Rais Kikwete akiingia katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani jijini Dodoma leo Oktoba 11, 2014 tayari kwa mkutano wake na wazee wa mji wa Dodoma leo waliouitisha ili kuzungumza naye maswala kadhaa ya maendeleo.
Makamu wa Rais Dkt Mohamed Gharib Bilali akiingia katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani jijini Dodoma leo tayari kwa mkutano wake na wazee wa mji wa Dodoma waliouitisha ili kuzungumza na Rais Kikwete maswala kadhaa ya maendeleo.
Wimbo wa Taifa.
Ngoma ya utamaduni ya kabila la Wagogo likitumbuiza kabla ya kuanza kwa mkutano wa Rais Kikwete na wazee wa mji wa Dodoma leo waliouitisha ili kuzungumza naye maswala kadhaa ya maendeleo.
Sehemu ya wazee wakati wa mkutano wao na Rais Kikwete mjini Dodoma leo waliouitisha ili kuzungumza naye maswala kadhaa ya maendeleo.
Meza kuu ikiomba dua kabla ya kuanza kwa mkutano wa Rais Kikwete na wazee wa mji wa Dodoma leo waliouitisha ili kuzungumza naye maswala kadhaa ya maendeleo.
Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani wakati wa Mazungumzo kati ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete na wazee wa mji wa Dodoma leo waliouitisha ili kuzungumza naye maswala kadhaa ya maendeleo.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipokea risala toka kwa Mwenyekiti wa Wazee wa Mkoa wa Dodoma Balozi Job Lusinde wakati wa mkutano na wazee wa mji wa Dodoma leo waliouitisha ili kuzungumza naye maswala kadhaa ya maendeleo.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na wazee wa mji wa Dodoma leo waliouitisha ili kuzungumza naye maswala kadhaa ya maendeleo.
PICHA NA IKULU
HOTUBA
YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA,
MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE,
AKIZUNGUMZA
NA WAZEE WA DODOMA, UKUMBI WA KILIMANI, DODOMA, 4 NOVEMBA, 2014
Ndugu
Wananchi;
Nakushukuru
sana Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Dodoma, Mheshimiwa Balozi Job Lusinde kwa
kuandaa mkutano huu. Wakati nilipofanya
ziara ya Mkoa wa Dodoma tulipanga tukutane lakini kwa vile ratiba yangu
iliingiliwa na mambo mengi, hivyo haikuwezekana, lakini leo imewezekana. Pengine hii ndiyo siku ambayo Mwenyezi Mungu
alipanga tukutane. Tumshukuru Muumba
wetu kwa rehema zake, na tumuombe ajaalie mkutano wetu uanze salama na uishe
salama. Nawashukuru kwa Risala yenu na
maudhui yake. Nawaahidi nitayafuatilia
na majibu mtapata. Pamoja na yaliyomo kwenye risala yenu mimi nina mambo manne
ambayo ni yatokanayo na ziara yangu nchini China na Vietnam, maradhi ya Ebola, uchaguzi
wa Serikali za Mitaa na hatua zinazofuata kwenye Mchakato wa Katiba.
Ziara
ya China na Vietnam
Ndugu
Wananchi;
Kuanzia tarehe 21
Oktoba, 2014 hadi tarehe 28 Oktoba, 2014 nilikuwa katika ziara rasmi ya kutembelea
nchi za China na Vietnam. Nilitembelea China tarehe 21 hadi 26 Oktoba, 2014 na
Vietnam tarehe 26 hadi 28 Oktoba, 2014. Ziara hizo nilizifanya kufuatia mwaliko
wa Rais wa China, Mheshimiwa Xi Jinping na mwaliko wa Rais wa Vietnam Mhe.
Truong Tan Sang. Ziara katika nchi hizo
zilikuwa za mafanikio makubwa sana hata kuliko nilivyotarajia. Nchini China tulipokelewa kwa namna
hawajafanya kwa miaka mingi.
Ziara
ya China
Ndugu Wananchi;
Nchini China, kwa
makubaliano na wenyeji wetu tulifanya hafla maalum ya kuadhimisha miaka 50 tangu
kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na China. Katika hafla
hii upande wa China uliwakilishwa na Makamu wa Rais Mheshimiwa Li Yuanchao. Pande zetu mbili ziliitumia fursa hiyo
kuzungumzia tulipotoka, tulipo sasa na mbele tuendako.
Kwa jumla wote
tumeridhika kuwa tumekuwa na nusu karne ya uhusiano wenye mafanikio
makubwa. Katika kipindi hiki nchi zetu
zimekuwa marafiki wa kweli, wa kuaminiana na kusaidiana kwa mambo mengi. Katika
medani za kimataifa nchi zetu zimekuwa zikielewana kwa mambo mengi na
kusaidiana. China ilikuwa ngome kuu
katika kusaidia kwa hali na mali harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika.
Wakati ule Tanzania
ilikuwa ikiongoza nchi za mstari wa mbele.
Wenzetu bado wanakumbuka sana jinsi
nchi yetu ilivyokuwa mstari wa mbele kuipigania nchi ya China kurejeshewa haki
yao hususan ya kuketi kiti chao katika Umoja wa Mataifa, baada ya Chama cha
Kikomunisti chini ya uongozi wa Mwenyekiti Mao Tse Tung kufanikiwa kukishinda
Chama cha Kuomintang na kiongozi wake Chian Kai Sheki na kulazimika kukimbilia
Taiwan. Mataifa makubwa ya Magharibi yalikataa kuitambua China mpya na
kuitenga. Katika kufanya hivyo, waliitambua
Taiwan na kuifanya kuwa ndiyo wawakilishi wa China katika Umoja wa Mataifa.
Baada ya hapo Jamhuri
ya Watu wa China ilipinga uamuzi ule na kuanzisha kampeni ya kudai haki yake
stahiki. Madai yao hayo yalipata nguvu
pale Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alipoamua kuwa Tanzania ishiriki
katika kampeni hiyo kwa nguvu zake zote.
Kwa kushirikiana na nchi nyingine rafiki, jitihada hizo za pamoja zilizaa
matunda na mwaka 1971, China ilipokubaliwa kuchukua nafasi yake stahiki katika
Umoja wa Mataifa na Taiwan kuondolewa.
Ndugu zetu wa China hawasahau msaada wetu huo na hawaoni haya kulisemea
waziwazi jambo hilo na vizazi vyote vya China vinafundishwa kuhusu wema ambao
Tanzania imewafanyia. Kwa sababu hiyo, Tanzania ina nafasi maalum nchini
China. Wao wenyewe wana msemo maalumu
kuhusu Tanzania kwamba ni “all weather friends”. Yaani marafiki wa majira yote.
Katika ziara yangu
nilifuatana na kaka yangu Dkt. Salim Ahmed Salim ambaye ndiye alikuwa Balozi wa
Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa wakati ule. Rafiki zetu wa China walifurahi sana kumwona
Dkt. Salim kwani yeye hasa ndiye aliyefanya kazi ya kushawishi nchi nyingine
kuiunga mkono Jamhuri ya Watu wa China.
Pia nilifuatana na Mheshimiwa Balozi Mstaafu Jenerali Mrisho Sarakikya
aliyekuwa Mkuu wa Majeshi wa kwanza wa Tanzania. Yeye ndiye alihusika sana kujenga uhusiano wa
mambo ya kijeshi baina ya nchi yetu na China.
Pia, nilikwenda na Balozi Mstaafu, Mzee Waziri Juma aliyewahi kuwa
Balozi wa Pili wa Tanzania nchini China.
Kama mjuavyo nchi ya
China imetusaidia mambo mengi kwa maendeleo yetu. Misaada mingine ilihusu vitu vikubwa ambavyo
katika hali ya kawaida isingewezekana kusaidiwa na nchi nyingine zinazotoa
misaada ya maendeleo na mikopo. Miongoni
mwa hayo ni ujenzi wa Reli ya Uhuru (TAZARA), misaada ya zana, vifaa na mafunzo
vilivyosaidia kujenga Jeshi letu jipya yaani JWTZ baada ya kuvunjwa kwa lile
tulilorithi kutoka kwa Wakoloni kuaasi Januari 20, 1964. Msaada wao mkubwa ndiyo uliotuwezesha mpaka kuweza kulinda na kukomboa nchi yetu
dhidi ya uvamizi na kutekwa eneo la Misenyi, Kagera na majeshi ya dikteta Iddi Amin
wa Uganda.
Hata sasa China imeendelea kuwa mshirika wetu
mkubwa kuliko wote katika kuimarisha na kuendeleza Jeshi letu. Msaada mwingine mkubwa ni ule mkopo wa dola
za Marekani bilioni 1.2 wa kujenga bomba jipya la gesi kutoka Mtwara na
Songosongo hadi Dar es Salaam.
Isingekuwa rahisi kupata mkopo mkubwa kiasi kile kutoka nchi nyingine au
Shirika lolote la fedha duniani. Mkopo
ule unalimaliza tatizo la upungufu wa umeme kutokea sasa mpaka mwaka 2020
inapokadiriwa kuwa nchi yetu itahitaji megawati 10,000. Hata wakati huo bomba hili ni muundombinu wa
msingi utakaorahisisha upanuzi wa miundombinu ya kuzalisha umeme kutosheleza
mahitaji hayo kama itaamuliwa gesi iendelee kuwa chanzo kikuu cha nishati ya
umeme nchini.
Katika mazungumzo
yangu na Waziri Mkuu Li Keqiang na Rais Xi Jinping wote wawili wameelezea
kuridhika kwao na uhusiano baina ya nchi zetu tangu siku za nyuma mpaka hapa
tulipo sasa. Hali kadhalika walielezea
kuwa wangependa kuona uhusiano wetu na ushirikiano wetu unaimarika na kukua
mpaka kufikia hatua bora na ya juu kabisa.
Niliwahakikishia kuwa hiyo ndiyo fikra yangu na Watanzania kuhusu
uhusiano baina ya nchi zetu mbili rafiki.
Kwa nyakati tofauti
viongozi wote wakuu wa China walinihakikishia utayari wao wa kuendelea
kuchangia maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiusalama ya Tanzania. Jambo lililonipa faraja kubwa mimi na
wenzangu ni kuwa mambo yote tuliyoomba ndugu zetu wa China watusaidie wamekubali. Hakika Wachina wameendelea kuwa marafiki wa
kweli wa nchi yetu na watu wake.
Tuliwaomba waendelee
kushirikiana nasi na wabia wenzetu wa Zambia kulijenga upya Shirika la Reli ya
TAZARA na wamekubali. Tuliwaomba pia tuendelee
kushirikiana kukuza uwekezaji na biashara baina ya nchi zetu mbili rafiki. Walilipokea jambo hilo kwa furaha. Ni ukweli
ulio wazi kwamba biashara na uwekezaji umekua sana kiasi cha kuifanya China
kuwa nchi inayoongoza kwa mambo yote mawili.
Hata hivyo, sote tumekubaliana kuwa biashara ya dola za Marekani
bilioni 3.7 na uwekezaji wa dola za Marekani bilioni 2.5 ni kidogo
mno hivyo tuongeze juhudi tufanye vizuri zaidi katika kipindi kifupi
kijacho.
Ndugu Wananchi;
Kulikuwa na mkutano
mkubwa wa uwekezaji uliohudhuriwa na makampuni ya kichina yapatayo 500
yaliyokuwa tayari kuwekeza na kufanya biashara na Watanzania. Kwa upande wetu miradi kadhaa tuliyopeleka
imepata wabia. Miongoni mwa
waliofaninikiwa sana ni Shirika la Nyumba la Taifa waliopata wabia
watakaowekeza dola za Marekani bilioni 1.7 kwenye ujenzi wa nyumba.
Aidha, kuhusu ujenzi
wa Ukanda wa Kiuchumi wa Mbegani ambao tuliwaomba watusaidie kusukuma
utekelezaji wake, viongozi wa China walielezea utayari wao kusaidia mradi huo
ufanikiwe. Tulipokuwa Shenzhen, tulipata
nafasi ya kutembelea Makao Makuu ya Kampuni ya China Merchants Ltd., na
kuzungumza na viongozi wake. Walitembezwa
kuangalia shughuli za kampuni hiyo ikiwa ni pamoja na jinsi Kampuni hiyo
ilivyoshiriki katika ujenzi wa mji wa Shenzhen kutoka kijiji cha uvuvi na kuwa
jiji kubwa la kisasa, lenye maendeleo ya kiuchumi, teknolojia na biashara. Waliahidi kutumia ujuzi wao, maarifa yao na
uwezo wao wa kifedha kujenga Mbegani kama ilivyotokea Shenzhen.
Siku ile pia
tulishuhudia Mfuko wa Akiba wa Oman wakitiliana saini na China Merchants na Mamlaka
yetu ya Uendeshaji wa Maeneo Huru ya Uwekezaji (EPZA) hati ya makubaliano kujiunga
rasmi katika kuwekeza na kushiriki katika utekelezaji wa mradi huo. Kilichonifurahisha sana siku ile ni kule
kuwepo kwa mpango kazi unaotarajia ujenzi wa bandari na ukanda wa maendeleo ya
kiuchumi wa Mbegani kuanza tarehe 1 Julai, 2015. Hali kadhalika, nilipokuwa Shenzhen nilipata
nafasi ya kutembelea kampuni za teknolojia ya habari na mawasiliano za Huawei
na ZTE. Nilifika mjini Jinan, Jimbo la
Shandong na kutembelea kampuni nyingine kubwa ya aina hiyo iitwayo INSPUR. Bahati nzuri kampuni zote zimewekeza Tanzania
na wanataka kupanua uwekezaji wao.
Nilipokuwa Jinan nilitembelea
Hospitali Kuu ya Jimbo la Shandgon, Mjini Jinan, ambayo imetoa madakatari wengi
na kupata nafasi ya kuwashakuru viongozi wa Jinan na Jimbo la Shandong kwa
kutuletea madakatari na wataalamu wengine wa afya kuja kufanya kazi nchini
Tanzania. Vile vile, nimewashukuru kwa
mchango wao muhimu uliotuwezesha kupata hospitali ya moyo katika Hospitali ya
Muhimbili. Pamoja na kuwashukuru
niliomba idadi iongezwe kwani mahitaji yapo na watu wanawapenda Madaktari wa
China. Yapo mambo mengi mazuri
yaliyofanyika katika ziara yangu nchini China ambayo tutakesha kama tutahitaji
kuyafafanua moja baada ya jingine. Hata
hivyo, napenda kuyazungumzia mambo mawili.
Kwanza ni taarifa aliyonipa Rais Xi Jinping kwamba wanaongeza ufadhili
wa masomo kwa kutupa nafasi 100 zaidi kwa vijana wa Tanzania kusoma China kwa kipindi
cha miaka mitano. Pia wamekubali kutusaidia
ujenzi wa chuo cha ufundi (VETA) cha Mkoa wa Kagera. Aidha, wamekubali ombi
langu la kuongeza idadi ya madaktari na wataalamu wa afya kutoka China kuja
kufanya kazi nchini.
Ziara
Vietnam
Ndugu
Wananchi;
Baada ya kumaliza
ziara yangu China nilitembelea Vietnam kwa siku mbili. Huko nako nilikwenda kuimarisha na kuendeleza
uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi zetu, na kujifunza zaidi kutoka kwa wenzetu ambao
wamepata mafanikio makubwa kiuchumi katika kilimo na viwanda kwa kipindi kifupi.
Hii ni nchi ambayo tulianza nayo mageuzi ya kiuchumi wakati mmoja mwaka 1986. Wenzetu wameweza kupata mafanikio makubwa
katika kilimo, viwanda, ufugaji wa samaki na mengine mengi. Kwa upande wa teknolojia ya mawasiliano ya
simu, wanayo kampuni ya Viettel ambayo imekuwa kubwa duniani na inakusudia
kuwekeza nchini.
Kwa kweli mafanikio
ambayo Vietnam imepata tangu mwaka 1986 yanatupa matumaini kwamba na sisi Tanzania
tunaweza kufanikiwa kama wao. Hatuna
budi kujipanga vizuri. Tumekubaliana
kushirikiana zaidi hasa kubadilishana uzoefu na maarifa katika kilimo na
viwanda.
Ugonjwa
wa Ebola
Ndugu
Wananchi;
Jambo
la pili ninalotaka kulizungumzia, si mara yangu ya kwanza kufanya hivyo. Hili si jingine bali ni tahadhari juu ya
maradhi ya Ebola yaliyoanzia huko Afrika Magharibi katika nchi za Liberia,
Sierra Leone na Guinea. Baadae yalifika Nigeria, Senegal, Mali, Marekani, Spain
na Uingereza. Inakadiriwa kuwa ugonjwa
huu hatari umekwishaua watu 4,960 na wengine 13,567 wameambukizwa
toka ulipoanza hadi sasa. Ugonjwa huu
umeendelea kuwa tishio la dunia kutokana na kasi kubwa ya kuenea kwake. Lakini hasa kwamba asilimia 70 mpaka 90 wanaoupata
ugonjwa huu hupoteza maisha. Bahati
mbaya hauna dawa wala kinga. Bado wataalamu wa dawa wanachuna bongo.
Taarifa
njema ni kuwa ugonjwa huu haujaingia nchini Tanzania. Hata hivyo, hii haiondoi ukweli kuwa unaweza
kufika kwani watu wanatembea kutoka nchi zenye maradhi haya na kuja nchini
kwetu. Hapa jirani na sisi upo Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo. Sitashangaa
pia kwamba wapo Watanzania wanaokwenda nchi zenye maambukizi makubwa hata
wakati huu. Watu hao wana hatari kubwa
ya kupata maambukizi.
Narudia kukumbusha
umuhimu wa kuchukua tahadhari kitaifa na kila mtu anayeishi hapa nchini. Sisi Serikalini tunaendelea kuchukua hatua
stahiki na kuimarisha jitihada na hatua za kuwachunguza wageni katika mipaka
yetu ya usafiri wa nchi kavu na usafiri wa anga. Tumejiandaa vya kutosha kutambua watu wenye
joto kubwa zaidi ya joto la kawaida la mwili wa mwanadamu. Hali kadhalika, tumewataka watu wanaoingia
nchini kueleza kama katika wiki tatu zilizopita wametembelea nchi za Guinea,
Sierra Leone na Liberia. Nia ya kutaka
waseme siyo kuwazuia wasiingie nchini bali kuwapa ushauri juu ya dalili za
ugonjwa wa Ebola na nini wafanye iwapo dalili hizo zitawatokea. Pia tunapenda kujua mahala watakapofikia ili
tuweze kuwafuatilia.
Ndugu Wananchi;
Ninawaomba
ushirikiano wa kila mmoja wenu kutoa taarifa kwa wakati mara mtakapoona mtu
mwenye dalili za ugonjwa huo ambazo ni homa kali ya ghafla, kutokwa na damu
mwilini, kutapika na kuharisha kwa wakati mmoja. Toeni taarifa ili wataalamu wenye ujuzi na
vifaa stahili vya kujikinga waweze kuja kuwahudumia ipasavyo wagonjwa wenye
dalili hizo. Jiepusheni na kumsogelea au
kugusana na mtu wa aina hiyo. Na, maiti aliyekufa
kutokana na ugonjwa wenye dalili hizo pia asiguswe. Kufanya hivyo ni kujiweka kwenye hatari ya
moja kwa moja ya kuambukizwa kwani huenda mtu huyo ni muathirika wa Ebola. Toa
taarifa upate maelekezo ya kitaalamu.
Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa
Ndugu Wananchi;
Kama mnavyofahamu
tarehe 14 Desemba, 2014 tutafanya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa ngazi ya
vitongoji, mitaa na vijiji. Tumelazimika
kufanya Uchaguzi huo mwezi Desemba, 2014 badala ya mwezi Oktoba kama
ilivyostahili kutokana na shughuli za Bunge Maalum la Katiba kuendelea hadi tarehe
4 Oktoba, 2014 kwa kupitisha Katiba Inayopendekezwa. Kutokana na Taifa kuwa katika jambo lile kubwa
ilionekana ni busara kuacha kwanza mchakato ule ukamilike kabla ya kufanyika
kwa uchaguzi huo.
Nimeambiwa
na TAMISEMI kwamba maandalizi ya uchaguzi huo yanakwenda vizuri na kwamba
ratiba imekwishatolewa, na majina ya mitaa, vijiji na vitongoji vipya nayo
yamekwishatolewa. Kazi ya kuandikisha wapiga kura itafanyika kuanzia tarehe 23 Novemba,
2014 na itamalizika kwa orodha ya wapiga kura kubandikwa mahali pa wazi hasa
kwenye mbao za matangazo katika vitongoji, mitaa, na vijiji husika ifikapo tarehe
30 Novemba, 2014. Kufanya hivyo kutawezesha
wananchi kukagua orodha hiyo kuona kama majina yao yapo, na kujiridhisha kuwa majina
ya wale walioandikishwa kwenye daftari hilo ni wapiga kura wenye sifa stahiki
za kupiga kura katika uchaguzi huo katika eneo husika. Nawasihi wananchi wote mjitokeze kwa wingi
kujiandikisha na kukagua orodha ya wapiga kura itakapobandikwa ili kufanikisha
zoezi hilo.
Kwa
mujibu wa ratiba ya uchaguzi vyama vya siasa vinapaswa kuwasilisha fomu za
wagombea wao kwa Msimamizi wa Uchaguzi kuanzia tarehe 20 hadi 22 Novemba,
2014. Kwa maana hiyo, wale wenye shauku,
nia na sifa za kugombea uongozi katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa,
wanapaswa kutega sikio ili kujua ratiba za uchaguzi na uteuzi ndani ya vyama
vyao ili wapate fursa ya kuteuliwa kugombea.
Napenda kuchukua fursa hii kuwahimiza wananchi wote wakiwa pia vijana na
wanawake wasibakie nyuma, wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi hizo na nyingine
katika Uchaguzi Mkuu ujao. Ratiba ya uchaguzi huo iliyotolewa na TAMISEMI
inaonyesha kwamba mikutano ya kampeni ya kuwanadi wagombea itafanyika kwa siku
14 kuanzia tarehe 30 Novemba, 2014 hadi tarehe 13 Desemba, 2014 siku moja kabla
ya siku ya kufanyika kwa uchaguzi huo.
Ndugu Wananchi;
Mfumo
wa utawala wa nchi yetu huanzia katika ngazi ya kitongoji na mtaa kisha kijiji,
kata na hatimaye taifa. Kwa hiyo
uchaguzi wa vitongoji, mitaa na vijiji ndiyo msingi wa uongozi na utawala wa nchi
yetu. Tukipata viongozi wazuri katika
ngazi hii ya msingi, tutakuwa tumefanikiwa sana katika kuimarisha utawala bora
na kuongeza kasi ya maendeleo yetu. Rai
yangu kwenu, wananchi wenzangu ni kuwa mjitokeze kwa wingi wakati wa kampeni kuwasikiliza
wagombea wetu wakijieleza, kisha tuwachague wale watu ambao sisi tunaona
wanatufaa. Lazima tutambue kuwa ngazi ya
vitongoji, mitaa na vijiji ndiyo msingi wa uongozi wa nchi yetu. Tukipata watu wazuri tutakuwa tumejenga msingi
imara wa uongozi katika taifa letu.
Watu wote
watakaojitokeza kugombea katika ngazi ya vitongoji, mitaa na vijiji vyetu ni watu tunaoishi nao
na kwamba tunawafahamu vizuri sana. Hatuna
budi kuvitendea haki vijiji, mitaa na vitongoji vyetu kwa kuwachagua viongozi wazuri
watakaokuwa chachu ya maendeleo katika maeneo yetu. Tukifanya makosa ya kuchagua watu wasiofaa
tuelewe kwamba tutakuwa tumejinyima fursa ya kuwa na viongozi bora kwa kipindi
cha miaka 5 ijayo. Pia tunaweza kuzua migogoro na kupunguza kasi
ya maendeleo katika maeneo yetu. Tusione
haya kuwashawishi watu wazuri wajitokeze kugombea.
Mchakato
wa Katiba na Kura ya Maoni
Ndugu wananchi,
Bunge
la Katiba lilikamilisha kazi yake ya kutunga Katiba mpya ilipofika tarehe 2
Oktoba, 2014 ambayo ilikuwa siku mbili kabla ya muda uliopangwa wa tarehe 4
Oktoba, 2014. Tarehe 8 Oktoba, 2014, Mwenyekiti wa Tume ya
Katiba aliikabidhi Katiba hiyo kwangu na kwa Rais wa Zanzibar kama yalivyo
matakwa ya Kifungu cha 28A(1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa mara nyingine tena nawapongeza kwa dhati aliyekuwa
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel John Sitta, Makamu wake Mhe.
Samia Suluhu na Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kwa kazi kubwa na nzuri. Wametupatia Katiba Inayopendekezwa inayojitosheleza
kwa kila hali. Nawapongeza pia Makatibu
wa Bunge, Sekretarieti yao na wafanya kazi wote. Bunge Maalum la Katiba linastahili pongezi nyingi
kwa kazi nzuri waliyofanya na hasa kwa kuikamilisha ndani ya muda wa uliopangwa
wa siku 130 tu. Baadhi ya nchi duniani
jukumu hili limechukua muda mrefu zaidi ya uliokusudiwa au hata kushindikana.
Tutakuwa
wachoyo wa fadhila tusipoipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uongozi
wa Mwenyekiti Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba na Makamu wake Mheshimiwa Jaji
Augustino Ramadhani pamoja na Wajumbe wote wa Tume hiyo. Tunawapongeza kwa
kutayarisha Rasimu nzuri ya Katiba ambayo ndiyo iliyoliongoza Bunge Maalum la Katiba
kupata Katiba Inayopendekezwa iliyo bora.
Kilichobakia ni kuwaachia wananchi kuamua kama wanaitaka Katiba
Inayopendekezwa au hapana. Watafanya
hivyo kwenye kura ya maoni itakayofanyika kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba na Sheria ya Kura ya Maoni iliyotungwa kutekeleza matakwa ya Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba.
Ndugu wananchi,
Miaka
ya nyuma kulikuwa na tangazo la sabuni ya Omo lililokuwa likisema “Uzuri wa
Ngoma Sharti Uicheze”. Uzuri wa Katiba Inayopendekezwa
siyo wa kuambiwa. Unahitaji uione, uisome na uielewe. Imeandikwa kwa Kiswahili rahisi na fasaha. Inasomeka na kueleweka kwa urahisi sana. Ni rai yangu kwamba wananchi wote muipate
nakala ya Katiba Inayopendekezwa na mjisomee.
Sheria imeniagiza kuichapisha Katiba hiyo kwenye gazeti la Serikali
ndani ya siku saba baada ya kukabidhiwa.
Nimekwisha kufanya hivyo. Aidha,
Sheria inaeleza kwamba Katiba Inayopendekezwa isambazwe kwenye magazeti ya
kawaida ndani ya siku 14. Zoezi hili ni
endelevu. Usambazaji wa Katiba Inayopendekezwa
unaendelea na utaendelea mpaka Kura ya Maoni itakapopigwa.
Wito
wangu kwenu Watanzania wenzangu ni kwamba msikubali kulaghaiwa na maneno ya wale
wachache wanaotaka kuturudisha nyuma na kutunyima fursa ya kupata Katiba iliyo bora
zaidi. Maana hapajawahi kutokea ushiriki
mpana kama huu katika kutengeneza Katiba katika nchi yetu. Pengine, hata kwingineko duniani si wengi
wametoa fursa kama tulivyofanya sisi.
Kura
ya Maoni
Ndugu wananchi,
Sheria
ya Kura ya Maoni iliniagiza kutangaza tarehe ya Kura ya Maoni katika Gazeti la
Serikali ndani ya siku 14 baada ya kupokea Katiba Inayopendekezwa. Nimefanya hivyo. Awali Sheria hiyo iliagiza Kura ya Maoni
ifanyike na matokeo yake yajulikane ndani ya siku 70. Waziri mwenye dhamana ya
Uchaguzi alipowauliza viongozi wa Tume ya Uchaguzi kuhusu utekelezaji wa
matakwa hayo ya Sheria, Tume ilisema isingweza kuendesha Kura ya Maoni ndani ya
muda huo. Mambo yanayojitajika ni mengi
mno ambayo hayawezi kukamilika katika muda huo.
Wakaomba wapewe muda zaidi.
Bahati nzuri Kifungu 51 cha Sheria ya Kura ya Maoni kimetoa mamlaka kwa
Waziri mwenye dhamana ya Uchaguzi baada ya kushauriana na Waziri anayehusika na
Uchaguzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kubadilisha masharti haya kama
kutakuwa na umuhimu wa kufanya hivyo.
Baada ya mashauriano
hayo, Mawaziri wenye dhamana ya uchaguzi wa pande zetu mbili za Muungano waliridhika
kuwa upo umuhimu wa kusogeza mbele muda ili kutoa fursa kwa Tume kukamilisha
taratibu inazowajibika kufanya. Hayo ni
pamoja na kuboresha Daftari la Kudumu la Mpiga Kura, matayarisho ya upigaji wa Kura ya Maoni na
mambo mengine kadhaa. Hivyo basi, tarehe
03 Oktoba, 2014, Waziri mwenye dhamana ambaye ni Waziri Mkuu kwa kutumia
mamlaka aliyopewa ya Kifungu cha 51 cha Sheria ya Kura ya Maoni, alitangaza kupitia
gazeti la Serikali kubadilisha sharti la siku 70 na kuacha Rais aamue siku ya
kupiga kura. Kwa sababu ya mabadilikio
hayo, tarehe 10 Oktoba, 2014 nilitangaza kupitia Gazeti la Serikali kuwa Kura
ya Maoni itakuwa tarehe 30 Aprili, 2015 ili kutoa fursa kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
kukamilisha taratibu zake. Katika
tangazo hilo pia, nilielekeza kuwa kampeni zitaanza tarehe 30 Machi na kuisha
tarehe 29 Aprili, 2014 siku moja kabla ya siku ya kupiga kura, kama ilivyo
desturi yetu katika upigaji kura hapa nchini.
Ndugu Wananchi;
Natambua
kuwepo dhana kuwa siku za kampeni ni 60.
La hasha! Siku za Kampeni
zinaamuliwa na Rais, kufuatia Kifungu cha 4 (2) b kisemacho: “Amri kwa ajili ya kura ya maoni
itakuwa kama ilivyo kwenye fomu iliyotajwa kwenye jedwali la Sheria hii, na
itaainisha:
(a) Katiba Inayopendekezwa kuandikwa;
(b)
Kipindi ambacho
kampeni kwa ajili ya Kura ya Maoni itafanyika;
(c) Kipindi ambacho Kura ya Maoni itafanyika”
Tume ya Uchaguzi ina
mamlaka ya kuruhusu vyama vya kijamii na vya kiraia kutoa elimu ya umma ndani
ya siku 60 kabla ya siku ya Kura ya Maoni.
Tume imepewa mamlaka hayo na Kifungu cha 5 (4) cha Sheria ya Kura ya
Maoni. Kwa sababu hiyo, nawaomba
Watanzania wenzangu tuzingatie matakwa ya Sheria ya Maoni ambayo imeelekeza
vizuri kuhusu lini Kura ya Maoni itafanyika na lini wadau watoe elimu kwa
umma. Naomba tuwe na subira mpaka hapo
Tume ya Uchaguzi itakapotoa maelekezo ya utekelezaji wa fursa husika kwa wadau.
Ndugu wananchi,
Ni
matarajio yangu kwamba wananchi wote mtajitokeza kwa wingi kwenda kuboresha
taarifa zenu kwenye Daftari la Kudumu la Mpiga Kura kama itakavyoelekezwa na
Tume ya Taifa ya Uchaguzi, na hatimaye itakapofika tarehe 30 Aprili, 2015
mtakwenda kwa wingi kupiga kura ya kuamua kuhusu hatma ya Katiba
Inayopendekezwa. Naomba mfanye uamuzi mzuri.
Fursa hii ni adhimu na ya kihistoria ambayo tukiipoteza huenda itachukua
miaka mingi kuipata tena. Mtakapokuwa
mnakwenda kupiga kura zingatieni maslahi yenu pamoja na ya watoto na wajukuu
zenu, maana Katiba ndiyo inayoweka misingi na mstakabali wa taifa letu sasa na karne
nyingine zijazo.
Hitimisho
Ndugu
Watanzania wenzangu,
Naomba
nimalizie kwa kuwasihi mjitokeze kwa wingi kushiriki katika Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa utakaofanyika tarehe 14 Desemba, 2014. Endeleeni kusoma Katiba Inayopendekezwa ili
muda utakapofika kila mtu atoe uamuzi stahiki na wenye maslahi kwa nchi
yetu. Nimezitaka Wizara na Taasisi zinazohusika
na utekelezaji wa makubaliano yetu na Serikali ya China na Vietnam kuchukua
hatua za ufuataliaji na wanipe taarifa. Narudia kutoa wito tuendelee kuchukua
tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Ebola. Nawaomba
muendelee kuiunga mkono Serikali yetu katika jitihada zake za kuiletea
maendeleo nchi yetu na watu wake.
Mwisho,
ingawa siyo kwa umuhimu, vijana wetu 297,488 wameanza mtihani wa taifa
wa kidato cha nne jana tarehe 3 Novemba, 2014.
Tuna imani wamejiandaa vya kutosha na wameandaliwa vyema na walimu,
wazazi na walezi wao kwa ajili ya mtihani huo.
Naungana na walimu, wazazi, walezi na Watanzania wote kuwatakia kila la
heri katika mtihani wao huo.
Mungu
Ibariki Afrika!
Mungu
Ibariki Tanzania!
Ahsanteni
Sana kwa kunisikiliza!
No comments:
Post a Comment