Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Rais mstaafu wa awamu ya pili , Ali Hassan Mwinyi ,amewataka watanzania kuwa makini kwa kutoruhusu tofauti za dini zilizopo hapa nchini kuwa chanzo cha mgawanyiko miongoni mwao.
Kauli hiyo ameitoa jana usiku jijini Dar es salaam wakati wa Futari iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Saidi Meck Sadiki kwa watoto wanaoishi katika vituo vya kulelea watoto yatima, wananchi na viongozi mbalimbali iliyofanyika katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam.
Mzee Ali Hassan Mwinyi ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati wa Futari hiyo amesema kuwa kila Mtanzania bila kujadili itikadi na dini aliyonayo ana wajibu wa kulinda na kutunza amani iliyopo kwa kuendelea kudumisha upendo na ukarimu kwa wenzake ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo yaliyomo katika vitabu vitakatifu.
“Nawasihi Watanzania wenzangu tuendelee kupendana, tuwe wamoja katika kushirikiana, kamwe tusiruhusu wala kukubali mgawanyiko wa dini wala itikadi zetu” Amesisitiza.
Amewashukuru viongozi wa mkoa wa Dar es salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Saidi Meck Sadiki kwa uamuzi walioufanya wa kuandaa Futari iliyowaunganisha watoto yatima, wananchi na viongozi mbalimbali bila kujadili itikadi na dini zao ikiwa ni ishara ya kuonyesha upendo na ukarimu walio nao.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Saidi Meck Sadiki akizungumza wakati wa Futari hiyo aliyowaandalia wageni hao amesema kuwa serikali ya mkoa inaendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ukarabati na ujenzi wa miundombinu iliyoharibiwa vibaya wakati wa msimu wa mvua jijini Dar es salaam.
Bw. Sadiki ameziagiza Halimashauri za Wilaya za Temeke, Ilala na Kinondoni na Wakala wa Barabara (TANROAD) mkoa wa Dar es salaam kuhakikisha kuwa wanarejesha hali ya kupitika kwa barabara iliyokuwepo mwanzo ili kuwaondolea kero ya usafiri wananchi.
Amezitaka mamlaka hizo kutumia fedha za ndani na zile zilizotolewa na Serikali Kuu kukamilisha ukarabati wa miundombinu hiyo yakiwemo madaraja yaliyosombwa na maji kwa muda muafaka ili kuruhusu magari kuweza kufika katika maeneo hayo.
Katika hatua nyingine Bw. Meck Sadiki ametoa wito kwa wakazi wa jiji la Dar es salaam kushiriki kikamilifu katika suala la usafi na uhifadhi wa mazingira kwa kujenga utaratibu wa kusafisha mazingira ya jiji ili kulinda heshima ya jiji huku akisisitiza kuwa dini zote zinamtaka mwanadamu awe mwadilifu na mwenye kuzingatia usafi.
Amezitaka mamlaka zinazosimamia utekelezaji wa sheria za kuhifadhi mazingira jijini Dar es salaam kufanya kazi kwa kuzingatia weledi ili kuhakikisha maeneo yote ya jiji yanaendelea kuwa katika hali ya usafi. Naye Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhadi Mussa Salum akuzungumza wakati wa Futari hiyo ameeleza kuwa viongozi wa dini na serikali kote nchini wanalo jukumu kubwa la kuwaongoza wananchi kutenda mema na kuendelea kuvumilia.
Rais Mstaafu wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi akiwasili katika viwanja vya Karimjee kuhudhuria Futari iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Saidi Meck Sadiki (wa pili kutoka kushoto) kwa watoto yatima kutoka vituo mbalimbali vya kulelea watoto hao vya jiji la Dar es salaam. Wengine wanaoonekana kutoka kulia ni Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es salaam, Kamishna Suleiman Kova na Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Alhadi Mussa Salum.
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es salaam, Kamishna Suleiman Kova (katikati) akifafanua jambo kwa viongozi wa mkoa wa Dar es salaam Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Bw. Saidi Meck Sadiki (wa pili kutoka kulia), Mkuu wa Wilaya ya Ilala Bw. Raymond Mushi(kulia) na Mkuu wa wilaya ya Temeke Bi. Sophia Mjema (kushoto) wakati wa Futari iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa huo katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam.
Mkuu wa wilaya ya Temeke Bi. Sophia Mjema (kushoto) akizungumza jambo na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Bw. Saidi Meck Sadiki (katikati), Mkuu wa Wilaya ya Ilala Bw. Raymond Mushi(kulia) na Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es salaam, Kamishna Suleiman Kova (wa pili kutoka kushoto) wakati wa Futari iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam.
Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Alhadi Mussa Salum (wa kwanza kushoto) na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Abdulrahmani Kinana wakijumuika katika Futari hiyo.
Baadhi watoto yatima kutoka vituo mbalimbali vya kulelea watoto hao vya jiji la Dar es salaam wakijumuika pamoja katika Futari iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Saidi Meck Sadiki.
Rais mstaafu wa Awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati wa Futari iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam kwa watoto yatima kutoka vituo mbalimbali vya kulelea watoto hao vya jiji la Dar es salaam akijumuika pamoja na watoto hao na wageni mbalimbali walioalikwa katika Futari hiyo.
Baadhi ya akina mama na watoto waliohudhuria Futari hiyo wakipata Chakula.
Rais wa Tanzania wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati wa Futari iliyoandaliwa na Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam akisisitiza umuhimu wa kulinda na kutunza amani iliyopo kwa kuendelea kudumisha upendo na ukarimu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo yaliyomo katika vitabu vitakatifu.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya (kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Songea Dkt. Christine Ishengoma(kulia) wakiungana na viongozi wengine kushiriki Futari iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam kwa watoto yatima kutoka katika vituo mbalimbali katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam. Picha na Aron Msigwa- MAELEZO.
No comments:
Post a Comment