Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Mafunzo na Usimamizi wa Kanda wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Benson Kigaila akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari.
Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Mafunzo na Usimamizi wa Kanda wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Benson Kigaila akionesha barua za kuomba vibali vya kufanya maandamano katika maeneo mbalimbali nchini.
Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Mafunzo na Usimamizi wa Kanda wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Benson Kigaila (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuhusu maandamano ya chama hicho yatakayoanza kesho nchini kote kupinga Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea Dodoma. Kulia ni Kada wa Chadema, Aron Mashuve na Mwanasheria wa chama hicho, John Malya.
Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene akimkaribisha Kigaila kuzungumza na wanahabari.
Mwanasheria wa Chadema, John Malya akifafanua baadhi ya vipengere vya sheria kuhusu ruhusa ya kufanya maandamano.
Mwanasheria wa Chadema, John Malya akiwa na kada wa chama hicho, Aron Mashuve.
Wanahabari wakiwa kwenye mkutano huo.
Dotto Mwaibale
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesisitiza kuwa migomo na maandamano yasiyokoma nchi nzima yapo palepale na kwamba yanaanza rasmi kesho kwa kishindo kikubwa na hakuna mtu wa kuyazuia kwani ni haki yao kikatiba.
Chadema kimesema lengo la maandamano hayo ni kuishinikiza Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kitoe tamko la kusitishwa Bunge Maalum la Katiba linaloendelea mjini Dodoma huku likifuja fedha za wananchi.
Kauli hiyo ilitolewa jana Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Organizasheni na Mafunzo wa chama hicho, Benson Kigaila wakati akizungumza na wanahabari Makao Makuu ya chama hicho Kinondoni.
"Maandamano yaliyotangazwa na Freeman Mbowe si ya kwake ni maazimio ya Mkutano Mkuu wa Chadema uliofanyika Septemba 14, mwaka huu.
"Tunasisitiza kuwa maandamano na migomo isiyokoma nchi nzima yapo palepale, lengo letu ni kuishinikiza Serikali isitishe Bunge la Katiba kwani mkutano mkuu uliazimia jambo hilo baada ya kuona kuwa kinachofanyika Dodoma hakitatupa Katiba Mpya, bali fedha za wananchi zinatafunwa bure"alisema.
Aidha, alisema maandamano yao yapo kisheria ambapo katika Katiba ya nchi, maandamano ni haki sheria namba 5 ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 kifungu cha 11 kifungu kidogo cha 1 inaruhusu jambo hilo.
Kigaila aliongeza kuwa sheria hiyo inataka waandamanaji kutoa taarifa ndani ya saa 48 kabla ya na si kuomba kibali taratibu ambazo wao wameshazipitia.
"Natoa mwito kwa Watanzania wote wakatae ufisadi unaofanywa na Bunge Maalumu la Katiba. Kilichoko Dodoma ni kumaliza fedha ambazo zingetumika kujengea nyumba za walimu au hata zahanati katika maeneo mbalimbali nchini,"alisema .
Kigaila alisisitiza kuwa wamepata barua kutoka Jeshi la Polisi kuwataka kusitisha maandamano lakini hawatasitisha kwa sababu, sababu za katazo hazina mashiko na hazijanukuu kifungu chochote cha sheria.
Alisema licha ya wao Chadema, maandamano yao hayo yamepata baraka kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Mkurugenzi huyo wa organizasheni wa chama hicho alisema maandamano hayo yanafanyika katika ngazi ya majimbo, wilaya na mkoa, ambapo kwa mkoa yataanzia maeneo tofauti kuishia ofisi za mkuu wa mkoa husika na kwa wilaya yatakwenda kwa mkuu wa wilaya husika.
Alisema maandamano hayo kila mahali yataanza asubuhi, huku kwa mikoa mitatu ya kanda ya Dar es Salaam yataanza keshokutwa Jumatano.
Kwa upande wale Mwanasheria wa chama hicho, John Mallya alisema sababu nyingine iliyotolewa na polisi kuwa maandamano hayawezi kufanyika kwa sababu kesi iliyofunguliwa Saedy Kubeinea ya kupinga Bunge hilo ipo mahakamani kuwa haina mashiko kwa kuwa Chadema ni taasisi inayojitegemea na inamaamuzi yake ya kichama.
No comments:
Post a Comment