Hassan Tofi mmoja wa washiriki wa Shindano la Dance 100% wa Kundi la Best Boys la Kigamboni jijini Dar es Salaam,akiwaongoza wenzake katika mazoezi yao yanayofanyika katika Viwanja vya Don Bosco Upanga ikiwa ni sehemu ya kujindaa na fainali ya shindano hilo litakalofanyika hivi karibuni. Shindano hilo limeandaliwa na EATV na kudhaminiwa na Vodacom Tanzania.
WADAU wa muziki nchini wamewapongeza waratibu wa shindano la Dance 100% ambalo limefikia hatua ya fainali, baada ya makundi matano kupenya nusu fainali, Jumamosi iliyopita.
Kivumbi hicho kilichoshindanisha makundi 10 yalipenya hatua ya robo fainali, Iliyofanyika Viwanja vya Don Bosco, jijini Dar es Salaam na kuvuta hisia za wengi kutokana na umahiri wa kila kundi.
“Nikiwa miongoni mwa watu waliojitokeza kushuhudia shindano hili, nimepata burudani kubwa na kujifunza mengi, vijana wameonyesha vipaji na uwezo wa kiwango cha hali ya juu,” alisema Ramadhan Malenge ‘Ramso.’
Malenge alisema kilichomvutia katika shindano hilo, ni kuona namna vijana walivyoonyesha uwezo mkubwa kiasi cha kuwapa wakati mgumu majaji kuamua ni kundi gani la kutoka.
Alisema, hata vijana walioishia hatua hiyo ya nusu fainali, bado ni wenye uwezo kwani wamenufaika na mengi katika shindano hilo na kuwasihi wasiache kujiendeleza kimuziki.
Malenge aliyejitambulisha kama mpenzi na shabiki mkubwa wa muziki, alisema kwa jinsi vijana walivyokuwa wakicheza staili mbalimbali kwa ustadi mkubwa, ungetamani makundi yote yavuke, japo ni kitu kisichowezekana.
Ramso alisema kwa umuhimu wa programu hiyo katika kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana, waratibu wa shindano hilo, kituo cha televisheni cha East Africa (EATV) na kudhaminiwa na Vodacom Tanzania, wanastahili pongezi.
Alisema, kama ngazi ya nusu fainali ilikuwa na ushindani wa kiwango alichokishuhudia Don Bosco, majaji wa shindano hilo watakuwa na kibarua kigumu zaidi siku ya fainali.
Makundi ya yaliyofanikiwa kuingia katika hatua ya fainali, ni Wazawa Crew, Best Boys Crew, The W.T, Wakali Sisi na The Winners Crew. Shabiki mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Blandina Kingu‘Queen B,’ mbali ya kupongeza uwepo wa shindano hilo, ametoa ushauri wa bure kwa mchujo uwe unafanyika mikoa yote kabla ya fainali kufanyika jijini Dar es Salaam.
Naye mratibu wa mashindano hayo, Happy Shame alikiri kuwepo kwa ushindani mkubwa zaidi ikilinganishwa na miaka mingine miwili iliyopita huku jamii ikizidi kulipa sapoti.
“Huu ni mwaka wa tatu EATV tunaandaa mashindano haya chini ya udhamini wa Vodacom Tanzania, safari hii yamezidi kuwa na umaarufu na ushindani kiasi cha kuwavutia vijana wengi ambao hujitokeza kushiriki,” alisema Shame.
Shame, aliongeza kundi litakaloibuka kidedea katika shindano hilo linalorushwa na kituo cha EATV kila Jumatano saa 1:00 usiku, litajishindia kitita cha shilingi milioni 5.
Naye Meneja Uhusiano wa Umma wa Vodacom Tanzania ambao ni wadhamini wakuu wa shindano hilo, Matina Nkurlu aliwapongeza vijana wote huku wakiwapa moyo walioshia hatua ya nusu fainali.
“Vodacom tunaamini, vijana ni chachu ya mapinduzi katika sekta mbalimbali kama watawezeshwa, hivyo tunadhamini mashindano haya tukiamini kuwa vijana wenye vipaji wanaoshiriki wataweza kujitangaza na kujulikana ambapo katika siku za usoni ni rahisi kujiajiri kupitia katika sanaa” anasema Nkurlu.
Alitoa wito kwa wakazi wa jijini Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi katika fainali ya shindano hilo itakayofanyika hivi karibuni kuwatia moyo vijana na kununua bidhaa za Vodacom kwa bei nafuu katika shindano hilo kama Modem na Simu aina ya Samsung E1205 zote zikiuzwa kwa shilingi 25,000.
No comments:
Post a Comment