Tuesday, August 26, 2014

SAFARI NGUMU YA MWANAHARAKATI FATUMA MISANGO MPIGANIA HAKI ZA WANAWAKE, WATOTO SONGEA

Fatuma Misango mwenye mtandio mweusi kichwani akizungumza na mmoja wa wanawake waliotendwa.
-------------------------
Mwandishi HANNAH MAYIGE, wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania – OUT, anaangazia safari ngumu ya mwanaharakati mwanamke mzaliwa wa Namtumbo,  Mratibu wa  Kituo cha wasaidizi wa sheria Songea, Bi. Fatuma Misango katika harakati za kupigania haki za wanawake, watoto na  kupinga ukatili wa kijinsia.

     “Mimi  naitwa  Fatuma  Misango,  ni Mratibu  wa  kituo  cha  wasaidizi  wa sheria  kiitwacho Songea Paralegal  Center  (SOPCE),” Bi  Fatuma alianza kujieleza  kwa mwandishi wa makala haya ofisini kwake mjini Songea.
Bi. Fatuma Misango anasema yeye ni  mzaliwa  wa  wilaya  ya  Namtumbo  mkoa  wa  Ruvuma,  mwenye  umri  wa miaka  takribani  hamsini sasa.

     Anasema alikwama kuipata elimu yake kwa mfululizo enzi hizo kutokana na majukumu ya  kifamilia, lakini aliamua  kujiendeleza  mwenyewe akiwa mtu mzima. Sasa ana elimu ya sekondari  kidato cha nne inayomsaidia sana katika kutekeleza majukumu yake katika kuwasaidia wanawake, watoto na wanaume wenye uhitaji hasa wanaoteseka na ukatili wa kijinsia majumbani na sehemu za kazi

     Kuhusu maisha, Mama  Misango  amejaliwa  kuolewa na  kupata  watoto  wanne na  mume  wake  ambaye  anaye  mpaka sasa.Katika   safari ya maisha  yake  alifanikiwa  kufanya  kazi  kama  karani  katika  Kampuni  ya Tumbaku  mjini  Songea. 

     Hata  hivyo,  mama  huyu ,  alikuwa  anashauku  na  kiu  ya  kujiendeleza, hivyo  aliamua  kuanza  masomo  ya  uuguzi  ambapo  alifanikiwa  na  kuhitimu  masomo  hayo  kwa  mwaka mmoja.
Bi. Misangu,  hakuridhika  na  fani  ya uuguzi  tu, hivyo  akajiingiza  katika  masuala  ya  siasa na kuwa  Diwani  viti  maalumu kupitia CCM. 

      “Hapo  ndio  nikaanza  kuangalia  ni  masuala  gani  ambayo  nitaweza  kusaidia  jamii  na  hususani wanawake na watoto,” anasema Bi. Misango na kufafanua kuwa baada   ya  hapo,  “nikapata  mafunzo  ya  sheria  kama  kiongozi  yaliyoendeshwa  na  Shirika lisilo la kiserikali liitwalo Mtandao wa Jinsia Tanzania  ( TNGP)  mwaka  2002,”. 
     Mafunzo ya TGNP  yalimpatia   msukumo  mkubwa  na  hamasa  kuweza  kuanza  kuwasaidia  wanawake  kwa  masuala  ya  sheria.
Bi. Misango anasema, wanawake  wengi  wakipata  matatizo  wanakuwa  hawana  pakwenda  kueleza  matatizo  yao.

Shirika   la TGNP  linalosimamia mambo   ya Jinsia na na kutetea haki za binadamu has masuala ya sheria  walimwaalika tena  kwenye  semina   jijjini Dar  es  salaam , baada ya kuona  ana  mwelekeo  mkubwa katika  uchangiaji wa  mada   mbalimbali hasa za utetezi wa wanawake.

       Alipokuwa kwenye semina  hiyo,  ndipo alipokutana na maafisa wa Shirika  ambalo  lilimtaka washirikiane  katika kazi  ya kisheria  au msaada wa sheria kwa  wanawake   katika  mkoa wa Ruvuma , shirika hilo linaitwa  Women Legal  Aid  Centre  (WLAC)  

        Bi. Misango akaanza ukurasa mwingine wa  kushirikisha  watu  wengine   na kufungua  Kituo   cha  wasaidizi wa Sheria Songea, Songea  Paralegal  Centre   (SOPCE)  kwa msaada mkubwa wa WLAC  na yeye akiwa ni Mkurugenzi wake.
     Walengwa   wa  Kituo hicho  hasa,  ni wale  wa kipato cha chini  ambao hawawezi   kusimamiwa mashauri yao na  Wakili kwa malipo ya fedha.Hivyo,  walengwa  wa jinsi zote  awe mwanamke au mwanaume  hupewa msaada na kituo hicho.        

     “Msaada wetu  unakuwa   ni bure, japokuwa  lengo   letu  hasa ilikuwa ni wanawake  na watoto zaidi,” anasisitiza Bi. Misangu .
Shirika   la SOPCE tangu lilipoanzishwa  mwanzoni mwa miaka ya  2000,  limeweza  kuwasaidia  watu takribani  elfu tano (5,000).

       Mwanamke mmoja mkazi wa Kijiji cha Lihangweni, Songea Bi. Maria Komba, anatoa ushuhuda alivyosaidiwa na SOPCE. “Mimi  ni mmoja  wapo  niliyepata  msaada  wa kisheria  kutoka  SOPCE  baada   ya   kunyang’anywa    ardhi   na   kijijii  cha   Lihangweni ,   na hatimaye  nikarudishiwa  ardhi   yangu licha ya umasikini wangu unaonikabili,” anasema Bi. Maria   Komba  .

     Ushuhuda mwingine ni ule wa migogoro inayosumbua sana familia hasa ndoa. Bw.  Dranus  Tadei  Njajula anasema bila   msaada    wa    Mkurugenzi   wa  SOPCE,      ndoa   yake   ingekuwa  tayari  imevunjika,   lakini  walimpatia  msaada  mkubwa  sana  na   sasa  ndoa  yake imenusurika kuvunjika. “Hawa wamenisaidia sana kisheria,  ndoa yangu  sasa ni shwari” anajigamba Bw. Njalula.

      Kwa  kuona  kazi  nzuri  SOPCE  Na  mkurugenzi wake  Fatuma   Misangu,  serikali  ya  mkoa  imekisaidia  kituo  hicho   kwa  kuwapatia  ofisi   bila  malipo  yoyote.  Zaidi  ya hapo   wateja  wengi  wanatoka ofisi ya   mkoa  na  ofisi  ya wilaya  ya  songea   vijijini.

       Mama  Misango  alieleza kesi  wanazo  kutananazo  zaidi  ni  kesi za ndoa  “wanandoa  wengi sana  wana  migogoro  katika  ndoa  zao  na  mara  nyingi  sababu  ni  hali  duni  ya  kiuchumi”.

     Kesi  nyingine  wanayo  kutana  nayo  sana  ni  ukatili  wa  watoto  “wanawake  wanafanya  ukatili  kwa  watoto  wao  kama  kuwachoma  moto  mikono  ukiuliza  sababu  eti  kaiba  shilingi mia  mbili  tu”. Mama  M isangu  alibainisha  kuwa   sababu  kubwa  ni  kuchoka  maisha  ya  shida  na  mara  nyingine  kutelekezwa  na  waume  zao,  hivyo  kupelekea  msongo  wa  mawazo.

      Mara  nyingi  hamna  kazi  au  shughuli  isiyo  kuwa  na  faida  na  changamoto.  “Nilipata  tuzo  ya  amani  2005  iliyo  julikana  kama  ONE  THOUSAND  PEACE  WOMEN  ACROSS  THE  GLOBAL.  Kati  ya  watu  elfu  moja  duniani  waliopendekezwa  basi  na  mimi  nilikuwemo,” anasema Bi Misango na kwamba faida  nyingine  ni  kuwa  maarufu.

        Changamoto  wanazo  kabiliana  nazo,  ni pamoja  na  wateja   wao  wengi kuwa   wa kipato  cha chini,  nao mara  nyingi  wanaamini  pia kupata  msaada  wa  fedha  kutoka  SOPCE. Changamoto  hiyo  inasumbua  kwasababu  shirika  la  SOPCE  halina  fedh za kuwahudumia watu kutatua matatizo yao.

Kuhusu malengo  ya  baadae,  SOPCE  inatarajia  kuona  jamii  yote  ya  mkoa  wa  Ruvuma  inaheshimu haki  za  binadamu  hususan  kwa  wanawake  na  watoto.     Pia  wanataka  wanawake wanasimama  wenyewe  katika  kutetea  haki  zao.

       Mama   Misango  alitoa  ushauri  kwa  wanawake  wajiunge  katika  vikundi  mbalimbali   vya ujasiriamali  ili  waweze  kujikimu   kimaisha.  Kuishi  bila  kujishughulisha  kuna   sababisha kukata tamaa  na  wakati  mwingine  kuamua  kufanya  ukatili  kwa  watoto   wao wenyewe .Biashara  ndogondogo  zinaweza  pia kuwakwamua   kimaisha .
Mwandishi wa makala anapatikana E-mail hannahmayige@gmail.com

No comments: