Mkuu
wa Wilaya ya Uvinza Mwalimu Hadijah Nyembo (kulia) akitoa nasaha zake
kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali
Mstaafu Issa Machibya (wa pili kulia) kuzungumza na wakazi wa wilaya ya
Uvinza kwenye sherehe za uzinduzi wa kituo cha redio jamii Uvinza FM
mkoani Kigoma. Kutoka kushoto ni Meneja wa huduma za kijamii wa Airtel
Tanzania, Hawa Bayumi, Mshauri na Mkufunzi kutoka Shirika la Umoja wa
Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambao ndio wadhamini
wakuu wa redio Uvinza FM, Bi. Rose Haji Mwalimu na Mkurugenzi Mtendaji
wa Uvinza FM Radio Bi. Nuru Kalufya.(Picha na Zainul Mzige wa MOblog).
Na Mwandishi wetu, Uvinza - Kigoma
Mkuu
wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya amesisitiza
uadilifu katika vyombo vya habari jamii kwa kutangaza habari zisizoumiza
hisia kwa wananchi wengine na kuepuka migogoro.
Akizindua
kituo cha redio jamii cha Uvinza FM, Luteni Kanali Mstaafu Machibya
alisema kuwa vyombo vina wakati mgumu hasa katika kipindi cha kuelekea
uchaguzi mkuu mwaka 2015.
“Changamoto hii inaweza kuepukika kwa kuhakikisha habari zinazotolewa
zinalenga kuendeleza utamaduni wa amani, upendo, utulivu na uvumilivu na
kuepuka viashiria vinavyoweza kusambaza chuki kwa lengo la kufanikisha
chaguzi salama.
Mkuu
wa Mkoa huyo amesisitiza umuhimu wa kuutumia uhuru wa kutoa na kupata
habari vizuri kwa kusema kwamba uhuru huo usitumike kutoa habari
zinazopendelea upande mmoja na kukandamiza mwingine kwa kuwa hali kama
hiyo husababisha machafuko.
“Kwa
mujibu wa Ibara ya 18 (b) ya Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania
ya mwaka 1977, kila mtu anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari
bila ya kujali mipaka ya nchi, lakini haki hiyo iende sambamba kwa
kuzingatia Sheria za nchi na kuhakikisha habari hizo haziumizi hisia za
wananchi wengine,”
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya akisoma
risala wakati wa uzinduzi wa kituo cha redio jamii Uvinza FM ambapo
alilipongeza shirika la UNESCO kwa juhudi kuwaweka karibu wananchi na
serikali kupitia mawasiliano ya redio.
Luteni
Kanali Mstaafu Issa Machibya ameitaka redio jamii Uvinza kuonyesha
uwezo wao ili waweze kujitangaza na kujijengea imani kwa wanajamii wao
kuwa wanaweza. “Ni kwa hali hiyo tu mtaweza kujulikana, kutambulika na
kupata udhamini na matangazo ya kutosha.”
Amewataka
wanajamii kukitumia vyema kituo chao cha redio ili kiwe chachu ya
kuleta na kukuza maendeleo katika vijiji, wilaya, mkoa na taifa kwa
ujumla.
Wakati
huo huo Mkuu wa Mkoa ameitaka redio jamii ya Uvinza kutangaza habari
zenye kuonyesha madhara ya mila potofu na kujenga uelewa wa jamii kuhusu
mila hizo hususan mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino),
kufichua wagonjwa wanaohofia kuwa na dalili za ugonjwa wa ebola na
uharibifu wa mazingira.
Amelipongeza
shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na
Utamaduni (UNESCO) kwa kutoa msaada wa vifaa vya kituo hicho na
kuendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo wanahabari jamii, Kampuni ya simu
za mkononi ya Airtel kwa kuruhusu matangazo ya Uvinza FM Redio yarushwe
kupitia mnara wake na waanzilishi wa kituo hicho.
Mwalikishi wa Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni
(UNESCO) ambaye pia ni mshauri na mkufunzi wa redio jamii, Bi. Rose Haji
Mwalimu akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkazi wa UNESCO Tanzania,
Zulmira Rodrigues kwenye sherehe za uzinduzi wa kituo hicho cha redio
jamii Uvinza FM uliofanyika wilayani Uvinza mkoani Kigoma.
“Ninayapongeza
mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa na Airtel kwa ufadhili wao, Ruchugi
Salt Works na Asasi za kiraia (EHENA) kwa ushirikiano wao kwa jambo
hili”.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Mwalimu Hadijah Nyembo
amewakumbusha waandishi wa habari kuepuka kutangaza habari zinazoleta
hofu katika jamii kwa kutangaza habari zinazotoa maelezo ya ufafanuzi
kutoka chombo husika.
Amekemea
matumizi ya lugha isiyo sahihi na kutoeleweka kwa wasikilizaji kwa
kusema kwamba redio inalenga makundi yote ya umri kwa hiyo Matangazo
yalenge wananchi wote.
“Redio
Uvinza isiwe chombo cha propaganda, zingatieni mojawapo ya madhumuni ya
kuanzishwa kwa redio zenu ambayo yanalenga kuhamasisha mshikamano,
Amani, upendo, utulivu, umoja na utaifa, alisema Mwalimu Nyembo.”
Chombo cha habari jamii Uvinza FM Redio ni cha kwanza kuanzishwa mkoani Kigoma katika halmashauri mpya ya Uvinza.
"Hongereni sana UNESCO serikali inatambua mchango wenu",......
Ni maneno ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa
Machibya akimpongeza Mshauri na Mkufunzi kutoka Shirika la Umoja wa
Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambao ndio wadhamini
wakuu wa redio jamii Uvinza FM, Bi. Rose Haji Mwalimu kwa niaba ya
UNESCO. Katikati ni Mkurugenzi Mtendaji wa Uvinza FM Radio Bi. Nuru
Kalufya.
Chombo
hicho kimetakiwa kutumika kuwaunganisha wanajamii, kuepuka kutangaza
hisia au uvumi kwa kueleza ukweli na kuwatunzia heshima wasikilizaji wao
kwa kuwa wana haki ya kuheshimiwa na kutoumbuliwa masuala yao binafsi.
Uzinduzi
huo umeshuhudiwa pia na Mkuu wa wilaya ya Uvinza Mheshimiwa Mwalimu
Hadijah Nyembo, viongozi wa chama na serikali, viongozi wa dini, Shirika
la Umoja wa Mataifa (UNESCO), Kampuni ya simu za mkononi AIRTEL,
wanakijiji na wananchi wa halmashauri ya Uvinza.
Wengine
ni wanahabari 30 wanaohudhuria mafunzo ya maadili, jinsia na habari za
migogoro kijijini Uvinza, kutoka redio jamii za wilaya 8 ambazo ni
Karagwe, Bunda, Mwanza, Kahama, Sengerema, Maswa, Simanjiro, Loliondo,
Mpanda, Ngara. Kutoka Zanzibar ni Unguja North, na Southern Pemba
(Pemba).
Meneja
wa huduma za kijamii wa Airtel Tanzania, Hawa Bayumi, akitoa salamu kwa
wakazi wa wilaya ya Uvinza kutoka kampuni ya simu za mkononi ya Airtel
ambao wametoa udhamini wa mnara wao kurusha matangazo ya kituo cha redio
jamii Uvinza FM ili kupanua wigo wa usikivu kwa redio hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Uvinza FM Radio Bi. Nuru Kalufya akitoa neno la
shukrani kwa mkuu wa mkoa na wadhamini wa kituo hicho cha redio jamii
Uvinza FM.
Meneja
wa huduma za kijamii wa Airtel Tanzania, Hawa Bayumi akishiriki kutoa
burudani na kikundi cha wakinamama wachimba chumvi Uvinza.
Baadhi
ya viongozi wa dini na jeshi la polisi waliohudhiria uzinduzi
huo...Kutoka kulia ni Sheikh Mkuu wa wilaya ya Uvinza Hassan Hamisi, OCD
wa Wilaya ya Uvinza S.P Nobert Mahala, Mchungaji wa SDA, Pius Mutani,
Mchungaji wa EAG Uvinza, Daniel Magunge na Diwani wa kata ya Ngumka,
Abdallah Masanga.
Baadhi
ya waandishi wa habari kutoka redio mbalimbali za jamii waliokuwa
wakihudhuria warsha ya siku nane iliyokuwa ikiendelea kwenye kituo cha
redio jamii Uvinza FM na wakazi wa wilaya hiyo waliohdhuria sherehe za
uzinduzi wa kituo hicho.
Mkuu
wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya akikata utepe
kuashiria uzinduzi rasmi wa kituo cha redio jamii Uvinza FM chini ya
ufadhili wa Shirika la UNESCO na kampuni ya simu za mkononi ya Airtel
Tanzania. Wanaoshuhudia tukio hilo kutoka kulia ni Meneja wa huduma za
kijamii wa Airtel Tanzania, Hawa Bayumi, Mwalikishi wa Shirika la
Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambaye pia ni mshauri
na mkufunzi wa redio jamii Bi Rose Haji Mwalimu pamoja na Mkurugenzi
Mtendaji wa Uvinza FM Radio Bi. Nuru Kalufya.
Sasa kimezinduliwa rasmi.
Mkuu
wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya akifanyiwa
mahojiano mafupi ndani ya studio za redio jamii Uvinza FM na Mtangazaji
wa kituo hicho, Kadisilaus Simon mara baada ya kuzindua rasmi redio
hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya akisaini kitabi cha wageni ndani ya studio za redio jamii Uvinza FM.
Mtangazaji
wa kituo cha redio jamii Uvinza FM, Kadisilaus Simon akitekeleza
majukumu yake kwa furaha kabisa mara baada ya kupewa baraka na Mkuu wa
Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya.
No comments:
Post a Comment