Imetolewa mjini Nzega, kwenye viwanja vya parking, Jumamosi tarehe 4, Oktoba, 2014.
UTANGULIZI: SAFARI YA KUAMINI/A JOURNEY OF BELIEVE!
Ndugu viongozi wa dini,
Ndugu viongozi wa kimila,
Ndugu wazee wangu mliopo hapa,
Ndugu Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya,
Ndugu Katibu wa CCM wa Wilaya,
Ndugu viongozi wa vyama rafiki mliofika hapa,
Waheshimiwa madiwani,
Wananchi wenzangu wa Nzega,
Mabibi na mabwana,
Salaams,
Awali ya yote nianze kwa kumshukuru mwenyezi mungu,
mwingi wa rehema na mwenye kurehemu, kwa kutujalia afya njema na kutukutanisha
hapa siku hii adhimu ya leo, maana ni kwa utashi wake tu tunaweza kuyafanya
haya yote.
Nitumie fursa hii kwa namna ya kipekee kuwashukuru
nyote kwa kuacha shughuli zenu kuja kunipokea na kushiriki mkutano huu. Mmenipa
heshima kubwa sana na mimi nawajibika tu kusema ‘ahsanteni sana’.
Mimi hapa ni aidha mtoto wenu, mjukuu wenu ama mdogo
wenu, mnapoacha shughuli zenu kuja kunisikiliza mimi, mnakuwa mmenitwisha mzigo
mzito sana. Ninajiona nawajibika kwenu kutoa utumishi uliotukuka. Ninajipa deni
la kuongeza bidii kubuni miradi itakayotatua shida zetu hapa Nzega, kupigana
kuondoa umaskini, ujinga na maradhi.
Sote tuliopo hapa ni mashahidi, kuwa tumefanya mengi
katika miaka hii minne ya uwakilishi wangu, maana kati ya hayo, mengi tumefanya
pamoja nanyi.
Tumeanzisha ujenzi wa High Schools nne, na zote ziko
katika hatua nzuri za utekelezaji. Tumeanzisha ujenzi wa barabara mpya zaidi ya
10 huko vijijini, barabara za lami zaidi ya km 10 hapa mjini, tumejenga
zahanati zaidi ya 20, tumejenga nyumba za walimu na wahudumu wa afya zaidi ya
30 huko vijijini, tumechimba visima zaidi ya 40 huko vijijini, tumefanikisha
kufufua kilimo cha zao la pamba na kukuza uzalishaji toka Kg 20,000 mwaka wa
kwanza mpaka zaidi ya Kg milioni 8 mwaka wa tano wa mradi, tumeweza kukuza
uzalishaji wa zao la alizeti toka Kg 50,000 mwaka wa kwanza wa mradi mpaka
zaidi ya Kg milioni 2 mwaka wa tatu wa mradi, tumeweza kuanzisha SACCOS mpya 9
na vikundi vya kushirikiana kiuchumi zaidi ya 100, tumeweza kuanzisha mradi wa
kuandikisha wanachama wa SACCOS, vikundi vya ushirika na vikundi vya kibiashara
kwenye hifadhi ya jamii ya NSSF. Tumeweza kulipia ada zaidi ya watoto 600
wanaotokea familia zenye uwezo duni kiuchumi na yatima. Tumeweza kudai haki
yetu ya ushuru wa huduma na miradi ya maendeleo toka Resolute Tanzania Ltd na
kufanikiwa kupata zaidi ya bilioni 3 na nusu mpaka sasa, na kujengewa High
School kule Lusu, Kituo cha afya kule Lusu, mabwawa ya maji vijijini,
kurekebishiwa mitambo ya kusafisha maji yanayokuja hapa mjini na kujengewa
maabara 10 kwenye shule zetu za Sekondari. Tusingedai haya, kwa hakika
tusingepewa. Orodha ni kubwa mno, siwezi kuyataja yote hapa.
Nitakuwa mtovu wa shukrani nisipokubali na kutambua ushiriki
wa karibu wa nyie wananchi wenzangu wa Jimbo la Nzega, Mbunge mwenzangu wa Jimbo
la Bukene, Madiwani wa Halmashauri yetu, Viongozi wenzangu kwenye Chama changu,
Viongozi wa vyama rafiki, Mkuu wa Wilaya, na Mkurugenzi na timu yake yote.
Leo si siku ya kukumbuka mapito yangu lakini ni siku
ya kutambua na kuthamini ugumu wa njia ya kuelekea mafanikio, ili tunapotamani
kusonga mbele tujue kinachotusubiri. Ugumu wa safari yangu umenipa umahiri,
ujuzi zaidi, ujasiri na uzoefu utakaohitajika sana kwenye ‘safari ya kuamini’ (a journey of believe) niliyotangaza kuianza.
Ugumu wa safari yangu umethibitisha usemi kuwa kwa
hakika mti wenye matunda matamu ndiyo unatupiwa mawe; falsafa hii ilinipa nguvu
ya kujitazama upya, kujitathmini na hatimaye kufanya uamuzi sahihi kuhusu hatma
yangu kisiasa na Tanzania yangu.
Si ugumu wa safari yangu kisiasa pekee ulionipa
ujasiri na utambuzi wa wajihi na uwezo wangu kiuongozi, bali pia historia ya
makuzi yangu, na mahitaji, matarajio, matamanio na kero za watanzania wenzangu.
ROHO YA UTHUBUTU
Nilipokuja nyumbani kugombea Ubunge kwa mara ya
kwanza, mwaka 2005, nilikuwa ndiyo kwanza tu nimehitimu mafunzo yangu ya digrii
ya udaktari, na nilikuwa kwenye mafunzo ya kazi ya udaktari kwa vitendo chini
ya usimamizi wa madaktari bingwa (yaani internship), sikuwa na ajira ya kudumu.
Sikuwa na uchumi wa kutisha. Nilikuwa nina ndoa changa sana. Sikuwa na nyumba
nzuri wala gari ya kifahari. Niliamini kwa kuwa mimi ni mzaliwa wa hapa, nina
ndugu na marafiki wengi, itawezekana tu kuwashawishi na kushinda ubunge.
Sikujua kuwa kuna zaidi ya undugu na urafiki kwenye siasa. HII INAITWA ‘Roho ya Uthubutu.’
ROHO YA KUTOKATA TAMAA
Kuna baadhi ya watu mwaka ule walinikejeli na kucheka
sana, kuna ndugu zangu na marafiki mbalimbali wa familia yetu walinikwepa kwa
kuwa tayari waliishatekwa na kambi nyingine. Hekima yangu ndogo ya ujana ule
ilinituma kuheshimu uamuzi na uchaguzi wao, maana ndiyo demokrasia, na
nilichokifanya ni kuendelea kuwaomba kura na kuwachangamkia kana kwamba tupo
nao pamoja.
Japokuwa niliona nafasi ya kushinda kwangu ni ndogo
sana, sikukata tamaa, nilijipa moyo na kuendelea kutumia fedha ndogo nilizokuwa
nazo kuwafikia wananchi wa jimbo letu katika kila kona. HII INAITWA ‘Roho ya Kutokata Tamaa.’
LIFT HUMKUTA ALIYE NJIANI!
Mwaka 2010 nikatia nia tena kuja kugombea Ubunge wa
jimbo la Nzega, mara hii nikiwa mgombea bora zaidi, mwenye matayarisho ya
kutosha. Kilichonitokea, sote hapa mashuhuda. Watu walioamini tumechezewa mchezo mchafu
walikuja nyumbani kwangu baada ya matokeo ya kura ya maoni, wengine na mabarua
ya kukata rufaa na ushahidi wa kilichofanyika, wengine na mapicha, wengine
wakilia, wengine wakitoa matamko makali sana dhidi ya viongozi wenzangu
chamani, wengine wakinishawishi nihame chama. Niliwatuliza, nikanyamaza,
nikaondoka Nzega. Mungu si Athumani, chama
changu kikanipa fursa ya kukiwakilisha kwenye uchaguzi ule. Nami sikukiangusha.
HII INAITWA: ‘Lift humkuta aliye
njiani.’
NCHI TAJIRI YENYE WATU MASKINI
Tanzania ni nchi tajiri sana lakini wananchi wake ni
maskini sana. Tanzania ina urithi wa kutosha wa watu, ardhi, siasa safi na
uongozi bora. Ni nchi yenye mlima mrefu kuliko yote Africa, ziwa lenye kina
kirefu kuliko yote Afrika, madini ya dhahabu na vito, gesi, ardhi yenye rutuba
na mabonde mengi ya nafaka, ng’ombe wengi, mito, maziwa, na watu wenye nguvu,
wastaarabu wanaopendana, walioshikamana kwa umoja wao na wanaoheshimiana na
kuvumiliana kwa tofauti zao.
Hizi ni tunu tulizorithi kwa wazee wetu.
Waasisi wa Taifa hili waliweka misingi ya nchi hii
kufanikiwa. Waliweka misingi ya Tanzania kutajirika. Hili ni fumbo kwa kizazi
chetu.
Waasisi waliweka
misingi ya kuthamini utu wa kila mmoja wetu, usawa wa kila binadamu, umoja na
mshikamano wa kitaifa, uhuru na mfumo wa kutuondoa kwenye umaskini na
kutupeleka kwenye uchumi imara wa kujitegemea.
Waasisi waliweka mfumo wa elimu ulionitoa mimi
uswahili kwetu Msoma Road na kunipeleka kwenye ulimwengu wa wasomi kwenye
makorido ya vyuo vikuu mashuhuri duniani. Waliweka mfumo ulionitoa mimi kwenye
lindi la umaskini wa kula mlo mmoja na kwenda shuleni bila viatu mpaka
ulimwengu wa kujenga hoja Bungeni na kuota ndoto ya kuwa Rais wa nchi yangu.
Wazazi wetu waliorithi nchi hii kwa waasisi wa taifa
letu wamefanya makubwa. Wameandaa mazingira na mikakati ya kututoa kwenye
uchumi wa nchi maskini zaidi duniani. Dira yetu ni kutoka huku na kuingia kwenye
uchumi wa daraja la kati kufikia mwaka 2025. Hii ina maana kwamba Rais
atakayerithi kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete atapaswa kuwa wa
kwanza kuiongoza Tanzania tajiri, Tanzania ya ndoto za waasisi wa Taifa letu.
JUKUMU LA KIZAZI CHETU
Waliotutangulia wamefanya kazi yao.
Ni jukumu la kizazi chetu sasa kuchukua wajibu huu
mzito wa kuliongoza Taifa hili kufikia ndoto za mababu zetu.
Ndoto za kwamba, tulipojitawala tulitaka uhuru wa kujitawala
wenyewe, uhuru wa kujiongoza wenyewe, uhuru wa kuchagua tunachotaka kufanya,
uhuru wa kuamua kuwa tunavyotaka.
Jukumu letu sasa ni kuhakikisha kuwa wale mama ntilie
na wamachinga wanaonyanyaswa kila siku na mgambo wa halmashauri zetu wanapewa
uchaguzi murua wa kufanya biashara zao kwa uhuru na ustawi bila wasiwasi wa
kumwagiwa chini chakula chao ama kunyang’anywa mali zao.
Wale wachimbaji wadogo wadogo wanaonyanyaswa na mfumo
kwa sababu ya ujio wa kasi wa ubepari na soko huria na ule wimbo mwanana wa
‘dunia ni kijiji’ na mwaliko wa wawekezaji kwa kisingizio cha kuleta mitaji na
teknolojia nao wana haki na uhuru wa kuchagua kuwa wachimbaji wa dhahabu, na ni
lazima awepo mtu atakayehakikisha kuwa uchaguzi wao wa kazi hii unalindwa na
mfumo wa uchumi wetu.
Wale waalimu, wauguzi, askari polisi, maafisa ugani na
watumishi wenzao wa umma waliojitolea kukubali kufanya kazi kwenye maeneo ya
mbali na mikoa ambayo ni ‘center’ kubwa za nchi na za wilaya zao, na wakakubali
kuishi kwenye nyumba zisizo umeme wala maji ya uhakika, wakakubali kuishi
kwenye vijiji visivyo na mawasiliano ya simu wala ya intaneti, wanastahili
kutambuliwa na kuthaminiwa kwa kuwa wanafanya kazi iliyowashinda wenzao. Lazima
awepo mtu atakayewawekea mfumo wa kipekee wa motisha unaoendana na uwiano wa umbali,
jiografia na mazingira ya kazi. Kwa akili ya kawaida tu, hatupaswi kuwalipa sawa
walimu wetu wa shule ya Sekondari Chifu Ntinginya na wale wa Shule ya Sekondari
Mwakashanhala. Mwakashanhala walimu wako wanne, na nyumba iko moja. Wote
wanaishi humo. Wa Mwakashanhala hana mahali atapata nyumba ya kupanga. Wa Nzega
Mjini ana chaguzi za kutosha za nyumba za kupanga.
Wale wakulima wanaotengeneza zaidi ya asilimia 80 ya
nguvu kazi ya Taifa letu ni lazima wapewe huduma bora za ugani, walime kisasa
na kwa tija; wajengewe miundo mbinu ya umwagiliaji, ili walime na wavune kwa
uhakika.
Wale wazee, walemavu, akina mama wajawazito na watoto
wapate ile haki yao ya kutibiwa bure mahospitalini bila kutakiwa kwenda kununua
dawa ama vifaa kwenye vituo vya private. Ni kwa faida gani sasa tunasema
tunawapa huduma za afya bure wakati hatuna dawa za kuwapa, ama vifaa vya
kutolea huduma?
Ni jukumu la viongozi wa kizazi hiki kubuni mbinu mpya
za kuhakikisha huduma za afya zinakuwa bora na za uhakika kwa kila mtanzania;
kwamba, watanzania wote wanakuwa na bima ya afya na bima ya maisha; kwamba
watanzania wote wanakuwa na hifadhi ya jamii bila kujali wapo kwenye ajira
rasmi ama ni wakulima, wajasiriamali ama wachuuzi wadogo wadogo.
Ni jukumu la viongozi wa kizazi hiki kubuni mbinu mpya
za kuhakikisha kila mtanzania anakuwa na motisha ya kufanya ugunduzi na
ubunifu; kwamba, watoto wetu wanapenda zaidi masomo ya sayansi na wanakuza vipaji
vyao.
Kwamba, wanamichezo wetu na wasanii wanang’aa si tu
ndani ya mipaka ya nchi yetu bali pia kimataifa na wanafaidika na kazi ya
ubunifu wao.
Ni jukumu la viongozi wa kizazi chetu kubuni mbinu
mpya zitakazodumisha nidhamu ya kazi na uwajibikaji, uzalendo na uadilifu, na
zitakazotokomeza mbali kabisa rushwa, ubadhirifu, unyonyaji, ukandamizaji, wizi
na matumizi mabaya ya ofisi za umma.
Ni jukumu la viongozi wa kizazi chetu kuhakikisha
tunatanua mtandao wa barabara zetu, tunaongeza ufanisi wa reli na bandari zetu,
tunarahisisha usafirishaji wa malighafi na bidhaa baina ya mikoa yetu,
tunaongeza ufanisi katika mfumo wa biashara zetu za ndani na za kimataifa.
Ni jukumu la viongozi wa kizazi chetu kuhakikisha
tunaboresha mfumo wa kibenki toka vijijini mpaka mijini ili kuona wakulima na
wafanyakazi wetu kule vijijini wana fursa za kupata huduma za kifedha na
mikopo, na wale wafanyabiashara wakubwa wanapata fursa za kuuza bidhaa
zinazozalishwa nchini kwa faida na kwa urahisi.
Tanzania ya leo si Tanzania ya mwaka 1990. Nzega ya
leo si Nzega ya mwaka 1985. Wazee wa leo
si wale wa miaka ile. Sura nyingi ni ngeni, si zile za utoto wangu. Nyumba
nyingi ni mpya, si zile za uswahili kwetu Msoma road.
Barabara za Nzega ya leo si zile za miaka ya 2000.
Kila kitu kimebadilika. Uongozi wa Taifa letu hauwezi kubaki ule ule. Majina ya
viongozi wa Taifa letu hayawezi kubaki yale yale. Fikra za kuongoza Taifa
haziwezi kubaki zile zile. Staili ya kuleta mapinduzi haiwezi kuwa ile ile.
WAZEE WETU WAMEWEKA MATUMAINI KWETU
Wazee mashuhuri wa Taifa hili wako wapi leo hii?
Wazee mashuhuri wa Nzega wako wapi leo hii? Akina Mzee
Mshindo, akina Mzee Ramadhani Mtwale, akina Sheikh Abdallah Kassa, akina RR
Nyembo, akina Chief Kisute, akina Chief Humbi, akina Chifu Msoma, akina Chifu
Ntinginya, akina Ibhambangulu, wako wapi leo hii?
Wote hawa walitenda mambo ya hekima katika uhai wao,
wakawa wenye kuvuma kwa sifa zao na matendo yao. Nasi tukajifunza kwao,
tukapata ujasiri, tukapata umahiri, tukapata hekima, tukapata nguvu ya kutamani
kufanya makubwa kwa ajili ya Nzega yetu, na makubwa zaidi kwa ajili ya Taifa
letu.
Huko waliko wazee wetu najua wanatutazama na
kutabasamu bila shaka wakiamini kuwa majukumu waliyotuachia tunayaweza. Nasi
tunawaahidi kuwa tutawaenzi kwa kutenda yaliyo mema kwa Taifa letu na watu
wake, kwa Nzega yetu na watu wake.
UONGOZI NA UJANA
Kuna watu wanakejeli ndoto za viongozi wenye taswira
ya ujana kama mimi, wanadhani na wanaamini kuwa uongozi ni uzee na uzoefu. Mimi
siwashangai wala sitaki kuwapinga, na hapa simaanishi kuwajibu. Ila nataka
wafahamu ya kuwa uzee ama ujana siyo sifa pekee ya kuwa kiongozi mzuri.
Kuna vijana walipewa uongozi bila ya kuwa na uzoefu
wowote ule kwenye serikali: akina Tony Blair wa Uingereza, Lee Kuan Yew wa
Singapore, Thomas Sankara wa Burkina Faso,Mwl. Julius Nyerere, Baba wa Taifa
letu, hawa wote walifanya makubwa ya kupigiwa mfano. Kuna wazee walipewa
uongozi, na wakafanya mabaya na ya aibu kubwa si tu kwa mataifa yao, hata kwa
walimu wao na familia zao.
Mimi ninaamini Tanzania ya leo inahitaji kiongozi
mbunifu, mweledi, mwenye uthubutu, mwenye msimamo thabiti, mwenye uzoefu wa
dunia ya biashara, dunia ya haki, fursa na usawa kwa watu wote, dunia ya
utandawazi na diplomasia ya kiuchumi, dunia ya utawala bora, awe anamuogopa
Mungu lakini asiyetumia dini kama silaha ya kimkakati ya kumpa uongozi, na mzalendo
anayechukia rushwa, pia asiyetumwa na kundi lolote lenye maslahi; na sifa kubwa
kuliko zote awe anayeweza kuleta mapinduzi ya mfumo wa uendeshaji nchi. Kwamba
awe mzee ama kijana, kwangu si hoja sana.
Uongozi ni kuwa tayari kusikiliza kero na matatizo ya
unaowaongoza, ukajua yanayowasibu na ukajipanga kuyatafutia ufumbuzi. Uongozi
ni kujua mahitaji, matamanio na matarajio ya watu wako, ni kujua ndoto zao na
ukazitafutia namna ya kuzitimiza. Uongozi ni wito wa utumishi kama ulivyo
udaktari, ualimu ama utumishi wa Mungu.
Uongozi wetu katika zama hizi ni lazima uwe wa
kimapinduzi na wenye fikra mpya na zinazoendana na wakati, unaoweza kuleta
mabadiliko katika hali za watanzania kwa haraka na kwa uhakika. Ni lazima ujue
kuwa hatuwezi kuendelea bila kuwa na mfumo imara wa kilimo na viwanda
vinavyoongeza thamani ya mazao na bidhaa za kilimo, mfumo ambao utazalisha
ajira za kutosha kwa watu wote, kuanzia wakulima wadogo mpaka wakubwa, wafanyabiashara,
wasomi na wachukuzi.
HITIMISHO
Ndugu wananchi wenzangu wa Nzega, nimalize kwa kuwashukuruni
nyote, kwa mara nyingine tena, kwa kuja kunipokea nyumbani, na zaidi kwa
kunisikiliza. Nimalize kwa kusema kuwa; tulianza safari ya kuamini kwa kumuomba
Mungu aliye juu, niwahakikishie kuwa tutaendelea kuwa naye safarini na
tutamaliza naye, na kwa hakika Mungu atafanya maajabu yake; maana hajawahi
kushindwa na kitu.
Mungu awabariki sana. Mungu ibariki Nzega, Mungu
ibariki Tanzania.
No comments:
Post a Comment