Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel Sitta akiongea na
Umoja Azaki za Vijana wakati alipofanya mkutano nao wakati wakiwasilisha
mapendekezo ya maboresho ikiwa ni msisitizo katika masuala yao ya vijana,
mkutano uliofanyika 02 Septemba, 2014 katika Ukumbi wa Spika Mjini Dodoma.
Kiongozi wa msafara wa Umoja wa Umoja wa Azaki za Vijana Alfred Kiwuyo
akisoma taarifa ya mapendekezo ya maboresho ikiwa ni msisitizo katika masuala
yao ya vijana, mkutano uliofanyika 02 Septemba, 2014 katika Ukumbi wa Spika
Mjini Dodoma.
Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Paul Makonda akisisitiza juu ya Katiba
kuweka kipengele cha kuwezesha kuundwa kwa Baraza Huru la Vijana la Taifa
wakati Umoja wa Azaki za Vijana wakiwasilisha mapendekezo ya maboresho ikiwa
ni msisitizo katika masuala yao ya vijana, mkutano uliofanyika 02 Septemba, 2014
katika Ukumbi wa Spika Mjini Dodoma.
Baadhi ya Vijana wanaounda Umoja wa Azaki za Vijana wakisikiliza kwa makini
maneno mazuri toka kwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba (hayupo
pichani) wakati walipokuwa wakiwasilisha mapendekezo ya maboresho ikiwa ni
msisitizo katika masuala yao ya vijana, mkutano uliofanyika 02 Septemba, 2014
katika Ukumbi wa Spika Mjini Dodoma.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakiwa kazini kufuatilia mambo yakiyoendelea
katika mkutano huo wa Umoja wa Azaki za Vijana uliofanyika 02 Septemba, 2014
katika Ukumbi wa Spika Mjini Dodoma.
Kiongozi wa msafara wa Umoja wa Umoja wa Azaki za Vijana Alfred Kiwuyo (kulia)
akikabidhi taarifa kwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel
Sitta wakati wakiwasilisha mapendekezo ya maboresho ikiwa ni msisitizo katika
masuala yao ya vijana, mkutano uliofanyika 02 Septemba, 2014 katika Ukumbi wa
Spika Mjini Dodoma.
(Picha zote na Benedict Liwenga, Malezo-Dodoma)
UMOJA wa Azaki za Vijana wakutana na Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba,
Mhe. Samuel Sitta wakiwa na lengo la kuja kuwasilisha mapendekezo yao kwa ajili
ya maboresho ya Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya.
Akizungumza kwa niaba ya vijana wenzake, Kiongozi wa msafara huo Alfred
Kiwuyo amesema kuwa Azaki hizo za vijana zilishiriki mchakato mzima wa Katiba
katika hatua zote muhimu ikiwemo kukusanya maoni na kuyawasilisha mbele ya
Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Pamoja na ushiriki huo, Bw. Kiwuyo ameeleza kuwa sehemu kubwa ya maoni
ya vijana yamejumuishwa katika kifungu cha 44 cha Rasimu ya Pili ya Katiba, na
mjumuisho huo wa haki na wajibu wa vijana umefinya sana maoni ya vijana katika
Rasimu hiyo.
“Lengo kuu la mtazamo huu sio kuleta hoja mpya, bali ni kuboresha Rasimu
ya Pili ya Katiba Mpya na katika maboresho hayo tunapendekeza mambo
matatu ya msingi, kwanza ni kuwekwa kwa tafsiri ya neno kijana katika Rasimu,
kutenganisha haki na wajibu wa vijana na mwisho ni kuweka kifungu kitakacho
wezesha kuundwa kwa Baraza huru la Vijana la Taifa”, alisema Kiwuyo.
Aidha, Kiwuyo ameongeza kuwa Azaki za vijana zinatambua kuwa haki ya uandishi
wa Katiba ni ya kila Mtanzania na kwa utaratibu waliojiwekea wao wenyewe
Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba ndiyo wawakilishi wao katika hilo, hivyo
wanamatumaini makubwa kuwa Katiba itaandikwa na Watanzania wa makundi
yote wakiwemo na vijana.
Naye Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel Sitta amesema kuwa
Ibara ya 44 katika Rasimu ya Tume inayuzungumzia mambo ya vijana imekuwa
fupi na imeacha baadhi ya mambo muhimu zikiwemo haki ambazo hazikuelezewa
vizuri, mambo ya haki na wajibu wa vijana na pia haijataja juu ya chombo cha
uwakilishi cha vijana.
“Hii Ibara ya 44 katika Rasimu ya Tume imekuwa fupi na imeacha baadhi
ya mambo muhimu, hivyo niwahakikishieni kuwa mawazo haya ya vijana
tutawafikishia wahusika ambao ni Kamati ya Uandishi na Uongozi wa Bunge
Maalum la Katiba ili yaweze kufanyiwa kazi, lakini pia suala la wajibu ambalo
mmeliomba ni jambo zuri kwa ninyi vijana kwani ni muongozo”, alisema Mhe.
Naye Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Paul Makonda amemshukuru
Mwenyekiti wa Bunge hilo, kwa kupokelewa kwa vijana hao kama kundi kubwa
katika jamii na amesisitiza juu ya Katiba kuwezesha kuundwa kwa Baraza Huru la
Vijana la Taifa kwani litawezesha kuwaunganisha vijana nchini.
“Baraza kwetu ni jambo la msingi kwani litakuwa ni chombo kitakachotusaidia
katika mambo ya uwakilishi kwa vijana nchini, kwani hivi sasa hatuna vijana
wenye kuwakilisha vijana wenzao katika mambo mbalimbali kupitia chombo kama
hiko, hivyo Katiba iweke kipengele kitakachowezesha kuundwa kwa chombo
hiko”, alisema Makonda.
Makonda alisisitiza kuwepo na haki, wajibu na uwajibikaji kutasaidia kuwa na
vijana waadilifu na wenye kuzingatia maadili.
Azaki za Vijana katika mchakato wa Katiba zinajumuisha Tanzania Youth Vision
Association (TYVA), FEMINA, Restless Development, Tanzania Youth Coalition
(TYC), Youth of United Nations Association of Tanzania (YUNA) pamoja na
TAMASHA.
No comments:
Post a Comment