Saturday, August 16, 2014

MH. PINDA AFUNGA KONGAMANO LA JIOLOJIA AFRIKA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda, akihutubia wakati akifunga Kongamano la 25 la Wajiolojia Barani Afrika lililofanyika tarehe 14-16 Jijini Dar es Salaam. Wakati akifunga Kongamano hilo, Waziri Pinda amewataka watafiti barani Afrika kufanya tafiti ambazo zina mahusiano ya moja kwa moja na jamii ili tafiti hizo zitumike katika kuwazesha wananchi kufaidika na rasilimali zilizopo barani Afrika.
Baadhi ya Wajilojia kutoka nchi mbalimbali barani Afrika wanaohudhuria Kongamano la 25 la Wajiolojia Afrika wakifuatilia hotuba ya kufungamano hiyo iliyosomwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda (hayupo pichani).
Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika picha ya pamoja na baadhi ya Wajiolojia waliohudhuria kongamano hilo kutoka nchi mbalimbali Barani Afrika. Wengine katika picha kutoka kushoto ni Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ,Sadik Meck Sadik na Rais wa Wajolojia Afrika Profesa Aberra Mogassie.

Na Asteria Muhozya, Dar es Salaam
Wajiolojia barani Afrika wametakiwa kufanya tafiti zenye uhusiano wa moja kwa moja na jamii na kuzionesha tafiti hizo ili ziweze kutumiwa  kama ufumbuzi wa  matatizo mbalimbali yanayolikabili bara la hilo, jambo ambalo litaiwezesha  Afrika  kunufaika  na rasilimali zilizopo na hivyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi , maendeleo ya watu na mapato ya mataifa yao.

“Najua watafiti wanaweza kusema serikali zetu hazitumii tafiti zetu, lakini mkifanya tafiti zenye uhusiano wa moja kwa moja na jamii, mkazitoa kwa jamii tutazitumia msizifungie makabatini,” amesisitiza Pinda.

Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda  leo jijini Dar  es Salaam wakati akifunga kongamano la 25 la Wajiolojia barani Afrika  na kueleza kuwa, ili Afrika  iweze kuendelea na kufaidika na rasilimali zake, inahitaji kuzalisha wataalamu wengi  katika taaluma ya sayansi ikiwemo wajiolojia.

“Hapa nchini Tanzania Profesa Muhongo anapambana sana na taaluma hii, jambo hili litasaidia kuzalisha wataalamu wengi katika sekta za mafuta na gesi. Lakini na ninyi, mnahitaji kuzalisha wataalamu ili tuisogeze mbele Afrika,” alibainisha Pinda.

Ameongeza kuwa, serikali ya Tanzania tayari inajipanga katika kuhakikisha inazalisha watalaam wengi wa sayansi kupitia programu za Vyuo Vikuu ambapo tayari imeanzisha masomo ya mafuta na gesi katika baadhi ya vyuo vikuu nchini, hususani Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu Dodoma (UDOM), ikiwemo kampeni ya kuhakikisha kwamba kila shule ya sekondari inakuwa na maabara ambazo zitachochea kizazi cha wanasayansi.

Vilevile, amezungumzia  tatizo  la Afrika kutokufaidika na rasilimali  zake zilizoko ardhini  na kuongeza  kuwa,  linatokana na matumizi kidogo ya sayansi  yanayofanywa na nchi nyingi za Afrika,  hivyo,  amewataka wataalamu hao kuhakikisha wanatoka na njia ambazo zitasaidia na kuliwezesha bara hilo kuitumia sayansi kwa maendeleo ya nchi zao kwa sasa na kwa kizazi kijacho.

Aidha, amewataka wataalamu hao kutumia kuitumia taaluma hiyo zaidi ya inavyotumika sasa ikiwemo kuhakikisha kwamba afrika inasimama imara kupitia rasilimali zilizopo na kuiondoa katika matatizo ya kiuchumi, kiafya na kimazingira.

Halikadhalika, amewataka wataalamu hao, kufikiria namna ambavyo nchi za afrika zitasimamia suala la uthaminishaji madini katika nchi zao kwa kuhakikisha kwamba, shughuli za uthamini madini zinafanywa ndani ya Afrika tofauti na sasa ambapo nchi nyngi bado zinasafirisha madini nje bila kuyathamini  jambo ambalo linachangia katika kuzikosesha nchi hizo mapato stahiki yanayotokana na rasilimali hiyo.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Madini,  Profesa Sospeter Muhongo akizungumza katika mkutano huo, amewataka wajilojia Afrika kufanya tafiti nyingi za kutosha ili kujua kiasi cha mafuta na gesi ambacho bado  kipo Afrika lakini bado hakifahamiki ili rasilimali hizo  zisaidie kubadilisha taswira ya afrika.

Ameongeza kuwa, Afrika inatakiwa kujikita zaidi katika kuzalisha wataalamu wa kutosha na kujua namna ya kuziendelea rasilimali hizo wakati huo huo ikihakikisha kwamba, zinchangia kwa kiasi kikubwa katika kuinua uchumi, kuvutia uwezaji na kuchangia katika maendeleo ya watu.

Ameongeza kuwa, bado afrika inazalisha kiasi kidogo cha nishati ya umeme wakati dunia inahitaji nishati hiyo kwa kiasi kikubwa hivyo, amewataka wataalamu hao kuhakikisha wanasaidia katika kuwezesha upatikanaji wa rasilimali hiyo kupitia taaluma zao.

Vilevile, amewataka wajiolojia afrika kuipa kipaumbele miradi ya umeme vijijini katika nchi zao, na kuhakikisha kwamba, miradi hiyo kama ilivyo miradi ya REA nchini, inafanyika na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa ikiwemo kufanya tafiti kuhusu miradi hiyo.

Katika hatua nyingine, Profesa Muhongo amekitaka  Chuo  Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu Dodoma kulifanyia kazi suala la ukosefu wa wahadhiri katika vyuo hivyo  katika fani za mafuta na gesi na wizara imehaidi kuhakikisha kwamba inawezesha upatikanaji wa wakufunzi katika masomo hayo kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Naye Mhadhiri wa  Chuo Kikuu cha Dar es  Salaam Profesa Nelson Boniface,   ameeleza kuwa, kongamnao hilo la siku tatu la wajiolojia barani Afrika limewawezesha washiriki kujadili masuala mbalimbali yanayoihusu taaluma hiyo yakiwemo kyanayohusu  nishati mchanganyiko, namna ya namna jilojia inavyoweza kusaidia matatizo ya umaskini, maji, afya na mengineyo yalijadiliwa katika kongamano hio.

Profesa Boniface ameongeza kuwa, washiriki wa kongamano hilo walijadili na kuona kwamba, uwepo wa  wataalamu waliobobea katika taaluma hiyo ni  jambo la msingi kutokana na nafasi na mchango wao katika kuendeleza , namna ya kutumia  Afrika na dunia zinavyoweza kufaidika  na rasilimali hizo.

Akielezea kuhusu mkutano wa Tatu wa Wanasayansi Vijana Duniani  ambao ulitangulia kabla ya kongamano hilo, ameleza kuwa,  mkutano huo uliweza kuwapa nafasi vijana kujadili masuala mbalimbali kuhusu namna jiolojia inavyoweza kuchangia kuondoa umaskini na kuwezesha maisha bora kwa jamii ya Afrika inavyoweza kunufaika na rasilimali asilia na masuala mengine muhimu.

Kongamano la 25 la Wajilojjia Afrika limewakutanisha wajiolojia  waliobobea katika taaluma hiyo kutoka nchi zaidi ya 42 Afrika na duniani . Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini imewezesha kufanyika kwa kongamano la wajilojia uliokuwa ufanyike nchini Brazil.

Aidha, mikutano yote miwili imedhaminiwa na taasisi na makampuni mbalimbali, ambapo pia kampuni inayofanya utafiti na uchimbaji wa gesi na mafuta ya BG-Tanzania ilikuwa ndio mdhamini mkuu wa kongamano hilo.

kongamano lingine la Wajiolojia Afrika linatarajiwa kufanyika nchini Afrika kusini.

No comments: