Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akihutubia Mkutano wa pili wa Kimataifa kuhusu Lishe na
Virutubisho (ICN2) uliofanyika katika ukumbi wa Makao Makuu ya Shirika
la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) jijini Rome, Italia juzi
Novemba 19, 2014.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akijadiliana jambo na baadhi ya wajumbe kutoka Tanzania wakati wa
mkutano huo wa ICN2 (kushoto) ni Balozi wa Tanzania nchini Italia,
James Nsekela na Msaidizi wa Rais katika Masuala ya Lishe Dkt. Wilbald
Lorri.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akibadilishana mawazo na Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango Maalum wa
Chakula Duniani (WFP) Ethria Cousin (kushoto) na Balozi Wilfred Ngirwa
wakati wa mkutano huo wa ICN2, uliofanyika juzi Novemba 19, 2014, Jijini
Rome Italy.
Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.
Mohammed Gharib Bilal, akifuatilia hotuba mbalimbali za viongozi
walioshiriki katika Mkutano huo wa ICN2. Kulia ni Mfalme Letsie III wa
Lesotho.
Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.
Mohammed Gharib Bilal (katikati) akibadilishana mawazo na Mkurugenzi
Mtendaji wa FAO Jose Graziano da Silva, wakati alipomtembea ofisini
kwake na kufanya naye mazungmzo, juzi Novemba 19, 2014. Kushoto ni
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Seif Rashid. Picha na OMR.
======= ======= =======
MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO AIWAKILISHA TANZANIA KATIKA
MKUTANO WA PILI WA KIMATAIFA KUHUSU LISHE NA VIRUTUBISHO JIJINI ROME,
ITALIA NOVEMBA 21, 2014
Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal Novemba 19,
2014 ameiwakilisha Tanzania katika Mkutano wa Pili wa Kimataifa kuhusu
Lishe na Virutubisho uliofanyika katika Makao Makuu ya Shirika la Kilimo
na Chakula la
Umoja wa Mataifa (FAO) jijini Rome Italia.
Mkutano
huu umefanyika ikiwa ni miaka 22 baada ya mkutano wa kwanza maarufu kwa
jina la ICN1 kufanyika katika jiji la Rome na kuazimia kuwa, upo
umuhimu wa kuhakikisha binadamu wanapata Lishe bora yenye virutubisho
ili kusadia kujenga afya ya binadamu duniani. Mkutano huu wa pili pia
umeandaliwa kwa pamoja na Shirika la Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO)
pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Mkutano
huo ulifunguliwa na Balozi wa Kudumu wa Italia katika Umoja wa Mataifa
Gianni Ghisi aliyesoma hotuba kwa niaba ya Rais wa Italia Giorgio
Napolitano ambapo alifafanua kuwa Rome inawakaribisha wawakilishi wan
chi mbalimbali na kwamba inatamani kuona mkutano huu unatoka na majibu
ya tatizo la lishe duni kwa watu wa mataifa mbalimbali.
Katika
siku ya ufunguzi pia hotuba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban
Ki-moon iliwasilishwa pamoja na uzoefu wa masuala ya Lishe kutoka Italia
ambapo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Italia
Paolo Gentiloni aliwasilisha hotuba yake huku akiwakaribisha washiriki
wa mkutano huu wa ICN2 katika jiji la Rome na kufafanua kuhusu matarajio
ya Italia katika mkutano wa sasa ukilinganisha na ule uliofanyika miaka
22 iliyopita.
Akiwasilisha taarifa ya
Tanzania, Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Bilal alitumia
nafasi hiyo kuwashukuru wadau wa Maendeleo ambao wamekuwa wakichangia
katika sekta za Afya na Kilimo na akafafanua kuwa Tanzania imepiga hatua
tangu ICN1 na sasa inahitaji kuona mkutano huu unatoka na maamuzi
yanayotekelezeka ili kuwasaidia wananchi wa mataifa mbalimbali hasa
watoto na akina mama wajawazito kuwa na uhakika wa lishe bora yenye
virutubisho.
Mheshimiwa Makamu wa Rais
alifafanua kuwa Tanzania imepiga hatua katika kupunguza vifo vya akina
mama na watoto ambavyo vingi vilitokana na lishe duni na kwamba serikali
ya Tanzania inaendelea kulipatia msukumo suala la lishe na virutubisho
kwa wananchi wenye uhitaji ili kujenga taifa lenye afya na lenye watu
wenye uwezo wa kusaidia nguvu zao katika kuleta maendeleo.
Akizungumza
siku ya pili ya Mkutano huo Baba Mtakatifu Fransis alisema haki ya
chakula bora si tu kuwa imetolewa na Mwenyezi Mungu kwa binadamu bali
pia ni haki inayoashiria utu na ambayo haipaswi kutolewa kama zawadi kwa
wanadamu.
Papa Fransis aliendelea kusema
kuwa, katika dunia ya sasa masuala ya chakula, lishe na mazingira
yametokea kuwaunganisha binadamu wa mataifa yote sasa kuliko ilivyokuwa
huko nyuma na akazitaka serikali za dunia kuhakikisha zinapunguza
utupaji wa vyakula sambamba na kuongeza mikakati ya kuhakikisha kila
mwanadamu anapata lishe bora.
ICN2 inatazama
pia kuhakikisha kuwa nchi zinakuwa na mikakati ya kupunguza utapiamlo na
kwamba chakula kinachopatikana kiwe kile kilichoboreshwa ama kuongezewa
virutubisho ili kusaidia jamii zinazokabiliwa na matatizo kama
utapiamlo kuepukana nayo
na hivyo kuwa na kizazi chenye afya
bora na chenye uwezo wa kutumika katika uzalishaji ama katika shughuli
mbalimbali za maendeleo.
Dkt. Margareth Chan,
Mkurugenzi wa WHO aliueleza mkutano huo kuwa suala la lishe ni mhimili
katika kufanya jamii inayoweza kukabiliana na magonjwa huku pia
Mkurugenzi wa FAO Jose Graziano da Silva akifafanua kuwa, shirika lake
linautumia mkutano huu unaoshirikisha nchi 172 kutoa mwongozo kwa dunia
kuhusu jambo hili muhimu katika maisha na hasa sasa ambapo tunaelekea
kukamilika kwa Malengo ya Milenia na kuanza malengo mapya.
Katika
mkutano huo, licha ya Mheshimiwa Makamu wa Rais, Tanzania pia
iliwakilishwa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Seif Rashid
pamoja na Waziri wa Mifugo Dkt. Titus Kamani sambamba na Naibu Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Dkt. Mahadhi Juma Maalim.
Sambamba
na kuhudhuria mkutano huo, Mheshimiwa Makamu wa Rais alipata fursa ya
kukutana na Jumuiya ya Watanzania wanaishi Italia na kufanya nao
mazungumzo kuhusu masuala mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa sambamba na
kukutana na Mkurugenzi wa FAO ambaye alionesha furaha yake kuhusu hatua
mbalimbali ambazo Tanzania imepitia na kuahidi ushirikiano zaidi katika
masuala ya Kilimo.
Mheshimiwa Makamu wa Rais
na ujumbe wake umeondoka kurejea nyumbani Tanzania tayari kuendelea na
shughuli nyingine za Kitaifa leo Ijumaa Novemba 21, 2014.
Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais
Rome, Italia
Novemba 21, 2014.
No comments:
Post a Comment