wameshaaza,
tuwape muda watimize wajibu wao kwa mujibu wa sheria.
Azimio
la Saba: “Bunge liliazimia kwamba Serikali iandae, na
kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria iliyounda TAKUKURU kwa lengo la
kuanzishwa Taasisi mahsusi itakayoshughulikia kupambana na kudhibiti vitendo
vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa
kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Kazi
ya kufanya mageuzi katika TAKUKURU inaendelea.
Tayari Sheria mbalimbali zimetungwa ikiwa ni pamoja na Sheria Mpya ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2008, Sheria ya Kudhibiti Matumizi ya
Fedha Haramu ya mwaka 1991 ambazo zote zinaweka utaratibu wa kushughulikia
vitendo vya rushwa. Tutaendelea
kuziboresha sheria hizo kwa kadri itakavyohitajika. Kazi iliyopo mbele yetu ni kuimarisha
usimamizi wa sheria hizo. Jambo hilo
nalo litazingatiwa katika maboresho hayo.
Ni dhamira yangu na ya Serikali ninayoiongoza kupambana na kushinda vita dhidi ya rushwa. Kwa hiyo tuko tayari kulifanyia kazi
pendekezo lolote linaloimarisha dhamira yetu hii njema.
Azimio
la nane: “Bunge linaazimia kwamba Waziri wa Nishati na
Madini, Waziri wa Ardhi na Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya
TANESCO wawajibishwe kwa kuishauri mamlaka ya uteuzi kutengua uteuzi wao.
Azimio
hili ndilo Azimio ambalo limevuta hisia za watu wengi, na pengine ndilo ambalo
utekelezaji wake unasubiriwa kwa hamu. Utekeelzaji
wake umeanza. Kwanza, ni kuhusu Bodi ya
TANESCO, tumeanza mchakato wa kuunda
Bodi mpya kwani iliyopo imemaliza muda wake.
Kuhusu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, kwa vile ni mtumishi wa umma anatawaliwa na Sheria
na Kanuni za Utumishi wa umma, hivyo nimeshaelekeza Mamlaka kuchunguza tuhuma
zake na hatimaye ikibainika ana makosa hatua za kinidhamu zitachukuliwa. Mwanasheria Mkuu wa Serikali
ameshajiuzulu. Tumelitafakari suala la Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi la kupokea fedha kutoka VIP Engineering
and Marketing ambazo kwa maelezo yake ni kwa ajili ya shule anayoimiliki na
kuiendesha. Mwenyewe ameeleza wazi
kupitia vyombo vya habari. Pamoja na hayo yapo mambo ya msingi kimaadili ambayo
hayakuzingatiwa, hivyo tumemwomba atupishe tuteue mwingine. Kuhusu Prof. Muhongo nimemuweka kiporo, kuna
uchunguzi niliagiza ufanywe na vyombo vyetu bado nasubiri taarifa hiyo ili
nifanye uamuzi ndani ya siku chache zijazo.
Hitimisho
Wazee
Wangu;
Nawashukuruni
kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment