Thursday, October 16, 2014

ELIMU YA URAIA NA UPIGAJI KURA HAIPASWI KUWA NA UTASHI WA KISIASA WALA UPENDELEO

DSC_0087
Afisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa shirika la kimataifa la sayansi, elimu na utamaduni (UNESCO) Bwana Al Amin Yusuph akielezea madhumuni ya warsha ya wadau wa mradi wa uchaguzi 2015 unaolenga kuboresha demokrasia amani nchini katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu ujao, unaofadhiliwa na Shirika La Kimataifa la Maendeleo (UNDP) ulioenda sambamba na mkutano wa tano wa Mtandao wa vyombo vya habari vya Kijamii nchini (COMNETA).

Na Mwandishi wetu
Uchaguzi huru na wa haki utafanikiwa iwapo wananchi watapewa elimu sahihi  ya uraia na upigaji kura itakayohamasisha wapiga kura kufanya maamuzi sahihi wakati wa uchaguzi.

Hayo yamesemwa na Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji John Mkwawa kwenye washa ya siku nne ya wadau wa utekelezaji wa mradi wa uchaguzi unaolenga kuboresha demokrasia na amani nchini kuelekea uchaguzi mkuu ujao .

Kamishina alisema elimu ya uraia ni muhimu kwa wananchi ili kuwahamasisha ushiriki wao katika demokrasia na kwamba haipaswi kuwa na utashi wa kisiasa au upendeleo kwa chama chochote cha siasa.

Akitoa mada katika warsha hiyo inayofadhiliwa na shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia maendeleo (UNDP) Jaji Mkwawa alisema katika kutoa elimu hiyo wanahabari hawana budi pia kuzingatia miongozo iliyowekwa ya kutofungamana upande wowote kisiasa na kutoa habari kwa usahihi kuhakikisha kwamba makundi yote yanapewa fursa na haki sawa.
DSC_0169
Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji John J. Mkwawa, akitoa mada kwa wadau wa utekelezaji wa mradi wa uchaguzi unaolenga kuboresha demokrasia amani nchini  (DEP) katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu ujao, unaofadhiliwa na Shirika La Kimataifa la Maendeleo (UNDP) ) katika warsha ya siku nne inayoendelea mjiji Dodoma. Kutoka kulia ni Afisa Habari na Mahusiano Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Bi. Salha Ali, Bi. Margaret Rugambwa mtalaam wa masuala ya jinsia na jamii kutoka UN Women na Mgeni rasmi Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo (UNDP) Godfrey Mulisa ambaye pia ni Mtaalam wa masuala ya utawala bora kutoka UNDP.
DSC_0124
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo (UNDP) Godfrey Mulisa akisoma risala ya ufunguzi wa warsha hiyo kwa niaba ya Philippe Poinsot inayoendelea kwenye ukumbi wa mikutano ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma.

“Pamoja na changamoto zinazozikabili redio jamii, zina mchango mkubwa katika mchakato wa uchaguzi kwa sababu idadi kubwa ya Watanzania hawajui kusoma na kuandika hivyo kutegemea redio. Kwa misingi hiyo ni vyema kwa waandishi wa habari wa redio jamii kusaini mwongozo wa maadili ambayo yataonyesha utekelezaji wao kwa kutopendelea chama chochote cha siasa au mgombea yoyote yule ”.

Amependekeza pia umuhimu wa kuielewa jamii inayolengwa wakati wa kutayarisha vipindi vya elimu ya uraia na utekelezaji ili  taarifa zinazotolewa kwao zikidhi matakwa ya sehemu hiyo.

Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji John Mkwawa ametoa mfano wa kuilewa jamii kuwa ni pamoja na kufahamu sababu zinazowafanya wananchi wasijitokeze kwa wingi katika upigaji kura iwapo kunasababishwa na ukosefu wa taarifa muhimu na sahihi, kukosa motisha ya kupiga kura, utashi na kutokuwepo kwa ushindani katika kugombea.

“Katika uchaguzi mkuu mwaka 2010 watu wachache sana walijitokeza kupiga kura pamoja na jitihada zote za kuhamasisha na kuelimisha upigaji kura, na baadhi ya sababu ni kwamba kupiga kura hakutampa faida yoyote mpiga kura, au kupiga kura hakutaleta mabadiliko yoyote na kutouamini mfumo mzima wa uchaguzi”.
DSC_0005
Mwenyekiti wa mtandao wa vyombo vya habari vya kijamii Tanzania (COMNETA) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Redio ya Jamii  FADECO wilayani Karagwe, Bw.Joseph Sekiku akieleza kwa ufupi maendeleo ya  COMNETA wakati wa sherehe za ufunguzi za mkutano wa tano wa Mtandao wa vyombo vya habari vya Kijamii nchini (COMNETA) unaofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma.

Masuala mengine yanayopaswa kufahamika ni sehemu wanakoishi walengwa ili kubaini iwapo kuna miundombinu ya kutosha hususan kiwango cha elimu na uelewa wao katika masuala ya uchaguzi ili kurahisisha utekelezaji wa mradi husika.

Amezishauri redio za jamii pia kuelewa ni mabadiliko gani yametokea katika uongozi wa uchaguzi, kanuni na maelekezo ya uchaguzi na sababu mbalimbali zinazotakiwa kuwafahamisha walengwa wa makundi mbalimbali wakiwemo wanawake, watu wenye ulemavu, vijana na makundi maalum hususan wazawa, wachungaji, watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi na Watu wenye ulemavu wa ngozi ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchaguzi.

Wakati huo huo Godfrey Mulisa akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkazi wa UNDP Philippe Poinsot alikumbusha baadhi ya masuala muhimu yanayotakiwa kufanyinywa na redio za jamii katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2015.


Ameyataja masuala hayo kuwa ni kuibua mapema maovu mbalimbali yanayohusiana na uchaguzi yanayoweza kujitokea ili yarekebishwe mapema, ukiukwaji wowote wa upigaji kura utakaoenda kinyume cha sheria, kuhamasisha watu wenye sifa za kupiga kura wajitokeze kwa wingi na kutoa ulingo kwa vyama vya siasa kuelezea sera za vyama vyao vya siasa kwa wapiga kura wao.

Mambo mengine ni kuibua matukio yanayohatarisha amani na utulivu, kuwaelezea wapiga kura kwa ufasaha na lugha rahisi sheria za uchaguzi, kuwaeleza wananchi umuhimu wa kupiga kura na masuala muhimu yanayowahusu hususan wazee, wanawake, maskini na wasiofikiwa kwa urahisi.

Mulisa pia amezitaka redio za jamii kuendesha mijadala kwa kuwashirikisha wananchi na vyama visivyo vya kiserikali, kuhoji miradi ya maendeleo ya taifa na kuchangia taarifa endelevu kwa maendeleo.

Akielezea madhumuni ya warsha ya wadau wa mradi wa uchaguzi 2015, Afisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa shirika la kimataifa la sayansi, elimu na utamaduni (UNESCO) Al Amin Yusuph, alisema kukutana kwa wadau wakubwa wa uchaguzi kunalenga kukumbushana majukumu yaliyoko katika uchaguzi hususan kujisajili kwa wapiga kura kutokana na mchango mkubwa wa redio jamii katika kufikisha ujumbe, kuwa na dhamana, kuwahamasisha na kuwaelimisha jamii na  pia kuboresha sera za mtandao wa redio jamii nchini.
DSC_0282
Sehemu ya washiriki wa redio mbalimbali za jamii nchini wakifuatilia kwa umakini mada zilizokuwa zikiwasilishwa kwenye warsha hiyo inayoendelea mjini Dodoma.

“ Matatizo ya vitambulisho vipya elimu ni muhimu, kuhamasisha mchakato wa demokrasia wananchi ambao uweo wao sio mkubwa kuwafikia hususan wanawake ambao wanakosa fursa za kupiga kura na hawana nyenzo za kupata habari, vijana nao hawapendi kujisajili na kupiga kura na vile vile kuna vijana waliofikia umri wa kupiga kura, wote hawa wanahitaji elimu”.
Warsha hiyo ya siku nne imeandaliwa kwa ushirikiano wa wadau wakubwa wa mradi huo wa DEP ambao ni UNESCO, Ofisi ya msajili wa vyama vya siasa (RPP), NEC na ZEC.

Warsha hiyo pia inawashirikisha washiriki 31 wa mtandao wa redio jamii Tanzania (COMNETA) unaotekeleza mradi wa demokrasia na amani kuelekea uchaguzi mkuu 2015 unaofadhiliwa na mfuko wa mashirika ya maendeleo 10 ambayo ni Canada, Uingereza (DFID), Denmark, Umoja wa Ulaya na Finland. Nyingine ni Ireland, Norway, Sweden, Switzerland na mfuko wa Umoja wa Mataifa.
DSC_0251
DSC_0214
Makamu wa Msajili wa vyama vya siasa nchini, Bw. Ibrahim Sapi Mkwawa, akitoa salamu kutoka ofisi ya msajili wa vyama vya siasa inayoratibu mradi wa uchaguzi unaolenga kuboresha demokrasia amani nchini  (DEP) katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu ujao, unaofadhiliwa na Shirika La Kimataifa la Maendeleo (UNDP) ) katika warsha ya siku nne inayoendelea mjiji Dodoma.
DSC_0063
Mtaalamu wa masuala ya uchaguzi kutoka UNDP, William Hogan akiwasalimia washiriki wa warsha hiyo.
DSC_0119
Baadhi ya maafisa kutoka ofisi ya msajili wa vyama vya siasa nchini wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikitolewa kwenye warsha hiyo inayoendelea mjini Dodoma.
DSC_0202
 Afisa Habari na Mahusiano Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Bi. Salha Ali, akielezea mahusiano ya tume yake na vyombo vya habari vya jamii visiwani Zanzibar.
DSC_0219
Mshauri na Mkufunzi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Bi. Rose Haji Mwalimu akihoji swali kwa watoa mada wakati wa warsha hiyo ya siku nne inayoendelea mjini Dodoma.
DSC_0259
Makamu Mwenyekiti wa COMNETA ambaye pia ni Meneja wa Kituo cha Habari na Mawasiliano cha Telecentre Sengerema FM mkoani Mwanza  Bw. Felician Ncheye akitoa maoni yake wakati wa kujadili mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa kwenye warsha hiyo.
DSC_0320
Nuru H. Chuo kutoka Tandabui Health Access Tanzania/Afya Radio Mwanza akishiriki kuchangia maoni kwenye vikundi kazi.
DSC_0302
Washiriki wakijadiliana kwenye vikundi kazi.
DSC_0348
Khadija Aboud kutoka Zanzibar Youth Organization Network (ZAYONET) akiwasilisha kazi ya kikundi wakati wa warsha hiyo ya siku nne inayoendelea mjini Dodoma.

No comments: