Monday, September 22, 2014

MKUU WA WILAYA YA MAKETE AFANYA KIKAO CHA MAENDELEO NA WANAMAKETE WAISHIO JIJINI DAR

 Mkuu wa wilaya ya Makete mh Josephine Matiro akizungumza katika kikao hicho.

Wananchi waliozaliwa wilayani Makete mkoani Njombe ambao wanaishi nje ya wilaya hiyo, wameshauriwa kuipenda wilaya yao kwa kuja kuwekeza pamoja na kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo ndani ya wilaya hiyo

Rai hiyo imetolewa hii leo na Mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro katika kikao baina yake na wananchi wa Makete waishio jijini Dar es Salaam kilichofanyika jijini humo
Katika kikao hicho mkuu wa wilaya amewashirikisha mambo mengi ya kimaendeleo katika wilaya ya Makete ikiwemo uwepo wa shule ya sekondari ya wasichana ya Makete Girls secondary ambayo pamoja na kuanza kufanya kazi bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali

Mh. Matiro amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukosefu wa bweni na kuwa wanafunzi wanalala kwenye vyumba vilivyojengwa kwa ajili ya madarasa, bwalo, jiko pamoja na maabara ambavyo vinatakiwa viwepo

Amewaomba wananchi hao kuunga mkono kwa jinsi Mungu alivyowajalia na kwamba yeyote atakayejisikia kuchangia anaombwa kufanya hivyo kwani kila mmoja kwa nafasi yake ana mchango katika shule hiyo ili iondokane na changamoto hizo
"Ndugu zangu wilaya yetu inawatambua sana. tunaomba na tunahitaji sana ushirikiano wenu katika maendeleo ya makete, tukishirikiana kwa pamoja kwa kadri Mungu alivyotujalia kwa hakika shule hii itaimarika sana" amesema Matiro

Kwa upande wao washiriki wameoneshwa kufurahishwa na maendeleo ya kasi katika wilaya ya makete huku wakiipogeza serikali kwa juhudi zake za maendeleo hasa katika elimu, barabara, umeme pamoja na mambo mengine huku wakisema wataunga mkono maendeleo ya wilaya yao kwa kadri ya uwezo wao
Pia wameonesha kufurahishwa na Mh Matiro kuwatafuta na kuzungumza nao kwani wamesema amekuwa mkuu wa wilaya wa kwanza kuzungumza nao toka wilaya hiyo imeanzishwa na kumtaka kuwa na moyo wa kuipenda wilaya ya Makete kama mkuu wa wilaya
 Wakiwa katika picha ya pamoja na mkuu wa wilaya.

Baada ya kushirikishwa hivyo wameahidi kushirikiana na mkuu huyo wa wilaya kutatua changamoto hizo.





Na Edwin Moshi, Dar es salaam

No comments: