Sunday, November 2, 2014

Kila la Kheri Spika Makinda, Urais Bunge la SADC

Spika wa Bunge Mhe. Anne Makinda akiteta jambo na Spika wa Bunge la Afrika Kusini Mhe. Baleka Mbete kabla ya kuanza kwa kikao cha Mkutano wa Jukwaa la Mabunge ya Nchi wanachama wa SADC jana mjini Victoria Zimbabwe. Uchaguzi wa Rais wa Jukwaa hilo unafanyika leo ambapo Spika Makinda anaungwa Mkono na Nchi nyingi za SADC 

Na Owen Mwandumbya, 
Victoria Falls, Zimbabwe
 
Mkutano wa 36 wa Jukwaa la Mabunge ya Nchi wanachama wa SADC (SADC PF) ulioanza wiki hii mjini Victoria Falls nchini Zimbabwe na unatarajiwa kumalizika tarehe 3 Novemba, 2014, ikiwa ni baada ya kukamilika kwa ajenda ya Mkutano huu pamoja na kufanyika kwa uchaguzi wa Rais wa chama hicho atakayeongoza jukwaa hilo kwa miaka miwili ijayo.
 
Kauli mbiu ya mkutano huu ni “Bunge la kikanda la SADC – Wakati ni huu”  ama kwa lugha ya kimombo inasema “ SADC Regional Parliament – the Future is Now”.
 
Maneno yaliyo katika kauli mbiu ya Mkutano huu yamebeba ujumbe mzito sana wa Mabunge ya Nchi za SADC ikiwa ni dhamira ya dhati waliyokuwa nayo wanachama hawa ya kuundwa kwa Bunge la kikanda litakalokuwa na nguvu si tu ya kuzisimamia Serikali za Nchi Wanachama bali pia kuwa na uhalali wa kuhakikisha kuwa maamuzi na hata mikataba mbalimbali itakayofikiwa na chombo hiki katika ukanda huu vinatekelezwa katika nchi wanachama.
 
Pamoja na kwamba yapo mengi yaliyojadiliwa katika Mkutano huu wa Umoja wa Mabunge ya SADC hapa Zimbabwe, muhimu limekuwa ni uchaguzi wa Rais wa Jukwaa hili ambaye ataongoza jitihada za kufanikisha malengo ya chama hiki ya kufikia kuwa Bunge kamili ndani ya Miaka miwili ijayo yanafanikiwa. 
Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Anne Makinda amekuwa akipigiwa chapuo na Wajumbe wengi wa Mkutano ili aweze kukamata usukani wa kukiongoza chama hiki kwa miaka miwili ijayo baada ya Rais wa sasa ambaye pia ni Spika wa Mauritius Mhe. Abdool Razack Mahomed Ameen Peeroo, kumaliza muda wake. Kutokana na uungwaji mkono mkubwa alionao Mhe. Makinda ameibuka kuwa mgombea pekee na hivyo ni dhahiri atapitishwa na kukabidhiwa jukumu la kuongoza Jukwaa hili.
Msukumo wa Wajumbe wa Mkutano huu wa 36 kutaka Spika Makinda aweze kuongoza Bunge hili unatokana na heshima  na ushawishi mkubwa ilivyonayo nchi ya Tanzania katika nchi wanachama wa SADC swala ambalo linafanya wajumbe wengi wa Umoja huu waamini kuwa Mtanzania Makinda atasaidia sana kusukuma masuala ya Jukwaa hili kwa Wakuu wa nchi wanachama, kazi ambayo inahitaji mtu kutoka nchi inayokubalika na yenye sifa za kidemokrasia ya kweli kwa na hivyo kuweza kupenyeza na kufanikisha matakwa ya Bunge hili. 
Kukubalika kwa Tanzania katika Ukanda wa huu wa Afrika Kusini na chapuo anayopigiwa Makinda ya kuongoza Bunge la SADC vinatokana na historia iliyoandikwa na Tanzania kupitia harakati za Ukombozi wa Bara la Afrika kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 1960. Kuanzia wakati huo nchi ya Tanzania chini ya Uongozi wa hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, iliongoza mapambano ya ukombozi Barani Afrika na kutoa msaada mkubwa kwa Vyama vya ukombozi vya nchi za Kusini mwa Afrika kama vile, Zimbabwe (ZANU), Afrika Kusini (ANC naPAC), Namibia (SWAPO), Angola (MPLA) na Msumbiji (Frelimo). 
Uchaguzi wa Rais wa Umoja huu unafanyika tarehe 2 Novemba, 2014. Kwa taratibu za Jukwaa hili la Kibunge, nafasi hii hushikwa kwa kuzunguka kwa zamu miongoni mwa nchi wanachama. Kwa mzunguko huo hivi sasa ni zamu  ya Tanzania, Msumbuji, na Seychelles kuweka mgombea. 
Licha ya kwamba nchi tatu zina nafasi ya kusimamisha wagombea, tayari wajumbe wa mkutano kutoka mabunge mbalimbali za SADC wamekuwa wakifanya jitihada za Makusudi ili Spika Makinda aweze kupewa nafasi hii waweze kutumiza malengo waliyokuwa wamejiwekea. 
Makinda sio kwamba ni mgeni katika Umoja huu, ushawishi unaojitokeza na wajumbe hawa pia unasukumwa na mafanikio makubwa yaliyopatikana huko nyuma katika kipindi alichoshika nafasi ya Makamu kuanzia mwaka 2008 hadi 2010 akiwa Naibu Spika wa Bunge la Tanzania.
Katika kipindi hicho, Makinda aliweza kushirikiana na Rais wa Chama hicho kuhakikisha kuwa nguvu ya umoja huu hususani katika kukuza uwajibikaji na demokrasia katika nchi wanachama inakuwa kubwa. Aidha, ni katika kipindi hiki ambapo Wabunge wengi kutoka nchi wanachama waliweza kushiriki zoezi la Uangalizi wa Chaguzi kwa lengo la kuangalia kiwango cha Demokrasia katika nchi zilizokuwa na uchaguzi. 
Pamoja na kuwa Makinda alishawahi kuwa Makamu wa Rais wa chama hiki, pia ndiye aliyeongoza zoezi la uangalizi wa uchaguzi katika uchaguzi Mkuu wa Botswana mwaka 2009. 
Moja ya mambo makuu anayokumbukwa nayo wakati wa uongozi wake ilikuwa ni pamoja  na kuongoza ujumbe wa Wabunge wanawake kutoka nchi za SADC kwenda katika nchi za Botswana,  Malawi, Msumbiji na Zambia kwa lengo la kushawishi Mataifa hayo kuongeza idadi ya uwakilishi wa wanawake katika mabunge yao kuweza kufikia angalau asilimia 30.
 
Uchaguzi wa Rais wa chama hiki mwaka huu, unakuja kukiwa na matarajio makubwa ya kuwa na Bunge madhubuti la SADC ambapo Katibu Mkuu wa umoja huu Dkt. Esau Chiviya, anasema kauli mbiu ya mwaka inazingatia na kuhitimisha matarajio ya waasisi wa umoja huu ya kuwa na Bunge imara la ukanda huu wa SADC ambapo anaamini kuchaguliwa kwa Rais kulenge kwenda sambamba na uwezo wa kuweza kufanikisha jambo hili haraka iwezekanavyo. 
 
Kuanzishwa kwa Umoja wa Mabunge wanachama wa SADC kulifanikiwa tangu tarehe 8 Septemba, 1997, mjini Blantyre, Malawi, baada ya wakuu wa Nchi za SADC kupitisha azimio la kuanzishwa kwa Umoja huu ikiwa ni jitihada za kuelekea kuwa na Bunge la Ukanda litakalo kuwa na majukumu ya kujadili masuala ya kibunge na yenye maslahi ya ukanda huu katika ngazi ya kibunge
 
Ni dhahiri sasa watanzania tuna kila sababu ya kumuombea Makinda aweze kupitishwa kuwa Rais wa Umoja huu ili aweze kutimiza ndoto ya wanachama wa Umoja wa Mabunge ya SADC ikiwa ni pamoja na kuendelea kuiletea heshima Tanzania katika nyanja ya kimataifa.
Mataifa mengi duniani hujitahidi sana kuhakikisha kuwa viongozi na wananchi wao wanashika nafasi mbalimbali kubwa katika vyombo vya kimataifa ili kuendelea kuyatangaza majina ya mataifa yao. Tanzania hatuna budi kupiga chapuo jitihada hizi kwa lengo la kuongeza ushawishi wetu katika masuala ya kidiplomasia. 
Kwa hivi sasa Rais Robert Mugabe ndiye mwenyekiti wa wakuu wa nchi za SADC. Ni mtarajio  kuwa baada ya uchaguzi wa Makinda katika Mkutano huu, atasaidia kuendelea kumshawishi Rais Mugabe kuwa sasa nia na matarajio ya Umoja huu yaliyokuwepo tangu kuanzishwa kwake ili liwe Bunge madhubuti katika Ukanda huu linakuwa moja ya ajenda kuu katika Mkutano ujao wa wakuu wa Nchi za SADC unaotarajiwa kufanyika Mwakani 2015 nchini Botswana. 
Umoja huu wa Mabunge kutoka SADC ulianzishwa mwaka 1996 na malengo makuu yake ni kujadili na kufanikisha masula ya kibunge yenye maslahi kwa wananchi ukanda huu na ikiwa ni sehemu ya Wawakilishi hawa wa wanachi kubadilishana uzoefu ambapo katika mikutano yake kila Bunge huwakilishwa na ujumbe usiozidi wabunge sita ikiwa ni pmaoja na Maspika wao na uwakilishi ni sharti uzingatie jinsia na uwakilishi wa vyama uliopo katika Bunge. 
Kwa upande wa Tanzania, Makinda anaongoza ujumbe wa Wabunge watano ambao ni Mhe. Seleman Jafo, Mhe. Anna Abdalah, Mhe. Mohamed Mnyaa, Mhe. Goodluck Ole-Medeye, na Mhe. Stella Manyanya. 
Zaidi ya Wabunge 100 ikiwa ni pamoja na Maspika wa Mabunge ya kutoka nchi za Angola, Democratic Republic of Congo (DRC), Lesotho, Malawi, Namibia, Seychelles, Afrika Kusini, Swaziland, Tanzania, Zambia na Wenyeji Zimbabwe wanashiriki Mkutano huu. 
Ni wabunge kutoka Mauritius na Botswana tu ambao kwa sasa hawajaweza kushiriki kutokana na kuwa Mabunge yao yalivunjwa kupisha uchaguzi mkuu katika nchi zao. 
Kama Mtanzania na sote kwa pamoja tuunge mkono Spika Makinda kushika nafasi ya Rais wa Jukwaa la Mabunge ya Nchi za SADC. Kila la kheri Spika Makinda,
 

No comments: