Thursday, July 3, 2014

WANAHABARI WAPATIWA ELIMU YA MFUMO UTAKAOTUMIKA KUBORESHA DAFTARI LA KUDUMU LA KUPIGA KURA.

 Mjumbe wa  Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu John Mkwawa  wakati akisoma taarifa wakati   akifungua mkutano wa siku moja na waandishi wa habari wa Mkoa wa Iringa unaohusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya kwanza na matumizi ya Teknolojia mpya ya Biometric Voter Registration uliofanyika katika ukumbi wa ofisi za mkuu wa mkoa wa Iringa. 
 Baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo wa NEC kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya kwanza na matumizi ya Teknolojia mpya ya Biometric Voter Registration uliofanyika katika ukumbi wa ofisi za mkuu wa mkoa wa Iringa mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Mkoa wa Iringa. 
Mkurugenzi wa Idara ya habari na Elimu kwa Wapiga Kura Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Ruth Mashama akizungumza kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya kwanza na matumizi ya Teknolojia mpya ya Biometric Voter Registration uliofanyika katika ukumbi wa ofisi za mkuu wa mkoa wa Iringa

Na Denis Mlowe,Iringa

TUME ya Taifa ya Uchaguzi imetoa elimu kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Iringa kuhusu kusambaza elimu juu ya  mchakato wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa wananchi juu ya mfumo mpya utakaotumika kuandikisha wapiga kura wa mkoani hapa wa teknelojia ya kibailojia(BVR).

Tume inatarajia kufanya uboreshaji wa daftari la Kudumu wa Wapiga kura kwa awamu ya kwanza hivi karibuni kwa kutumia Teknolojia mpya ya Biometric Vote Regstration (BVR).

Hayo yamebainishwa juzi  mjini hapa na Mjumbe wa  Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu John Mkwawa  wakati  akifungua mkutano wa siku moja na waandishi wa habari wa Mkoa wa Iringa unaohusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya kwanza na matumizi ya Teknolojia mpya ya Biometric Voter Registration uliofanyika katika ukumbi wa ofisi za mkuu wa mkoa wa Iringa.

Jaji Mkwawa alisema lengo ni kuhakikisha kuwa wale wote wenye sifa za kuwa wapiga kura  waliofika umri wa miaka 18 na hawapo katika daftari la kudumu la kupiga kura,waliohama makazi yao ya awali walikojiandikisha na  wanajitokeza kwa wingi katika vituo vya kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.

Alisema mfumo huo mpya ni wa kuchukua au kupima taarifa za mtu za kibaiolojia au tabia ya mwanadamu na kuhifadhi katika kanzi data kwa ajili ya utambuzi na kutumia kitambulisho kipya cha kupiga kura.

“Mfumo huu hutumika katika kumtambua mtu na kumtofautisha na mwingine, ingawa tabia hizo za binadamu ziko nyingi, lakini kwa ajili ya kuandikisha wapiga kura watachukuliwa alama za vidole vyote kumi  vya mikono, picha na saini ndizo zitachukuliwa na kuhifadhiwa kwenye Kanzi Data (Database) ya wapiga kura” Alisema Jaji Mkwawa

Jaji Mkwawa alisema kupiga kura kwa Watanzania walio wengi sio lazima hivyo  hawaoni thamani ya kupiga kura, hivyo Vyombo vya Habari vinawajibu mkubwa wa kuelimisha umma juu ya  umuhimu wa kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura na ni tofauti na nchi ya Shelisheli ambayo kujiandikisha na kupiga kura ni lazima.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya habari na Elimu kwa Wapiga Kura Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Ruth Mashama akiwasilisha mada inayohusu maandalizi ya uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura  kwa kutumia teknolojia ya Biometric Vote Registration (BVR) ameeleza kuwa Tume inatarajia kuboresha Daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya kwanza hivi karibuni na maandalizi yake tayari yamekamilika kwa sehemu kubwa na baadhi ya vifaa vimeanza kuwasili nchini Tanzania.

Alisema matumizi ya mfumo mpya utatumika katika zoezi la uandikishaji  pekee tofauti na nchi nyingine zilizotumia mfumo hadi katika kupiga kura na kugundua mafanikio yaliambatana na changamaoto mbalimbali za kiteknolojia na kimfumo.

Mashama alizitaja baadhi ya nchi za Kiafrika zilizokwisha tumia mfumo wa BVR kuwa ni Nigeria 2007,Ghana 2009,Liberia2005,Guinea 2005,Mali 2005, Uganda 2008,Kenya 2013,Zambia 2008, Afrika Kusini na Zanzibar 2009. 

No comments: