Rais Mstaafu wa awamu ya Tatu,
Mhe. Benjamini Wiliam Mkapa akiwahutubia Wajumbe waliohudhuria mkutano wa
Jiolojia uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa J.K Nyerere Jijini Dar es
Salaam.
Baadhi wa Wajumbe waliohudhuria
mkutano wa Jiolojia wakifuatilia kwa makini hotuba iliyokuwa ikitolewa na mgeni
rasmi katika Ukumbi wa Kimataifa wa J.K Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Wanasayansi Vijana wakifuatilia
mada wakati wa mkutano wa tatu
wa Wanasayansi Vijana Duniani wenye lengo la kuhakikisha kuwa vijana
wanashiriki vyema katika rasilimali za duniani kwa ajili ya maendeleo na ukuaji
wa uchumi thabiti. (Picha na Makala na Benedict Liwenga, Maelezo-DSM)
======== ====== ========
Na Benedict Liwenga, Maelezo-DSM.
Vijana nchini hawanabudi kupenda kujifunza masomo ya
Sayansi na teknolojia ili waweze kupata ujuzi na mitazamo katika sekta ya gesi
ambayo inakuwa kwa kasi kubwa hapa nchini na Duniani kwa ujumla.
Kiukweli sayansi na teknolojia inasadikiwa kuwa
mihimili mikubwa ya sasa katika kuleta maendeleo katika nyanja mbalimbali kwani
mambo mengi yenye kuhitaji haraka hutegemea sayansi na teknolojia kwa kiasi
kikubwa.
Licha ya kuwepo kwa changamoto zinazozikabili baadhi
ya nchi nyingi za Afrika katika kupata maendeleo ikiwa ni pamoja na kutowekeza
katika sayansi na teknolojia, hali inayopelekea baadhi ya nchi nyingi kukosa
Wataalam wa kutosha katika mambo ya sayansi na teknolojia, hivyo nchi za Afrika
zinahitaji kujikwamua na changamoto hiyo kwa kuhakikisha kuwa zinawekeza katika
sayansi ili kubadilisha uchumi wa Afrika.
Sayansi na teknolojia hapa duniani huleta maendeleo
makubwa hivyo Vijana wanatakiwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kujituma
katika mambo ya sayansi na teknolojia ili kuweza kuleta uchumi endelevu.
Sambamba na hilo, katika Kongamano liloandaliwa hivi
karibuni na Wizara ya Nishati na Madini nchini Tanzania ambao ulifunguliwa
rasmi na Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt Mohammed Gharib Bilal ambao
ulikuwa ni mkutano wa tatu wa Wanasayansi Vijana Duniani wenye lengo la
kuhakikisha kuwa vijana wanashiriki vyema katika rasilimali za duniani kwa
ajili ya maendeleo na ukuaji wa uchumi thabiti, Wakala wa Jiolojia nchini,
Profesa Mruma alisema kuwa Mkutano huo una lengo la kurithisha taaluma ya
jiolojia inayohusisha madini, rasilimali, gesi na mafuta kutoka kizazi kimoja
hadi kizazi kingine.
Kongamano hilo la Vijana liliwakutanisha vijana toka
nchi zaidi ya 42 zikiwemo baadhi ya nchi za Afrika Tanzania ikiwemo na ambaye
ndiyo alikuwa mwenyeji wa Kongamano hilo.
Katika kongamano hilo, Naibu Waziri wa Wizara ya
Nishati na madini, Mhe. Masele alisema kuwa Serikali ya Tanzania imewekeza
nguvu zake kwa katika kuendeleza sayansi ya mambo ya gesi na mafuta pamoja na
afya kwa kuanzisha Vyuo mbalimbali na kuwapeleka baadhi ya Watanzania kwenda
kusoma nje ya nchi ili waweze kupata ujuzi na kuwa wataalam na wakaguzi katika
sekta ya gesi, mafuta na afya kwa lengo la kuja kuisaidia nchi.
Aidha, Mhe. Masele alisisitiza kuwa wajibu wa Serikali
kuamua kwa makusudi kusomesha vijana katika nchi mbalimbali ni kuwawezesha
vijana waweze kupata elimu juu ya sayansi na teknolojia hasa katika masuala ya
gesi ili kupata wataalam na wakaguzi wa kutosha nchini ambao watalisaidia taifa
kuinua uchumi wake.
“Hivi sasa
Serikali imeanzisha vyuo mbalimbali nchini, programu mbalimbali za mafunzo kwa
watanzania, imetoa ufadhili wa masomo kwa watanzania na imedhamini makongamano
ya vijana ili wapate fursa ya kujiendeleza’, alisema Masele.
Mhe. Masele pia aliyataka Makampuni ambayo ndiyo
yalikuwa Wadhamini wa kongamano hilo kuendelea kuwekeza nchini pamoja na
kuendelea kulipa kodi ili serikali iweze kukusanya mapato na wananchi wapate
kunufaika na mapato hayo.
Halikadharika, katika mkutano mwingine uliohusiana na
mambo ya Jiolojia uliowakutanisha Wataalam mbalimbali wa mambo ya jiolojia
ulimwenguni jijini Dar es Salaam, Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Mhe. Benjamini
William Mkapa ambaye alikuwa ndiye mgeni rasmi wa mkutano huo aliziasa jamii
hizo za Kiafrika kuwa na uelewa wa kutosha kuhusiana na mambo ya sayansi na
teknolojia ili ziweze kujikwamua kimaendeleo.
Mhe. Mkapa alisema kuwa jamii nyingi za kiafrika
hazijaelewa mchango mkubwa wa sayansi na teknolojia katika kuleta maendeleo
licha ya ukweli wa kwamba maendeleo daima yanatokana na rasilimaliwatu iliyopo
juu ya ardhi na chini ya ardhi, mchango wake huo hauthaminiwi na wengi lakini
wanaoweza kufanya hivyo ni Wanasayansi.
“Serikali
licha ya kudhamini mafunzo mbalimbali na masomo kwa vijana nje na ndani ya
nchi, fedha za kutosha bado zinahitajika katika kuhakikisha kuwa kazi hiyo
inakuwa endelevu”, alisema Mhe. Mkapa.
Bila shaka kuna haja ya kizazi kilichopo na kijacho
kurithishwa uelewa mzuri kuhusiana na mambo ya jiolojia ya jamii, jiolojia ya
madini, mazingira na mabadiliko ya tabianchi, vyanzo vya nishati, matatizo
yanayotokana na milipuko kama jiolojia na kuunganisha elimu ya Tehama na
jiolojia kwani hii itawasaidia vijana wengi kuelimika vya kutosha kuhusiana na
mambo ya jiolojia na pamoja na maendeleo kwa manufaa yao wenyewe.
Naye Mwenyekiti wa Mtandao huo kwa upande wa Tanzania
Bw. Stephen Joseph Nyagonde alitaja kauli mbiu ya mkutano huo kuwa ni ”Kuhakikisha ushiriki wa vijana katika
rasilimali za duniani kwa ajili ya maendeleo endelevu na ukuaji wa uchumi
imara”.
Katika mikutano hii yote, wadau mbalimbali wakiwemo Wanasayansi
Vijana walipata fursa ya kujadiliana kwa kina na kutoa mapendekezo ya kisayansi
ya namna ya dunia inavyotakiwa kupiga hatua za kimaendeleo na kuboresha maisha
ya wakazi.
Jamii nyingi za Kiafrika kiuhalisia hazina uelewa wa
kutosha kuhusiana na mchango wa sayansi na teknolojia katika kuleta maendeleo
nchini hali inayopelekea kuzorota kwa maendeleo ya nchi nyingi za Kiafrika.
Hivyo Wanasayansi ulimwenguni wanatakiwa kujenga
utamaduni wa kukutana mara kwa mara na kujadili mambo yanayohusu Sayansi na
teknolojia ili kuondoa changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii hizo.
Endapo vijana nao wakichangamkia fursa mbalimbali za
masomo yanayohusiana na mambo ya rasilimali zipatikanazo nchini mwao kama vile
gesi asilia, mafuta na madini mengine wataweza kutatua kitendawili cha
umasikini Barani Afrika na nchini mwao, hasa vijana wa kike kujenga utamaduni
wa kujikita katika masomo ya sayansi ili waweze kuwa wabunifu na kujikwamua na
maisha yao.
No comments:
Post a Comment