Thursday, October 30, 2014

Spika Makinda apigiwa chapuo Urais Bunge la SADC


Na Owen Mwandumbya, Victoria Falls, Zimbabwe

Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Anne Makinda ameendelea kuungwa mkono na wajumbe wa Mkutano wa 36 ambao ni Maspika na Wabunge kutoka Umoja wa Chama cha Mabunge ambao ni wanachama wa  nchi za kusini wa Jangwa la Sahara (SADC PF) kugombea nafasi ya Urais ya Umoja huo ili aweze kuongoza kwa kipindi cha miaka 2 ijayo katika chama hicho.

Jitihada hizo zimeendelea kujitokeza hapa Victoria Falls ambako mkutano huo unafanyika baada ya baadhi ya Maspika wa Nchi za SADC pamoja na wabunge wao kuomba miada ya kukutana naye na kumwambia dhahiri kuwa nchi zao wanamuunga mkono na wangependa aweze kushiriki uchaguzi huo ili waweze kumchagua awaongoze katika kipindi cha miaka miwili kutimiza malengo waliyojiwekea katika umoja huo.

Mkutano huo wa 36 wa Wabunge wa SADC umeanza tangu tarehe 26 Oktoba 2014 hapa mjini Victoria Falls nchini Zimbabwe na unatarajiwa kumalizika tarehe 3 Novemba, 2014, na mojawapo ya agenda za mkutano huo ni uchaguzi wa rais wa chama hicho baada ya rais anaemaliza muda wake ambaye pia ni Spika wa Mauritius Mhe. Abdool Razack Mahomed Ameen Peeroo,kutakiwa kukabidhi madaraka kwa rais Mwingine atakayepatikana katika Mkutano huu baada ya kipindi chake kumalizika.


Uchaguzi wa rais wa Umoja huu wa mabunge ya SADC utafanyika tarehe 2 Novemba, 2014, ambapo kwa kuwa nafasi hii ni ya mzunguko kwa nchi za ukanda huu, kwa mzunguko uliopo hivi sasa nchi zinazopewa nafasi ya kuleta mgombea ni tatu ambazo ni Tanzania, Msumbuji, na Seychelles ambapo kila Spika kutoka nchi hizi atapigiwa kura ili aweze kupatikana mmoja wapo atakayeongoza Umoja huu kwa miaka miwili ijayo.

Licha ya kwamba wagombea ni watatu, tayari wajumbe wamkutano kutoka nchi mbalimbali za SADC wamekuwa wakifanya jitihada za Makusudi ili Spika Makinda aweze kupewa nafasi hii waweze kutumiza malengo waliyokuwa mamejiwekea.


Akizungumza na Mhe. Makinda mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Bunge hilo la SADC Mhe. Sylvianne Valmont kutoka Ushelisheli  amesema “tunajua kuwa wewe  sio kwamba ni mgeni katika Umoja huu, ushawishi unaojitokeza kutoka kwetu  unataokana na  mafanikio makubwa uliyoyaleta katika chama hiki pindi ulipokuwa Makamu wa rais wa Umoja huu mwaka 2008 hadi 2010”

Akielezea zaidi baadhi ya mafanikio ya uongozi wake akiwa Makamu wa rais Mhe. Valmont anasema ni jitiohada za makusudi  za kuongoza ujumbe wa Wabunge wanawake kutoka nchi za SADC kwenda katika nchi za Botswana,  Malawi, Mozambique na Zambia kwa lengo la kuwashaiwshi viongozi wa Mataifa hayo kuongeza idadi ya uwakilishi wa wanawake katika mabunge yao angalau kwa asilimia 30, zoezi ambalo lilifanikiwa sana.


Nae Mjumbe kutoka Swaziland Mhe. Sikhumbazo Ndlovu anasema Mhe. Makinda anaweza kuongoza umoja huu na kuupeleka kwenye mafanikio zaidi kutokana na ushawishi Mkubwa iliyonayo Nchi ya Tanzania  katika nchi wanachama wa SADC swala ambalo linafanya wajumbe wengi wa Umoja huu kuamini kuwa chini ya uongozi wake atasaidia sana kusukumu baadhi ya maswala ya chama hiki kwa Serikali za nchi wanachama.

 Kwa upande wake Makinda amewahakikishia Wajumbe wa Mkutano huo kuwa atahakikisha anatimiza matarajio ya wanachama wa umoja huu hususani kuufanya umoja huu kuwa bunge madhubuti la SADC cha msingi ni kuhakikisha wanampigia kura kama wanavyo ahidi.

Pamoja na hilo Mhe. Makinda anasema kukubalika kwa Tanzania katika Ukanda  huu wa SADC na kampeni inayofanywa ili aweze kuongoza Bunge hili la SADC unatokana na historia Tanzania iliyojiwekea tangu wakati wa Ukombozi wa Bara la Afrika mwanzoni mwa miaka ya 1960, ambapo Tanzania chini ya Uongozi wa hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, nchi yetu ilijitwalia heshima mbele ya uso wa kimataifa kutokana na mchango wake wa kulikomboa bara la  Afrika kutoka katika uongozi wa kikoloni hususan katika Kutoa mchango wa ukombozi kwa vyama vya ukombozi vya nchi za Kusini mwa Afrikakama vile, Zimbabwe (ZANU), Afrika Kusini (ANC na PAC),Namibia (SWAPO), Angola (MPLA) na Msumbiji (Frelimo).


Uchaguzi wa Rais wa chama hiki mwaka huu, unakuja kukiwa na matarajio makubwa ya kuanzishwa kwa Bunge madhubuti la SADC ambapo Katibu Mkuu wa umoja huu Dk Esau Chiviya, anasema kauli mbiu ya mwaka huu ambayo inasema “Bunge la kikanda la SADC – Wakati ni huu” inazingatia na kuhitimisha matarajio ya waasisi wa umoja huu ya kuwa na Bunge imara la ukanda huu wa SADC ambapo anaamini kuchaguliwa kwa rais wa umoja huo lazima kwende sambamba na uwezo wake kuweza kufanikisha jambo hili haraka iwezekanavyo. 

“ Tunaaamini rais tutakayempata katika mkutano huu unaweza kuharakisha kuweza kushirikiana na wakuu wanchi za SADC kuweza kufanya umoja huu kuwa Bunge kamili la SADC na lenye nguvu kimaamuzi” anasema Dkt. Chiviya

Kwa hivi sasa Rais Robert Mugabe ndiye mwenyekiti wa wakuu wa  nchi za SAD ambapo endapo  spika Makinda atachaguliwa kuwa rais wa chama hiki atasaidia kuendelea kumshawishi Rais Mugabe ili suala la kuanzishwa kwa Bunge hilo la ukanda wa SADC linakuwa moja ya agenda kuu katika Mkutano ujao wa wakuu wa Nchi za SADC unaotarajiwa kufanyika Mwakani 2015 nchini Botswana.

Katika mkutano huo wa mwaka wa umoja wa Mabunge ya SADC Mhe. Makinda anaongoza ujumbe wa Wabunge sita kutoka Tanzania ambao ni Mhe. Seleman Jafo, Mhe. Anna Abdalah, Mhe. Mohamed Mnyaa, Mhe. Goodluck Ole-Medee, na Mhe. Stella Manyanya.

Zaidi ya Wabunge 100 ikiwa ni pamoja na Maspika wa Mabunge ya nchi za SADC wanashiriki Mkutano huu.

No comments: