Mkurugenzi wa Kitengo cha Uthaminishaji wa Madini ya Almasi na Vito cha
Wizara ya Nishati na Madini (TANSORT), Archard Kalugendo (mwenye
shati la batiki), akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Taasisi ya
Wafanyabiashara wa Madini ya Vito wa Thailand, walipotembelea Banda
la Tanzania katika Maonesho ya 54 ya Vito na Usonara ya Bangkok,
yaliyofanyika Septemba 9 hadi 13 mwaka huu.
Makamu wa kwanza wa Rais wa Taasisi ya Wafanyabiashara wa Madini
ya Vito na Usonara wa Thailand, Bw. Sutipong Dumrongsakul, akimkabidhi
zawadi maalumu Mkuu wa Ujumbe kutoka Tanzania ulioshiriki maonesho
ya vito ya Bangkok, Archard Kalugendo, mara baada ya kikao kati ya
Ujumbe huo na Viongozi wa Taasisi hiyo ya Wafanyabiashara wa Thailand.
Wateja mbalimbali wakihudumiwa katika Banda la Tanzania kwenye
maonesho ya vito na usonara ya Bangkok yaliyofanyika hivi karibuni nchini
Thailand.
Baadhi ya Watanzania walioshiriki maonesho ya vito na usonara nchini
Thailand, wakimsikiliza mmoja wa wateja aliyetembelea Banda la
Tanzania.
Ujumbe wa Tanzania (Kulia) wakiwa katika kikao na Uongozi wa juu wa
Taasisi ya Wafanyabiashara wa Madini ya Vito na Usonara wa Thailand,
ambao ndiyo waandaaji wa maonesho ya vito na usonara ya Bangkok.
Baadhi ya Watanzania walioshiriki maonesho ya vito na usonara ya
Bangkok, wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungwa rasmi
kwa maonesho hayo.
Makamu wa Rais wa Taasisi ya Wafanyabiashara wa Madini ya Vito –
Thailand, ambao ndiyo waandaaji wa Maonesho ya Vito ya Bangkok,
Tony Brooke akizungumza na baadhi ya Watanzania walioshiriki katika
Maonesho hayo nchini Thailand alipotembelea Banda la Tanzania.
Sambamba naye (mwenye shati la kitenge) ni Mkuu wa Ujumbe wa
Tanzania katika maonesho hayo, Archard Kalugendo.
Na Veronica Simba – Aliyekuwa Bangkok
Wafanyabiashara wa madini ya vito na usonara wa Thailand wameonyesha
nia ya kushirikiana na Tanzania katika sekta hiyo kwa lengo la kukuza
uhusiano na kuzinufaisha pande zote mbili.
Hayo yalibainika hivi karibuni katika kikao kilichokutanisha Ujumbe wa
Tanzania ulioshiriki Maonesho ya Vito na Usonara yaliyofanyika Bangkok
nchini Thailand na Uongozi wa Taasisi ya Wafanyabiashara wa madini
hayo kutoka nchini humo.
Akiwasilisha maoni na mapendekezo kutoka upande wa Tanzania katika
kikao hicho, Kiongozi wa Ujumbe kutoka Tanzania, Archard Kalugendo
ambaye ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Uthaminishaji wa Madini ya Almasi
na Vito cha Wizara ya Nishati na Madini (TANSORT), alisema Tanzania
inapenda kushirikiana na Wa-Thailand katika sekta hiyo ili pamoja na
mambo mengine kuiga na kujifunza kutoka kwao.
“Ninyi wenzetu mmeendelea sana katika sekta hii ya madini ya vito na
usonara. Tunapenda kujifunza na kuiga kutoka kwenu ili nasi tufike hapo
mlipofikia na hata zaidi ya hapo,” alisema Kalugendo.
Aliongeza kwamba, lengo la Serikali ya Tanzania ni kufanya kila
linalowezekana ili kuhakikisha inawawezesha wananchi wake hususan
wanaojishughulisha na biashara ya madini ya vito na usonara ili wanufaike
ipasavyo kupitia kazi hiyo na pia kulinufaisha Taifa kwa ujumla kwa kukuza
uchumi wa nchi.
Alisema, Serikali inayo nia na imejipanga kuhakikisha Tanzania inakuwa
kitovu cha biashara ya madini ya vito na usonara katika Bara la Afrika
na kwamba inatumia njia mbalimbali kufanikisha hilo ikiwemo kuendelea
kuboresha Maonesho ya Vito na Usonara ya Arusha (Arusha Gem Fair –
AGF) yanayofanyika kila mwaka.
Kalugendo alitumia fursa hiyo kuwakaribisha Wafanyabiashara wa
Thailand katika Maonesho ya Vito ya Arusha yanayotarajiwa kufanyika
mapema mwezi Novemba mwaka huu jijini Arusha.
“Tanzania inayo mazingira mazuri sana ya uwekezaji na ninawahakikishia
kuwa ushiriki wenu katika maonesho hayo utakuwa wenye tija kwenu na
kwetu pia,” alisema.
Aidha, Kalugendo alitoa maombi ya Tanzania kupatiwa nafasi kubwa
zaidi katika Maonesho ya Vito na Usonara ya Thailand ili washiriki wengi
zaidi wakiwemo wachimbaji na wafanyabiashara wa madini hayo waweze
kushiriki na kujipatia uzoefu utakaowasaidia kuboresha utendaji wao na
hivyo kumudu ushindani katika soko na viwango vya kimataifa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Maonesho ya Vito na Usonara ya
Arusha, Peter Pereira alisisitiza umuhimu wa Thailand kushiriki katika
maonesho ya Arusha na kuwahakikishia kuwa mazingira mazuri
yameandaliwa kwa ushiriki wenye tija ikiwemo kuondoa gharama za kodi
ya thamani katika bidhaa (VAT) kwa kipindi chote cha maonesho.
Akijibu hoja na mapendekezo kutoka upande wa Tanzania, Makamu wa
Rais wa Taasisi ya Wafanyabiashara wa Madini ya Vito – Thailand, ambao
ndiyo waandaaji wa Maonesho ya Vito ya Bangkok, Tony Brooke alisema
Thailand inapenda kushirikiana kwa ukaribu zaidi na Tanzania katika sekta
hiyo.
Alisema Wafanyabiashara wa Thailand watashiriki katika maonesho ya vito
ya Arusha na kuahidi kuboresha ushiriki wa Tanzania katika maonesho ya
vito ya Bangkok.
Brooke alitoa changamoto kwa Tanzania kujiandaa vema zaidi katika
ushiriki wa maonesho kama hayo kwa kuhakikisha inapeleka madini na
bidhaa kwa wingi kulingana na uhitaji wa wateja.
“Wateja wengi wanatembelea banda la Tanzania kuliko madini na bidhaa
zilizopo. Ongezeni wingi wa bidhaa maana uhitaji ni mkubwa,” alisisitiza
Brooke.
Alikubaliana na wazo la kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha madini ya vito
na usonara katika bara la Afrika na kusisitiza kufanya kazi kwa bidii, weledi
na kujituma kwa hali juu ili kuhakikisha lengo hilo linatimia.
“Hatua mnayoona tumefikia katika sekta hii ya madini ya vito na usonara
imekuja kwa kufanya kazi kwa bidii, weledi na kujituma, hivyo nanyi ili
mfanikiwe mnapaswa kufanya hivyo,” alisema.
Nchi ya Thailand ina uzoefu wa miaka 40 katika biashara ya madini ya
vito na usonara na imekuwa ikiandaa maonesho makubwa kila mwaka
katika kipindi hicho chote ili kuuza bidhaa zitokanazo na madini ya vito na
kujitangaza zaidi kimataifa.
Maonyesho ya Vito na Usonara ya Bangkok kwa mwaka huu yalifanyika
kuanzia Septemba 9 hadi 13 na kushirikisha mataifa mbalimbali duniani.
No comments:
Post a Comment